Kama ungekuwa unaishi Jangwani, ungefanyaje?

Galacha Maestro

JF-Expert Member
Sep 29, 2011
1,353
2,220
KAMA UNGEKUWA UNAISHI JANGWANI, UNGEFANYAJE?

Ugumu wa maisha yetu unaanzia kwenye macho ya watu wengine, wale wanaotuzunguka. Hawa wamekuwa chanzo kikubwa kwetu kuwa na maisha ambayo hatuyapendi, kufanya kazi ambazo hatuzipendi na kuwa na vitu ambavyo hatuvifurahii.

Binadamu tunapenda uhuru lakini hatupo huru kwa wale wanaotuzunguka. Huwa tunafungwa na watu hawa, kwa kujikuta tukifanya kile ambacho kila mtu anafanya au kufanya ili kuonekana kwamba na sisi tupo, na sisi tunaweza.

Wakati mwingine hufanyi kwasababu kila mtu anafanya, bali unafanya ili tu upate ule ufahari wa kuonekana na wengine kwamba unaweza au umefanya. Huu ni mzigo mkubwa sana ambaye hakuna yeyote anayeweza kuubeba, huu ni mzigo ambao umefanya wengi kukimbiza maisha na sio kuyaishi.

Njia moja nzuri ya kuutua mzigo huu ni kujiuliza swali hili muhimu sana;
Kama ningekuwa naishi jangwani mimi na familia yangu tu, hakuna anayenizunguka, je ningefanya haya ninayofanya sasa? Kama jibu ni hapana unaacha mara moja, kama jibu ni ndio unaweka akili, moyo na nguvu zako zote.

Ukishaweza kujitenganisha maisha yako na macho ya wengine, hapo unakuwa umefikia hatua nzuri ya uhuru na sasa unaweza kufikia mafanikio makubwa.

Sikuambii hivi ili uchague kuishi maisha ya hovyo kwa sababu hujali wengine wanafanya nini au wanasema nini, bali nataka wewe uishi yale maisha ambayo ni bora sana kwako. Mwisho wa siku utakachokumbuka ni maisha uliyoishi na sio mashindano uliyofanya.
 
Back
Top Bottom