NILIJIPA fursa ya kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete wakati alipokuwa akilihutubia taifa kupitia kwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Dar es Salaam Ijumaa ya wiki iliyopita.
Iwe ni kwa mtazamo wake binafsi au kwa ushauri wa wengine, uamuzi wake wa kukutana na wazee na kutoa maelezo kuhusu masuala kadha wa kadha yanayolikabili taifa katika siku za hivi karibuni ulikuwa ni wa msingi.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba, aliamua kukutana na wazee na siyo wahariri na wakuu wa vyombo vya habari akijua kwa uhakika kuwa, mkutano huo ungempa fursa ya kutoa hotuba pasipo kukabiliana na changamoto za maswali mepesi na magumu.
Kwa kiongozi asiye na uwezo wa kujenga hoja thabiti na aliyekosa kipaji cha kujibu maswali kwa ufasaha na kwa weledi, uamuzi wake wa kuwahutubia wazee wa CCM na si wahariri ulikidhi matarajio yake binafsi na viongozi wenzake serikalini.
Ni dhahiri pia kwamba, kwa wadadisi wa mambo, utaratibu alioutumia wa kuzungumza na wazee unaweza kuchukuliwa kama mkakati mahususi wa kukwepa maswali na changamoto nyingine za kihoja kutoka kwa wanahabari wenye mitazamo na miguso tofauti.
Pasipo kujali ukinzani huo wa kimtazamo, bado uamuzi wa Kikwete kuona haja ya kuzungumzia masuala ya kitaifa ambayo yamekuwa yakigusa hisia na maisha ya wananchi moja kwa moja ulikuwa ni wa kimsingi.
Binafsi niliguswa kwa maana ya kufikirishwa na maelezo aliyoyatoa kuhusu namna anavyouona mchakato wa mabadiliko ya katiba na hatua ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wale wa NCCR Mageuzi kuupinga na pengine kuususa ndani ya bunge.
Ninakubaliana kwa asilimia 100 na uamuzi wa Rais Kikwete wa kutilia shaka kiwango cha ustahimilivu kilichoonyeshwa na wabunge wa vyama hivyo viwili vya upinzani hususan katika masuala yanayohitaji mijadala ya kidemokrasia na ushawishi wa nguvu ya hoja. Kama nilivyosema katika safu hii wiki iliyopita, nilisononeshwa na hatua ya wabunge wa CHADEMA na wale wa NCCR-Mageuzi kuamua kutoka nje ya Bunge wakipinga kile ambacho walikitafsiri kuwa ni hatua ya Spika wa Bunge kuwaburuza na kubeba maslahi ya chama chake.
Ni wazi kwamba, hatua ya wapinzani hao kususa ndiyo iliyompa fursa Rais Kikwete kupata ujasiri wa kuhoji kuhusu kiwango cha ustahimilivu na utayari wa wabunge wa CHADEMA kusikiliza mawazo au maoni ambayo hawakubaliani nayo.
Lakini pengine jambo baya zaidi katika hili ni kwamba, hatua ya wabunge hao wa upinzani kususa mjadala wa muswada wa mabadiliko ya katiba ulitoa fursa kwa wabunge wa CCM na wale wa vyama vya CUF waliobakia kuweka kando jambo la msingi na kuanza kuwapiga vijembe vikiwemo vya kipuuzi kabisa wabunge wa CHADEMA.
Kosa hilo la wabunge wa CHADEMA na wale wa NCCR likasababisha fursa adhimu ya kulijadili jambo nyeti linalogusa maisha ya Watanzania ambalo limepiganiwa kwa nguvu kubwa kwa miaka mingi ikapotea bure.
Kwa bahati mbaya kwa taifa, ushabiki wa wabunge wa CCM na wale wa CUF katika mjadala mzima wa muswada huo na kosa la msingi la wenzao wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi likazaa mhemuko wa aina ya kipekee katika jamii.
