Wakati kukiwa na taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari kuwa akaunti ya escrow iliyofunguliwa benki kuu ( BOT ), kwa mujibu wa makubaliano yaliyofanyika julai 5, 2006, zilikuwa sh bilioni 306.6, kabla kutolewa kwa fedha hizo mwaka 2013, taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ( CAG ), imethibitisha sio kweli.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CAG , ambayo Rais Kikwete ameagiza iwekwe hadharani, ili Watanzania waisome na kuielewa, katika ukurasa wa 40 mpaka 42 imebainika kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa katika akaunti hiyo, kilikuwa Sh bilioni 182.7. Ambapo TANESCO iliweka kiasi cha sh bilioni 142 na wizara iliweka sh bilioni 40.7, taarifa hiyo ilieleza.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kama akaunti hiyo ingekuwa na sh bilioni 306.6 basi TANESCO wangepaswa kuweka kiasi cha sh bilioni 123.9 zaidi ya fedha zilizowekwa katika akaunti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, mpaka sasa IPTL inaidai TANESCO sh bilioni 123, ambazo ni nyingi kuliko kodi ambayo TRA inaidai IPTL, ya sh bilioni 26.9.