JK kaweza, sisi tutashindwaje? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK kaweza, sisi tutashindwaje?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Sep 24, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Na Absalom Kibanda

  KILA dalili inaonyesha kwamba, joto la Uchaguzi Mkuu wa mwakani linazidi kupanda kila kukicha kwa kiwango kinachotofautiana kutoka eneo moja na jingine na kutoka katika chama kimoja hadi kingine.

  Matukio ya hivi karibuni ya vurugu za kisiasa zinazochagizwa na kazi ya uandikishaji wapiga kura katika visiwa vya Unguja na Pemba ni matokeo hayo hayo ya kupanda kwa joto hilo la kisiasa.

  Mabishano makali kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa upande mmoja na Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu vurugu hizo za Zanzibar na hususan matukio ya matumizi makubwa ya nguvu katika Kisiwa cha Pemba ni kielelezo kingine cha kuendelea kupanda kwa kasi kwa joto hilo.

  Kupanda huko kwa joto la Uchaguzi Mkuu wa mwakani, ambao utatanguliwa na ule wa vijiji, vitongoji na mitaa unaofanyika hivi karibuni, ulichagizwa na mazungumzo aliyoyafanya Rais Jakaya Kikwete na wananchi kupitia Shirika la Utangazaji nchini (TBC).

  Ni jambo la heri kwamba, kupanda huko kwa joto la uchaguzi kumeenda sambamba na kuendelea kuimarika kwa hisia za kipinzani dhidi ya CCM na serikali yake katika maeneo mbalimbali nchini.

  Hali hii ya kuzorota kwa mambo ndani ya chama hicho tawala kumesababishwa na mambo mengi lakini pengine sababu kubwa kuliko zote katika hili ni uwezo mdogo wa kiutawala, kioganaizesheni na kiuongozi ulioonyeshwa na unaoendelea kuthibitishwa na Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Kikwete.

  Udhaifu wa kiutendaji ulioonyeshwa na serikali hii umefanikisha kuibuka kwa hoja na nadharia nyingi katika vichwa vya watu katika siku za hivi karibuni ambazo aghalabu sina budi kuziorodhesha na kuzijadili moja baada ya nyingine.

  Nadharia ya kwanza miongoni mwa nyingi vichwani mwa watu iliyozalishwa na udhaifu huo ni ile ambayo ilitufanya baadhi yetu tufikie hatua ya kuanza kuiona Ofisi Kuu katika taifa hili (Ikulu) ambayo Baba wa Taifa alipata kutusadikisha kuwa ni mzigo mzito na ni mahali patakatifu, kuanza kidogo kidogo kupoteza maana hiyo.

  Kudorora huko kwa Ikulu ndiko ambako kumenifanya mimi na baadhi ya watu wenye mtazamo kama wangu, kuanza kufikiri kwamba, pengine moja ya urithi ambao Kikwete atatuachia Watanzania mara atakapoondoka madarakani, iwe ni mwakani au mwaka 2015 (kwani lolote linaweza kutokea) ni ukweli kwamba; Ikulu si mzigo wala mahali patakatifu tena.

  Chini ya nadharia hii hii, kumeibuka kundi la Watanzania ambao kwa mara ya kwanza sasa wanaanza kuutazama wadhifa wa urais kuwa ni kazi au wajibu wa kisiasa unaofanana na nyadhifa nyingine za uteuzi ambazo kuzipata kwake ni matokeo ya turufu ya kuitafuta fursa kwa staili ya kunyangÂ’anyana.

  Matokeo haya ambayo kwa kiwango kikubwa yanachagizwa na udhaifu mkubwa wa kiuongozi, ndiyo ambayo yamewafanya wanasiasa wa ndani ya CCM na wa nje ya chama hicho wakipita mitaani wakisema kwa kujiamini kabisa kwamba, iwapo JK kaweza, ni nini kitatushinda sisi?

  Katika mwamvuli huo huo ikaibuka nadharia ya pili ambayo ilianza kujengwa kidogo kidogo nje ya CCM kabla ya kutekwa nyara na wajanja wachache ndani ya chama hicho tawala.

  Nadharia hii ya pili ni ile ambayo ilikaribia kabisa kuwafanya Watanzania mmoja mmoja na kisha ikapata nguvu kidogo kidogo kuanza kumuona Rais Kikwete kuwa kiongozi ambaye alipaswa kupewa fursa moja tu ya miaka mitano ya kuliongoza taifa hili.

  Chimbuko hasa la nadharia hii ya pili kuanza kuibuka, ni kwa mawazo kwamba, Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya uongozi wa Rais Kikwete ilikuwa imeshindwa kutimiza wajibu wa msingi wa kimadaraka unaojengwa katika misingi ya kuonyesha njia.

