comrade igwe
JF-Expert Member
- Jan 12, 2015
- 7,295
- 3,945
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amewaonya watu wanaozusha na kusambaza taarifa za uongo kuacha mara moja.
Sirro alisema kitendo cha kuibua na kusambaza taarifa za uongo juu ya Serikali katika mitandao ya kijamii na magazeti, kinaleta picha mbaya kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuwayumbisha wananchi.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi baada ya mwanzoni mwa wiki hii gazeti la kila wiki (si MTANZANIA), kuchapisha taarifa ya kuvunjwa kwa paa la Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali na kuibiwa kwa nyaraka muhimu.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Sirro, alisema ni kweli upo uhalifu uliofanyika katika ofisi hiyo, lakini hakuna nyaraka yoyote muhimu ya Serikali iliyoibwa kama ilivyoripotiwa.
Alisema uhalifu huo umefanywa na vibaka na wala hakukuwa na njama zozote za kuihujumu Serikali na uchunguzi wao umebaini kuwa hakuna mtumishi yeyote wa Serikali aliyehusika.
“Hakuna nyaraka ya Serikali iliyoibwa, zaidi ya seti moja ya televisheni, king’amuzi cha runinga na kompyuta mpakato,” alisema Sirro.
Aliongeza kuwa tayari jeshi lake limeshawakamata baadhi ya wahusika wa tukio hilo na kufanikiwa kupata baadhi ya vifaa vilivyoibiwa.
Pia alisema kwa sasa wanakamilisha upelelezi na wakati wowote wahusika watapandishwa mahakamani.
Kuhusu suala hilo kushughulikiwa kwa siri kubwa, alisema hakuna ukweli juu ya hilo, kwa sababu kila kitu kinawekwa wazi kwa mujibu wa utendaji kazi wa jeshi lake.
Alisema si jambo jema kuripoti taarifa za uongo kwa nia ya kuifanya iwe kubwa.
“Nawaonya watu wote wanaoibua na kusambaza taarifa zenye nia mbaya dhidi ya Serikali, ni vema vyombo vya habari vikatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi.
“Kitendo cha kuripoti kuwa nyaraka za Serikali zimeibwa kina hatari kubwa kwa nchi, nawaasa ndugu zangu wanahabari, tushirikiane kuyapinga matendo ya namna hii,” alisema Sirro.