Jifunze Kujieleza, Epuka Migogoro

Jifunze Kujieleza, Epuka Migogoro

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
1,125
Reaction score
879
Unaweza kuwa sahihi, unaongea jambo la kweli lakini usipojifunza namna ya kujieleza unaweza kuishia kueleweka vibaya, ukaumiza hisia za mwenzako na ukazalisha mgogoro usio wa lazima. Hapa nina mifano michache ya kuzungumza kwa namna inayopunguza migongano katika lugha:

✳️ Tafsiri, mara nyingi, ndizo zinazogombanisha watu. Ukitafsiri kilichofanyika, aghalabu unazusha ugomvi. “Umenikera” “Umenipuuza”, “Umeniumiza.”
Unaweza kusema hisia zako kuhusu jambo lililotokea bila kutanguliza tafsiri.
“Nimekasirika,” “Nimehuzunika,” “Nimeumia kusubiri muda mrefu” badala “Hujali muda wangu,” “Sijui umenionaje kuniweka muda wote.”

✳️ Ukikosa msamiati wa kusema hisia zako, badala ya kulaumu, bado unaweza kutafuta namna ya kusema hitaji lako kwa lugha chanya:
“Nilitamani sana tupate muda wa kuwa pamoja tuzungumze.”
“Nilitamani bidii yangu itambuliwe.”
Kumbuka muhimu ni hitaji hilo ulilonalo sio lawama na kumfanya mtu ajione mkosefu.

✳️ Unapozungumzia kosa alilofanya mwenzako, unaweza kukwepa kutumia lugha ya lawama, malalamiko na kumuwekea maneno madomoni. Ukisema ulichoona na kusikia bila lawama unakaribisha mahusiano badala ya ugomvi.
“Tulikubaliana turudi mapema tule pamoja. Jana umerudi saa 6 usiku.”
“Umezungumza na simu kwa dakika 40. Tulikubaliana tukutane hapa kwa mazungumzo.”

✳️ Katika mazingira ambayo mwenzako tayari anakulaumu, anakushambulia, kuliko kujitetea na kumgeuzia kibao bado, unaweza kufanya jitihada za kutambua hitaji lake. Huenda amekasirika na anahitaji tu uelewe kilichomkasirisha na mambo yanaisha.
“Unahitaji nirudi mapema nyumbani.”
“Hukupenda nilivyokujibu mbele za watu.”
Wakati mwingine hata kurudia kile tu anachokisema kwa maneno yako humfanya mtu aone unamuelewa na mapambano yanaishia hapo.

Lugha hii isiyotafuta ugomvi haikuhakikishii amani na mtu lakini angalau inakuwekea mazingira ya kutuma ujumbe kuwa una mtazamo chanya na mtu, si mgomvi, si mbabe, hujihesabii haki, humbebeshi mwenzako lawama na una staha kwa hisia za mwenzako.
 
Agiza castle lager baridi na kitimoto kilo popote ulipo mkuu
 
Back
Top Bottom