Watanzania kwa ujumla kuanzia viongozi wa kitaifa mpaka wa vitongoji hawaonyeshi kabisa kwamba kuna anayejali hii nchi itakuwa wapi miaka 20 ijayo. Kila mtu anataka chap chap cha sasa hivi. Ndio maana hakuna anayejali elimu inavyoporomoka. Hakuna anayejiuliza kwamba vijana watakaomaliza shule na vyuo katika miaka kumi ijayo watakuwa wanafanya nini. Tunabaki kujisifu tuna amani wakati amani haiwezi ikawepo ikiwa watu wengi mno watakuwa wana njaa na hawana ajira. Badala ya kuhakikisha vijana wasomi ambao wamekoda ajira wanajiajiri kwenye kilimo na kuhakikisha masoko ya mazao hayo yanapatikana, nchi inatumia nguvu na rasilimali nyingi kwenye miradi ambayo hata kama itaendeshwa kwa faida kubwa namna gani, kamwe hiyo faida haiwezi kufikia faida ambayo ingepatikana kwa kuwezesha vijana laki mbili kujiajiri kwenye kilimo ambacho mazao yake yatauzika haraka. Tunashindwa kuelewa kwamba ni rahisi sana vijana waliokata tamaa (maana hawana ajira wala hawajui kesho yao ikoje) kutumiwa na maadui wa nchi kuleta machafuko. Mungu atusaidie tu maana kwa hali ya uchumi wa sasa ilivyo, na kwa vile hayaonekani matumaini ya haraka, sijui tutakuwa wapi miaka kumi ijayo