Je, kuna maendeleo ya watu na ya vitu?

Oct 6, 2020
27
50
Hivi karibuni kumekuwa na hoja kutoka kwa vyama vya upinzani nchini hasa CHADEMA wakidai kuwa maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Raisi Magufuli ni maendeleo ya vituna sio maendeleo ya watu. Hoja yao inajikita kwenye mambo kama ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa vituo vya afya nchi nzima, Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa barabara za chini, barabara za juu na madaraja makubwa. Mambo yote haya kwa jicho la CHADEMA wanaona kuwa ni upuuzi mtupu kwani ni “maendeleo ya vitu na si maendeleo ya watu”. Makala haya yamelenga kujadili hoja hii kuntu; hususani Inalenga kujibu maswali yafuatayo, Je, Maendeleo ni nini? Je, tunawezakuwa na maendeleo ya vitu bila watu au watu bila vitu? Na Je, ni upi mtazamo sahihi kuhusu maendeleo kati ya huu wa serikaliya awamu ya tano na ule wa CHADEMA?

Maendeleo; maana na ufafanuzi

Maendeleo ni moja ya vitu muhimu sana katika maisha ya binadamu na hutamkwa karibu kila siku na watu wa aina mbalimbali. Wanakijiji wanataka maendeleo, wanafunzi wanataka maendeleo, wanasiasa wanasema wataleta maendeleo, kila mtu, katika ngazi ya familia, mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla anawaza, anataka na anatafuta maendeleo. Je, maendeleo ni nini hasa?

Maendeleo ni mchakato, ni mchakato wa jamii nzima kuondoka katika hali moja ya chini, ya kinyonge kwenda katika hali nyingine ya juu na iliyobora zaidi. Katika hili wapo wanazuoni wanaoona kuwa hatua hiyo inasababishwa na juhudi za mtu mmoja mmoja, mfano mwekezaji, mjasiriamali, mwanasiasa n.k. kisha huyu mtu mmoja ukimjumlisha na mwingine tena ukamjumlisha na mwingine basi unapata WATU. Yaani tunapata maendeleo ya watukwa kuwa mtu mmoja mmoja amenufaika, kila mmoja amepata hela zake kwa haraka; hivyo wakiwa kumi tunasema watukumi wamepata maendeleo kwa kuwa mradi X umewaletea pesa za moja kwa moja. Lakini pia wapo wanazuoni ambao hawakubaliani na mtazamo huo, wao hutazama maendeleo kama mchakato wa jamii yote, mchakato wenye manufaa kwa wotena si kwa mtu mmoja mmoja. Jambo laweza kufanyika, lisilete pesa ya moja kwa moja kwa mjasiriamali mmoja mmoja, lakini likawa na manufaa makubwa na ya muda mrefu sana kwa taifa zima.

Raisi magufuli na serikali yake ya awamu ya tano kwa kiasi kikubwa wanatumia nadharia hii ya pili katika kuleta maendeleo. Hii inamaana kuwa wanatumia muda mwingi kuweka miundombinu ya kudumu yenye manufaa ya muda mrefu sana kwa watu wotebila kujali tofauti zao. Kwa mfano ujenzi wa reli ya kisasa utaleta faida ya kudumu kwa taifa, vilevile ujenzi wa bwawa kubwa la umeme litawanufaisha watanzania wotekwa muda mrefu sana. Ukitaka kujua hilo fikilia miradi iliyowekwa na wakoloni; Reli iliyojengwa na wakoloni iliwanufaisha sana wakoloni na mpaka leo bado inatumika na inatunufaisha vizazi vya leo.


Image for post
Mtazamo huu wa pili pia unatufikisha kwenye hatua nyingine za maendeleo, hizi ni Uhuruna Kujitegemea. Maendeleo halisi ni yale yanayochochea jamii kuwa huru katika nyanja zote ikiwemo uchumi, siasa na utamaduni. Uhuru huo unasababisha taifa kujitegemea na hasa kujinasua na tatizo la ukoloni mamboleo unaofanywa na mataifa makubwa duniani. Hata hivyo, ukweli ni kwamba uhuru wa aina hiyo hauji kwa kumwezesha mwananchi mmoja mmoja kupata pesa. Kama ingelikuwa hivyo hata sasa taifa lingelikuwa na uhuru wa kiuchumi kwani tayari kuna mamilionea wengi nchini.

