JKT ni Shule ya Uongozi na Uzalendo

JKT ni Shule ya Uongozi na Uzalendo

CHAGOSI GERALD

Senior Member
Joined
Jan 25, 2020
Posts
162
Reaction score
284
Makala ya Tatu

Ndugu zangu,

Kila taifa linalodumu na kustawi huwa na shule ya uzalendo, mahali ambapo vijana wake hujifunza siyo tu kupiga risasi au kufanya kazi ya mikono, bali kujifunza hekima ya waasisi. Nilipokuwa JKT niliiona shule hiyo lakini haikuwepo. Niliona ni mahali ambapo kijana wa Kitanzania angeketi, asome, ajadili, na aelewe falsafa zilizozaa taifa hili.

Ni wapi kijana wa taifa hili atajifunza maana ya uhuru, kama si pale ambapo analazimika kuishi na wenzake bila ubaguzi wa kabila au dini? Ni wapi atajifunza mshikamano, kama si pale ambapo anasoma maneno: “Uhuru bila umoja ni kivuli, na mshikamano bila uhuru ni mtego”?

Ni wapi kijana atajifunza maana ya maendeleo, kama si pale ambapo analetwa uso kwa uso na ukweli kwamba: “Maendeleo si mitambo, si majengo, ni watu”?

Ni wapi ataelewa wajibu wa kiongozi, kama si pale anaposoma na kutafakari: “Uongozi ni wajibu, si heshima; ni sadaka, si nafasi ya kunufaika”?

Ni wapi ataelewa hadhi ya utu, kama si pale ambapo anasoma: “Binadamu ndiye kipimo cha kila sera, kila maendeleo, na kila mfumo wa kijamii”?

Ndugu zangu, JKT ilipaswa kuwa chuo cha falsafa ya taifa letu. Vijana walipaswa wasome maneno haya, wajifunze kuyaishi, na kuyageuza kuwa mwongozo wa kesho. Lakini leo, JKT imesahaulisha lengo hilo. Wala halitumiki kama darasa la kuandaa viongozi wa kesho; limebaki kama kivuli kinachoahidi ajira badala ya kuotesha fikra.

Vijana wa JKT walipaswa kuibuka wakiwa ni mabalozi wa mshikamano, watu waliotoka kambini wakiwa na hekima ya kusema:

“Kiongozi si bwana, ni mtumishi.”

“Maendeleo si heshima ya wachache, ni haki ya wote.”

“Uhuru si kivuli cha bendera, ni utu unaoishi ndani ya kila mmoja wetu.”

Lakini leo, ni wangapi wanaoacha kambini wakiwa na roho hii? Ni wangapi wanarudi wakiwa na maandiko ya uzalendo mioyoni mwao?

Ndugu zangu, taifa lisilo na vijana waliopikwa kwa falsafa zake ni taifa lililokosa roho. JKT ilipaswa kuwa shule ya kujifunza maana ya uhuru, mshikamano, ujamaa, utu, na uongozi wa kweli. Bila hilo, taifa hubaki giza.

Chagosi Gerald
 
Back
Top Bottom