Joshua Nassari, ETI Habari hizi ni za Kweli?

Dr Mathew Togolani Mndeme

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
201
808
1552792650943.png

Mh Joshua Nassari, ETI nimesikia na kusoma mitandaoni kwamba wewe sio mbunge tena. Kwamba mimi na wananchi wenzangu wa jimbo la Arumeru Mashariki hatuna mwakilishi kwa sasa wa kutusemea kwenye vikao vya kamati za bunge zinazoendelea na baadaye mule mjengoni mkutano utakapoanza. ETI habari hizi mbaya ni za kweli? Tafadhali nijibu maana bado nimeamua kuwa mbishi kama Tomaso. Kinachonifanya nikatae habari hizi ni kuambiwa ETI umesimamishwa ubunge na Mh Spika Ndugai kwa kosa la utoro kwa kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo. ETI hilo nalo ni la kweli? Mimi ninaendelea kubisha hadi unijibu. Ninabisha kwa sababu nakufahamu vema na tumezoeana kuitana “homeboy”. Nabisha kwa kuwa najua makeke yako na ninatambua kwamba wewe ni msomi makini wa ngazi ya uzamili. Nimekataa kukubali habari hizi kwa sababu kwa ninavyokufahamu, kwa vyovyote vile haiwezeani ukasahau mikutano ya bunge. ETI kwamba hukuandika barua za kuomba ruhusa kama inavyotakikana na hata ulipoandika hakujishughulisha kufuatilia majibu. ETI hii ni kweli?

Wakati ninabisha hili, mpigakura mwenzangu wa Arumeru Mashariki ameamua kuniletea ushahidi. Kanionesha barua toka bungeni ambayo kwa maelezo yake ndicho chanzo kikuu cha habari hizi. Nikamkatalia na kuhoji mbona barua ya bunge haijasainiwa? Akaniambia haijalishi maana hata wewe umekiri kuipokea. Pia akanionesha barua yako uliyoandika kutoa taarifa za udhuru mwezi January. Nayo nikaikataa na nikamkemea aache kukuzushia mambo mbunge wangu. Haiwezekani. “Homeboy” asingeacha kunijulisha kwamba amechukua likizo ya malipo bungeni lakini bila ruhusa. Kwa hasira (unajua tena wameru tulivyo na hasira karibu) akafungua simu yake na kunionesha ujumbe alionijulisha umeandikwa na wakili msomi Mh Tundu Antipas Mwigai Lissu akijulisha umma kwamba umewasiliana naye kumuomba ushauri wa kisheria juu ya suala hilo. Kusema ukweli niliukataa ujumbe ule na nimegoma kulala tangu jana kwa hasira maana naona kama kuna mtu kaigilizia uandishi wa Mh Lissu kwenye ujumbe ule. Kwanza hauna sahihi ya kalamu ya wino wala muhuri wa kisheria kama nilivyozoea kuona kwenye maandishi ya mawakili.

Nimemweleza kuwa haiwezekani mbunge wetu akakumbwa na mkasa kama huu wakati ana mikakati mingi ya jimbo letu. Nilimkumbusha kwamba, mara ya mwisho tulipoonana tuliongelea maendeleo ya jimbo letu kwa kirefu kidogo. Nimemwambia pamoja na ukweli kuwa mimi sio mwanachama wa chama chako, lakini umekua ukinipa nafasi ya kuuliza maswali, kukukosoa, kukushauri, na kukusumbua juu ya changamoto za kiuongozi jimboni. Ikabidi nimwoneshe mambo tuliyoongea mara mwisho tulipoonana na ambayo kwayo nilidhani una uwezo wa kuyafuatilia kimkakati. Baadhi ya mambo hayo ni:
  • Moja, nilikukumbusha hali ya mazingira ilivyokua jimboni kwetu miaka kama 25 iliyopita kabla ya kuangauka kwa soko la kahawa. Meru ilikua ya kijani kwa wingi wa miti na migomba. Ulikua ukishuka pale Usa River haikuwezekani kuona Mlima Meru vizuri kwa kua ulifunikwa na miti. Hivi sasa Meru inabadilika sana na kwa tunaojua muonekano wake miaka ya 1980 na kuelekea 2000 tunaona kama kunakuwa jangwa. Miti ya asili na ya kupandwa inakatwa hovyo na hakujawa na mkakati mkubwa na endelevu wa kuhakikisha iliyoko inatuzwa na tunapanda mipya. Nilikueleza kua ajenda hii ya mazingira sio kete nzuri sana kisiasa maana haina matokeo ya haraka lakini kunahitajika uongozi na ufuatiliaji wa kimkakati wa kuboresha ukijani wa Meru. Nilikushauri utumie ushawishi na nafasi yako kushirikiana na uongozi wa wilaya na wadau wengine kufanikisha hili. Nilikuambia hii itakua alama ya kudumu jimboni hata utakaposita kuwa mbunge.
  • Mbili, tuliongea tatizo la unywaji pombe ovyo jimboni. Nilikuambia kuna vilabu vya pombe kila kona na vingine viko katikati ya makazi ya watu vijijini. Vimeondoa ustaarabu na kumepeleka vijana wengi wenye nguvu jimboni kuharibikiwa, kutozalisha mali, na kubobea kwenye uvutaji wa “Cha Arusha” na vilevya vingine. Pombe imeharibu wanafunzi, watoto, familia nyingi, na inachangia sana umaskini wa Meru.
  • Tatu, uliponishirikisha juu ya mpango wako wa kuweka kompyuta na internet kwenye shule za sekondari, nilikuuliza maswali kadhaa. Kisha nikakushauri umuhimu wa mradi huo kufanyika kitaalamu badala ya kisiasa kwani siasa hazijawahi fanikisha mabadiliko ya kiteknolojia na kupata manufaa tarajiwa hasa katika nchi kama yetu. Nilikuonesha hatari ya kufanya miradi ya kitalaamu (hasa ya TEHAMA) kwa kutumia siasa badala ya wataalamu. Nilikwambia hili nalo halina matokeo ya haraka kisiasa lakini kama unataka matokeo chanya lazima mradi husika utumie taarifa sahihi na wataalamu. Kwa kuwa ni eneo langu, nilikuahidi kukupa ushirikiano utakapohitaji.
  • Nne, nilikueleza juu ya tatizo la utunzaji wa vyanzo vya maji. Nilikupa mfano wa Chemchem ya Teema ambapo pamekua tegemeo kuu la chanzo cha maji kwa wakazi wa vijiji vya karibu tangu enzi lakini sasa inakauka kutokana na uharibifu wa mazingira na maamuzi mabovu ya viongozi fulani wa Kijiji waliomruhusu mtu binafsi kujimilikisha chemchem hiyo. Nilikukumbusha kwamba mimi na wewe tumekunywa maji yale tangu utoto wetu.
  • Tano, nilikukumbusha kuwa baadhi ya wananchi ambao nyumba zetu ziliathirika vibaya na uchimbaji wa mchanga katika makazi yetu hatujalipwa fidia hadi leo pamoja na ufuatiliaji tangu mwishoni mwa 2016. Uchimbaji wa mchanga uliotumika katika ujenzi wa bararara ya Arusha mjini hadi Tengeru ulifanyika katika makazi yetu bila kufuata taratibu na jambo hili lilifika hadi Wizara ya Mazingira ofisi ya Makamu wa Rais na Mh January Makamba alifika kushuhudia ukubwa wa tatizo hilo.
  • Mwisho, nilikushauri kwamba jitahidi kutumia wasomi na wataalamu waliotoka Meru walioko mijini na kwingineko duniani katika miradi yako ya maendeleo. Ingawa kundi hili sio mtaji mzuri sana wa kura, lakini unaweza kutumia utaalamu wao kubadilisha Maisha ya watu.
Kumbukumbu zangu zinanionesha kwamba ulikubaliana nami juu ya mambo haya na ukaniahidi kuyafanyia kazi. Sasa iweje leo ETI mtu aniambie wewe sio mbunge tena? Nani atafatuatilia mambo haya kama wewe haupo? Au umemwachia nani jukumu hilo? Niambie, umemrithisha nani? Niambie haraka kabla sijapiga NDURU majirani wajitokeze.

Kilichionipa hasira za kimeru zaidi ni kitendo cha mwenzangu huyu kuniletea video mbili toka mitandaoni. Moja ETI ni ya Mh Freeman Aikaeli Mbowe ambaye alikiri jambo hilo mbele ya waaandishi wa habari na akasema hataongea sana maana mchana wa juzi ungetoa kauli wewe mwenyewe na kwamba alikuagiza kuongea na watanzania. Nikamgomea kuwa ile sio kauli ya Chairman wako maana mbona basi hadi leo hujaongea lolote? ETI inawezekana ukaacha kutii maagizo ya mwenyekiti wako? Nayo nimeikataa kama ile ya Lissu maana naye alisema utaongea na umma lakini umekua kimya. ETI inawezeana ukaacha kufuata ushauri wa mwanasheria wenu mkuu?

Video ya pili inayoonesha baadhi ya wapigakuwa wa Arumeru Mashariki wakiongozwa na baadhi ya washili chini ya Mshili Mkuu kwamba ETI walikutana chini ya Mringaringa pale Poli kumpongeza Mh Spika kwa wewe kusimamishwa ubunge. ETI nini? Chini ya Mringaringa? HAPANA. Nilimwambia eneo lile ni tukufu kwa wameru maana ndipo wanapofanyia mambo yao ya mila, matambiko, kuvunja chungu, na mikutano mingine ya mambo magumu ya kikabila na kudumisha kimila. Nilimwambia wakati tunakua, ukisikia kuna kikao chini ya Mringaringa lazima uogope na kutetemeka. Tulikua hata hatupasogelei kirahisi. Sasa iwaje leo ETI washili wakutane pale na wananchi kufurahia wewe mshili mwenzao kusimamishwa ubunge? Mimi Nimekataa nikusikie. Tena nilimjibu kwa lafudhi ya kimeru nikwambia, "haiwesekani kapisa bwana. Chiwaa ndi mbe!!".

Hii ndio sababu imenifanya nikutafute sana na sijafanikiwa hadi sasa huku nikiwa nakosa usingizi. Uko wapi “Homeboy”? Mbona umenyamaza? Mbona umepotea na hunijibu kwa simu wala kwa wasapu? Utaongea lini? Utanithibitishia habari hizi lini? ETI ni kweli kwamba wewe sio mbunge? Kwani chama chako kilikua wapi wakati ulipokua uhudhurii vikao bungeni iwapo shutuma hizo ni za kweli? Mbona Mh Spika anasema viongozi wako hawakampekelea taarifa za udhuru wako? ETI ni kweli kwamba nao walisahau kutoa taarifa kama wewe? HAPANA. Mimi ninakataa maana najua chama chako hakiwezi kuzembea kwa jambo zito kama hili. Sasa nini Kimetokea “Homeboy”? Katika mazingira kama haya, wameru tumezoea kusema, "Chenda chasa cheenda. Kwa! kwani nini pwana!!" lakini leo mimi sisemi. Nimegoma.

Tafadhali sana nipe uhakika wa habari hizi ili KAMA NI ZA KWELI basi niwasiliane na washili wa Meru, wapiga kura, na chama changu kuwaomba wanisimamishe kugombea ubunge wa jimbo hili ili kuziba nafasi yako. Na kama hayo yatafanikiwa nitakuomba sana ukiombe chama chako ruhusa ili unisahidie kufanya kampeni uchaguzi utakapokaribia. Sio lazima uvue magwanda na kuvaa sare ya kipande hii maana magwanda yanakupendeza na nisingependa kukulazimisha uyavue. Utawaambia unamsaidia "Homeboy".

Sijalala siku ya pilii sasa nikingoja kukusikia juu ya habari hizi ambazo hadi sasa ninaziona ni za kuvumishwa. Tafadhali tuma hata mjumbe aniletee uhakika wa bahari hizi. Kama ni barua utampa, basi hakikisha pale mwishoni kuna sahihi yako ikisomeka "Homeboy".

Shiisanie mbee.

Mwalimu MM.
 

Attachments

  • 1552791886700.png
    1552791886700.png
    666.5 KB · Views: 88
Hivi inamaana Nassari hana marafiki wa karibu bungeni?

Hawakustushwa na kutokuwepo kwake bungeni muda mrefu? Hawakumuuliza vipi mbona hauhudhurii? Aliwajibu nini?

Au alipata deal la kazi isiyo na pressure akapuuzia ubunge + kumuuguza mke.
 
Ishatoka hiyo ikirudi pancha .....halafu sijui kwanini naona hii ni kama game fulani hivi

Ikitokea wewe chama chako kikakupitisha kugombea ubunge kama unavyosema basi hili bandiko uliloweka ni zuga tu na kwamba unajua kila kitu kuhusu "Homeboy" wako hapa umekuja kutuchora tu
Sijui kwanini hisia zinanituma hivi kama nimekosea utanisamehe

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Swali.

#1. Je chadema kilishamuonya Nasari juu ya Utoro wake Bungeni??

#2. Je! Chadema hawana utaratibu wa kusimamia Wabunge wao kutimiza majukumu yao??
 
Ishatoka hiyo ikirudi pancha .....halafu sijui kwanini naona hii ni kama game fulani hivi

Ikitokea wewe chama chako kikakupitisha kugombea ubunge kama unavyosema basi hili bandiko uliloweka ni zuga tu na kwamba unajua kila kitu kuhusu "Homeboy" wako hapa umekuja kutuchora tu
Sijui kwanini hisia zinanituma hivi kama nimekosea utanisamehe

Sent using Jamii Forums mobile app
Mayb...lakin mm nimemsoma ni kma ana mkejeli homeboy!maana ule ni zaidi ya utoto
 
Hivi inamaana Nassari hana marafiki wa karibu bungeni?

Hawakustushwa na kutokuwepo kwake bungeni muda mrefu? Hawakumuuliza vipi mbona hauhudhurii? Aliwajibu nini?

Au alipata deal la kazi isiyo na pressure akapuuzia ubunge + kumuuguza mke.


Swali zuri sana!inafikurisha sana jaman..
 
Back
Top Bottom