Jambo la kujitegemea kama taifa haliletwi na mtu mmoja mmoja kupata pesa bali ni mfumo wa taifa ambao unalenga kuweka misingi imara ya maendeleo. Je, kuna faida gani kuwawezesha watu kumi, watu mia moja au watu mia nane kupata pesa lakini bado wakawa wanatawaliwa na mataifa mengine? Kila siku taifa lako linakuwa ombaomba? Kila siku unakubali sera na uongo wa wakoloni hao kwa sababu huna uchumi imara, huna uhuru, huwezi kujitegemea! Sasa basi, ili kuepuka kutawaliwa, ili kuepuka kuwa ombaomba wa kudumu, ili kuepuka unyonge wa kila aina ni lazima kutumia mtazamo wa pili juu ya maendeleo kama ambavyo Raisi Magufuli anafanya. Mtazamo unaoweka misingi ya maendeleo iliyo imara na yakudumu kwa vizazi vya sasa na vya baadae.

Licha ya ukweli huo, CHADEMA hawawezi kuona umuhimu wa miradi yenye manufaa kwa taifa zima na kwa muda mrefu. Mtazamo wa CHADEMA katika maendeleo ni mtazamo finyu, kwani unaona maendeleo ni ya mtu mmoja mmoja; ni kitendo cha mtu mmoja mmojakupata pesa, kujenga nyumba na kujinufaisha yeye kama yeye. Ndio maana wanasema kazi za serikali ya awamu ya tano hazijawanufaisha watukwa sababu wao wanaangalia manufaa ya sasa tu, je, umepata pesa au hujapata? Lakini vitu vya kudumu vinavyoleta manufaa vizazi na vizazi hawayataki. Wanasema ni maendeleo ya vitu. Je, vitu vyaweza kuendelea bila watu? Je, watu waweza kuendelea bila vitu? Sehemu inayofuata inaeleza haya kwa kina.

Watu na vitu katika maendeleo

Hapa tuanze na mfano wa nchi za Ulaya ambazo wengi tunaamini ni nchi zilizoendelea. Swali ni je, katika nchi hizo nini kimeendelea? Ni Vituau Watu? Ukweli ni kwamba katika nadharia tena nadharia za wasomi wanaokubalika kimataifa, Wanafalsafa nguli kama Marx, Lenin na wenzao wanaamini kuwa maendeleo yanahusisha vyote viwili yani vitu na watu. Kwa maneno mengine vitu na watu vyote vinatakiwa kuendelea. Hata hivyo, katika hivi viwili kimoja hutangulia, haviwezi kuendelea vyote viwili. Vitu,yaani miundombinu (productive forces) hutangulia kuboreshwa/kuendelezwa kwanza kabla ya watu. Kwanini? Kwa sababu miundombinu inapoendelea inawapa urahisi watu wote kuendelea. Miundombinu inaweka misingi ya watu kuendelea na kubuni vitu vingine vingi zaidi (multiplier effect). Hata huko Ulaya tunakoona wameendelea kilichoanza kuendelezwa sio watu bali ni miundombinu hasa usafiri, mawasiliano, uzalishaji, umeme nk. Maendeleo ya watu walio wengi yamekuja baadae.

Kwa mfano; utengenezaji wa ndege za kisasa ambazo leo zinatumika kwa usafiri ulianza tangu miaka ya 1700, Lakini kwa mara ya kwanza ndege ilifanikiwa kusafirisha watu kwa usalama mwaka 1903. Japokuwa jambo hilo lilichukua muda mrefu na kutumia rasilimali nyingi lakini limeleta manufaa mengi sana kwa watu wengi ulimwenguni. Je, vipi kama watengenezaji wa ndege wangesema tusitengeneze hili likitu,tuwape pesa watu watumie? Je, leo tungekuwa na ndege?

Vilevile teknolojia ya trekta, gari, kompyuta n.k ni matokeo ya uwekezaji katika mambo ya msingi na yakudumu. Kwa macho ya kawaida unaweza ukasema “haya ni maendeleo ya vitu” lakini ukweli ni kwamba watu wengi wananufaika na vitu hivi kwa namna mbalimbali. Vipi kama mataifa/wagunduzi husika wa vituhivi wangesema havina maana? Jibu ni kwamba leo dunia ingekuwa haina ndege, gari, trekta, kompyuta nk. Na hata hizo hela wangegawiwa watu(ili kuwapa maendeleo) wangekuwa wameshazitafuna zikaisha zote. Hivyo kuna kila sababu ya kutazama maendeleo kwa kuanza na mambo ya msingi, mambo ya kudumu ambayo yanaleta manufaa kwa watu wote, kwa kizazi hiki na cha baadae.



Image for post

Mtazamo huu wa kisomi kuhusu maendeleo ndio unaotumiwa na Raisi Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano. Kwa watu ambao ni wavurugaji au wasiotaka kufikiri sawasawa hawawezi kumwelewa Raisi na mipango yake. Ukweli ni kwamba ujenzi wa Reli ya kisasa, Barabara za chini na juu, Zahanati, Bwawa la umeme nk. Ni miundombinu inayoleta mawndeleo kwa watanzania wote. Japokuwa kwa sasa inaonekana ni vituvinajengwa lakini ukweli ni kwamba haya ni maendeleo ya watu, ni maendeleo ya watanzania wa leo na vizazi vijavyo. Labda nitoe mifano; Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere litakapokamilika litaondoa shida ya umeme Tanzania, umeme utakuwa haukatiki hovyo, umeme utashuka bei, kama ulikuwa unatumia umeme wa shilingi elfu kumi kwa mwezi sasa utatumia shilingi elfu saba; je, hapa watu hawajapata maendeleo?

Je hayo ni maendeleo ya bwawa au watanzania? Mfano wa pili; Reli ya kisasa ikikamilika watu watasafiri kwa muda wa saa sita hadi saba kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza. Safari hii kwa sasa inatumia saa 18 hadi saa 24. Je, Reli hii ikikamilika itakuwa imemuendeleza nani? Watu au vitu? Unaweza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kisha ukarudi siku hiyohiyo; ni biashara kiasi gani zitafanyika? Ni muda kiasi gani utaokolewa? Je watu hawatanufaika kwa Reli hii? Maswali kama haya tunaweza kujiuliza kwa miradi ya vituo vya afya, zahanati, ndege, na barabara za chini na juu zinazojengwa nchini Tanzania.


Image for post


Mambo haya yanayofanywa na Raisi Magufuli na serikali yake ni makubwa, mazuri, yenye manufaa kwa wote na yanaleta maendeleo ya kweli kwa watanzania. Tofauti na miundombinu iliyowekwa na wakoloni, hii miundombinu ya sasa inalengo la kuwanufaisha watanzania wenyewe. Miundombinu ya kikoloni ililenga kuwanufaisha Wazungu, kusafirisha rasilimali zetu kwenda Ulaya na Amerika, lakini leo hii zinafanyika juhudi za kuhakikisha rasilimali za Watanzania zinawanufaisha Watanzania wenyewe; hii ni pamoja na kujenga miundombinu hii ya kudumu na kuepuka unyonge wa kuombaomba misaada Wazungu. Kama tutaendelea hivi, ndani ya miaka kumi ijayo nchi yetu itakuwa imejikwamua na utegemezi wa misaada kutoka nje na hivyo kuboresha maisha ya watu wake pamoja na miundombinu yake.

Kwa kuzingatia hoja hizi, ni ukweli usiofichika kuwa CHADEMA wanawadanganya Watanzania. Kusema kuwa maendeleo yanayofanywa na serikali ya CCM ni maendeleo ya vituni upotoshaji mkubwa na inaonesha dhahiri kuwa hawaelewi maana ya maendeleo wala hawajui muingiliano uliopo kati ya watu na vitu. Hata mtu ambaye hajaenda shule anatambua ya kuwa ujenzi wa nyumba unaanza na msingi. Huwezi kujenga nyumba ukaanza na kununua misumali ya bati. Hivyo serikali ya Magufuli inachokifanya na kuweka msingi imara wa maendeleo ya taifa kwa sasa na baadae. CHADEMA wao wanataka tuanze kujenga nyumba kwa kununua misumali. Hicho ni kichekesho cha karne, haijawahi kutokea na haitatokea popote ujenzi wa nyumba uanze kwa kufikiria kununua misumari ya bati badala ya kuimarisha msingi kwanza.

Hitimisho
Makala haya yalilenga kujadili dhana ya maendeleo ya watuna vitukama ambavyo inaelezwa na wanasiasa. Wakati serikali ya awamu ya tano ikijinasibu kuwa imefanya mambo ya maendeleo hapa nchini, wapinzani wamekuwa wakikejeli kuwa hayo ni maendeleo ya vitu na si maendeleo ya watu. Katika hili imeonekana kuwa vijembe vya wanasiasa wa upinzani hasa CHADEMA ni vya kupuuza kwani hawajui hata maana ya maendeleo wala uhusiano uliopo kati ya watu na vitu.

Wakati CCM na Raisi Magufuli wamejikita katika kuweka misingi imara ya maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo, CHADEMA wao wanajishughulisha na hoja ndogondogo, ni sawa na mtu anayetaka kujenga nyumba huku akianza kufikilia misumali ya bati badala ya msingi imara. Ninatoa wito kuwa Watanzania wasirudi nyuma, waendelee kushirikiana na Raisi Magufuli katika harakati zake za kuweka misingi imara ya maendeleo huku wakiwapuuza wapinzani ambao wana nia ya kupotosha umma.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom