JK kaiweka tena nchi kwenye Auto Pilot?? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK kaiweka tena nchi kwenye Auto Pilot??

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Consultant, Jan 15, 2011.

 1. Consultant

  Consultant JF-Expert Member

  #1
  Jan 15, 2011
  Joined: Jun 15, 2008
  Messages: 5,780
  Likes Received: 6,265
  Trophy Points: 280
  Kikwete kaiweka tena nchi kwenye auto pilot?

  CHANZO: Johnson Mwambo, Raia Mwema – January 12th

  KWA kuwa Januari haijakatika, naamini sijachelewa kuwatakia wasomaji wangu heri ya mwaka mpya na kuwapa pole kwa tatizo la mgao wa umeme linalotuumiza sote. Nafarijika kuwafahamisha nyote kwamba nilirejea Dar, wiki iliyopita, baada ya likizo ya mwezi mmoja kijijini.

  Niitumie pia fursa hii kuwashukuru baadhi ya wasomaji walioendelea kuwasiliana nami kwa njia ya simu nikiwa kijijini; wakinipasha hili na lile jipya katika kipindi hiki kigumu ambacho nchi yetu inapitia.
  Nilichojifunza ni kwamba ombwe la uongozi jasiri na imara ambalo tunalishuhudia mijini, limesambaa hadi vijijini. Angalau katika wilaya yangu ya Same ilikuwa ni dhahiri kwangu kwamba viongozi – kuanzia DC, mbunge, OCD nk kila mmoja anapuyanga vyake!

  Labda nitoe mfano wa mbunge wangu Anne Kilango (CCM). Huyu alinishangaza kwa kumjia juu OCD kwa kutoa kibali kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA wa jimbo hilo, Anna Kaboyoka kufanya kikao cha ndani cha chama chake kijijini Ndungu.

  Ilikuwa hivi: Siku chache kabla ya Krismas, Kaboyoka alifika kijijini na kuitisha kikao cha ndani cha CHADEMA baada ya kunyimwa kibali cha kufanya mkutano wa hadhara. Katika kikao hicho aliwaeleza viongozi wa CHADEMA kwamba anakusudia kutekeleza baadhi ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni licha kwamba hakushinda ubunge.

  Aliwaelekeza viongozi wa chama hicho washirikiane na uongozi wa kijiji kuunda vikundi mbalimbali vya vijana ambavyo angevipatia matrekta madogo ya power tiller ili yawasaidie katika kilimo na katika shughuli nyingine za uzalishaji.

  Kwa kijiji ambacho umaskini umekithiri na mitaji imeota mbawa, hizo zilikuwa ni habari nzuri kwa vijana. Hata hivyo, yaelekea habari hizo hazikumfurahisha Anne Kilango kwani, siku nne baadaye, alifunga safari ya haraka kuja kijijini akiwa na jazba. Naye pia aliitisha kikao cha viongozi wa CCM wa kijiji ambapo si tu aliiponda hatua ya Kaboyoka ya kuwasaidia vijana power tiller; lakini pia kwenye mkutano wa hadhara aliwashawishi wanakijiji kutochangamkia msaada huo; huku akitamba kwamba badala yake atawaanzishia saccos!

  Hatua hiyo ya Anne Kilango ilinishangaza kuliko mambo mengine yote niliyoyashuhudia kijijini. Na nikiri kwamba nilijitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuwapa elimu ya uraia baadhi ya wanavijiji waliokuwa tayari kunisikiliza kwenye mazungumzo yasiyo rasmi mitaani.
  Na ujumbe wangu kwao ulikuwa ni kwamba hakuna kiongozi yeyote duniani mwenye haki ya kumchagulia raia apokee msaada kwa nani; na hivyo katika hilo la power tiller wanapaswa kumpuuza mbunge wao.

  Niliwahimiza wajenge utamaduni wa kujisaidia wenyewe na wasitegemee misaada kujikomboa; lakini nikawasisitiza kwamba misaada inapopatikana wasiikatae eti tu kwa vile inatolewa na mtu ambaye ni wa CHADEMA au wa CCM. Waikatae tu kama inaambatana na masharti magumu lakini si kwa vigezo vya mitazamo ya vyama vya siasa. Niliwaambia wamwache Anna Kaboyoka amwage power tillers zake kijijini na wamwache pia Anne Kilango amwage saccos zake kijijini! Lojiki ni kwamba wawili hao hawana sababu kugombea fito ilhali wote wanajenga kibanda hicho hicho kimoja.

  Lile la Anne Kilango kumjia juu OCD nalo pia halikunifurahisha. Habari za uhakika kutoka wilayani zinasema kwamba mama huyo alimjia juu OCD kwa kumruhusu aliyekuwa mpinzani wake huyo kufanya kikao cha ndani cha CHADEMA. Niliarifiwa kwamba OCD alielekezwa kutotoa tena vibali kwa Kaboyoka kufanya vikao si vya hadhara tu; bali hata vya ndani, na kwamba eti hayo ndiyo maelekezo ya CCM na Serikali yake nchi nzima! Ni kweli hiyo? Na kama ni kweli; haki iwapi na demokrasia i wapi?

  Kwa sababu ya ombwe hili la uongozi bora lililopo hivi sasa nchini, pengine OCD yule, mpaka leo, yupo njia panda na kachanganyikiwa. Nadhani mpaka sasa anajiuliza iwapo asalimu amri kwa ukali wa mbunge huyo, na hivyo kutoipa tena CHADEMA vibali vya kufanya hata vikao vya ndani au aheshimu kanuni za kazi yake zinavyomtuma.Vyovyote vile; hivyo ndivyo ninavyomaanisha ninaposema kwamba ombwe la uongozi bora nchini ni dhahiri hata ngazi za vijijini ambako kila kiongozi anapuyanga kivyake kwa mwelekeo anaoujua yeye mwenyewe.

  Ndugu zangu, hayo ndiyo ya kijijini; lakini nimerejea mjini na kukutana na ombwe hilo hilo la uongozi bora. Ukitafakari suala la Katiba mpya ambapo kila kiongozi anajisemea vyake, ukitafakari suala la malipo ya mabilioni kwa Dowans ambapo pia mawaziri wanatofautiana, ukitafakari suala la mgao wa umeme ambapo Rais Kikwete amekaa kimya; huku wananchi wakiteseka siku hadi siku, na hata ukiyatafakari mauaji ya Arusha kwenye maandamano ya CHADEMA ambapo kauli za viongozi wa serikali zinatofautiana, utakubaliana nami kwamba ombwe la uongozi bora ni kubwa kuliko wengi wetu tunavyodhania.

  Kwa mtazamo wangu, ni kama vile Rais Kikwete ameiweka tena serikali yake katika auto pilot! Rubani wa ndege kubwa za masafa marefu huiweka ndege kwenye mitambo ya kujiendesha yenyewe (automatic pilot) ili yeye na wasaidizi wake wapate kupumzika kidogo.
  Yaelekea baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 Rais Kikwete amechoka mno, na sasa ameamua kuweka serikali yake kwenye auto pilot ili apumzike kidogo! Tofauti ni kwamba rubani huiweka ndege kwenye auto pilot baada tu ya kuipa maelekezo (settings) ya kimo cha kuruka kutoka usawa wa bahari (altitudes), kasi, mwelekeo nk, lakini Rais Kikwete yeye ameweka auto pilot bila kwanza kuipa ndege (serikali) maelekezo na mwelekeo!

  Ndiyo maana tunashuhudia (hivi sasa) wasaidizi wake wakilumbana wenyewe kwa wenyewe na kutoa kauli zinazotofautiana katika masuala nyeti yanayoligusa taifa; huku sauti ya Rais Kikwete ikiwa haisikiki kabisa kuweka msimamo katika masuala hayo.
  Chukulia kwa mfano suala hili la malipo ya Dowans na mgao wa umeme. Sauti ya Kikwete haijasikika kwa kishindo ikiweka msimamo. Sauti tunayoisikia ni ya mawaziri wake kulumbana wenyewe kwa wenyewe.

  Wakati Waziri wa Nishati aliposema kwamba deni la Sh. bilioni 94 za Dowans lazima lilipwe kufuatia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Kibiashara , wengi tuliamini kuwa huo ndio uamuzi wa Baraza la Mawaziri. Tuliamini hivyo hadi Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alipoibuka na kauli tofauti.
  Sitta aliibuka hivi karibuni na kusema kwamba atapinga Dowans kulipwa mabilioni hayo hadi ndani ya kikao cha kebineti kwa kuwa dili nzima imegubikwa na ufisadi mtupu. Hapo ndipo wengi wetu tulipozinduka na kutambua kwamba kumbe uamuzi wa kuwalipa Dowans si wa kebineti, na kwamba kumbe suala hilo la malipo ya Dowans bado halijajadiliwa ndani ya kebineti!

  Kama hivyo ndivyo, kina Ngeleja, Pinda, Werema nk walipata wapi ujasiri wa kuutangazia umma uhalali wa Dowans kulipwa mabilioni hayo? Waliupata ujasiri huo kutoka kwa Rais Kikwete mwenyewe? Je, Rais Kikwete naye alifikia uamuzi huo bila kushirikisha kebineti yake, na je; huo ndio utawala bora?

  Chukulia mfano mwingine wa tatizo la mgao wa umme ambalo linamuumiza kila Mtanzania. Mwanzoni Ngeleja aliahidi umma kwamba tatizo hilo lingemalizwa haraka, na kwamba lilisababishwa na kuharibika kwa mitambo. Siku zikawa wiki, wiki zikawa mwezi na mwezi ukawa miezi, na bado tatizo lipo pale pale. Kilichobadilika ni ‘hadithi’ ya chanzo chake. Sasa tunaambiwa kuwa si mitambo tena bali eti maji yamepungua kwenye mabwawa ya kuzalishia umeme!

  Watanzania hawajui ni kiongozi gani tena wa kumwamini linapokuja suala hilo la mgao wa umeme ambao unazidi kuwafanya Watanzania wengi kuwa masikini. Imani inapotea zaidi hasa Rais mwenyewe anapokuwa bubu juu ya suala hilo bila kuwafahamisha wananchi nini kinaendelea na lini tatizo hilo litamalizwa.

  Nilidhani tatizo hilo la mgao wa umeme lingechukuliwa kuwa ni dharura inayohitaji vikao vya mara kwa mara vya dharura vya kebineti. Nilidhani ni crisis inayohitaji ufuatiliaji shupavu na wa karibu wa Rais mwenyewe; hasa kwa sababu athari zake kiuchumi ni kubwa mno.
  Hivi rais aliyeahidi kujenga fly overs Dar es Salaam na miradi mingine kadhaa mikubwa nchini, anashindwaje kutatua mama wa kero zote kubwa nchini; yaani ukosefu wa maji na umeme? Kama maji na umeme tu vinatushinda miaka 50 baada ya Uhuru, tunapata wapi ujasiri wa kuzungumzia miradi hiyo mikubwa inayohitaji mabilioni ya pesa?

  Tukija kwenye mauaji ya Arusha yaliyofanywa na polisi wakati wa maandamano ya CHADEMA, ububu wa Rais Kikwete ni huo huo. Mpaka sasa hatujasikia sauti yake ikilizungumzia kwa kishindo suala hilo la kusikitisha lililoitia doa nchi yetu.

  Tukio pekee ambapo alilizungumzia suala hilo kwa kupita ni wakati wa tafrija yake ya wiki iliyopita aliyowaandalia mabalozi ambapo alisema eti mauaji hayo ya Arusha yalitokea kwa bahati mbaya, na kwamba hayatatokea tena. Kama kweli anataka tumwamini kuwa ilikuwa ni bahati mbaya, mbona mpaka sasa hajawaomba radhi Watanzania (na hasa wakazi wa Arusha) kwa mauaji hayo? Mbona hajakwenda Arusha kuwapa pole wafiwa kama kweli anaamini kuwa lilitokea kwa bahati mbaya?
  Na mbona kauli hiyo ya ‘bahati mbaya’ aliitoa kwa mabalozi na si kwa Watanzania, na tena bila kuonyesha huzuni au masikitiko yoyote? Hivi anawajibika kwa mabalozi au anawajibika kwa wananchi waliompigia kura?

  Vyovyote vile ni wachache wanaoiamini kauli hiyo ya JK ya “bahati mbaya” kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa huko nyuma aliwahi kuwatishia wafanyakazi matumizi ya vyombo vya dola endapo wangeshiriki mgomo ulioitishwa nchi nzima na TUCTA.

  Katika suala hilo la mauaji ya Arusha, tumeshuhudia pia wasaidizi wa Kikwete kila mmoja akipuyanga kivyake, na kila mmoja akieleza hadharani mtazamo wake tofauti. Kwa mfano, Rais anasema mauaji yalitokea kwa bahati mbaya lakini IGP wake anasema kuwa polisi walitekeleza wajibu wao!
  Tena IGP huyo anayasema hayo mbele ya waandishi wa habari bila kuonyesha majuto (remorse) yoyote. Sasa tumwamini Rais au tumwamini IGP? Isitoshe, Rais anapotofautiana na IGP wake katika suala nyeti kama hilo la mauaji, inaashiria nini?

  Kama vile hiyo haitoshi; wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha anasema kuwa tatizo hilo la Arusha ni la kisiasa, na hivyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa kwa CHADEMA na CCM kukaa mezani kulimaliza, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, anakejeli pendekezo hilo la waziri wa serikali ya chama chake.

  Makamba anakejeli pendekezo la waziri bila hata kuonyesha majuto au masikitiko kwa kilichotokea, na hakuna wa kumkemea! Wa kumkemea alipaswa kuwa Mwenyekiti wake wa Chama, Rais Kikwete lakini hatujasikia sauti yake; na badala yake tumesikia sauti ya kukemea ya Mzee Malecela ambaye, kwa sasa, wala hana wadhifa mkubwa kichama. Angalau yeye kanena na kuonyesha jinsi alivyochukizwa na tukio hilo la Arusha.

  Wakati hayo yakiendelea, Waziri anayesimamia Serikali za Mitaa, George Mkuchika na Waziri anayesimamia Utawala Bora, Mathias Chikawe ambao ndiyo hasa wanaoguswa na mgogoro huo unaotokana na kukiukwa kwa kanuni na taratibu za uchaguzi wa umeya, nao mpaka sasa wameamua kuwa bubu!

  Nihitimishe kwa kusema kwamba ni dhahiri tutaendelea kusikia kauli nyingi zaidi za mawaziri zinazokinzana kuhusu mauaji hayo ya Arusha, malipo ya Dowans, bei mpya ya umeme, kero ya mgao wa umeme, Katiba mpya nk, kwa sababu yaelekea Rais ameiweka serikali yake kwenye auto pilot!

  Tukumbuke tu kwamba hii si mara ya kwanza kwa JK kuiweka ndege kwenye AP. Aliwahi kufanya hivyo mwaka 2008 wakati serikali yake na nchi nzima ilipokumbwa na malumbano makubwa kuhusu ufisadi. Usiniulize safari hii ataiondoa ndege kwenye auto pilot baada ya siku ngapi; maana sina jibu, lakini nadhani ni baada ya uchovu wa uchaguzi wa Oktoba 31, 2010 kumwishia!

  Tafakari.
   
 2. M

  MabaoFungaFunga Member

  #2
  Jan 15, 2011
  Joined: Jan 13, 2011
  Messages: 22
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  :fish::pout:Kutokana na viongozi wa juu wa serikali ya wezi wakubwa wa nchi hii CCM ,imepelekea kuona nchi ikijiendesha yenyewe kama ndege iliyokuwa ktk aAUTOPILOT, wadau mnaonaje hapa ??????:clock::lever:
   
 3. G

  Gad ONEYA JF-Expert Member

  #3
  Jan 15, 2011
  Joined: Oct 26, 2010
  Messages: 2,641
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  let us take a ride in the flight!
   
 4. coscated

  coscated JF-Expert Member

  #4
  Jan 15, 2011
  Joined: Nov 17, 2010
  Messages: 1,498
  Likes Received: 250
  Trophy Points: 180
  yap! Uko sawa kabisa
   
Loading...