Jk asujudia wahisani na siyo wapiga kura wake

PMNBuko

JF-Expert Member
Dec 27, 2010
967
154
"Jambo moja ambalo limekanganya au kukoroga vichwa vya wananchi katika kila kona ya nchi yetu tangu polisi wawaue waandamanaji kwa kuwapiga risasi mjini Arusha wiki iliyopita, ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya bila hata kutuma rambirambi kwa ndugu na jamaa wa marehemu hao.

Ukimya huo wa Rais umeibua maswali mengi, lakini swali moja lililo katika ndimi za wananchi wengi ni kwanini amekataa kuwasiliana na wananchi ambao ndio waliompa mamlaka ya urais, lakini badala yake amewasiliana na mabalozi wa nchi za nje waliopo hapa nchini, akawaomba radhi kwa yale yaliyotokea Arusha na kuwaahidi kuwa unyama huo wa polisi hautarudiwa tena.

Tafsiri ya harakaharaka ya kitendo hicho cha kushangaza kilichofanywa na kiongozi ambaye ni miezi miwili tu tangu wananchi wamrejeshe tena madarakani kama rais, ni kwamba pengine anaona kwamba hawahitaji tena wapiga kura, kwani hii ni ngwe yake ya mwisho katika urais. Kwake yeye na serikali yake mabalozi wa nchi wahisani ndio watu muhimu, kwani ndio wanawawakilisha wafadhili ambao fedha na misaada yao ndio hasa inaiendesha Serikali kwa kiwango kikubwa.

Vinginevyo ni kitendo tunachodhani kuwa hakiwezi kuelezeka kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Kwamba watu wanaoandamana kwa amani wanauawa kinyama kwa kupigwa risasi na polisi na kiongozi wa nchi anakaa kimya bila kukemea au hata kutoa pole kwa wafiwa, ni jambo lisilofikirika kwa namna yoyote ile.


Inatia uchungu kuona baadhi ya wanasiasa katika chama tawala wakishangilia na kuwapongeza polisi kwa kufanya kazi ‘nzuri' ya kuwadhibiti waandamanaji wanaodai walikiuka agizo la polisi la kutoandamana.
Tungetegemea mkuu wa nchi, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, aingilie kati kwa kukemea kauli hizo na hata kulaani baadhi ya matamko ya baadhi ya viongozi wa Chadema yaliyoashiria kuhatarisha amani.


Wakati wote huo tangu balaa hilo la Arusha litokee, limekuwapo ombwe kubwa la uongozi. Kila mtu ameachwa kusema atakalo, wakati wananchi wakipaza sauti kuomba rais wa nchi ajitokeze na kuchukua hatua kwa kutafuta suluhu ya matatizo yaliyozaa mgogoro huo kati ya Chadema na CCM katika Jiji la Arusha.


Badala ya kufanya hivyo, watawala walikata mawasiliano na wananchi, badala yake wakaanza kuhangaika kutafuta njia za kuwaweka sawa wafadhili ili wasisitishe misaada kwa Serikali kwa kukiuka haki za binadamu. Ni baada ya wafadhili kuibana Serikali na kutaka maelezo kuhusu mauaji hayo ya polisi na kuhoji ukimya wa Serikali ya Rais Kikwete, ndipo viongozi wakaahidi kuwa Serikali ingetoa tamko hivi karibuni.


Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernald Membe juzi naye aliwaomba radhi mabalozi wa nchi wahisani na kukiri kwamba polisi walikurupuka na kuua watu kikatili na kuyavuruga maandamano ya amani ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakishinikiza kurudiwa kwa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Arusha.

Membe alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya kubanwa na mabalozi hao waliotaka kujua sababu za polisi kuwafyatulia risasi za moto wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaandamana kwa amani. Mabalozi hao walimwambia Membe kuwa Tanzania ilikuwa mfano wa nchi yenye amani katika Afrika, lakini mauaji ya Arusha yameipa sura nyingine, kwani sio tena kisiwa cha amani duniani."


Source: Mwananchi, Jumatano 12th January 2011



My opinion: Kwa kuwa JK anaona ni heri kutoa ufafanuzi na kuwaomba radhi mabalozi wa nchi wahisani, badala ya kufanya hivyo kwa wananchi waliompa kiburi alichonacho, kwanini tusiunge Mkono Maandamano nchi nzima ili akimbie Ikulu??? Naomba Mawazo yenu - Great Thinkers!!
 
Back
Top Bottom