Juma Thomas Zangira: Mtanzania wa kwanza kushtakiwa kwa kosa la Ujasusi (Espionage)

Mshana Jr

Platinum Member
Aug 19, 2012
269,634
697,904
1. Usuli
Takribani miongo minne na ushee hivi iliyopita, ilitokea kesi ya Ujasusi iliyomkabili Mtanzania, Juma Thomas Zangira. Kesi hiyo ya kihistoria na ya aina yake ilimstua si tu aliyekuwa Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Baraza zima la Mawaziri, bali pia ilizua kimuhemuhe kikubwa nchini na ilitaradadi vilivyo kwenye vyombo vya habari enzi hizo; Radio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) na magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Daily News & Sunday News.

Leo, Jumamosi tulivu ya Julai 1, 2023, ikiwa imetimia miaka 46 toka SASP Ali Juma Guguru apokee taarifa za kiintelligentsia Julai 27, 1977 kuwa Bw. Zangira alikuwa anajihusisha na ujasusi uliokuwa ukimpatia maokoto, "Mzee wa Atikali" amewiwa kuielezea kiunagaubaga kesi hiyo iliyokuwa kesi ya kwanza ya Ujasusi nchini.
"Mzee wa Atikali", kwa kutumia hadubini yake, amefukunyua makavasi na makabrasha anuai na kupata habari kedekede kuhusu kesi hiyo. Aidha, "Mzee wa Atikali " amedahili na kufanikiwa kupata taarifa nyingi za kusisimua toka kwa waliohusika kwa namna moja au nyingine na mchakato wa kesi hiyo.


2. Wasifu wa JUMA THOMAS ZANGIRA
Bw. Juma Thomas Zangira alikuwa ni Afisa Uhusiano wa Kilimanjaro hotel, Afisa Usalama wa Taifa na mmoja wa Watanzania wachache waliokuwa wamepata mafunzo ya aina yake ya ukomandoo toka nchi mbalimbali duniani. Huyu alikuwa ni Komandoo aliyewiva ambaye alikuwa shupavu sana na mwenye ujuzi mkubwa wa mapambano katika ukanda huu wa Afrika. Mkono wake wa kushoto ulikuwa na nguvu kama bondia hodari wa zamani wa Marekani, Sonny Liston. Aidha, Bw. Zangira alikuwa ni mbobevu sana kwenye masuala ya intelligentsia na alikuwa ametunukiwa nishani nyingi kwa umahiri wake. Hivyo, alikuwa ni tegemeo kubwa kwa Taifa lake la Tanzania.

Kutokana na unyeti wa kazi zake, serikali ilimfungulia ofisi ya "Travel Agency" ya kupokea na kusafirisha wageni wa nje, pale "Ground floor" ya Kilimanjaro hoteli.

Miaka ya 1960s & 1970s, Tanzania ilikuwa kiota cha wapigania uhuru toka nchi za Kusini mwa Afrika na Makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika yalikuwa Dar es Salaam. Hii ilipelekea vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika kufungua ofisi zao hapa nchini mf. FRELIMO, ZANU, SWAPO, PAC & ANC na viongozi wengi wa nchi hizo waliishi nchini mf Edward Mondlane, Samora Machel, Robert Mugabe, Sam Nujoma nk. Viongozi hawa na wageni mbalimbali walikuwa hawakauki hotelini Kilimanjaro. Hivyo, ofisi ya Bw. Zangira iliwekwa pale mahsusi ili kupata taarifa mbalimbali nyeti na yeye akawa ndiye jicho na sikio la serikali.

3. Taarifa ya Ujasusi wa Bw. ZANGIRA
Jumatano, Julai 27, 1977, saa 1.30 asubuhi, SASP Guguru alipokea taarifa za kiintelligentsia kuwa Bw. Zangira alikuwa akijihusisha na ujasusi!. SASP Guguru alipigwa na butwaa na awali hakuamini maskio yake!. Ilielezwa kwamba badala ya kutafuta na kuchakata taarifa za wageni zenye ukakasi ili ziisadie serikali, Bw. Zangira alikuwa anasaka siri za serikali na za vyama vya ukombozi na kuzituma kwenye mataifa ya Kusini mwa Afrika.

4. "Surveillance Team" Yaundwa
Baada ya kupatikana taarifa hizo, ikaonekana kwamba kwavile Bw. Zangira ni Komandoo mahiri, isingekuwa busara kumuendea kichwakichwa. Hivyo, ikabidi mpango kamambe uandaliwe. Hatimaye, ikakubalika iundwe timu "Surveillance Team" ili kumnasa. Timu hiyo ikaundwa mara moja ikiwa na wajumbe toka taasisi mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi. Abdallah Msika, ambaye wakati huo alikuwa "Detective Sergeant" kabla ya kuja kuwa Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi miaka ya hivi karibuni kabla hajastaafu, ndiye aliyeteuliwa toka Jeshi la Polisi. Bw. Msika alikuwa amesoma hadi darasa la 8 "Malangali Middle School" kisha akaenda "Nursing" Muhimbili kabla ya kujiunga na Jeshi.

Timu hii ikajiapiza kuwa, aslan abadan, ni lazma ifanikishe jukumu hilo kwa weledi na uzalendo mkubwa kwa Taifa lao. Kisha, ikatayarisha adidu za rejea na kuanza kufuatilia kwa ukaribu nyendo zote za Bw. Zangira toka alipokuwa akitoka nyumbani kwake asubuhi hadi usiku. Bw. Zangira alikuwa akiishi mtaa wa Nkrumah ambako kulikuwa na ghorofa lililokuwa makao makuu ya FRELIMO, mkabala na "Co-Cabs", yeye akikaa ghorofa ya pili. Timu ilikuwa na magari na ilifanya kazi kwa zamu isipokuwa Msika ambaye alilazimika kuwepo muda wote kwani ndiye aliyekuwa na jukumu la kumkamata.

5. Barua za Bw. ZANGIRA Zanaswa
Timu ilifanikiwa kubaini kwamba Bw. Zangira alikuwa akiwasiliana na genge lake lililokuwa nje ya nchi kwa njia ya posta. Hivyo, barua zake zote alizokuwa akituma na alizokuwa akitumiwa kama majibu zilikuwa zinatolewa kopi na kurudishiwa kwa ustadi mkubwa.

6. Bw. ZANGIRA Akamatwa Kininja
Baada ya Timu kumfuatilia Bw. Zangira kwa muda mrefu na kukusanya ushahidi usio na mawaa, Timu ilitoa taarifa na mara moja ikatolewa amri akamatwe.

Siku ya ukamatwaji, Timu hiyo ilifika nyumbani kwake na kumsubiri kwa nje. Akiwa hajui hili wala lile, Bw. Zangira alianza kuelekea kazini kwake hoteli ya Kilimanjaro kupitia Posta. Timu ikawa inamfuata huku ikihakikisha kuwa lije jua, ije mvua lazma Bw. Zangira awekwe chini ya ulinzi. Bw. Zangira alipofika eneo la Posta mpya, akaenda yaliko masanduku ya barua. Msika, aliyekuwa amefundishwa vilivyo jinsi ya kumkabili na namna ya kukwepa mkono wake hatari wa kushoto, akawa anamnyatia kwa umakini wa hali ya juu. Bw. Zangira, kwa bashasha kubwa, akaitoa barua toka kwenye sanduku la barua. Afanalek, ile anageuka tu ili aondoke, ghafla Msika akamvaa na kumwambia "hands up" huku wale wenzie nao wakisogelea huku wakimuonesha Bw. Zangira mitutu ya bunduki! Ilikuwa ni kama sinema ya "James Bond 007"!. Bw. Zangira akanywea kama kobe aingizavyo kichwa ndani ya jumba lake!.

Ukomandoo wote ukawa kwishnei na akawa anafuata kila alichoelezwa. Akatii sheria bila shuruti! Hatimaye, aliingizwa ndani ya gari huku akitweta na akiwa chini ya ulinzi mkali ambapo watu wawili walikuwa kushoto na wawili kulia kwake "sandwich"!.

Alipofikishwa "Central Police Station" ikaamuliwa akasachiwe nyumbani kwake. Zoezi hilo lililoongozwa na Maafande, Alfred Tibaigana na Adadi Rajab, lilifanyika kama utaratibu wa sheria unavyoeleza. Kisha, Bw. Zangira alihojiwa na akapelekwa gereza lenye ulinzi mkali la Ukonga.

