Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,267
BARAZANI KWA RAJAB
Khashoggi: “Sema unayotaka kusema ujiendee zako”
Na Ahmed Rajab
NILIKUTANA na Jamal Khashoggi siku moja tu katika maisha yangu. Ilikuwa mwezi wa Ramadhan nilipoalikwa futari, jijini London, na Turki bin Faisal bin Abdulaziz al Saud. Turki ni mtoto wa Mfalme Faisal (aliyetawala 1964 hadi 1975) na mjukuu wa Abdulaziz bin Abdulrahman al Saud (1876-1953), muasisi wa Saudi Arabia na mfalme wa kwanza wa taifa hilo .
Turki ni rafiki wa chanda na pete wa marafiki zangu wawili wakubwa. Aliponialika futari alikuwa balozi wa Saudi Arabia nchini Uingereza.
Kabla ya hapo, na kwa miaka mingi, alikuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la ujasusi la Saudi Arabia (Al Mukhabarat Al ‘Ammah). Alipokuwa balozi Uingereza (2003-2005), mshauri wake alikuwa mwanahabari Jamal Khashoggi aliyekuwako kwenye futari.
Jina la Khashoggi limekuwa midomoni mwa watu dunia nzima tangu Oktoba 2 alipotia mguu katika ubalozi mdogo wa Saudia, ulio Istanbul, Uturuki, akatoweka. Hakuonekana tena akitoka nje ya jengo hilo. Aliyayuka au aliyayushwa?
Waturuki wanasema wana ushahidi madhubuti kwamba Wasaudi walimtesa Khashoggi, wakamuua na maiti yake wakaikatakata. Wasaudi wanasema huo ni uongo lakini hawasemi Khashoggi yu wapi.
Khashoggi hakuwa mwanahabari wa kawaida. Kwa muda mrefu alikuwa chini ya mbawa za Turki, alipokuwa mkuu wa ujasusi na ninavyofahamu ni kwamba Khashoggi akitumiwa mara kwa mara na Turki.
Khashoggi hakuwa mtu niliyekuwa nikijuana naye. Nikizijua fikra zake kutokana na maandishi yake na mahojiano aliyokuwa akifanyiwa na steshini mbalimbali za televisheni duniani. Sikukubaliana na nyingi ya fikra zake kuhusu siasa za Mashariki ya Kati.
Katika miaka ya hivi karibuni, alikuwa mkosoaji makini wa watawala wa Saudi Arabia. Hakuwa muasi; wala hakuwa mwanachama wa kundi lolote la upinzani. Alikuwa akiuunga mkono mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Nikimuona kuwa ni mmoja wa wapambe wa watawala wa Saudi Arabia, kwani madikteta nao huwa na wapambe wao, miongoni mwao wakiwa hata wasomi wa kuheshimika.
Khashoggi, mwenye asili ya Kituruki, alikuwa karibu mno na aila ya kifalme ya al Saud na ukoo wake ni wa kitajiri. Babu yake, Mohamed Khaled Khashoggi, alikuwa daktari muhtasi wa Mfalme Abdulaziz.
Alikuwa mtoto wa mjomba na shangazi na Dodi al Fayed, aliyekuwa na mahusiano ya kimapenzi na Princess Diana wa Uingereza, aliyewahi kuwa mke wa Prince Charles, mrithi wa ufalme wa Uingereza. Dodi na Diana walikufa pamoja katika ajali ya gari jijini Paris, Agosti 31, 1997.
Bilionea Adnan Khashoggi, ami yake Jamal, akivuma katika miaka ya 1960,1970 na 1980 kwa jinsi alivyokuwa akinuka fedha na alivyokuwa akizitumia kwa ubadhirifu uliopindukia mpaka.
Zamani, na kwa miaka mingi, Jamal Khashoggi alikuwa akiutetea ukoo wa al Saud. Walio kwenye ukoo huo wanaamini kwamba nchi hiyo ni milki yao na wanaweza kujifanyia watakavyo ndani yake na nje yake.
Hiyo ni nchi pekee duniani yenye jina la aila au ukoo wenye kutawala: “Saudi Arabia”, Uarabuni ya Saudi (Arabia ya Saudi).
Tangu ufalme wa al Saud uanzishwe kwa upanga, milki hiyo imekuwa ikitawaliwa kimabavu. Damu nyingi imemwagwa; waliomwagiwa damu zao walikuwa na maoni tofauti na ya watawala.
