Kaburi bila Msalaba

Wakili wa shetani

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2022
Posts
2,111
Reaction score
3,970

I Mumbi ahojiwa

Asubuhi, Siku ya Ijumaa, jua lilitokea mapema na kufukuza baridi kali iliyopenya hata ndani ya mifupa ya mahabusu. Askari alipofungua mlango, mahabusu wote walitoka nje na kuota jua waliolingojea kwa muda mrefu. Hata na inzi nao walikuwa wanalingojea, na wao vile vile walitoka nje na kuliota. Mumbi alimwona inzi mmoja akitafuta chakula, na kwa macho yake akamfuata kila alipokwenda. Hata hivyo hakuwa akifikiri habari yake, kwani fikira zake zilikuwa juu ya njaa aliyoisikia tumboni mwake.

Mumbi alipokuwa akiota jua, huku akiwatazama inzi na kufikiri vile alivyokuwa na njaa, Chifu na askari wake walifika. Yeye hakuwaona mpaka Chifu alipomwuliza, "Je wewe jina lako ni nani?"

Mumbi aliinua kichwa chake na kumtazama Chifu huku akijibu, "Mumbi," "Umekula viapo vingapi?" Chifu akamwuliza.

Mumbi hakujibu. Aliinama na kutazama chini. Akiwekelea mkono wake wa kushoto juu ya tumbo lake, alianza kuumauma kucha za mkono wake wa kulia.

"Nimekuuliza umekula viapo vingapi?" Chifu akauliza tena. Askari wake waliomlinda Chifu po pote alipokwenda, walianza kuonyesha hasira walipoona kwamba Mumbi hakumjibu Chifu. Maina, mmoja wao, alianza kushikashika kiboko cha ngozi ya kifaru, alichokichukua kila mahali walipokwenda. Chifu na askari wake walikitumia kiboko hiki kwa kuwapiga wale watu walioshitakiwa kuwa ni wafuasi wa Mau Mau. Kwa mara ya tatu Chifu alimwita Mumbi tena, "Msichana we!"

"Humm," Mumbi akajibu.

"Umekula viapo vingapi?"

Mumbi aliona kwamba Maina alikuwa tayari kumchapa kiboko dakika yoyote. Hapo aliyakumbuka majeraha aliyoyaona miilini mwa mahabusu wengine waliokuwa wamepigwa. Aliogopa 'asije naye akapigwa vile. Kwa sauti ya chini akajibu, "Sikula."

Chifu kusikia hivyo alifyatuka kwa ukali na hasira akasema, "Sikula! Wafikiri tulikuleta hapa bila kujua kwamba umekula kiapo? Ninataka uniambie upesi ni viapo vingapi umekula, ama sivyo utaona wanachopata Mau Mau wengine."

Mumbi hakusema neno lolote. Alisimama tu kimya, huku akiuma kucha zake. Moyoni alijua hakuwa na lolote la kufanya, ila alijua kwamba hata kama akisema amekula au hajala kiapo, ilikuwa sawa tu. Alikumbuka rafiki yake Nyaguthii. Yeye alikubali kwamba alikuwa amekula viapo viwili. Aliwataja wote waliomlisha na wale waliokula pamoja naye. Lakini hata hivyo, alihukumiwa na kutiwa korokoroni huko Kamiti kwa muda wa miaka minne. Alipokuwa huko alipigwa na askari wa jela mpaka akafa, lakini watu wa jela wakasema alikufa baada kuugua.

Alikumbuka vile vile yaliyompata Maciira. Yeye alikuwa kijana aliyesoma mpaka darasa la kumi. Sura na tabia zake ziliwapendeza watu wote wa Lokesheni yake. Lakini Chifu alimchukia sana. Alifikiri pengine angepewa kazi ya uchifu badala yake. Kwa sababu hii, aliwachukua Maciira na vijana wengine rafiki zake, na kuwapeleka mpaka karibu na msitu wa Kabaru. Walipofika mahali palipokuwa na miti mikubwa, aliwaambia, "Hii ndiyo nchi mnayoipigania. Tokeni sasa mwende mkaishi huko."

Maciira na wenzake walikataa kutoka, na hapo Chifu akawaamrisha askari wake wawatoe kwa nguvu, kutoka juu ya motokaa. Waliposhuka chini, Chifu aliwapiga risasi na kuwauwa papo hapo. Huko kijijini, aliwaambia watu kwamba Maciira na wenzake walikuwa wakijaribu kutoroka kuelekea msituni kwa hivyo askari wakalazimika kuwapiga risasi na kuwauwa. Hakuna mtu aliyethubutu kutokubaliana na habari hii, kwani angefanya hivyo, yeye vile vile angefanyiwa kama wao.
Mumbi alisimama kimya. Chifu naye akamtazama kila sehemu ya mwili wake. Aliona vile uso wake ulivyokuwa umenyooka. Nywele zake ndefu zilikuwa zimesokotwa zikawa mfano wa nanasi. Miguu yake nayo ilikuwa mirefu na yenye kupendeza. Kusema kweli Mumbi alikuwa mzuri kweli kweli. Chifu hakuweza kujua kwa nini msichana mzuri kama vile amekula kiapo cha Mau Mau.

Moyoni alikata shauri kwamba angefanya lolote mpaka kumfanya Mumbi ageuze nia zake, na ikiwezekana, awe mmoja wa wasichana wengi waliokaa hapo kambini wakiwapikia, na mara wakitembea na Chifu na askari wake.

Mumbi naye alikuwa akifikiri jambo jingine. Moyoni alikuwa amekata shauri kwamba hata ikitokea nini hatasema amekula kiapo. Alijua akikubali kwamba amekula kiapo, ni lazima atasema ni nani aliyemlisha, na ni watu gani wengine waliokula kiapo pamoja naye. Alikumbuka usiku wa manane, na wenye giza, usiku ambao yeye, mama yake, na wasichana wengine walipokula kiapo. Alimkumbuka vile vile mpenzi wake Maciira, ambaye ni nyumbani mwao walimolia hicho kiapo. Alijua akikubali kuwa amekula kiapo, ni lazima angewatia taabuni wote waliokula kiapo siku hiyo. Alipofikiri hali ya mama yake vile alivyokuwa mnyonge kwa kuugua mifupa, alikata shauri kuwa kufa au kupona, hangekubali kuwa amekula kiapo.

Baada ya kuhojiwa hivi kwa muda bila yeye kusema kama kwamba amekula kiapo, Chifu aliwaamrisha askari wake wamshike Mumbi na kumpeleka mpaka kambi ya Githunguri. Mumbi aliposikia hivyo machozi yalianza kumtoka bila yeye kupenda.

Kambi ya Githunguri ilijulikana sana katika nchi nzima. Kati ya watu watatu waliopelekwa hapo, ni mmoja tu aliyerudi hai, na yeye vile ilikuwa ni lazima awe amevunjwa mguu, mkono au afanywe kutokuwa mwanamume tena.

Kambi ya Githunguri ndipo alipoishi Waiwai, kijana wa kizungu ambaye alikuwa mnyama kuliko vile alivyokuwa mwanaadamu. Wote waliopelekwa kwake, wakishitakiwa kula kiapo, aliwapiga risasi papo hapo. Waliokuwa na bahati, aliwapiga kwa kiboko mpaka wasijijue wenyewe.

Mumbi aliposikia kwamba atapelekwa Githunguri, alikufa moyo kwa hofu. Mwili wake ulianza kutetemeka, na machozi yakazidi kumtoka. Ingawaje, alizidi kukazana kwamba hatakubali kuwa amekula kiapo. Hata kama akiuawa, hatasema kamwe kwamba amekula. Kwa moyo mshupavu aliwafuata Maina na askari wengine wawili na wote wakaelekea upande wa Githunguri.

Kila askari alivaa fulana nyekundu yenye mikono mirefu na hali shingoni imefungwa kamba iliyofungiwa filimbi. Kiunoni walijifunga mshipi wenye upana wa inchi mbili hivi, wenye rangi nyeusi. Wote walivaa suruali fupi za kaki zilizofuliwa na kunyooshwa sawa sawa. Miguuni walivaa viatu vya buti vyenye rangi nyeusi na juu yake wakafunga patisi. Kichwani walivaa kofia ndogo nyeusi ambazo hapo upande wa mbele palitiwa nishani iliyoandikwa "On Her Majesty's Service," yaani "Katika Utumishi wa Malkia."

Askari wote walijiona wamevalia vizuri sana. Hii ilikuwa ni kweli kwa sababu watu wengine wote walikuwa wachafu na wamerarukiwa na nguo zao sana. Watu wote, waume, wake na watoto, walikuwa ni lazima kukaa vijijini mwao bila kutoka nje. Wakati huu walikuwa wameishakaa pale kwa karibu mwezi mzima. Wote walikuwa wameishakula chakula chote, na kutumia pesa zote walizokuwa nazo hapo mwanzo. Hata senti za kununua sabuni hawakuwa nazo. Maji yenyewe walikubaliwa kuteka mara moja tu kwa juma nzima, huku wakilindwa na askari. Haya ndiyo yaliyokuwa chakula chao.

Askari tu ndio waliopata chakula, maji na pesa za kununua sabuni. Hata na nguo walizipata bure kutoka serikalini. Wao tu ndio waliopata nafasi ya kuoga, kula na kulala vizuri. Hali hii iliwavutia wasichana wengine, na ikawa kwamba kila askari aliweza kujipatia wake wachanga zaidi ya mmoja. Huko vijijini, wake hawa walipewa jina la "Wake wa Hali ya Hatari." Wengine ambao hawakuolewa, walipewa jina la "Rarua" kwa vile walizoea kurarua chapati nyumbani mwa askari.

Ingawaje, kulikuwako na wasichana wengine kama Mumbi, ambao walichukia sana hali hiyo ya kutangatanga, katika kambi za askari. Ingawa walijua kwamba vijana waume walikuwa wengine wameishaingia misituni, wengine wamehamishwa, na wengine wameuawa, wao waliona ni lazima kungoja mpaka hali ya Hatari iishe. Walitumaini vijana marafiki zao watarudi, na hata wasiporudi, pengine wangepata vijana wengine wazuri na ambao wangependana. Kwa kutumaini hivi, walikaa tu nyumbani mwa mama zao, huku wakila taabu kama watu wengine. Hawakupenda kamwe kupoteza sifa zao.

Wasichana kama hawa walichukiwa sana na askari, na yeyote kati yao aliyeshitakiwa kwamba amekula kiapo, aliteswa sana.

Maina na wenzake walichukua kila mmoja bunduki ya .303, ambayo ni bunduki kubwa na iwezayo kutupa risasi mbali. Mau Mau walipenda sana bunduki hii, na kila walipopata nafasi, waliwashambulia hawa askari na kuwanyang'anya hizo bunduki. Kijana Mzungu aliyeongoza kikundi cha Askari Walinda Nyumba, aliwaonya sana wazichunge bunduki zao. Lakini askari wengi waliposhambuliwa na Mau Mau waliona ni heri kutupa bunduki wakijua kwamba Mau Mau wakishapata bunduki hawatawafuata tena.

Itaendelea. . .
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…