7. RTD Yamtangaza Bw. ZANGIRA
RTD ikautangazia umma kukamatwa kwa Bw. Zangira kwa tuhuma za ujasusi. "Bongolanderz" nchi nzima hawakuamini kile walichokuwa wakikisikia toka redioni kwani hawakuwahi kusikia tukio kama hilo na hawakujua Tanzania ina Jasusi !.

Kesho yake, magazeti ya "Uhuru" na "Daily News" yakaeleza jinsi Rais Nyerere na Baraza zima la Mawaziri lilivyosikitishwa na mkasa huo. Baada ya hapo, taratibu zote muhimu za kuitayarisha kesi zikataradadi.

Siku ya Jumapili, Septemba 25, 1977, RTD, katika taarifa yake ya habari saa mbili usiku, ikaeleza kwamba Bw. Zangira atapelekwa mahakamani kesho yake, Jumatatu. Kisheria, Ujasusi ni kosa kubwa ambalo ni lazma lisikilizwe na Mahakama Kuu na lazma wawepo Wazee wa Baraza kumsaidia Jaji kama yalivyo makosa mengine makubwa kama vile Mauaji au Uhaini .

8. Bw. ZANGIRA Afikishwa kwa Pilato
Jumatatu kuntu ya Septemba 26, 1977, Bw. Zangira alifikishwa Mahakama Kuu, toka gereza la Ukonga akiwa amefungwa pingu na akiwa chini ya ulinzi mkali.

Kutokana na upekee na unyeti wa kesi hii, ilibidi Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP)wa wakati huo, Bw. Damian Meela, aiendeshe mwenyewe kesi hiyo. Aidha, kutokana na ukweli kwamba kesi hiyo ilikuwa ni ya aina yake, ikabidi isikilizwe na Jaji Mkuu wa wakati huo, Mhe. Francis Nyalali, mwenyewe. Mhe. Nyalali alisaidiwa na Wazee wa Baraza watatu ambao ni Bw. Zuberi Ally, Bw. Hussein Hamis na Bw. Simba Salum. Bw. Zangira alikuwa akitetewa na wakili mashuhuri Thomas Mkude, wa lililokuwa Shirika la Sheria Nchini (TLC). Wakili Msomi Mkude baadaye alikuja kuwa "Chief Corporation Counsel" wa TLC na kisha akawa Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha akaja kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Hivyo, walioshiriki kwenye kesi hiyo iliyomkabili Bw. ZANGIRA walikuwa "WAMBA" watupu !.

9. Kesi ya Bw. ZANGIRA Yarindima
Siku ya kwanza ya kesi, Septemba 26, 1977 saa 3 asubuhi, umati mkubwa wa "Bongolanderz" ukiwa umefurika mahakamani, DPP Meela alimsomea Bw. Zangira Mashtaka Matatu :

Shtaka la Kwanza lilikuwa ni Kukusanya Habari kisha kuzitoa kwa raia wa Uingereza aliyeitwa John Wilson kwa nia ya kuvuruga usalama wa nchi yetu na kwamba taarifa hizo zingeweza kutumiwa na mataifa ya nje yanayoichukia Tanzania kuvuruga usalama wa nchi yetu.

Kosa la Pili lilikuwa ni Kumpatia Bw John Wilson habari ambazo zingeharibu jitihada za TANU na vyama vya ukombozi vya SWAPO, FRELIMO, PAC, ANC na ZANU.

Kosa la Tatu lililokuwa ni Kutoa Taarifa za OAU kwa John Wilson.

Mashtaka haya yote matatu yalidaiwa ni kinyume na Kifungu cha 9(1)(a) na 9(2)(1), Sheria ya Usalama wa Taifa, 1970.

Katika kesi hiyo, Bw. Zangira alikana mashtaka yote hayo matatu ambayo ilidaiwa aliyatenda kati ya mwaka 1971 na 1977. DPP Meela akaita mashahidi nane.

Shahidi wa kwanza alikuwa ni SASP Ali Juma Guguru ambaye alieleza kwamba Julai 27, 1977 alipokea habari za ujasusi na ikaundwa timu. Moja ya majukumu ilikuwa ni kuchunguza nani alikuwa anatumia sanduku la posta Na. 3900 DSM. D/Sergeant Abdallah akatumia mbinu za medani na kugundua kwamba aliyekuwa analitumia si mwingine bali ni Bw. Zangira.

SASP Guguru alieleza kuwa siku tatu tu baadaye, yaani Julai 29, 1977, saa 2 asubuhi, Bw Zangira aliondoka nyumbani kwake akawa anaenda ofisini kwake Kilimanjaro hoteli kwa kupitia Posta mpya bila kujua kuwa alikuwa anafanyiwa "surveillance" kali ya nyendo zake.

Bw. Zangira alipofika Posta akafungua sanduku lake la barua na akachukua barua moja aliyoikuta. Kufumba na kufumbua, akakamatwa na polisi! Bw. Zangira alikiri kuwa barua hiyo ni yake na ilipofunguliwa ilikuwa na £ 150. Barua hiyo ilikuwa imeandikwa na John Wilson wa Parkside, Derry Hills, Calne, Wits, UK ikimtaka Bw. Zangira atafute na kumpa habari juu ya namna uhusiano kati ya China na Tanzania ulivyokuwa ukiharibu uhusiano wa Tanzania na majirani. Pia ilimtaka aeleze kuhusu vyama vya ukombozi ambavyo makao yake makuu yalikuwa Dar es Salaam. Aidha, ilimtaka kutotumia jina lake halali na kwamba atalipwa £ 150 kwa mwezi na akileta habari zaidi ataongezwa.

Nyumba ya Bw. Zangira ilisachiwa na ofisi yake nayo ilisachiwa na zikapatikana barua 33. Barua zote hizo zilipokelewa mahakamani kama vidhibiti. Ilibainika kwamba Bw. Zangira alikuwa anatuma barua kwenda Uingereza kwa Bw. John Wilson. Barua inapofika kule, huwekwa bahasha mpya na kutumwa mataifa ya Kusini mwa Afrika. Aidha, mtiririko huo huo hufuatwa barua zitumwapo kwa Bw. Zangira.

Barua ya kwanza iliandikwa tarehe 29.11.1971 na ikafuatiwa na zingine tarehe 18.2.1972, 29.2.1972, 11.3.1972, 25.3.1972 na 12.4.1972. Barua hizo zilihabarisha taarifa mbalimbali za kijasusi huku zilionesha Bw. Zangira alikuwa ametumiwa jumla £ 485. Baadhi ya barua hizo zilikuwa zikimpongeza Bw. Zangira kwa kazi nzuri alizokuwa amefanya na zingine zikimlaumu kwa kukaa kimya kwa muda mrefu. Zingine zilimtaka atoe habari za OAU na ziliko kambi za wapigania uhuru nchini. Aidha, zingine zilimtaka aeleze kama Rais Julius Nyerere alikuwa akipendwa na wapigania uhuru na ni Mtanzania gani angekuja kuchukua nafasi yake.

Bw. Zangira pia alitakiwa kutoa taarifa za ofisi zote za ubalozi na maeneo ziliko na ni zipi zinawaunga mkono wapigania uhuru. Barua hizo pia zilionesha alikuwa akipokea fedha mara kwa mara na kuna wakati alimwandikia Bw. John Wilson akiomba apewe fedha za kujengea nyumba na kununua gari kutokana na kazi kubwa aliyokuwa ameifanya ya kupeleka taarifa nyeti. Alijibiwa kwamba apekeke "Account No" na avute subira. Mwisho, barua zilionesha pia alisafiri kwenda Kenya (22.7.1974) na Malawi (7.4.1976) ambako aliambiwa na John Wilson hoteli ya kufikia na watu atakaokutana nao.

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa kwa siku nne mfululizo, Upande wa Mashtaka ulimaliza kuita mashahidi wake hivyo ukafunga kesi yake.

10. Bw. ZANGIRA Aanza Kujitetea
Ijumaa, Septemba 30, 1977, Bw. Zangira akaanza kujitetea. Katika utetezi wake, Bw. Zangira alikiri kuwa barua hizo zote ni zake na kweli alikuwa akimuandikia barua Bw. John Wilson ila alikuwa akifanya hivyo kama Mwandishi wa Habari kwani hizo zilikuwa ni habari za kawaida tu na zikipatikana magazetini. Aidha, alidai habari alizokuwa akituma zilikuwa za biashara tu. Alieleza zaidi kuwa zamani alikuwa akifanya kazi Subuzani Tours & Safaris, Arusha ambako alikuwa akipeleka watalii mbugani.