Hivyo ndivyo damu inavyomwagika na kuchuruzika katika tawala za kidikteta. Udikteta ni udikteta; hauna sura moja. Madikteta wa Saudi Arabia huvaa kanzu na mabushti na hujifanya wanyenyekevu lakini kwa kweli wana hulka zilezile za kikatili kama madikteta wengine.
Mfumo wao wa utawala ni wa kishenzi. Hauna adabu; hauna sheria; wala hauna huruma.
Shughuli kubwa ya udikteta ni kuzinyamazisha sauti huru zenye kuwakosoa watawala. Wakati mwingine utawala wa kimabavu huziandama na kuzichimba taasisi zenye kuzilinda au kuzipa hifadhi sauti huru.
Katika miaka ya karibuni moja ya hizo sauti huru ndani ya Saudi Arabia ilikuwa ya Jamal Khashoggi.
“Sema unayotaka kusema ujiendee zako,” hiyo ndiyo tafsiri ya kaulimbiu ya Kiarabu kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Nadhani dhambi yake kubwa ni kwamba alikuwa hayafichi yaliyokuwa moyoni mwake kumhusu Mohammed bin Salman. Ingawa mfalme ni Salman bin Abdulaziz lakini mwenye kuiendesha nchi ni mwanawe Mohammed bin Salman, kijana wa miaka 33. Inasemekana kwamba bin Salman hamsikilizi mtu isipokuwa labda mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed al Nahyan.
Mohammed bin Salman anataka ulimwengu uamini kuwa yeye ni mwanamageuzi atayeibadili Saudi Arabia. Na wapo walioghilibika alipowaruhusu wanawake waendeshe magari, wende sinema, wahudhurie mechi za soka na waruhusiwe mambo mengine ya anasa.
Tangu apewe dhamana kubwa katika serikali amekuwa akiuma na kupuliza. Amewapa wanawake ruhusa ya kuendesha gari na wakati huo huo amekuwa akiwakamata wanaharakati wanaopigania haki za wanawake.
Amekuwa akiwafunga wafanyabiashara, hata jamaa zake wa kifalme kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi, na papo hapo amekuwa akiwahimiza wawekezaji waingize rasilmali zao Saudi Arabia na kuwekeza.
Bin Salman ana amini kwamba anaweza kufanya uovu autakao na akavuka kwa sababu ana kinga. Ngao anayofikiri kuwa ataitumia ni usuhuba mkubwa alionao na Jared Kuchner, mkwewe Rais Donald Trump.
Marekani imekuwa ikizichezea nchi za Ghuba kwa sababu nchi zenyewe zimekuwa zikijiachia zichezewe na zimekuwa zikijiachia zichezewe kwa sababu za kimaslahi. Maslahi yenyewe ni ya kulindwa tawala zao za kidikteta.
Katika nchi ambako watu wanakuwa na haki ya kusema na uhuru wa kusema, si rahisi kwa watawala kuwakaba koo wenye kuwakosoa. Si kwamba hawajaribu. Hujaribu; lakini hukwama kwa sababu ya taasisi za kidemokrasia zilizopo na pingamizi za kisheria.
Lakini katika nchi kama Saudi Arabia isiyo na utawala wa kisheria na ambako watu hunyimwa haki ya kusema na hawana uhuru wa kusema, wanapojaribu kusema hujikuta wanapoteza sauti zao pamoja na maisha yao. Ndio maana wanaoweza kuikimbia nchi huikimbia.
Hivyo ndivyo alivyoamua kufanya Khashoggi kama mwaka hivi uliopita.
Aliamua kwenda kuishi Marekani alipotanabahi kuwa wenye maoni tofauti na yale ya mwenye nguvu Saudi Arabia wamekuwa wakitoweka, mmoja mmoja, na kutumbukizwa gerezani.
Septemba mwaka jana Khashoggi aliandika kwamba aliamua kuihama nchi ili aweze kuipaza sauti yake kuwatetea wanaoselelea gerezani. Alikuwa akisema pia kwamba siku hizi hakuna nafasi ya kuvuta pumzi Saudi Arabia.
Wote hao walio kifungoni hawakubaliani na Mohammed bin Salman ama juu ya hili au juu ya lile. Bin Salman ndiye mwenye nguvu kushinda wote nchini mwao.
Baadhi ya hao waliokamatwa ni rafiki zake Khashoggi na wengine ni watu aliokuwa akiwajua. Wote walithubutu kuyasema asiyotaka kuyasikia Mohammed bin Salman. Kila mmojawao alitafutiwa kisingizio cha kuwekwa korokoroni.
Hao ndio waliobahatika. Wasiobahatika walikatwa vichwa, miongoni mwao wakiwa mashekhe wa Kishi‘a.
Kuna wanaokatwa vichwa hadharani ati kwa kuwa wanaamini uchawi.
Khashoggi aligeuka na kuwa mwiba wenye kumchoma bin Salman alipoanza kumkosoa na kumuonya kuhusu Rais Trump.
Kwa mara ya mwanzo katika historia ya Saudi Arabia nchi hiyo inaendeshwa na kijana lakini ni kijana asiye na busara.
Miezi 16 imepita tangu ateuliwe mrithi wa ufalme. Katika kipindi hiki kifupi amefanya mambo kadhaa ya kushtusha. Watu wanajiuliza iwapo sasa anatisha na kuitikisa nchi namna hii atakuwaje atapokuwa mfalme?
Bin Salman ni mkaidi, kichwa mchungu, ana kibri na hujifanyia atakavyo kwa papara, bila ya kufikiri mara mbilimbili. Lililo baya zaidi ni kwamba kijana huyu ana tabia ya kulipiza visasi na ana husuda. Ninaamini kwamba tatizo lake kubwa na watawala wa Qatar, kwa mfano, ni kwamba anawaonea kijicho kwa utajiri walio nao kutokana na mauzo yao ya gesi asili na ushawishi wao katika jukwaa la siasa za kimataifa, hususan za Mashariki ya Kati.
Jengine lenye kumla roho ni chuki. Ana chuki, tena za kitoto, dhidi ya waumini wa madhehebu ya Shi‘a. Ana chuki dhidi ya Iran na utawala wake wa Kiislamu. Chuki hizo zinamfanya azidi kujipendekeza kwa Marekani na Israel. Na hufanya hivyo kwa kuzionesha nchi hizo kuwa lengo lake kuu ni kuuangamiza utawala wa Kiislamu wa Iran na kwa kuiunga mkono Israel dhidi ya maslahi ya Wapalestina.
Chuki zake dhidi ya Iran na ushi‘a ndizo zinazomfanya achukue hatua anazochukua Yemen ambako anatumia dola bilioni tano za Marekani kwa mwezi kupigana na wapiganaji wa Houthi.
Akili zake bin Salman zinamwambia kuwa ni halali kila siku, usiku na mchana, kuiogesha Yemen kwa damu. Damu hiyo naiwe baridi naiwe moto, naiwe kongwe naiwe mbichi, ya vikongwe au ya vitoto.
Hajali ni watu wangapi wa Yemen anawaua, kila uchao, kwa kuwatwanga kwa mabomu. Mabomu na makombora ya Saudi Arabia yamekuwa yakinyesha kama mvua kwenye miji na vijiji vya Yemen. Yamewapiga na kuwaua watoto walipokuwa wakirudi skuli wakiwa ndani ya basi. Yamewaua wanawake waliokuwa wakipiga vigelegele harusini. Mabomu hayo hayachagui mume wala mke, mdogo wala mkubwa, soko wala hospitali.
Udikteta wa Saudia ni udikteta wa kurithiana, wa ndugu kumrithi kaka na tangu Salman awe mfalme 2015 kurithiana huko kutakuwa kwa mwana kumrithi baba. Ni udikteta wenye kulindwa kwa silaha za Uingereza na nguvu za kijeshi za Marekani.
Rais wa sasa wa Marekani,Trump, ana mazoea ya kuupindisha ukweli, kuwababaisha watu na kudanganya. Anapofanya hayo huwa hana haya wala haoni kuwa anafanya jambo la aibu. Huo ndio uzuri wake kwa sababu juu ya uongo wake katika nyakati kama hizo ndipo yaliyo kweli hupenya mdomoni mwake.
Mfano ni maneno aliyoyasema hivi majuzi kuhusu jinsi Marekani inavyoulinda ufalme wa Saudi Arabia. Alimwambia wazi hadharani Mfalme Salman kwamba hawezi kusalia madarakani hata kwa wiki mbili kama halindwi na Marekani. Maneno hayo yalimdhalilisha Salman lakini Trump hakujali, hajali wala hatojali.
Kwa sasa Trump na Wasaudi wanatiana ndaro. Trump anasema Marekani itaichukulia hatua kali Saudi Arabia ikibainika wazi kwamba imemuua Khashoggi. Watawala wa Saudia nao wanasema watalipiza kisasi kwa hatua kali zaidi watapochukuliwa hatua kuhusu kadhia ya Khashoggi.
Juu ya hayo, sidhani kama Marekani iko tayari kuacha kuwalinda vibaraka wao wa Saudi Arabia na kwingineko katika Ghuba.
Baruapepe: hamidurubawa@gmail.com