259.-(1) Vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa vitakuwa ni:
(a) Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania;
(b) Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano; na
(c) Idara ya Usalama wa Taifa.
(2) Wajibu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa na mfumo wa
usalama ni kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano, rasilimali za nchi, maslahi
ya raia na watu wengine, mali zao, haki na uhuru, mamlaka za nchi, amani na
umoja wa kitaifa.
(3) Katika utekelezaji wa majukumu yao, vyombo vya ulinzi na usalama
wa Taifa na kila mtumishi wa vyombo hivyo hataruhusiwa:
(a) kuwa na upendeleo kwa njia yoyote;
(b) kujiunga na chama chochote cha siasa au kuendeleza maslahi ya
chama chochote cha siasa au sera zake;
(c) kuhujumu maslahi ya kisiasa au mpango wa kisiasa ambao ni halali
chini ya Katiba hii;
(d) kutishia, kudhulumu au kuwatendea ukatili raia na watu wengine; na
(e) kutii amri yoyote isiyokuwa halali.
(4) Mtu hataruhusiwa kuanzisha taasisi, kampuni, jumuiya au shirika
linalohusiana na ulinzi na usalama wa Taifa au ushirika wa kijeshi, isipokuwa
kama inavyoruhusiwa na Katiba hii au sheria.
(5) Vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa vitakuwa chini ya mamlaka
ya Amiri Jeshi Mkuu.
(6) Bunge litatunga sheria kuweka masharti kuhusu utekelezaji wa
majukumu, uratibu na usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa.