Jeshi la Polisi sasa lijisafishe dhidi ya vitendo vya rushwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jeshi la Polisi sasa lijisafishe dhidi ya vitendo vya rushwa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Jun 7, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 7, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Taarifa kadhaa za tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi mbalimbali nchini zinabainisha kwamba Jeshi la Polisi nchini ni kinara wa vitendo vya rushwa.


  Moja ya ripoti za utafiti ni uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa mwaka 2011na kuzinduliwa Mei 28, mwaka huu ilieleza kuwa Polisi nchini ni taasisi ya serikali inayoongoza kwa rushwa.


  Utafiti mwingine uliofanywa hivi karibuni na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) katika Jeshi hilo umegundua maeneo yaliyokithiri kwa vitendo vya upokeaji wa rushwa na ukiukwaji wa maadili kuwa ni eneo la mapokezi katika vituo vya polisi, Idara ya Upelelezi na Kikosi cha Usalama wa Barabarani.


  Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo, alipokuwa akifungua mafunzo ya wakuu wa upelelezi wa wilaya nchini.


  Kivuyo alisema katika taarifa hiyo mambo ambayo yalianishwa ni pamoja na mapokezi duni kwa wateja, ucheleweshaji wa upelelezi wa mashauri ya jinai, ubambikizaji wa kesi, wizi wa mali za mahabusu, kuombwa rushwa ili kupatiwa huduma wanayohitaji wananchi wanapofika katika vituo vya polisi.


  Kivuyo alisema kutokana na matokeo ya utafiti huo, DFID limekubali kufadhili mafunzo kwa jeshi hilo ili kukabiliana na vitendo hivyo.


  Alisema kuwa ufadhili huo umefuatia matokeo ya utafiti uliofanywa na mtafiti kutoka Uingereza na ambao umeonyesha kuwa jeshi hilo linalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa na kuwepo ukiukwaji wa maadili vinavyosababisha kuwepo kwa taswira hasi katika vituo vya polisi na maeneo yote ambayo Jeshi hilo linatoa huduma.


  Matokeo ya utafiti huo wa taasisi hiyo ya Uingereza kwamba rushwa imekithiri ndani ya Jeshi la Polisi nchini sio jambo jipya kwa kuwa tafiti nyingi zinazofanyika nchini mara kwa mara nchini kuhusu utawala bora zimekuwa zikibainisha kuwa Jeshi hilo ni moja ya taasisi za serikali ambazo zinaongoza kwa rushwa.


  Mbali na taarifa za utafiti zinazobainisha uwepo wa vitendo vya rusha katika Jeshi la Polisi, pia yamekuwepo malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi kuhusu kudaiwa rushwa na askari wa Jeshi hilo.


  Malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi ni kubambikiwa kesi na polisi pale wanaposhindwa kutoa rushwa na kudaiwa rushwa kabla ya kupewa huduma.


  Wananchi pia wanawalalamikia askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwamba wanadai na kupokea rushwa kutoka kwa wamiliki wa magari, madereva na makondakta wa mabasi ya abiria.


  Malalamiko hayo dhidi ya polisi yamekuwa yakisababisha wananchi kukosa imani kwa Jeshi hilo kiasi kwamba hali hiyo katika miaka ya karibuni imewalazimisha wananchi kuchukua sheria mikononi kwa mfano, kuwashambulia watuhimiwa na kuwaua kikatili.


  Aidha, yako matukio mengi ya wananchi kuvamia vituo vya polisi kwa lengo la kuwadhuru watuhumiwa kutokana na kuamini kuwa polisi watawaachia huru bila kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.


  Pia baadhi ya wananchi wamekuwa wakivamia vituo vya polisi kwa lengo la kuwatoa watu ambao wanaamini kuwa wamekamatwa na polisi kwa uonevu.


  Ingawa Jeshi la Polisi halikubainisha sababu za kuipa DFID kazi ya kufanya utafiti kubainisha ukubwa wa tatizo la rushwa ndani ya taasisi hiyo muhimu kwa taifa, lakini sisi hatukuona umuhimu wa kufanyika kwa utafiti huo kwa kuwa malalamiko ya umma dhidi yake ni ya siku nyingi na yanafahamika kwa kila Mtanzania.


  Kama uamuzi huo umefanywa kwa nia ya dhati ya kutaka kupanua wigo wa taarifa na takwimu kabla ya kuchukua hatua, basi Jeshi hilo litakuwa limepanga mkakati mzuri wa kupambana na tatizo hilo.


  Hatua ya DFID ya kuamua kufadhili mafunzo kwa polisi baada ya kubaini tatizo kubwa la rushwa ni muhimu sana, lakini pia Jeshi la polisi linatakiwa kubuni mikakati zaidi ya kukabiliana na rushwa ili kurejesha imani ya wananchi kwa chombo hicho cha kulinda usalama wao na mali zao.


  Wakati nchi yetu iko katika vita dhidi ya ufisadi, Jeshi la Polisi halipaswi kujiweka kando na vita hiyo hivyo linatakiwa kuwa mstari wa mbele.


  Ushauri wetu ni kwamba Jeshi la Polisi sasa lichukue hatua kujisafisha dhidi ya rushwa.  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Z

  ZIGZAG Member

  #2
  Jun 7, 2012
  Joined: May 31, 2012
  Messages: 54
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  rushwa kwa polis wa tanzania imekithiri, imo ndani ya damu zao. lakini kwanini aliyewaondoa kina mkulo kipindi kile hakumuondoa wazir wa mambo ya ndani?
   
Loading...