Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwanaharakati Mange Kimambi inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Soma: Kesi ya Mange Kimambi ya utakatishaji wa fedha kuunguruma leo Desemba 4, Kisutu
Mange, anayeishi Marekani, ameshitakiwa kwa utakatishaji fedha TZS milioni 138.5, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022 Dar es Salaam; kufanya uandishi wa habari bila kibali, pamoja na kudai fedha kupitia vitisho.
Kesi hiyo, chimbuko lake ni mashitaka ya mwaka 2022, imezua maswali kuhusu ni kwa nini imefufuliwa wakati huu.
Shauri hilo la jinai namba 000021172/2025, lililofunguliwa na Jamhuri Agosti 28, 2025, linadai kuwa kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Mange alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu kuwa ni fedha za uhalifu.
Inadaiwa pia alipata fedha hizo kupitia kazi ya uandishi wa habari bila kibali na kwa vitisho. Mashitaka hayo yanatokana na kifungu 12(1) (d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423 ya mwaka 2019, kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi
Desemba 4, 2025, shauri hilo liliitwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube. Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama kuahirisha kesi kwa maelezo kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kwa upande wa utetezi, Mange hakuwa na wakili, hivyo Hakimu Makube aliutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha taratibu zote zimekamilika ili kesi ianze kusikilizwa katika tarehe itakayopangwa.