Jiandae na hili katika Uongozi wako Ili usije ukakimbia nafasi yako

Samson Ernest

JF-Expert Member
Aug 28, 2014
404
651
"Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?" Kut 17:3 SUV.

Musa alikutana na mengi katika uongozi wake wa kuwatoa Waisraeli Misri, tunaona hata walivyofika bahari ya Shamu na wakaona jeshi la Misri likiwajia kwa kasi nyuma yao, walimgeukia Musa na kuanza kumlalamikia.

Tunaona walipofika mahali wakakosa chakula walikumbuka masufuria ya nyama Misri, wakasahau kabisa yale mateso waliyokuwa wanayapata, wakaona ni heri kula nyama kwenye utumwa kuliko kufa njaa jangwani, bila kukumbuka aliyewatoa Misri anaweza kuwapa chakula.

Unaweza kujiuliza mwanadamu huwa anataka nini haswa? Jua likiwaka atalalamika, baridi ikiingia atalalamika, mvua zikinyesha atalalamika, na mvua zikiacha kunyesha atalalamika, wakati mwingine hatueleweki tunataka nini.

Miili yetu inakinai haraka na kuchoka inasahau tuliomba au tulihitaji nini, kitu kikituzidi kidogo tu huwa ni wepesi wa kulalamika, hasa tunapolitazama jambo kwa mtazamo wetu na sio wa Kimungu. Wakati Mungu anatuwazia hatua nyingine nzuri mbele, sisi tunaona bora tungebakia hivyo tulivyo, jambo la kushangaza kabisa hili.

Ukiwa kiongozi wa watu na hupendi kulalamikiwa, nikushauri ubadilishe huo mtazamo, moja ya kitu utakachokutana nacho kwenye uongozi wako ni kunung'unikiwa au kulalamikiwa na watu unaowaongoza. Hili weka akilini mwako na jifunze namna kukabiliana na hali hii itakapokukuta, maana lazima ukutane nayo kwenye uongozi wako.

Kiongozi unapaswa kuwa karibu mno na Mungu wako, na mambo yanapokuwa mangumu uhakikishe unajua sehemu yako ya kukimbilia ni ipi? Ambayo moja kwa moja itakuwa kwa Mungu wako aliyewekuweka kwenye nafasi hiyo, yeye atakupa njia ya kupita au akili ya kufanya.

Hili tunajifunza kwa Musa, baada ya kuona ananung'unikiwa na Waisraeli, alienda mbele za Mungu kumuuliza afanye nini juu ya changamoto iliyokuwepo wakati huo, badala ya kiongozi kubaki kuwalaumu na kuwa kundi la wanaolalamika, unapaswa kumuuliza Mungu cha kufanya.

"Musa akamlilia BWANA, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe", Kut 17:4 SUV.

Mambo mengine sio kana kwamba wewe umeyasababisha, kama suala la kukosa maji, Musa halikulisababisha hilo yeye, lilikuwa nje kabisa ya uwezo wake, lakini kwa sababu alikuwa ni kiongozi wao walianza kumnung'unikia yeye.

Hakuna kitu kinaumiza moyo kama mtu kukulalamikia au kukulaumu, wakati mwingine kwa mambo ambayo wewe hukusababisha, hupaswi kukasirika tu, unapaswa kuwa na suluhisho la hilo tatizo, bila kuonyesha njia ya kutoka kwenye hilo tatizo utaendelea kulaumiwa.

Huwezi kukwepa kulalamikiwa au kunung'unikiwa na wale unaowaongoza, hili utakutana nalo sana kwenye uongozi wako, haijalishi unaongoza watu wengi au wachache, ujue utakutana na malalamiko ambayo unaweza kushangaa na kusema "na hili wa kulaumiwa ni mimi?" Ndio ni wewe maana ni kiongozi.

Umekuwa kiongozi sasa hivi au utakuwa kiongozi baadaye? Jiandae na haya, sio tu kulaumiwa, utasemwa vibaya kwa mambo ambayo hukustahili kabisa kusemwa, utapewa majina mabaya, utaonekana huna akili, utaonekana huelewi chochote. Tena maneno haya utayasikia kwa watu wako wa karibu, ambao walipaswa kuwa sehemu ya kukutia moyo, wanakuwa sehemu ya kukushambulia na kukusema vibaya.

Uwe mvumilivu katika uongozi wako, jua ni kawaida ya mwanadamu kulalamika, jua husahau wema wote uliofanyika kwake, mtazame Yesu katika uongozi wako, kimbilio lako kuu liwe kwake, yapo magumu mengi utakutana katika uongozi wako. Usije ukachoka na kuacha uongozi, Mungu alikuweka hapo kwa kusudi maalumu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081
 
Hakuna dini yeyote inayoruhusu kuuza mali za watu bila ridhaa.Acha kutumia vifungu vya dini tofauti na inavyotakiwa.Kwa hiyo wewe unaona ni sawa hao watu kupewa mkataba usio na kikomo?Wewe ni mchumia tumbo na ndio maana umeweka namba hapo chini .Kijana tumia akili kufikiri usitumie tumbo.Afrika itabaki hivi hivi kwa ajili ya watu kama nyinyi
 
Hakuna dini yeyote inayoruhusu kuuza mali za watu bila ridhaa.Acha kutumia vifungu vya dini tofauti na inavyotakiwa.Kwa hiyo wewe unaona ni sawa hao watu kupewa mkataba usio na kikomo?Wewe ni mchumia tumbo na ndio maana umeweka namba hapo chini .Kijana tumia akili kufikiri usitumie tumbo.Afrika itabaki hivi hivi kwa ajili ya watu kama nyinyi
Suala la mkataba limeingiaje kwenye Makala hii? Tumia akili kabla ya kukomenti.
 
Back
Top Bottom