Kiasi ina maana gani katika ukristo?

Kiasi ina maana gani katika ukristo?

John Achila Mukumwa

Senior Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
113
Reaction score
222
Kiasi Ina Maana Gani Katika Ukristo

Kiasi ni nini
Kiasi kama tafsiri yake ilivyo ni kuwa na uwezo wa kudhibiti jambo/tendo lisipitilize mipaka yake, yaani litendeke kwa sehemu fulani tu.

Katika Ukristo, kiasi ni moja ya matunda 9 ya Roho Mtakatifu
. Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, KIASI; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”. Hii ina maana kuwa ukipungukiwa nacho (kiasi), ni uthibitisho mojawapo kuwa Roho wa Mungu hayupo ndani yako. Kwa sababu huu ulimwengu una mambo mengi, ambayo ni mazuri, lakini yakipitiliza matumizi yake, yanabadilika na kuwa mabaya na sumu kubwa, kuliko hata matendo yenyewe mabaya.

Sehemu muhimu ambazo Roho Mtakatifu anataka sisi tuwe nazo na KIASI

1. Kwenye ndoa

1Wakorintho 7: 4 “Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. 5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.
Kukosa kiasi katika tendo la ndoa, hupelekea watu wengi sana kumtenda Mungu dhambi. Tuishi kama vile, hakuna jambo jipya tumeongeza, pale tulipooa au kuolewa, hiyo itatusaidia sana, kuishi maisha ya utakatifu na kumcha Mungu, katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho duniani.

2. Kwenye shughuli za ulimwengu
Bwana ametuweka duniani tufanye kazi, pia tujitafutie riziki. Lakini anatutahadharisha, tusipitilize, mpaka kufikia hatua ya mioyo yetu kuzama huko moja kwa moja tukamsahau yeye, hata muda wa ibada, au kuomba au kuwaeleza wengine Habari Njema tukakosa. Hiyo ni hatari kubwa sana.
1Wakorintho 7:31 “Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita”. Yaani, fanya kazi huku ukijua mahusiano yako, au ratiba yako na Mungu haivurugwi hata kidogo. Kwa sababu ukiupeleka moja kwa moja moyo wako huko, ni lazima tu ulale kiroho, na matokeo yake, utakufa na bado hujayatengeneza mambo yako vizuri na Mungu.

Vitabu vya Ayubu 15:32 na Zaburi 55:23, vinasema: Usiwe mwovu kupita kiasi, wala usiwe mpumbavu: kwa nini kufa kabla ya wakati wako?

3. Kwenye huduma

Mungu anataka watumishi wake pia wawe na kiasi. Haimaanishi kiasi katika kumtumikia Hapana. Anataka sana tuzidi kumtumikia kwa bidii, bali inamaanisha kiasi katika karama.
Anasema katika Warumi 12: 3 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. 4 Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; 5 Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake”.

Hii ni kutuonyesha kuwa hakuna hata mmoja wetu mwenye karama zote, Ni Yesu tu peke yake. Hivyo ridhika, na ulichokirimiwa. Ukiwa ni mchungaji, usitake wewe wewe ndiye uwe ni nabii, na mwalimu, na mwimbaji, na mwinjilisti, na mtume n.k. Huwezi kuwa Yesu.

4. Kwenye haki
Mhubiri 7:16 “Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe? Hapa pia Mungu hamaanishi kwamba tusiwe na haki nyingi kupitiliza, Hapana. Anapenda sana tuwe hivyo. Lakini maana yake ni kuwa tusiwe watu wa kujihesabia haki kupitiliza (yaani kujisifia), kwani matokeo yake ni kujiangamiza wenyewe.
Yesu alisema katika Luka 18:14 “…kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”. Uendapo mbele za Mungu, au mbele za wanadamu, kuwa na kiasi. Mwache Mungu akuhesabie haki mwenyewe. Wewe mwenyewe usijifisie kwa lolote.

5. Kwenye kunena
Biblia inasema: Mithali 10:19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili”.
Kwa nini haisemi, katika uchache wa maneno, hapakosi kuwa na maovu? Ni kuonyesha kuwa, unapokuwa mzungumzaji kupitiliza, ni rahisi sana kujikwaa ulimi, lakini ukiwa si mwepesi wa kuzungumza zungumza, yaani kila habari au kila jambo unachangia, basi utajiepusha na maovu mengi.
Mhubiri 5:2 “Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache”.

6. Kwenye vyakula na vinywaji
Vinywaji kama divai, vilikuwa ni vya kitamaduni Israeli, wakati ule, kwa sababu pia ndani yake waliamini kuna tiba (1Timotheo 5:23). Hivyo, vilikuwa vinanyweka kwa kiasi sana, kwa sababu vilikuwa na kiwango cha kileo ndani yake. Paulo akamwagiza Timotheo kuhusiana na Mashemasi na wazee wa kike katika makanisa, akamwambia: 1Timotheo 3:8 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana, si watu wanaotamani fedha ya aibu”

Biblia imeweka wazi kabisa, walevi wote sehemu yao itakuwa katika lile ziwa la moto (1Wakorintho 6:10). Siyo kila kitu ule, au unywe. Zuia koo lako, zuia tumbo lako. Wakati mwingine funga, Litunze hekalu la Mungu. Utaona faida yake.

7. Kwenye mwenendo
Hapa Tito anatoa angalizo, katika mienendo yetu na mionekano, hususan kwa vijana.
Tito 2:6 “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi”.
Jiulize kwa nini hasemi, wazee au watoto?
Anasema vijana kwa sababu anajua kabisa vijana wengi wa kike na wa kiume waliookoka, wanakosa kiasi katika ujana wao. Hakuna sababu ya kukesha katika muvi au magemu, au mipira kutwa kuchwa. Ukiwa umeokoka, ili hali unajua kabisa kusoma biblia, kuomba na kuhubiri kunakusubiria.
1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani”.
Kijana, hana sababu ya kunyoa kiduku, aonekane kama msanii fulani. Kumbuka kuwa muonekano wako unaweza kuwa na athari katika kukupunguzia utukufu wako.

Katika kuhitimisha ni kuwa kiasi katika mambo yote ni muhimu sana. Hivyo tujitahidi kwa upande wetu kila mmoja aangalie ni wapi amekosa kiasi, kisha arekebishe mapema, na Roho Mtakatifu atajaa tena ndani yetu kutusaidia kuushinda ulimwengu. 2Tim 4:5: “Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa injili, timiliza huduma yako".

Ibilisi anatufuta WATU WANAOKOSA KIASI ili awameze, usiwe mmojawapo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom