Katiba Mpya: Spika, Jaji Mkuu watoa Maoni kwa Tume

Mwanaukweli

JF-Expert Member
May 18, 2007
4,786
1,710
MIHIMILI miwili ya Dola; Bunge na Mahakama, jana ilitoa maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaka kuwe na mabunge mawili na kupendekeza kuwa Spika wa Bunge na mawaziri wasiwe wabunge.

Wakati Spika Makinda akitoa maoni hayo, Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman amesisitiza umuhimu wa Mahakama kutoingiliwa na wanasiasa na akapendekeza usawa katika upatikanaji wa haki kwa wananchi wote wa Tanzania.


Makinda akiwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na viongozi wengine wa mhimili huo, alisema ni muhimu kuwe na Bunge la kuchaguliwa na wananchi na jingine la Seneti litakalotokana na wataalamu mbalimbali na viongozi wa zamani wenye uzoefu na walioitumikia nchi.


Alisema ni muhimu kukawa na aina hiyo ya mabunge pamoja na utaratibu wa wabunge kutokuwa mawaziri ili kulinda demokrasia ya kweli nchini.


“Tunataka Spika wa Bunge asiwe mbunge na pia mawaziri wasiwe wabunge. Wakuu wa mikoa na wilaya nao wasiwe wabunge. Pia tunataka Ibara ya 67 ya Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho ili kulinda demokrasia,” alisema Spika Makinda na kuongeza;


“Ibara hiyo inasema ili mtu awe mbunge lazima atokane na chama cha siasa, sasa Katiba Mpya ikataze kuwavua uanachama wabunge ambao wamechaguliwa na wananchi hata kama wanatokana na vyama vya siasa.”
Spika Makinda alisisitiza kwamba Bunge la Seneti litasaidia kuondoa mambo ya itikadi za vyama bungeni kama ilivyo sasa na kujali maslahi ya taifa katika kila jambo.

Spika asiwe mbunge
Makinda alisema umefika wakati Spika wa Bunge asitokane na wabunge na kwamba kama atachaguliwa kuwa Spika akiwa mbunge, ajiuzulu nafasi moja ili kuweza kulitumikia Bunge kiukamilifu.


Alisema Spika wa Bunge ni mwenye kazi nyingi hivyo ni vyema akapunguziwa majukumu hayo ili kutoa nafasi za kuendesha na kusimamia vizuri shughuli za Bunge.


“Tumependekeza Katiba Mpya itamke kwamba nafasi ya Spika wa Bunge haitatokana na ubunge na kama nafasi hiyo akipewa mbunge, atalazimika kujiuzulu nafasi moja,” alisema na kuongeza:


“Tumependekeza hivyo kutoa nafasi ya maspika wa Bunge kufanya kazi zao kikamilifu kwani nafasi hiyo ina mambo mengi sasa, ni vyema mabadiliko hayo yakatokea ili kuwapa nafasi wananchi wanaowachagua wabunge wao kutumikiwa kikamilifu,” alisema.

Mawaziri wasiwe wabunge
Makinda alisema ili kuhakikisha mgawanyo wa madaraka unaonekana kikamilifu wamependekeza Katiba Mpya ikataze mawaziri kuwa wabunge.
“Tumetaka kuondoa mgongano wa kimadaraka. Sisi tumependekeza kwamba Katiba Mpya ikataze mawaziri kuwa wabunge,” alisema Makinda na kuongeza:
“Mfano ni kwamba mbunge ana shida ya kupata fedha za maendeleo na waziri naye ana shida hiyohiyo katika jimbo lake, lazima atajijali yeye kwanza kwa kuwa ndiye anayepanga bajeti.”
Pia alisema wamependekeza Katiba Mpya ikataze wakuu wa mikoa na wilaya kuwa wabunge na kwamba wabunge wachaguliwe na wananchi tu.


Uhuru wa Mahakama
Jaji Mkuu Othman alisema Mahakama imewasilisha mapendekezo yake 12 kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, moja likiwa ni Katiba yenyewe kuwa msingi wa kutawala nchi.


“Katiba iwe ndiyo kitu bora chenye hadhi ya juu na kinapaswa kuwa chombo pekee cha kuongoza nchi na kusiwepo na mwanya wowote wa mtu au mhimili fulani kuikiuka. Tunataka Katiba ibaki kama dira ya kuongoza nchi kwa kuzingatia utawala wa sheria,” alisema Jaji Mkuu.


Pia alisema Katiba ijayo inatakiwa kusimamia utoaji haki sawa kwa wananchi wote. Jaji Mkuu alisema Katiba haina budi kutambua haki ya wananchi kupata haki katika mambo mbalimbali ikiwamo kuabudu na kuishi.


Katika hoja hiyo ya upatikanaji wa haki, Jaji Mkuu alisema kuna mikoa 12 na wilaya 25 nchini ambako hakuna Mahakama Kuu na Mahakama za Wilaya.
Alisema wananchi wanalazimika kutafuta haki zao kwenye mikoa na wilaya nyingine, tatizo ambalo Katiba Mpya inapaswa kuliondoa ili kuwafanya wananchi wote kuwa na fursa sawa katika kupata haki.


“Pia tumependekeza Katiba Mpya ilinde kwa hali na mali mhimili wa Mahakama kwa kuwa siyo wa kisiasa. Mahakama ni mhimili huru na haufungamani na upande wowote na hiyo ndiyo nguvu ya Mahakama. Isiwe na mambo ya kisiasa, upendeleo au kufungamana na upande mmoja,” alisema Jaji Mkuu.


Aidha, Jaji Mkuu alisema wamependekeza Rais aendelee kuwa mteuzi wa majaji nchini kwa kuwa ndiye mkuu wa nchi. Alisema atafanya uteuzi huo kwa kufuata ushauri atakaopewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na si vinginevyo.


“Katiba ya sasa inasema kuwa Rais atafanya uteuzi kwa kushauriana na Mahakama, lakini sisi tumependekeza asishauriane na Mahakama, bali ateue kwa kufuata ushauri atakaopewa na Tume ya Utumishi ya Mahakama,” alisema.


Alisema haki za binadamu zinapaswa kupanuliwa na kulindwa katika Katiba ijayo. Alisema ilivyo sasa haki za kisiasa na kiraia ndizo zinazoonekana kupewa kipaumbele zaidi kuliko haki nyinginezo kama vile za uchumi na kijamii.


Tume ya Mipango
Kwa upande mwingine, Tume ya Mipango imependekeza Katiba Mpya iwe na ibara itakayoelezea uwajibishwaji na uwajibikaji wa viongozi wa Serikali.


Katibu wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango alisema wametaka Katiba Mpya iwe na ibara itakayoelezea uwajibikaji wa viongozi wa Serikali pamoja na uwajibishwaji ili kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo.


Habari hii imeandikwa na Matern Kayera, Aidan Mhando na Daniel Mwingira
 
Naona Makinda amezingatia mengi ambayo ndio msimamo wa vyama vya upinzani.

Chande amependekeza kuwa Rais aendelee kuchagua majaji lakini kwa kufuata ushauri wa mahakama. Ana maana Rais awajibike kikatiba kuchagua wale waliopelekwa kwake na mahakama.

Nadhani angeenda zaidi na kuweka wazi mchakato wa mahakama kupata hao watu. Kenya wanawafanyia mchuano wale wote wanaotimiza vigezo, na kisha kutokana na mchuano huo waliojitofautisha na wenzao kwa ubora wanapelekwa kwa Rais kwa kutajwa.
 
Mh makinda na mh jaji othuman chande hayo ni mawazo mazuri tunamuomba jaji warioba natume yake wayachukue nakuyaingiza mojakwamoja,kwenye katiba mpya.
 
Mh makinda na mh jaji othuman chande hayo ni mawazo mazuri tunamuomba jaji warioba natume yake wayachukue nakuyaingiza mojakwamoja,kwenye katiba mpya.
Naona maoni yao ni mazuri lakini wacwac wangu ni kuona waliofaidi matunda fulani kuendelea kutetea matunda hayo kama Mhe. Jaji Mkuu anapopendekeza Rais aendelee kuteua kwa sababu alizozitoa, malalamiko yamekuwepo kwamba anateua watu wasio na sifa yawezekana hata huyu CJ hana sifa ndo maana anapendekeza mfumo huo uendelee. Nashauri wakulima kama wanataka haki, neema nk waangalie namna nyingine maana waliopo madarakani hawataki tugawane kwa ulinganifu bali waendelee kunyonya.
 
Naona maoni yao ni mazuri lakini wacwac wangu ni kuona waliofaidi matunda fulani kuendelea kutetea matunda hayo kama Mhe. Jaji Mkuu anapopendekeza Rais aendelee kuteua kwa sababu alizozitoa, malalamiko yamekuwepo kwamba anateua watu wasio na sifa yawezekana hata huyu CJ hana sifa ndo maana anapendekeza mfumo huo uendelee. Nashauri wakulima kama wanataka haki, neema nk waangalie namna nyingine maana waliopo madarakani hawataki tugawane kwa ulinganifu bali waendelee kunyonya.
Lakini msisitizo wake ni kuwa Rais asiwe na vyanzo vyake, bali Rais alazimike kufuata mapendekezo ya mahakama.
 
Back
Top Bottom