SEHEMU YA 2
Siku moja Mfalme fulani alijiwa na wazo kwamba ikiwa angejua muda muafaka wa kutenda kila kitu; kama angejua nani ndio watu sahihi wa kuwasikiliza, na nani wa kuwakwepa; na, juu ya yote, kama nyakati zote angejua nini ndicho kitu muhimu kuliko vyote cha kutenda, hangeshindwa katika lolote ambalo angeamua kulifanya.
Na wazo hilo lilipomjia, alitangaza katika ufalme wote kwamba angetoa zawadi kubwa kwa mtu yeyote ambaye angemfundisha mfalme ni wakati upi ulio muafaka kwa kila tukio, na nani ndio walikuwa ndio watu muhimu kuliko wote, na ni vipi angefahamu kipi kilichokuwa ndicho kitu muhimu kuliko vyote kukitenda.
Ndipo wasomi wakaenda kwa mfalme, lakini kila mtu alijibu maswali ya mfalme kivyake.
Katika kujibu swali la kwanza, wengine walisema ili kujua muda muafaka kwa kila tukio, lazima mtu achore jedwali la ratiba ya siku, miezi, na miaka, na lazima aishi bila kukosea kuifuata ratiba hiyo. Ni hivyo tu, walisema, ingewezekana kufanya kila kitu kwa wakati wake muafaka. Wengine wakasema haiwezekani kujua kabla ya muda sahihi wa kila kitu, lakini kwamba, mtu akiacha kuzolewa na tabia za kizembe, mtu anatakiwa muda wote ashughulike na yatukiayo muda huo, na kutenda analoliona vema. Wengine, tena, wakasema kwamba hata Mfalme akifanyaje kujua yanayojiri, isingewezekana kwa mtu mmoja kuamua kwa usahihi muda muafaka wa kila tukio, lakini kwamba angekuwa na baraza la wazee wa busara ambao wangemsaidia kupanga muda muafaka wa kila kitu.
Lakini tena wengine nao wakasema palikuwa na mambo mengine ambayo hayangeweza kusubiri kikao cha baraza, lakini ambayo mtu alitakiwa mara moja kuamua kuyatenda au la. Lakini ili aweze kuamua hivyo, mtu lazima ajue mapema iwapo tukio hilo litakuja kutokea. Ni wapiga ramli tu wanaojua hayo; na, hivyo, ili kujua muda muafaka wa kila tukio, mtu shurti aende kwa wapiga ramli.
Kadhalika kulikuwa na majibu mengi kuhusu swali la pili. Wengine walisema watu ambao mfalme aliwahitaji sana walikuwa ni washauri wake; wengine, viongozi wa dini; wengine, madaktari; wengine wakasema maaskari ndio waliokuwa muhimu kuliko wote.
Kwenye swali la tatu, la ipi ndio ilikuwa kada muhimu kuliko zote, wengine walijibu kwamba kitu muhimu kuliko vyote duniani ni sayansi. Wengine wakasema ni mbinu za kivita; na wengine, tena, kwamba ilikuwa ni ibada ya kidini.
Kwa vile majibu yote yalikuwa yakipishana, mfalme hakukubaliana na jibu lolote, na hakumpa yoyote zawadi. Lakini kwa vile alitamani kupata majibu sahihi kwa maswali yake, aliamua kwenda kumuuliza mzee mmoja aishie maporini huko, akijulikana sana kwa busara zake.
ITAENDELEA SEHEMU YA 3