Bw. Zangira alieleza kuwa mwaka 1971 alimpeleka mtalii Wiltshire Mikumi na kwamba Bw. Wiltshire alimwambia ana rafiki yake yuko Uingereza anatafuta Mwandishi wa habari hivyo akampa Bw. Wiltshire "Contacts" zake. Baada ya wiki chache akaanza kupokea barua kutoka kwa Bw. John Wilson. Alieleza zaidi kuwa alikuwa akilipwa kwa habari zote alizokuwa akipeleka toka 1971 hadi 1977.

Bw. Zangira alizua kicheko mahakamani alipoeleza kuwa alishangazwa alipostukia anakamatwa, yeye akiwa Mwandishi wa habari, asubuhi ya Julai 29, 1977 mara tu baada ya kuchukua barua toka kwenye sanduku lake la barua iliyotoka kwa John Wilson. Huo ndio ukawa mwisho wa utetezi wake.

11. Wazee wa Baraza Watoa Maoni
Mhe Jaji Mkuu Nyalali aliwafafanulia Wazee wa Baraza maelezo yote ya kesi na akauchakata ushahidi na kisha akawataka watoe maoni yao. Baada ya hapo, Wazee wawili (Simba Salum na Hussein Hamis) walitoa maoni kuwa wanaona ushahidi umethibitisha mashtaka wakati Mzee wa tatu (Zuberi Ali) aliona mashtaka hayakuthibitishwa.

Mhe. Nyalali akaihairisha kesi hiyo hadi Jumatano, Oktoba 5, 1977 ambayo ilipangwa kuwa ndiyo siku ya hukumu.

12. "Bongolanderz" Waisasambua Kesi
Kwavile "Bongolanderz" nchi nzima, toka Naliendele- Mtwara hadi Kahororo- Bukoba, walikuwa wakiifuatilia kwa umakini kesi hii, kila mmoja alikuwa akitoa maoni yake kuhusu hatma ya Bw. Zangira kwa kuzingatia ushahidi uliokuwa ukitolewa mahakamani kwa mujibu wa magazeti yaliyokuwa yakiripoti kesi hiyo.

13. Bw. ZANGIRA Atiwa Hatiani
Siku ya hukumu, asubuhi na mapema, "Bongolanderz" lukuki walifika Mahakama Kuu kujionea wenyewe kitakachojiri. Ulinzi ulikuwa mkali sana na wote waliotaka kuingia ndani, walisachiwa sana. Kufumba na kufumbua, Mahakama ikawa imejaa hadi pomoni. Hatimaye, Mhe. Nyalali akasoma hukumu iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu. Hukumu hiyo iliyoandikwa kwa weledi mkubwa ilikuwa ndefu na ilimchukua Mhe Nyalali masaa matatu kuimaliza. Mwishowe, Mhe Nyalali alimtia hatiani Bw. Zangira kwa makosa yote matatu aliyoshtakiwa nayo.

Mhe Nyalali, pamoja na mambo mengine, alieleza:

"John Wilson alikuwa ni jasusi aliyekuwa akitumiwa na mataifa fulani ili kuangamiza usalama wa Taifa letu. Utetezi wa Bw. Zangira kuwa alikuwa akimtumia Bw. Wilson habari za biashara hauna hoja. Hizo habari hazikuwa za kumfaa mfanyabiashara yeyote bali haini Smith na kaburu Vorster wa Afrika Kusini. Vilevile, kama ni za biashara iweje atakiwe kutumia jina bandia? Tanzania ni moja ya nchi zilizo mstari wa mbele Kusini mwa Afrika hivyo kitendo cha Zangira kutoa siri za vyama hivyo na OAU ni sawa na Uhaini".