Nje ya Bunge CHADEMA huku kikitumia ushawishi wa kauli mbiu yake ya nguvu ya umma inayoungwa mkono na wananchi walio wengi, chama hicho kikajijengea uhalali zaidi na kuungwa mkono zaidi kinyume cha matarajio ya wengi.
Ni wazi kwamba, dalili za wazi za kupwaya kwa mjadala ndani ya Bunge na hatua ya wananchi walio wengi kuonekana wakibebwa kwa maana ya kuunga mkono msimamo na hoja za CHADEMA, ndiyo uliomsukuma Kikwete kuitisha mkutano wa wazee wa CCM Dar es Salaam na kukisuta chama hicho.
Sina uhakika iwapo, Rais Kikwete ambaye kwa walio wengi anaonekana kuwa kiongozi aliyepwaya na anayeongoza chama kilichozeeka na kuchakaa kifikra alifanikiwa kubadili upepo katika hotuba yake hiyo.
Pamoja na kuwapo kwa hali hiyo, ni dhahiri kwamba, hotuba hiyo ya Kikwete kama ilivyokuwa kwa vijembe vya wabunge waliojadili muswada wenyewe ilisababisha makada na wapenzi wa CCM na wale wa CUF kuziweka kando hoja za msingi na kurejea katika mstari wa kuvishabikia vyama vyao dhidi ya CHADEMA.
Kwa upande mwingine hotuba hiyo ya Kikwete kama ilivyokuwa katika muswada wenyewe ilishindwa kutoa majibu yanayojitosheleza kuhusu hoja za wabunge wa CHADEMA kuhusu suala zima linalogusa muungano.
Kwa staili na historia ile ile ya viongozi wa CCM kuogopa kuuzungumzia na kuutetea muungano katika muktadha wa utaifa wetu, Kikwete akaishia katika kusisitiza tu kwamba ajenda ya kuuvunja haikuwa moja ya masuala ya kuyajadili wakati wa mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba.
Ni wazi kwamba, katika mazingira ambayo muungano wenyewe una makovu na vidonda vya kuraruliwa na wanasiasa hao hao wakiwamo wale walio ndani ya CCM ambao baadhi yao wanaficha sura yao ndani ya hoja za CHADEMA kwa kuhofia kutimuliwa, majibu ya Kikwete yalikuwa mepesi sana katika kujibu hoja nzito zilizoibuliwa na wapinzani.
Kwa rais anayetokana na genge la mtandao ambao wakati likimpigania ili atwae uteuzi kwa mara ya kwanza ndani ya CCM mwaka 2005 lilifanya kazi kubwa kuzima na kuipiga vita hoja ya kuufanya urais wa muungano kuwa ni suala la kupokezana kati ya Watanganyika na Wazanzibari msimamo wake kuhusu muungano ni jambo linalotia shaka.
Upo uwezekano wa wazi na ushahidi wa kihistoria unaoonyesha kwamba, Kikwete kama walivyo wana CCM wenzake anaugua maradhi ya kuogopa kuonekana wasaliti wa ushawishi na hoja za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu muungano.
Hivi nani hasa hajui kwamba, makada wengi waandamizi wa CCM wanateswa na kivuli cha maneno ya Mwalimu Nyerere ambaye wakati fulani alipata kuuita mfumo wa muungano wa serikali mbili ni sera ya chama hicho tawala na yeyote anayehoji hilo anapaswa kufanya hivyo akiwa nje ya chama hicho.
Miaka 12 baada ya kifo cha Mwalimu, CCM ya Kikwete imeshindwa kuandaa semina elekezi, midahalo ya wazi au ya ndani ili kuujadili kwa kina mfumo huo wa muungano na kuyaweka katika mizani inayostahili maneno hayo ya Mwalimu.
Ni wazi kwamba, kwa mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kuchanganua mambo na kufahamu mifumo ya kitawala duniani kama alivyokuwa Mwalimu, kauli yake ya kuudhalilisha ‘utaifa wetu' hata kuufanya ni sera ya chama chake.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba hata baada ya viongozi wengi ndani ya CCM na wale walio serikalini kutambua kwamba kauli hii ya Baba wa Taifa ilichochea mijadala ya kuhoji kuhusu uhalali wa muungano, hakuna kiongozi yeyote anayetokana na chama hicho aliyewahi kuthubutu kulihoji achilia mbali kulisahihisha.
Jaribio pekee la CCM kujaribu kuligusa jambo hili lilifanywa miaka miwili au mitatu hivi ya mwisho ya serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi ambayo baada ya kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere ilitangaza kwamba sera ya chama hicho ilikuwa ni kutoka katika mfumo wa serikali mbili na kuelekea serikali moja.
Kwa bahati mbaya sana, kwa sababu ya hofu ya Wazanzibari wengi kuhofia kumezwa na mfumo huo, CCM kwa namna ambayo haijapata kuiweka sawa, iliachana na azma yake hiyo ya kuundwa kwa serikali moja ya muungano tangu wakati huo.
Udhaifu huo wa kiuongozi ndani ya chama hicho tawala ambao umeendelea kurithiwa ndiyo ambao ulisababisha takriban vyama vyote vya upinzani vijikute vikiingiza katika ilani zao kila nyakati za uchaguzi sera ya serikali tatu katika muungano.
Kwa namna ya kustaajabisha na inayoeleza unafiki wa kisiasa uliovuka mipaka kwa njia za siri na vificho vigogo wengi wa CCM wamekuwa wakikutana na viongozi wa vyama vya upinzani na kuwahimiza waendelee kushikilia msimamo wa kuhimiza mabadiliko ya mfumo wa muungano.
Wakati wakifanya hivyo ‘uvunguni mwa vitanda vyao' katika mikutano ya hadhara, viongozi hao wa CCM wamekuwa mabingwa wa kuwaponda kweli kweli wanasiasa wa upinzani wanaohoji kuhusu masuala ya muungano. Huu ni unafiki unaopaswa kukemewa hadharani.
Katika mazingira ya namna hii, Rais Kikwete aliyetokana na kundi la mtandao ambalo kwao Zanzibar ilikuwa ni shuruti la lazima la kisiasa alipaswa katika hotuba yake na pengine katika zama hizi awe ni kiongozi wa kwanza kuliweka hili bayana na kugoma kuingizwa katika mtego wa kuwashambulia na kuziponda hoja za CHADEMA na NCCR-Mageuzi pasipo kuzisikiliza.
Ni dhahiri pia kwamba, kwa Kikwete ambaye wapambe wake wa mwaka 2005 na mabingwa wa mkakati wake wa ushindi ndani ya CCM walifikia hatua ya kuwa tayari kuishawishi CHADEMA impokee na kuwa mgombea wake wa urais iwapo chama hicho tawala kingemtema, anapaswa kuwa ni mtu wa mwisho kuzidharau hoja za CHADEMA.
Lakini pamoja na makosa waliyofanya CHADEMA ndani ya Bunge katika kulipigania suala hili, uzito wa hoja zao kuhusu mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba na hofu yao katika mambo kadhaa yaliyokuwa katika muswada ule, ni sehemu ya mambo mengine muhimu yanayopaswa kumfanya Kikwete aone unyeti wa kuwapa sikio viongozi wa chama hicho cha upinzani ambao sasa wako tayari kukutana naye.
Mwisho. Kikwete na CHADEMA kwa pamoja na kila mmoja kwa sehemu yake, wanao wajibu wa kutambua kwamba, mzaha wa namna yoyote katika kulishughulikia suala hili ambao leo tunauona kuwa ni turufu ya ushindi wa kisiasa, huko tuendako itakuwa ni hukumu ya kihistoria. Hatuko tayari kusubiri majuto.
|
| |