  Hoja zilizozaa mtazamo huu, zilianza kuonekana mapema kabisa baada ya Kikwete kuingia Ikulu wakati ule yeye na viongozi wenzake walipoanzisha mbwembwe ambazo leo hii zimebakia kufananishwa na ndoto za alinacha za Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, semina elekezi na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo.

  Mbwembwe hizi zilifuatiwa na ziara za kusisimua za Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa, ambazo ziliandamana na matukio mengi ya kushitua na wakati mwingine kutia moyo, kabla hazijageuka na kuwa shubiri kwa serikali.

  Katika ziara hizo zilizoandamana na kila aina ya vibwagizo, chini ya usimamizi wa Lowassa, Serikali ya Awamu ya Nne ikaja na ajenda ya shule za sekondari za kata ambazo baada ya kufumuka kwa mfano wa uyoga ghafla zilianza kupoteza mwelekeo, kabla Kikwete mwenyewe ajathibitisha kupotea kwa matumaini wakati alipozungumza na wananchi wiki mbili zilizopita.

  Kupwaya na kufa kifo cha mende kwa kaulimbiu za kila namna za Kikwete na viongozi wenzake kuanzia ile ya Nguvu, Kasi na Ari Mpya na hata ile ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, kulijenga msingi imara wa kupoteza mwelekeo wa serikali.

  Matokeo ya ufa huu mkubwa katika serikali kulikochagizwa na nadharia zote mbili, kukasababisha kuibuka kwa mitazamo inayokinzana ndani ya serikali na nje, ndani ya CCM na nje ya chama hicho.

  Ufa huu mkubwa wa kimadaraka ulipoendelea kukua na kuchukua sura tofauti ndani ya serikali, kidogo kidogo ulianza kuzibwa kwa nguvu iliyoanza kujengwa kwanza ndani ya vyombo vya habari, kisha vyama vya upinzani, kabla ya kunyakuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Nguvu kubwa ya vyombo vya habari ilianza kujionyesha mapema hata kabla ya Bunge kuitumia kuisambaratisha serikali kupitia katika hoja ya Richmond, Februari mwaka jana.

  Tukio hilo la Februari ambalo lilishuhudia Lowassa akijiuzulu uwaziri mkuu na mawaziri wengine wawili na kisha likampa fursa Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake akiwaweka kando kina Zakia Meghji, Basil Mramba na Joseph Mungai, lilionekana kuwa lenye nafuu kubwa serikalini.

  Kwa kiwango kikubwa tukio hilo ambalo kwanza lilivipa ushindi vyombo vya habari na kisha likaanza kulijengea uhalali Bunge kwa gharama za udhaifu mkubwa wa kiuongozi serikalini, kidogo kidogo liliendelea kufichua ufa mkubwa zaidi.

  Wadadisi wa mambo ni mashahidi wazuri kwamba, tangu msambaratiko huo wa serikali wa Februari mwaka jana, jinamizi la Richmond mbali ya kulijengea Bunge uhalali ambao halikuwa nao kabla, limeendelea kuitafuna serikali ya Kikwete kwa kiwango kikubwa na pengine kuendelea kufichua udhaifu zaidi wa kiuongozi badala ya kuuficha.

  Kile ambacho baadhi yetu tulikuwa tukikiona kuwa ni kivuli kisichofaa cha Lowassa kumfunika na wakati mwingine kumharibia Kikwete, kidogo kidogo kilianza kupotea na kufichua siri za nyufa nyingi zaidi ndani ya CCM na serikalini kwa ujumla.

  Vikao vya mwisho vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na kile cha kabla yake cha Kamati Kuu ya chama hicho (CC), vilivyomalizika kwa kuundwa kwa kamati ya wazee ili kuangalia msingi wa kuibuka kwa uhasama mkubwa miongoni mwa wabunge wa chama hicho, ni ushahidi wa namna jinamizi la Richmond na ombwe la uongozi linavyoitafuna serikali.

  Ni jambo la kusikitisha kwamba, Kikwete anayeongoza vikao vya chama chake anafikia hatua ya kukubali kuundwa kwa kamati hiyo, huku akijua kuwa msingi wa kuibuka kwa uhasama huo ni hatua ya serikali yake kushindwa kuchukua hatua za haraka na za dharura za kudhibiti mambo kabla ya maji kuuzidi unga nguvu.

  Hivi Kikwete, viongozi wenzake na chama chake wanataka kutuaminisha Watanzania kwamba uamuzi wao wa kuwatuma Mzee Ali Hassan Mwinyi, Abdulrahman Kinana na Pius Msekwa wa kutafuta kiini cha mzozo wa wabunge wa CCM na kurejesha taarifa waliufanya kwa kuwa hawaujui uhusiano uliopo kati ya hali hiyo na ombwe la uongozi serikalini?