14. DPP Aomba Adhabu Kali
Baada ya Mhe. Nyalali kumtia hatiani Bw. Zangira, DPP Meela aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine hasa ukizingatia umuhimu wa Tanzania kwenye ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

15. Wakili MKUDE Aomba Huruma
Bw. Mkude aliiomba mahakama imhurumie mteja wake na izingatie ukweli kwamba hilo lilikuwa ni kosa lake la kwanza na pia alikuwa akitegemewa na nduguze.

16. Bw. ZANGIRA Afungwa Miaka 20
Mhe Nyalali, baada ya kusikiliza na kuzingatia kwa makini maelezo ya DPP Meela na Wakili Mkude, alitoa kifungo cha miaka 20 !. Urefu wa kifungo hiki ulishangaza "Bongolanderz" wengi kwani kifungo cha urefu huo kilikuwa hakijazoeleka enzi hizo. Mara baada ya kuhukumiwa, ndugu, jamaa na marafiki wa Bw. Zangira walitoka mahakamani na simanzi kubwa huku Bw. Zangira akichukuliwa chini ya ulinzi mkali kwenda kuanza maisha mapya Lupango!


17. Tamati
Hii ndio kesi ya kwanza ya Ujasusi nchini na leo, Julai 1, 2023, imetimia miaka 46 toka taarifa za kiintelligentsia zilifikie Jeshi la Polisi kuwa Bw. Juma Thomas Zangira, Komandoo aliyekuwa akiaminiwa sana na serikali, alikuwa anakengeuka majukumu yake na akawa Jasusi, kazi aliyoifanya kuanza mwaka 1971. Kama Wahenga walivyonena "Za Mwizi ni 40", hatimaye akakamatwa mwaka 1977 na kupewa Mvua 20.

Mzee wa Atikali
0754 744 557

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Pengine zangira aliangushiwa jumba bovu na mchonga baada ya kutofautiana nae hivyo Waka mframe na kumuingiza kingi....

Maana kipindi hicho Cha Giza lolote lingeweza kukutokea na usipate utetezi.

Mawazo yangu lkn.
Hawakumfunga out of blues. Kulikuwa na ushahidi beyond reasonable doubts

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Abdallah Msika namkumbuka huyu mhehe. Alipata kuwa OCD Oysterbay. Askari mmoja mstaarabu sana. Namkumbuka vema. Ahsante Mshana Jr kwa kuleta kumbukumbu.
Kitu kimoja binafsi nimekua msahaulifu sana wa matukio mengi ya zamani na hata ya sasa. Isingelikua hivyo ningekua naeleza mengi humu jamvini.
 
Abdallah Msika namkumbuka huyu mhehe. Alipata kuwa OCD Oysterbay. Askari mmoja mstaarabu sana. Namkumbuka vema. Ahsante Mshana Jr kwa kuleta kumbukumbu.
Kitu kimoja binafsi nimekua msahaulifu sana wa matukio mengi ya zamani na hata ya sasa. Isingelikua hivyo ningekua naeleza mengi humu jamvini.
Nadhani badala ya neno mstaarabu ungetumia neno Bishoo. Alikuwa anatembea na perfume Aina 4 - 6 kwenye gari la serikali. Miongoni mwa binadamu waliojaa dharau Kwa watu wa chini Muda wote.
 
Hii ndio kesi ya kwanza ya Ujasusi nchini na leo, Julai 1, 2023, imetimia miaka 46 toka taarifa za kiintelligentsia zilifikie Jeshi la Polisi kuwa Bw. Juma Thomas Zangira, Komandoo aliyekuwa akiaminiwa sana na serikali, alikuwa anakengeuka majukumu yake na akawa Jasusi, kazi aliyoifanya kuanza mwaka 1971. Kama Wahenga walivyonena "Za Mwizi ni 40", hatimaye akakamatwa mwaka 1977 na kupewa Mvua 20.
Yu wapi baada ya kumaliza kifungo
 
Abdallah Msika namkumbuka huyu mhehe. Alipata kuwa OCD Oysterbay. Askari mmoja mstaarabu sana. Namkumbuka vema. Ahsante Mshana Jr kwa kuleta kumbukumbu.
Kitu kimoja binafsi nimekua msahaulifu sana wa matukio mengi ya zamani na hata ya sasa. Isingelikua hivyo ningekua naeleza mengi humu jamvini.
Jitahidi yale unayokumbuka ushiriki nasi..yana mvuto wake

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom