Kamati Kuu CCM kuketi Dar leo
.
Na Tumaini Makene
SAKATA la Kampuni 'tata' ya Dowans inayotakiwa kulipwa mabilioni ya fedha na serikali baada ya kushinda katika Mahakama ya usuluhishi wa Biashara (ICC) na vurugu za kisiasa za Arusha, ni mambo yanayotarajiwa
kutinga katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) inayotarajiwa kuketi leo.
Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini waliozungumza na Majira jana juu ya kikao hicho ambacho ni moja ya vikao nyeti na vya ngazi ya juu katika uendeshaji na ufikiaji wa maamuzi ya chama hicho, wamesema kuwa ni vigumu kwa CC kutozungumzia sakata la Dowans ambalo kwa sasa ni moja ya mijadala iliyochukua nafasi kubwa katika duru za siasa nchini.
Ugumu huo, kwa mujibu wa wachambuzi hao, unatokana na ukweli kuwa sakata hilo mbali ya kuwa limevuta hisia za watu mbalimbali na kuibua mijadala mikali nchini, kila wananchi wa kada mbalimbali wakitoa maoni yao tofauti tofauti, limewagawanya baadhi ya viongozi waandamizi serikalini na ndani ya CCM yenyewe.
Pia mkutano huo umeitishwa muda mfupi tu baada ya kuibuka mgogoro wa umeya Arusha, ambapo CHADEMA walipinga uchaguzi ulioipa ushindi CCM, na kuamua kufanya maandamano ya amani yaliyozimwa kwa risasi na polisi hadi watu watatu wakauawa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, CC itakutana leo Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika kikao chake cha tatu tangu kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo kinatarajiwa kuwa na ajenda tatu.
"Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, itakutana tarehe 20 Januari, 2011 mjini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete. Katika kikao hicho, Kamati Kuu pamoja na mambo mengine, itapokea na kujadili mambo yafuatayo;
"Hali ya kisiasa nchini, maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 34 na matembezi ya mshikamano na kupokea taarifa ya mkutano wa makatibu wakuu wa vyama vya ukombozi kusini mwa Afrika uliofanyika mjini Luanda, nchini Angola kuanzia tarehe 7-10 Desemba, 2010, ambao Chama Cha Mapinduzi kiliwakilishwa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya CCM.
Kikao hicho kinafanyika siku chache baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichokutana chini ya mwenyekiti wake, Rais Kikwete, ambacho taarifa zinasema suala la Dowans kulipwa mabilioni ya fedha, ni moja ya hoja zilizopata nafasi kubwa kujadiliwa barazani, ambapo kumekuwepo na mgawanyiko wa wazi na wa chini chini, kundi moja likipinga, lingine likiunga mkono serikali kutekeleza uamuzi wa ICC.
Suala jingine kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na Majira ni juu ya mjadala mwingine mkali wa katiba mpya, ambapo imeanza kudaiwa kuwa CCM kinaonekana kukosa mtu wa kuzungumzia mchango wa chama hicho, hata baada ya Rais Kikwete kuweka bayana kuwa haliepukiki.