Kesi ya Bilionea Msuya: Licha ya mateso ya Polisi bado mshitakiwa akana kuwa na ukaribu na Chussa

byembalilwa

JF-Expert Member
Aug 7, 2012
2,034
918
Moshi. Mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed ameiambia mahakama kuwa hajawahi kukutana gerezani na mfanyabiashara Joseph Mwakipesile maarufu Chussa na kupanga mauaji ya Erasto Msuya.

Mbali na kukana kuwa na ukaribu na Chussa, aliyakana pia maelezo ya kukiri kosa yanayodaiwa kuwa ni ya kwake yakimtaja Chussa akidai yalitengenezwa na polisi ili kumbambikia kesi hiyo.

Akihojiwa na wakili Majura Magafu baada ya kumaliza kutoa utetezi wake, Sharifu alienda mbali na kudai hawafahamu washtakiwa wenzake wote na kwamba alikutana nao alipofikishwa kortini.

Mshtakiwa huyo alidai maelezo ya kukiri kosa yanayodaiwa ni ya kwake yaliyosomwa na shahidi wa 27, Inspekta Damian Chilumba, yakisema aliwahi kumtembelea Chussa gerezani ni ya uongo.

“Sijawahi kufika gereza la Babati wala Hospitali ya Babati na wala sikuwa na ukaribu na Chussa hadi niende kumtembelea. Sijawahi kumtembelea hospitalini wala sijui hiyo hospitali iko wapi,” alidai.

Pia, mshtakiwa huyo alikana maelezo yaliyomo katika maelezo yanayodaiwa ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu na wa saba, Ally Mjeshi, waliodai ndiye aliyewezesha mauaji hayo.

“Ushahidi kuwa mimi ndiye niliwezesha kusajiliwa kwa laini za simu na kununua pikipiki zilizotumika katika mauaji ni uongo wala sijawahi kushiriki kupanga mauaji ya Erasto Msuya,” alieleza.

Alipoulizwa na Magafu kama alisikia maelezo yake mwenyewe na ya Mangu yaliyosomwa kortini kuwa ndiye aliyewezesha kupatikana kwa SMG iliyotumika kwenye mauaji, alidai ni uongo.

Magafu alimuuliza anazungumziaje katika maelezo yake kuwa aliwataja watu wawili, Chussa na Kaburu, alidai Chussa anamfahamu kama mfanyabiashara mwenzake lakini hamfahamu Kaburu.

Akihojiwa na wakili Emmanuel Safari anayemtetea Mangu, kuwa anazungumziaje kama maelezo yake kuwa alimtaja Chussa, Sharifu alidai kama ingekuwa ni kweli angekuwa miongoni mwa washtakiwa.

Awali, akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wake, Hudson Ndusyepo, Sharifu alidai siku ya mauaji ya Erasto, yeye alikuwa katika machimbo ya madini ya London, yaliyopo Ikungi, Singida.

“Huko London nilikwenda kuanzia tarehe 15/07/2013 na nilikuwa huko hadi tarehe 10/07/2013 niliondoka kuelekea Arusha na nikafika alfajiri ya tarehe 11/07/2013,” alidai mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo alidai baada ya kufika Arusha aliendelea na shughuli zake hadi Agosti 13, 2013 na alikamatwa na polisi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi (RCO) Mkoa wa Arusha, Duan Nyanda.

Alieleza kuwa siku hiyo alfajiri akiwa nyumbani kwake, alisikia watu wakigonga lango kuu na alipotizama katika kamera za usalama (CCTv), aliona magari mawili ya polisi yakiwa nje kwake.

“Nilifungua gate (lango kuu) nikaona polisi lakini nilimtambua RCO Duan na nikamsikia akimwambia Samwel (shahidi wa tisa) kuwa huyu ndiye Sharifu muingizeni kwenye gari.

“Samwel alinikamata na kuniingiza kwenye gari mojawapo akanifunga pingu na kitambaa usoni na gari lile liliondoka na kuendeshwa kwa takriban saa moja na kufika kwenye eneo nisilolijua.

“Niliingizwa katika chumba kimojawapo na nilifunguliwa kitambaa. Hapo ndipo nilipomuona Chilumba na Herman (shahidi wa nane) wakiwa hapo na polisi wengine siwafahamu.

“Chilumba aliniuliza kwa nini nilishiriki kupanga mauaji ya Erasto Msuya. Nikamwambia mimi sikuhusika wala kushiriki. Chilumba aliamuru niwekwe lockup (mahabusu).

“Niliwekwa mahabusu bila kupewa chakula hadi tarehe 14/08/2013 asubuhi, Chilumba alikuja kunitoa lockup akaniingiza kwenye chumba akiwa na makaratasi akinilazimisha niyasaini,” alieleza Sharifu.

Abubujikwa machozi
Wakati akieleza hayo, ilipofika saa 6:55 mchana, ghafla mshtakiwa huyo aliomba kukaa kwenye kiti kwa kuwa hajisikii vizuri na hapo hapo akaanza kububujikwa na machozi akiwa kizimbani.

Jaji Salma Maghimbi alimuuliza wakili Ndusyepo iwapo shahidi wake angeweza kuendelea kutoa ushahidi wake akiwa amekaa, lakini Sharifu akasema ataendelea kutoa ushahidi akiwa amesimama.

Sharifu alidai alikataa kusaini maelezo hayo bila kufahamu yameandikwa nini, baada ya kueleza hivyo alirudishwa mahabusu huku akinyimwa kuonana na ndugu wala mwanasheria wake.

Alidai kuwa Agosti 18, 2013 alikuja Chilumba akiwa na polisi wengine na kumueleza kuwa hawataki hadithi nyingi zaidi ya kumtaka asaini makaratasi ambayo yeye alikuwa hajui yameandikwa nini.

“Waliniambia sali sala zako za mwisho au siyo tukupeleke msitu wa TPC tukuue. Kwa vile kabla ya hapo alishanipiga kofi niliona hawatanii na kwa jinsi nilivyokuwa nimedhoofu nilisaini,” alidai.

Shahidi huyo alisisitiza kuwa siku alipokamatwa, hakuwahi kupelekwa ofisi za RCO Arusha wala kuandika maelezo yake katika ofisi hizo, zaidi ya kujikuta yupo mahabusu ya Chuo cha Polisi Moshi (CCP).

“Niko chini ya kiapo na naiambia mahakama kuwa ushahidi wote uliotolewa mahakamani dhidi yangu ni wa kubambikiziwa, sihusiki kwa chochote wala sifahamu lolote juu ya mauaji haya,” alieleza.

Akihojiwa na upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla, alidai tukio la kukamatwa kwake lilishuhudiwa na mkewe, mdogo wake na mlinzi wake.

Alipotakiwa kuieleza mahakama kama ni kweli katika maelezo yake ya onyo ya kukiri kosa aliyoyatoa polisi alisaini na baadaye kuweka dole gumba, alidai ni kweli na alifanya hivyo kwa kulazimishwa.

Katika maswali hayo, Chavulla anayesaidiana na Kassim Nassir alimtaka shahidi huyo aeleze kama ni kweli mwisho wa maelezo yake aliandika uthibitisho kwa mwandiko wake.

Akijibu swali hilo, mshtakiwa huyo alidai ni kweli aliandika uthibitisho kwa mwandiko wake mwenyewe lakini akadai alifanya hivyo baada ya kulazimishwa na Chilumba na polisi wenzake.

Alipoulizwa inakuaje anakana kumfahamu mshtakiwa Mangu, wakati katika usikilizwaji wa kesi ndani ya kesi hawajawahi kusema hamfahamu, alijibu hakupata nafasi ya kuongea na wakili wake.

Mmoja aachiwa
Awali kabla ya kuanza kujitetea, Jaji Maghimbi alitoa uamuzi wake na kuwaona washtakiwa sita kati ya saba kuwa wana kesi ya kujibu na kumwachia mshtakiwa wa nne, Jalila Zuberi.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 27 walioutoa ushahidi wa moja kwa moja, mashahidi watano ambao ushahidi wao ulisomwa, na vielelezo 27, Jalila hana kesi ya kujibu.

Jaji Maghimbi alisema wakati washtakiwa wanafunguliwa mashtaka mwaka 2013, walikuwapo wanane lakini kuna mshtakiwa mmoja ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina aliachwa njiani.

Mfanyabiashara Joseph Mwakipesile maarufu Chussa, alikuwa miongoni mwa washtakiwa lakini mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kwa kutumia mamlaka yake, alimfutia shtaka hilo Aprili 17, 2014.

“Suala la ni kwa nini aliachiwa njiani hilo ni suala la DPP. Kwa sasa hivi mahakama inaona ushahidi unaonyesha washtakiwa sita mliobaki mna kesi ya kujibu na mtapaswa kujitetea,” alisema.

Baada ya uamuzi huo, wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea Sharifu alieleza kuwa mteja wake atajitetea kwa kiapo na kuita mashahidi wawili na kutoa kielelezo kimoja ambacho ni mashine ya DVR.

Washtakiwa wote sita mbali na kutoa ushahidi wao kwa njia ya kiapo, walidai wataegemea utetezi wa kisheria kuwa hawakuwapo eneo la tukio (alibi), siku mfanyabiashara huyo anauawa.

Mawakili wao, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu, waliwataja washtakiwa watakaojitetea kwa alibi ni Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Majeshi.

Mshtakiwa Mussa Mangu mbali na kujitetea kwa kiapo, atawasilisha kielelezo ambacho ni tiketi za basi huku mshtakiwa Ally Majeshi, akielezwa atawasilisha kielelezo ambacho ni cheti cha ndoa.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi sasa inawakabili washtakiwa sita ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Muss.

Chanzo: Mwananchi

Pia tembelea >> SHAHIDI: Chusa alipanga mauaji ya Bilionea Msuya
 
mm naona hii kesi imejaa usanii mwingi naona kama chussa ayupo hapo ....basi haki aitopatikana maana kuna usanii wakutaka kuwabamkizia watu kesi.
Hii case toka mwanzo walikua wanataka chusa wamuingize kwa vile ndgu wa marehemu ndio walikua wanamtaja,upelelezi wa police ulionyesha sharifu hakuwahi kwenda magereza au hosp ya manyara kumuona chusa ndio mana case ikawaangukia wahusika tu
 
Hii case toka mwanzo walikua wanataka chusa wamuingize kwa vile ndgu wa marehemu ndio walikua wanamtaja,upelelezi wa police ulionyesha sharifu hakuwahi kwenda magereza au hosp ya manyara kumuona chusa ndio mana case ikawaangukia wahusika tu
huyo Chusa alikuwa na ugomvi na marehemu?
 
Mwenyezi Mungu awasimamie ili haki itendeke..
FB_IMG_15263210501073076.jpg
 
Hii case toka mwanzo walikua wanataka chusa wamuingize kwa vile ndgu wa marehemu ndio walikua wanamtaja,upelelezi wa police ulionyesha sharifu hakuwahi kwenda magereza au hosp ya manyara kumuona chusa ndio mana case ikawaangukia wahusika tu
Aisee kwa inavyoelekea hata huyo sharif mwisho wa siku ataachiwa huru, swali gumu litabaki muuwaji hasa ni nani?
 
Aisee kwa inavyoelekea hata huyo sharif mwisho wa siku ataachiwa huru, swali gumu litabaki muuwaji hasa ni nani?
Sharifu na team yke wanaachiwaje?wakti hata redio mbao zinasema kweli alionekana na wasiwasi toka siku yametokea mauaji ya marehemu,kuna maneno hayo kwa watu wke wa karibu kua ni mhusika hata kabla hajakamatwa kuna watu walisanuka kua yeye mhusika
 
Duuuuuhh"" police kwenye tuhuma "" huyo chusa vipi !? wanamuonea au ""? anatafuta public sympathy
 
Wajuvi wa mambo mtujuze.

Huyu bwana Chusa ni nani? Mbona ametajwa na kila aliyetoa ushahidi lakini hayupo miongoni mwa washitakiwa. Huyu bwana ni nani? Alikuwa na mahusiano gani na Msuya na kwanini Msuya aliuawa?

Nawasilisha.
 
Back
Top Bottom