Kauli ya Museveni ndio suluhu DRC

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
DESEMBA 9 mwaka huu, Tanzania iliadhimisha miaka 51 ya Uhuru wake wakati huo ikiitwa Tanganyika, maadhimisho ambayo yaliambatana na mkutano muhimu sana jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ni ule wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambao ulifanyika chini uenyeji wa Rais Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wawakilishi kutoka nchi wanachama.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili kwa kina kuhusu hali tete ya amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inayosababishwa na uasi wa kundi la M23, pamoja na magenge mengine ya wahuni.

Kabla ya kuendelea, ni vema kumpongeza Rais Kikwete na timu ya maofisa wake kwa kukubali jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo, hatua ambayo inatukumbusha miaka iliyopita ambapo Tanzania ilikubali kuwa kitovu cha harakati za kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Pamoja na gharama kuwa kubwa kugharimia vikosi vya kulinda amani, gharama ambayo itachangiwa na nchi wanachama na zile rafiki, bado Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia kutokana na imani kubwa iliyoonyeshwa na nchi wanachama, kwa kuiteua Tanzania kuongoza vikosi vya SADC vitakavyokwenda DRC kulinda amani na kuwakabili waasi itakapobidi.

Pia hatua hiyo imeonyesha Afrika na Waafrika tukiamua kwa dhati, uwezo wa kulinda amani miongoni mwetu tunao, na hatuhitaji kuletewa majeshi ya kigeni kutoka nchi za Magharibi au kwingineko duniani wakiwamo ‘watalii’ wanaokuja kwa kivuli cha Umoja wa Mataifa (UN) wakidaiwa kulinda amani.

Miongoni mwa viongozi waliozungumza wakati wa kuhitimisha Mkutano wa SADC, ni Rais Yoweri Kaguta Museveni wa nchi jirani ya Uganda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Museveni ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioingia madarakani kwa mtutu wa bunduki zaidi ya miongo miwili iliyopita, alizungumza kwa uwazi huku akitumia uzoefu wake katika migogoro ya kisiasa na kijeshi kwenye eneo husika, kuhusu ni nini kinapaswa kufanywa kukomesha uasi na machafuko yasiyoisha mashariki mwa DRC.

Moja ya mambo ya msingi kabisa aliyozungumza Museveni ni uwepo wa askari zaidi ya 17,000 wa UN katika eneo hilo, lakini hakuna wanachokifanya zaidi ya kuponda starehe.

Alisema pamoja na uwepo wa vikosi hivyo vya UN ambavyo vilipelekwa kulinda amani kwa maana ya raia na mali zao miaka kadhaa iliyopita, lakini waasi na wahuni wengine ambao aliwaiita magaidi, wamekuwa wakitamba kadri wanavyojisikia na kuendelea kuua, kubaka, kupora mali na kuzalisha maelfu ya wakimbizi kila kukicha.

Katika hili la vikosi vya UN, ni vigumu kwa mtu yoyote kufahamu mantiki ya kuwapo kwake, kwa sababu vitawezaje kulinda raia dhidi ya magaidi kama haviruhusiwi kujibu mapigo pale raia wanaposhambuliwa? Hili kwa hakika lina utata.

Matokeo yake ni walinda amani hao kugeuka watalii ambao badala ya kuangalia vivutio vya utalii kama ilivyozoeleka popote pale duniani, wao wapo maeneo hayo wakiangalia raia wasio na hatia wakitaabika na kuuawa.

Binafsi nimebahatika mara kadha wa kadha kwenda DRC ambako walinda amani wapo katika maeneo kadhaa, hata kuna wakati walikuwapo kwa wingi katika Mji Mkuu wa Kinshasa, ukiwakuta ni askari wenye silaha nzito na za kisasa yakiwamo magari ya deraya na mengineyo, lakini cha kushangaza wapo huko kama watazamaji tu, na silaha hizo ni kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe.

Ni rahisi kwa mtu kushawishika kuwa, hatua ya UN, ambayo inaendeshwa na Wazungu kupeleka walinda amani maeneo kama mashariki mwa DRC, ambao wengi wao ni kutoka mataifa ya magharibi, ni njia mojawapo ya kutafutia ajira watu wao, lakini si kulinda amani.

Museveni alisema waasi waliopo mashariki mwa DRC ni magaidi kama walivyo magaidi wengine. Pia magaidi hawa ni hatari zaidi kuliko magaidi tuliozoea kuwasikia katika nchi za Mashariki ya Kati, Afghanistan na kwingineko.

Magaidi ambao tumewazoea kuwasikia ni wale ambao wanapambana na mataifa ya kibeberu kama Marekani, Uingereza na washirika wao, lakini hawa magaidi wa DRC wanapambana na kuua baba na mama zao, kaka na dada zao, watoto wao na ndugu zao wengine, hawa ni magaidi hatari kabisa ambao hawapaswi kupewa nafasi kabisa.

Hivyo kauli ya Museveni kuwa vikosi vya SADC vipewe jukumu la kujibu mapigo pale magaidi hao wanaposhambulia raia wasio na hatia, kwa hakika ndio suluhu pekee na njia thabiti ya kukomesha maovu na mauaji ambayo wanasiasa wetu wanayaita uasi.

Katika kuonyesha umuhimu wa mkakati huo mpya, Rais Museveni alitoa mfano wa majeshi ya Uganda yaliyokwenda Somalia, ambapo yalitakiwa kulinda uwanja wa ndege na Ikulu, na hayakutakiwa kujibu mapigo.

Lakini alisema baada ya kuona magaidi wa Al Shabab wanawashambulia, majeshi ya Uganda yaliamua kujibu mapigo kimamilifu, na ndio ukawa mwisho wa mashambulizi kutoka kwa magaidi hao.

Bila shaka ‘mhadhara’ alioutoa Rais Museveni jijini Dar es Salaam, tunaamini maudhui yake yameshawafikia magaidi wa M23, na kama wana masikio, basi wamesikia.
0755 530066

http://www.rai.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=158%3Akauli-ya-museveni-ndio-suluhu-drc&catid=13%3Asiasa&Itemid=39
 
Sijaelewa hapa M7 anawafananisha askari wa UN na magaidi ama anamaanisha M23 Ndio magaidi.unafki wa KAgame na M7 ushajulikana,wao wawili ndio chanzo cha vurugu DRC
 
Muwe mnasoma na kuelewa. Kila kitu kimeandikwa waziwazi ila unarukaruka na kuanza kuweka mahitimisho ya uongo.

Vurugu za Congo zimeanza wakati Kagame na Museven hawajazaliwa. Nenda kasome historia kijana.
Sijaelewa hapa M7 anawafananisha askari wa UN na magaidi ama anamaanisha M23 Ndio magaidi.unafki wa KAgame na M7 ushajulikana,wao wawili ndio chanzo cha vurugu DRC
 
Back
Top Bottom