Kati ya ukweli na ukimya, miaka mitano John Pombe Joseph Magufuli

Kati ya ukweli na ukimya, miaka mitano John Pombe Joseph Magufuli

Joined
Aug 15, 2023
Posts
10
Reaction score
18
KATI YA UKWELI NA UKIMYA,MIAKA MITANO (5) TANGU KIFO CHA John Pombe Joseph Magufuli

Magufuli, umelala ndio,Na sote tunajua hautoamka tena.
Lakini historia haifi pamoja na mtu bali inaishi,inauliza na inaandika.

Ni kweli hatutakusahau,sio kwa sababu ulifanya mema makubwa kiasi cha kufuta kila kitu kingine, bali kwa sababu uliiacha nchi ikiwa na kumbukumbu zinazogawanya zile za wachache wanaosifu, na za wengi wanaoishi na majeraha ya kimya nikiweko Mimi.

Ni ukweli usiopingika kuwa wapo watakaosema marehemu hasemwi vibaya Lakini je, ukweli nao uzikwe?
Je, haki nayo inyamazishwe kwa kisingizio cha heshima?

Ukiwa umelala huko Chato, leo nachagua kusema yale ambayo wengi wanayaficha moyoni na wale wa upande wa pili nilioutaja hapo juu hawataki kuskia na ninajua watanishambulia.

Magufuli, umelala lakini hadi leo familia ya Ben Rabiu Saa Nane bado inamtafuta mtoto wao aliyepotea katika mazingira ya kutisha chini ya utawala wako.
✓Umelala lakini kumbukumbu za kifo cha Kamanda Alphonse Mawazo bado inauma, na maswali yake hayajapata majibu toshelezi.

✓Umelala lakini kivuli cha hofu kilichotanda katika kipindi chako bado hakijatoweka kabisa.

✓Ni katika utawala wako ambapo demokrasia ilianza kubanwa kwa nguvu,
✓Ni katika kipindi chako ambapo sauti za ukosoaji zilianza kuchukuliwa kama uadui.
✓Ni katika miaka yako ambapo vyombo vya habari vilijifunza kunyamaza ili viendelee kuishi.
✓Ni katika utawala wako ambapo neno “wasiojulikana” liligeuka kuwa sehemu ya maisha ya wananchi watu wakipotea, wakichukuliwa, wengine wakipatikana wakiwa wamejeruhiwa, wengine kutopatikana kabisa.
✓Ni katika utawala wako ambapo uhuru wa Bunge ulilegea, na mihimili ya dola ikaanza kupoteza uwiano wake.
✓Ni katika utawala wako ambapo waliothubutu kusema walikumbana na vitisho, kesi, au hata risasi za hadharani mchana kweupe .
✓Ni katika kipindi chako ambapo uchawa ulipandikizwa kwa nguvu, ukalishwa, ukakuzwa hadi leo umeota mizizi na kuwa sehemu ya utamaduni wa uongozi.

Magufuli umelala lakini athari za utawala wako hazijalala.
✓Zipo katika hofu kwa baadhi ya wananchi.
✓Zipo katika kumbukumbu za waliopoteza ndugu.
✓Zipo katika ukimya wa wale waliowahi kuumizwa na hawakuwahi kupata haki.

Kwa hayo machache kamwe sitasimama hapa kuhesabu mazuri yako ijapo wapo wengi wanaofanya hivyo kila siku,lakini mimi nimechagua kuwa sauti ya upande ule ambao haupendwi kusikika.

Kwa sababu taifa linalojenga kesho bora ni lile linalokubali kuikabili jana yake kwa ujasiri bila woga, bila kujipendekeza,l na bila kuficha ukweli.

Endelea kulala, Jiwe.
Kwa baadhi, wewe ni shujaa.
Lakini kwa wengine na mimi nikiwa miongoni mwao ulikuwa ni kiongozi aliyebeba sura ya udikteta uliopindukia mipaka ya haki.

Historia haitakumbuka kelele za sifa pekee, Bali itakumbuka pia vilio vilivyonyamazishwa.

Endelea kulala Jiwe......
Revocatus James Ng'oja
Reha-Rombo-Kilimanjaro.
17 March,2026.
 
Back
Top Bottom