Je Sitta anarusha madongo ki aina ama ndiyo ukweli wenyewe ? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je Sitta anarusha madongo ki aina ama ndiyo ukweli wenyewe ?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Lunyungu, Sep 7, 2009.

 1. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #1
  Sep 7, 2009
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  Date::9/7/2009Spika Sitta: Msichague mafisadi 2010[​IMG]
  *AONYA NI WATU HATARI WANAWEZA HATA KUUA

  Na Ramadhan Semtawa

  SPIKA wa Bunge Samuel Sitta, ameibuka kwa kasi mpya akionya wananchi wasifanye makosa kwa kuchagua mafisadi kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.

  Tayari joto la uchaguzi mkuu mwakani limeanza kupanda katika kona mbalimbali nchini, huku kambi mbalimbali za kisiasa ikiwemo za wanasiasa wenye msukumo na nguvu za kifisadi na zile zinazosukumwa na fikra za uzalendo zikizidi kujiimarisha kwa ajili ya kujijengea himaya ya kisiasa mwakani, huku CCM ikizuia wabunge wake akiwemo Spika wasikirarue chama hadharani.

  Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam kuhusu ziara yake ya mkoani Singida, Spika Sitta alisema mafisadi ni watu hatari ambao wako tayari kufanya mambo yoyote hata kuua, ili kuweza kutimiza malengo yao.

  Ingawa Spika alikataa kuzungumzia kabisa mambo ya CCM kwa madai ya kuheshimu kamati ya akina mzee Ali Hassan Mwinyi, lakini habari kutoka vyanzo huru vilisema mafisadi walitenga takriban Sh 100 milioni, kumng'oa Spika kwa kuhakikisha ananyang'anywa kadi ya CCM katika mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) uliofanyika Dodoma hivi karibuni huku hadi sasa wakiendelea kupita mikoani na jimboni kwake kumwaga sumu ya fedha na uzushi.

  Tayari, mafisadi hao walitumia Waziri mmoja kutoka kanda ya Ziwa na Naibu wake (majina tunayo), wote kutoka wizara moja, kwa ajili ya kugawa fedha za kummaliza Spika.

  Naibu huyo alielezwa kukaa bandarini Dar es Salaam kusubiri wajumbe kutoka Zanzibar, kugawa fedha kiasi cha Sh 500,000 kwa kila mmoja kwa maelezo ya kwamba ni fedha za mafuta.

  Fedha za mafisadi hao wawili waandamizi ndani ya CCM, ziligawiwa kwa kisingizio cha mafuta wakati huo wajumbe walikuwa wamepanda basi kwenda Dodoma, huku Mwenyekiti wa chama hicho kutoka mkoa mkubwa nchini na Katibu wake, wakiwa ni askari wa mbele wanaotumwa na mafisadi kumdhoofisha Spika.

  Pia tukio la kutaka kuchomwa kisu Dk Harrison Mwakyembe, mbunge wa Kyela ni moja ya vitisho vinavyohusishwa na watuhumiwa wa ufisadi nchini.

  Tukio la kutaka kuchomwa kisu Dk Mwakyembe, limestua watu ambalo wadadisi wa mambo ya kisiasa wanalichukulia kama vita kuu zaidi ya kisiasa na makundi ndani ya CCM.

  Akina Dk Mwakyembe chini ya mwavuli wa wabunge 12 juzi walikuwa Nzega, Tabora kwenye uzinduzi wa benki ndogo ya vijijini ambayo iko kwenye jimbo la mbunge mwenzao kinara wa vita ya ufisadi Lucas Selelii.

  Hata hivyo, Spika Sitta ambaye ni mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, akifafanua zaidi, alisema akiwa mkoani humo alieleza bayana wananchi kuhusu kitisho cha mafisadi nchini na mustakabali wa uchaguzi mkuu mwakani.

  Akiweka bayana kauli hiyo, Sitta ambaye karibuni alibanwa na chama chake kwa nia ya kumziba mdomo, aliwaambia wananchi hao wachukue fedha, lakini wasithubutu kuchagua mafisadi.

  "Mimi nazungumza kama mwanasiasa si kiongozi wa dini, naomba viongozi wa dini mnisamahe," alianza Spika na kuongeza:

  "Kuna fedha chafu zinazunguuka, zichukueni, lakini msichague mafisadi katika uchaguzi mkuu ujao, hawa hawafai."

  Spika akisisitiza, alisema wananchi wanapaswa kutathmini na kukumbuka michango ya waasisi akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ambaye aliijenga nchi kwenye misingi ya uadilifu.

  Kuhusu mwelekeo wa chama chake CCM kwa sasa, Spika alisema hilo asingependa kulijadili kabisa kwani tayari ipo Kamati chini ya mzee Mwinyi, ambayo inafanya kazi zake.

  "Nisingependa kuanza kuzungumzia mambo ya chama tuache kamati ya mzee Mwinyi ifanye kazi zake kwa ufanisi, hayo mambo ya chama tuwaachie akina mzee Mwinyi," alifafanua Spika.

  Alisema alichokizungumza Singida kilikuwa ni kuhusu mafisadi wala si chama na asingependa kujiingiza huko, kwani ni sawa na kupuuza kamati ya akina mzee Mwinyi.

  Kuhusu kitisho dhidi ya mbunge Dk Mwakyembe, alisema hilo liko chini ya mamlaka ya vyombo vya dola kwani ndivyo vinapaswa kuangalia na kuona athari za matukio kama hayo.

  Spika Sitta alipoulizwa ziara yake mkoani Singida na hiyo ya akina Dk Mwakyembe mkoani Tabora kama ni sehemu ya mpango wa kuendeleza kampeni zao dhidi ya ufisadi, alijibu: "Ahaa, hapana mimi sijui sina ratiba yao."

  Akisisitiza, alisema anachoamini yeye ni kwamba ziara yake ni ya kichama kama mlezi na si vinginevyo, hivyo hiyo ya kina Dk Mwakyembe, inatokana na ratiba zao.

  Hali ya kisiasa nchini kwa sasa imekuwa tete kufuatia msuguano wa makundi ndani ya CCM ambacho ni chama kinachoshika hatamu ya dola.
  Mbali ya CCM, joto hilo hivi karibuni lilihamia upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kilifanya uchaguzi wake ambao ulitikiswa na nusura ukipasue baada ya mvutano kati ya kambi mbili ile ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Freeman Mbowe, kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya uenyekiti taifa.
  Tuma maoni kwa Mhariri
   
Loading...