  Je, CCM na Serikali ya Awamu ya Nne wanataka kutuaminisha Watanzania kwamba leo hii wanapoamua kuwatuma wazee wao kutafuta kiini cha mizozo hii ya wabunge wa chama hicho, hawajui kwamba jinamizi la Richmond lililoiteka nyara vita ya ufisadi kabla ya kuipotosha na kuifanya ajenda ya kusaka madaraka ni kiini kikubwa kilichowafikisha hapa walipo leo?

  Ninao uhakika kwamba, iwapo malezi ya ndani ya CCM yasingekuwa ni yale ya zidumu fikra za mwenyekiti ambazo leo hii zimejipambanua kwa staili ya kumpigia makofi Kikwete kwa kila analofanya hata pale anapojikwaa na kuanguka, ripoti kamilifu ya kamati ya Mwinyi ingekuja na jibu mojawapo la kumnyoshea kidole Kikwete kiongozi wao mkuu na serikali yake, kwa kupwaya na kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.

  Siku zote nimelisema hili na leo ninalirudia tena kulisema kwamba, iwapo kungekuwa na dhamira moja safi na ya wazi miongoni mwa viongozi wakuu wa CCM na serikali yake, leo hii taifa lisingefikia hatua ya kutafuta dawa ya mizozo kama ile ya Richmond na Dowans kwa kiwango ambacho tumefikishwa leo. Kukosekana kwa dhamira njema kwa nchi hii na upeo mdogo wa viongozi wetu wa kuziona hatari zinazokuja mbele yao ni msingi mmoja mkubwa ambao leo hii umesababisha taifa liendelee kupiga maktaimu likishindwa kusonga mbele. Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, haya yote yanatokea na kujidhihirisha wakati taifa hili likiongozwa na Serikali ya Awamu ya Nne ya CCM ambayo Kikwete amethibitisha kwamba imechoka kuongoza, hivyo kumfanya pengine awe ndiye rais wa mwisho atakayetokana na chama hicho. Tusubiri tuyaone hayo yakitimia huko tuendako.
   
 2. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #2
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Mara nyingi sana napenda sana kusoma Habari za Mwandishi huyu maana ni mdadisi sana na mtu mwenye hulka za Kizalendo kweli kweli na asiye yumba ovyo ovyo kama wengine
   
 3. Kevo

  Kevo JF-Expert Member

  #3
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2008
  Messages: 1,332
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Kinachosikitisha sana ni Watanzania wachache sana wenye elimu kama hii ya udhaifu wa Jk na CCM na Serikali yake kwa ujumla.Hii elimu ingewafikia wale wa vijijini na wakaielewa nadhani tungeweza kutengeneza mfumo mpya wa Kiserikali ambao ni imara zaidi na ambao upo accountable kwa Wananchi wake bila kuweka maslahi ya Chama mbele!
   
 4. n

  nakasongola New Member

  #4
  Sep 24, 2009
  Joined: Aug 5, 2009
  Messages: 2
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Thank you very much for this informative and educative thread.
   
 5. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #5
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Kuna baadhi ya waandishi ambao wanamshambulia Kibanda, Hao nao wanatumiwa na watu wao na sisi tunawajua, Lakini Uwandishi wake kweli ni Makini sana na pia huwa anapenda kuibua maswali mengi sana katika makala zake
   
 6. B

  ByaseL JF-Expert Member

  #6
  Sep 24, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 2,223
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Kuna hadithi moja ya Kihaya inasema hivi: Fisi mmoja alifanikiwa kumeza tonge la nyama yenye moto. Nyama hiyo ilipo muunguza mdomoni fisi akaanza kulalamika. Fisi wenziye wakamwabia imeze haraka sana. Fisi akawajibu " siwezi maana ni ya moto!" kuona hivyo fisi wengine wakamshauri fisi mwenzao aiteme hiyo nyama na fisi huyo huyo akajibu " siwezi kuitema maana ni tamu!"

  Kama anavyosema Kibanda kuhusu JK, baadhi ya wasaidizi wake na rafiki zake ni kama nyama ya moto ambao hataki "kuwameza (kuwa nao beneti) au kuwatema (kuachana nao kabisa)! Matokeo yake wanamkwaza na kumfanya Rais kama mtu asiye na msimamo dhabiti.
   
  Last edited: Sep 24, 2009
 7. N

  Nyauba JF-Expert Member

  #7
  Sep 24, 2009
  Joined: Jul 10, 2008
  Messages: 1,098
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  mkuu hadithi tamuu sana na yenye sura nzuri ya uongozii ndani ya CCM.
   
 8. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #8
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Waandishi kama hawa ndio wanaweza kumsaidia Jk kuliko wale wa Kupamba mambo ili waonekane wazuri kwa watawale
   
Loading...