Kanuni ya Hofu; mshinde Adui

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,890
KANUNI YA HOFU, MSHINDE ADUI

Na, Robert Heriel


Hii ni sehemu katika kitabu cha Nadharia za Taikon.
Haki zote zimehifadhiwa.

Maandishi ya Robert Heriel kwa Lugha ya Kiswahili.

Hofu ni hali ambayo mtu huwa nayo pale anapokabiliwa na jambo fulani lenye madhara. Mara nyingi hofu hujengwa na mambo yaliyozidi mtu uwezo, hata hivyo binadamu wengi huwa na hofu kwa mambo wasiyoyajua, wasioyaona, mambo ya kufikirika zaidi kuliko mambo halisi, ambayo huambiwa yatatukia au yapo mbioni kutokea.

Hofu huweza kuwa na visawe vingine kama Wasiwasi, mashaka, woga miongoni mwa maneno mengine.

Binadamu huwa na hofu kwa mambo yasiyoyakawaida. Mtu hawezi ogopa jambo la kawaida, hii ni kusema ili mtu aogope sharti jambo hilo lisiwe la kawaida kulingana na akili, umri, mtizamo, utamaduni, na jinsia ya mtu. Hofu hutofautiana baina ya mtu na mtu, jinsia, mtazamo, akili, utamaduni, mazingira, wakati, na elimu.

AINA SABA (7) ZA HOFU
Zipo aina Saba za hofu kama nilivyoamua kuzigawanya hapo chini, nazo ni;
1. HOFU YA KUFIKIRIKA/DHAHANIA
2. HOFU YA MAUMBILE
3. HOFU YA MATENDO
4. HOFU YA ALA/SAUTI
5. HOFU YA MUDA/WAKATI
6. HOFU YA MATOKEO
7. HOFU YA USIRI

HOFU YA KUFIKIRIKA/DHAHANIA

Hii ni hofu ambayo mtu au binadamu huwa nayo kulingana na fikra zake pamoja na imani. Hofu hii duniani ndio kubwa kwani haiwezi kuthibitika katika ulimwengu halisi. Jamii huunda dhana za kufikirika kama vile uchawi, mashetani, mizimu, Malaika, miungu, majini, vibwengo, vigagula.

Pia huunda dhana kama laana, baraka, bahati, mikosi miongoni mwa mambo mengine. Kwa namna hiyo mambo hayo ya kufikirika huunda hofu kwa mtu licha ya kuwa hayathibitiki.

Kwa mfano: Mtoto huweza kuambiwa na wazazi wake kuwa asipowatii basi anaweza kupatwa na laana. Hivyo mtoto hata kama jambo halitaki lakini kwa kuwa anaogopa laana basi itabidi atii maagizo ya wazazi wake hata kama ni maagizo mabaya.

Mfano wa pili; Makanisani tunaambiwa tusiwasonde vidole viongozi wa dini hata kama wanafanya maovu, na kama tukikaidi tukawasonda basi tutapata laana. Hivyo watu ndani ya jamii hata kama kiongozi akifanya uovu huogopa kumsema kwa kuogopa laana.

Baadaye tutaona kama kuna ukweli wowote katika mambo hayo.

2. HOFU YA MAUMBILE

Hii ni hofu ambayo binadamu huwa nayo kulingana na maumbile ya kitu husika kama vile, ukubwa, rangi, ubaya, umbo la kustaajabisha miongoni mwa mengine.

Viumbe wenye sura zenye kutisha huogopesha hata kama havina madhara, viumbe wenye rangi zenye kutisha huleta hofu, viumbe vikubwa kimiili pia huleta hofu. Mfano kiumbe kama KAA, NGE, TANDU, BUIBUI AUMAYE, MAMBA N.K

Binadamu wenye maumbo makubwa huogopwa zaidi ukilinganisha na binadamu wenye maumbo madogo. Watu warefu kwa kimo na wenye vifua vipana na mikono mikubwa huogopwa.

Usishangae walinzi wa viongozi wakubwa na watu mashuhuri wakiwekwa wenye miili mirefu. Aina hii hutumika.
Watu wafupi wa kimo huwa hawaogopwi na mara nyingi hudharauliwa.

Kwa upande wa mimea, miti yenye maumbo makubwa mfano, mibuyu, mikuyu huogopwa na kuundiwa imani kuwa miti hiyo inaviumbe wa ajabu na wakutisha. Hata zamani miti hiyo ilikuwa sehemu za ibada wakiamini miti hiyo wanaishi mizimu au miungu.

3. HOFU YA MATENDO
Hii ni hofu ambayo binadamu huwa nayo kulingana na matendo ya kiumbe au jambo fulani. Kiumbe chenye matendo ya kikatili, kuua, kudhalilisha, kudhuru, na kudhoofisha huogopwa.

Binadamu mwenye matendo ya kupiga, kudhuru, na tabia za kuumiza wengine huogopwa.

