JICHO LA MWEWE: Yanga ya kweli inahitajika zaidi Kigamboni kuliko Jangwani

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
Mara ya ngapi umesikia jengo la Yanga linakarabatiwa? Mara ya mwisho ilikuwa wiki iliyopita. Bosi wa timu, Mzee Mshindo Msolla aliwaita waandishi wa habari akatangaza ukarabati wa jengo hilo. Kila chumba kitagharimu shilingi milioni sita za Kitanzania.

Hapo miaka ya katikati Yanga waliwahi kukarabati hilo jengo. Hapo miaka ya nyuma Yanga pia waliwahi kukarabati jengo lao. Zamani pia walishawahi kulikarabati mara nyingi. Kila uongozi huwa unajaribu kupata umaarufu kwa kukarabati jengo hilo. Sikuwepo katika mkutano wa Bosi Msolla na waandishi wa habari. Kama ningekuwepo ningemuuliza maswali haya muhimu. Yanga wanakarabati jengo kwa sababu gani? Litazamike vizuri kwa wapita njia? Au ili wachezaji waweke makazi yao hapo? Kwa maana ya kwamba Yanga ihame kutoka katika kambi yao nzuri ya Kigamboni na kurudi hapo?

Majibu yake ni magumu lakini kitu muhimu cha kwanza kwa watu waliojenga jengo hilo kilikuwa kuhakikisha wachezaji wanapata usingizi katika jengo na kisha asubuhi na jioni wanashuka Uwanja wa Kaunda kwa ajili ya kufanya mazoezi yao. Kwa nyakati zile lengo lilitimia na Yanga ilikuwa moja kati ya klabu chache ukanda huu kumiliki uwanja huu.

Kwa jambo hili tu rafiki zao Simba walikuwa wanawaonea donge Yanga. Simba walikuwa wanahaha bila ya uwanja. Leo wako hapa, kesho pale, keshokutwa kwingineko. Yanga walikuwa wanashuka vyumbani kwenda kufanya mazoezi chini. Katika uwanja ambao ulikuwa ni mali yao binafsi.

Miaka imesogea, dunia imebadilika, maisha yamebadilika, leo Simba wana makazi yao Bunju, Yanga wanaishi Kigamboni katika makazi mazuri zaidi kuliko Jangwani. Katika hali halisi ulitazamia Yanga watamani kuishi katika maisha mazuri zaidi kuliko yale waliyoishi Jangwani lakini kumbe bado wana ndoto fulani nzuri kuhusu Jangwani.

Hapa ndipo linapoibuka swali. Wanataka kurudisha wachezaji mastaa Jangwani au wanataka kulipendezesha jengo kwa ajili ya wapitanjia? Hauwezi kujua, inawezekana katika wapitanjia hao wakajitokeza wawekezaji kwa lengo tofauti. Inawezekana.

Vyovyote ilivyo, kwa sasa mastaa wa Yanga akina Saido Ntibanzokonza, Fiston, Calinhos, Farid Mussa, Tuisila Kisinda, Tanombe Mukoko na wengineo hawawezi kuishi Jangwani. Akina Kenneth Mkapa, Edibily Lunyamila, Sunday Manara na wengineo waliweza kwa sababu zama ziliwaruhusu. Hawa wa leo hawawezi.

Yanga inahitaji kambi yenye vyumba vyenye hadhi hadhi, viwanja zaidi ya vitatu vya mazoezi, hosteli za kisasa, bwawa kubwa la kuogelea, gym, bustani kubwa ya mapumziko kwa wachezaji, na mengineyo mengi. Hauwezi kuyapata haya Jangwani kwa sasa.

Kinachonifurahisha katika hili ninalowaza ni kwamba majuzi tu Yanga walikuwa bize kutangaza tenda kwa kampuni inayotaka kufanya mambo kama haya kule Kigamboni. Wana eneo kubwa walipewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Dar es salaam, Paul Makonda.

Yanga ninayoiwaza inabidi iishi Kigamboni katika lile eneo walilopewa na Makonda. Yanga ninayoiwaza inapaswa kuzingatia uwepo wa eneo kubwa kama ambalo Azam FC wanamiliki pale Chamazi na sio kila siku kukurupushana na ukarabati wa jengo lao chakavu.

Yanga ninayoiwaza inapaswa kuwa na viwanja vinne kwa pamoja ambavyo vitajumuisha timu ya wakubwa, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, chini ya umri wa miaka 15, watoto pamoja na ile timu yao ya wanawake ambayo majuzi ilicheza na Simba pale uwanja wa zamani wa Taifa na kufungwa kwa bahati mbaya. Ndiyo, tuseme ni bahati mbaya kwa sababu wana timu nzuri.

Yanga ya Kigamboni ni sahihi zaidi. Pale Jangwani panapaswa kuwa na mradi mpya usiohusisha sana masuala ya timu. Tatizo nadhani bado kuna ndoto ya kurudisha wachezaji Jangwani. Kama si hivyo basi nadhani kuna ndoto ya kupendezesha wapitanjia. Yanga wangeweza kuingia ubia na kampuni kubwa kisha likajengwa jengo kubwa la kibiashara pale Jangwani na Uwanja wa Kaunda ungekarabatiwa kuwa sehemu ya maegesho ya magari tu. Najua watu wanapenda kuona Jangwani panabakia kuwa sehemu ya historia ya klabu lakini ukweli ni kwamba kuna namna nyingine ya kubakisha historia.

Kuna viwanja maarufu, au makazi maarufu yaliwahi kuvunjwa huko nyuma. Arsenal waliwahi kuivunja Highbury, West Ham waliwahi kuivunja Upton Park, Tottenham waliivunja White Hart Lane na hata Waingereza kwa ujumla waliwahi kuivunja Wembley.

Kitu cha msingi katika ndoto zangu ni kuona jengo jipya zuri na la kisasa ambalo linasimama pale likiitwa YOUNG AFRICANS BUILDING. Yanga wanaweza kuwa na ofisi zao hapo. Historia itaendelea kusomeka hapo lakini ukweli ni kwamba kwa makazi ya wachezaji pale haiwezekani. Hauwezi kuwalaza wachezaji wa kisasa pale wakati chini kuna watu wamekuja kupiga soga, wanakunywa kahawa, wanacheza bao, wamekuja klabuni bila kuitwa, na wanafanya vurugu za hapa na pale. Sidhani kama ni sawa sana.

Najaribu kufikiria Simba haikai hotelini na badala yake akina Chama, Miquissone, Morrison na wengineo wanalala Msimbazi na kuamka pale kwa ajili ya kwenda mazoezini. Kwa vurugu zile za Msimbazi wangeweza wapi

Eddo Kumwembe
 
Back
Top Bottom