Hata jamii zenye ukatili, kuumiza, kupiga hovyo, kuua, kubaka huogopwa zaidi. Huhofiwa. Radi, tetemeko, tufani, kimbunga, mafuriko huogopwa kwa sababu ya matokeo ya matendo yao ambayo ni madhara. Wanyama kama Nyoka aina ya Koboko, huogopwa kwa sababu ya matendo yao.

4. HOFU YA ALA/SAUTI

Hii ni hofu inayotokana na sauti. Zipo sauti zenye kuleta hisia za hofu, wasiwasi na woga.
Sauti zenye kutisha kama Radi, sauti ya simba, sauti ya paka, sauti ya bundi, sauti mvua kubwa, sauti ya upepo wa jangwani au baharini.
Mwanaume amepewa sauti nzito tofauti na mwanamke na lengo kubwa ni kujenga hofu, yaani kuhofiwa kwa lengo la mamlaka na utawala.
Zipo sauti za kutengeneza kulingana na ukuaji wa teknolojia. Sauti hizo huwekwa kwenye filamu kimsingi ili kuibua hisia za hofu kwa watazamaji.

5. HOFU YA MUDA/WAKATI

Hii ni hofu inayotokana na wakati, nyakati, muda na majira. Binadamu wengi wanakuwa na hofu wakati wa usiku bila shaka ni kutokana na giza. Lakini wapo wachache wanakuwa na hofu mchana, hii inaweza ikakushangaza lakini ipo hivyo. Hii inategemea na aina ya mtu, na kazi anayoifanya.

Usiku unaundiwa nadharia njama(conspiracy theory) nyingi kwa sababu binadamu wengi huogopa usiku. Wajanja wengi hasa wachungaji, waganga wa kienyeji, na masheikh huunda uongo kuwa usiku kuna viumbe hutembea, majini na wachawi huloga usiku kwa vile wanajua watu wengi huogopa kutokana na giza la usiku basi nao wanapitia humo humo.

Wakati ujao watu wengi huogopa kwa sababu hawajui jinsi utakavyokuwa. Wajanja pia hutisha watu zaidi kwa kuwadanganya watu kwa sababu wanajua watu wengi huiogopa kesho kuliko leo au jana.

Kikawaida mtu hawezi kukutisha ikiwa unaujua ukweli, ndio maana wao kwa vile wanajua huijui kesho yako basi hutumia kesho hiyo kukudanganya.

6. HOFU YA MATOKEO

Hii ni hofu ambayo huzingatia zaidi matokeo ya jambo fulalni au matokeo ya kile mtu alichokifanya.

Binadamu wengi huogopa matokeo. Watu huogopa Ugonjwa wa UKIMWI kwa sababu ya matokeo ya kuumwa ugonjwa huo. Ukiumwa UKIMWI huwezi kupona tena, yaani utaishi kwa matumaini. Wote walioumwa walikufa. Sio kama magonjwa mengine haufi lakini walau kuna uwezekano wa kupona.

Gonjwa la Corona lilileta hofu duniani kutokana na kasi ya mauaji na kasi ya usambaaji wake. Hiyo yote ni hofu ya matokeo.

7. HOFU YA USIRI

Hii ni aina ya mwisho kabisa ya Hofu. Aina hii huzingatia zaidi usiri, uficho, fumbo, methali, kitendawili, ajabu n,k. Binadamu huogopa kwa mambo asiyoyajua vizuri, mambo yaliyojificha, mambo ambayo macho yake hayayaoni vizuri ndio maana hata usiku mtu akitembea anaweza kuona kichaka kwa mbali akakiogopa kwa sababu ya kutokukiona vizuri.

Mungu anaogopwa huenda sio kwa sababu ya nguvu zake, bali usiri wake, uficho wake, pengine binadamu wangejua siri za Mungu huenda wasingemuogopa kabisa.

Hata katika jamii mtu msiri huhofiwa zaidi ya mtu muwazi, mtu msiri hutoa matokeo yasiyotarajiwa, hatabiriki, hakadiriki lakini mtu muwazi hutabirika na kukadirika.

Mambo yanayofichwa fichwa hogopwa zaidi kuliko yaliyowazi.

Aina hizo ndizo msingi mkuu wa hofu katika kiumbe chochote kile.

Katika kukabiliana na adui yeyote yule katika maisha yetu ni lazima mtu azingatie aina hizo za hofu.
Ni lazima ujue adui yako anahofia nini kwenye maisha yake? Anahofia nini kwako? Kipi anaringia ambacho mara nyingi kitu hicho lazima akifanye kuwa siri yake ya ushindi?

Hofu ndio huamua mshindi, kwani kile mtu anachohofia mara nyingi ndio udhaifu wake ulipo.

Ukifanikiwa kupandikiza hofu kwa adui yako basi ni wazi umemuweza adui yako na kumshinda. Lakini kama hutoweza kupandikiza hofu kwa adui yako utamuweza kwa siku moja lakini hujamshinda kwa maana bado hakuhofii.

Kwa leo tuishie hapa, tutaendelea panapo majaliwa.
Maoni yako ni muhimu, pia share kwa wengine wajifunze.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Back
Top Bottom