Je, hili la Bandari likoje?

ubongokid

JF-Expert Member
Apr 30, 2017
2,033
3,916
Mengi yamesemwa na kujadiliwa kuhusu Bandari, Wanasiasa wamesema yao, Wataalamu wa Sheria wamesema yao, Wabunge wamesema yao na hata Wananchi wamesema yao. Nimewasikia hata Viongozi wa dini wakisema yao.

Hata hivyo katika kusikiliza hao wote nimekuwa nikitafuta msimamo ambao unaweza kututoa hapa tulipo na tuende mbele. Nimekuwa nikitafuta sababu ya kwa nini iwapo tayari Tuna TPA Tanzania Port Authority au mamlaka ya bandari bado tunahitaji DPWorld, je, tatizo ni nini au ni nani?

Bunge letu limefanya baadhi ya marekebisho ya sheria na pia kupitisha sheria ambazo ukizitazama kwa jicho la karibu utaona yote yanalenga kujenga mazingira ya kuvutia uwekezaji huu wa DP World.

Kuvutia uwekezaji ni jambo zuri, kupata Uwekezaji kutoka nje ni jambo zuri na sio jambo baya. Ninachojiuliza mimi ni kwa nini Bandari? Je, tuseme kwamba hatuna wataalamu wa kuweza kuendesha mitambo zile cranes pale bandarini?Je, hatuna mitambo ya kuchimba ili bandari yetu iwe na kina cha kutosha? Je, hatuna Makampuni ya ujenzi ambayo yanaweza kutengeneza Magati ya kutosha kuweza kupokea Mizigo ya kutosha? Kwa nini bandari?

Je, Chuo chetu cha Bandari hakina uwezo wa kuzalisha wataalamu wa kuweza kuzalisha na kusimamia bandari zetu? Au Chuo chetu cha DMI nacho pia hakina uwezo wa kuzalisha wataalamu wa Bandari? Au chuo chetu cha NIT hakina uwezo wa kuzalisha wataalamu wa logistics ili kuweza kusimamia shughuliza usafirishaji na uendeshaji wa bandari? Kwa nini Bandari?

Je, tuseme kwamba labda mamlaka yetu ya Mapato TRA nayo haina uwezo wa kusimamia mapato pale bandarini na hivyo na hivyo basi inahitaji DP World iwasaidie kukusanya Mapato pale na Wao waendelee kufukuzana na Wamachinga huku mtaani? Kwa nini Bandari?

Je, tuseme kwamba labda hatui historia ya dunia na dhana ya Ukoloni Mamboleo? Au Hatujui Kuhusu Ubepari? Au hatujia kwamba kuna aina mpya ya ukoloni ambao unatumia Makampuni Makubwa ya kimataifa katika kumilikia na kusimamia rasilimali muhimu za kimkakati hasa katika nchi Maskini? Kwa wale wanaopenda kusoma vitabu tafuteni Kitabu kinaitwa "Confession of the Economic Hitman" mkisome kama hamjakisoma then mtaelewa hili swala zaidi.Kwa nini bandari?

Binafsi nafahamu kidogo historia iliyop kati ya Tanzania na nchi za kiarabu. Uhusiano ambao ni wa karne nyingi sana, Uhusiano ambao ulikuwa wakinyonyaji na kitumwa? Uhusiano ambao ulilenga kutukandamiza na kutufanya raia wa daraja la 20 na hata ukitazama kwa undani utaona kwamba hata sasa huu ni muendelezo tu wa yale ambayo yalifanyika karne kwa karne. Ni wajukuu wa kina Seyyid Said wanakuja kuendeleza Urithi wa Babu zao.

Ndugu zangu, Afrika na Tanzania tunahitaji ushirika na Dunia, tunahitaji ushirikiano na Dubai na dunahitaji Ushirikiano na DP WORLD lakini sio aina ya ushirikiano kama ulivyokuwa enzi za babu zetu ambapo walichukua vile vinono na kutuacha watupu. Hatuhitaji aina hii ya ubia na uwekezaji tunahitaji uwekezaji na ubia ambao utakuwa na TIJA kwetu na kwa vizazi vijavyo.

Kabla sijahama kwenye Mjadala nirudi kwenye swali la Msingi? Je, kwa nini Bandari? Kwa nini tuwape DP World Bandari zetu?Wao wana kipi cha maana wanacholeta ambacho sisi tukiamua kukifanya tunashindwa? Kwamba kwa sababu wao wanavaa kanzu na wana hela za mafuta kwamba basi tuwape Bandari bila hata kujua hizo hela watazileta kwetu?

Kama bandari yetu inahitaji uwekezaji ni kwa nini serikali yetu isianzishe kampuni ya umma raia wote na hata DP world wanunue HISA humo na kuwa wamiliki wawekezaji na kutugawia FAIDA kama Investors badala ya kutulisha vibudu?

Kama bandari yetu inahitaji wataalamu kwa nini tusiamue kupeleka hata watoto wa Rais, au Watoto wa Waziri Mbarawa au hata watoto wa Makamu wa Rais au hata watoto wa Waziri Mkuu kama wanaona wakipelekwa watoto wa maskini na wakulima watafaidi ili wakasomee huo utaalamu kisha waje hapa Wasimamiee na kuendesha bandari zetu bila kutuletea Sarakasi za DP world?

Kama tatizo la bandari ni upigaji, wizi na upotevu wa Mapato Suluhisho lake haliwezi kuwa DP world. Kwanza wakija hao DP world watatuibia na kupeleka huko kwao Sijui Dubai Sijui Wapi huko walikotoka.

So ukiniuliza mimi nitakwambia bora tuibiane hapa hapa kwani vikiibiwa si vinakuja huku mtaani vinazunguka humu ndani? Kwani akiiba mbongo atakuja kutumia pesa yake humu ndani so angalau utajiri wetu utabaki hapa hapa?

Kama tatizo la bandari ni wizi na viongozi wetu wanakiri hili nafikiri wao ndio watuhumiwa wa kwanza wa huo wizi kwani kimsingi Mkurugenzi wa bandari anao huo wajibu wa kusimamia usalama bandari kama kashindwa kazi basi aondoke apishe mtu mwenye weledi?

Kama DP World orld wanakuja kuchukua nafasi ya kazi iliyokuwa inafanya na TICTS basi tupeni kwanza taarifa ya Utendaji wa TICTS kwa uwazi kabisa ili tujue TICTS alishindwa nini?Ameweza nini?na DP world atabadilisha nini iwapo atakuwa nafanya kazi za TICTS na Pia tuambieni iwapo mkataba wa TICTs nao ulikuwa na IGA kama hii ya DP world na iwapo nao ulipitishwa bungeni nakwa masharti kama haya.

Najua huu mjadala bado ni mbichi sana, ila nataka nitoe angalizo hapa mapema kabisa kwamba huu mkataba tunaojadili kwa sasa ni the Tip of Iceberg ili kiuhalisia kuna mikataba mingi ambayo inafanana na hiyo ambayo hatujaweza kuiona.

Kwa mfano Ukitazama huu mkataba umeletwa Bungeni Muda mrefu sana baada ya kusainiwa. Swali ni je, vipi kuhusu hiyo mingine ambayo haijaja Bungeni? Je, huu ulikuja Bungeni kwa utashi wa serikali au kwa kuvujishwa na Presha kutoka kwa wazalendo fulani ambao walitaka kuuweka wazi na hivyo serikali yetu ikaamua kuja na Pre emptive strategy ya kujiosha?

Maana ulitumika muda mfupi sana kutaka watu waje kutoa maoni yaani less than 24 hours mtu awe ametoka Lake Tanganyika Kigoma na Lake Victoria, na Lake Nyasa,na Lake Rukwa na Bandari za Tanga, Dar, Kilwa, Mtwara kufika hadi Dodoma kwenda kutoa maoni yake.

Hivi watanzani wangapi ambao wanamiliki Ndege au wana uwezo wa kupanda Ndege au hata hiyo Air Tanzania ina uwezo wa kufika huko kote ndani ya Masaa 24 na kuwaleta watu Dodoma?

Ndugu zangu tujadili hili la bandari ila tusiache kuulizia pia mikataba mingine ambayo inahusu uwekezaji wowote ule ambayo hatujui kilichoandikwa humo wala kinachoendelea na kama kuna wazalenda ambao wanaweza kuileta hapa, waileta tu ili ijadiliwa kwa pamoja.

Zaidi pia nipendekeze kwa wale ambao wana uwezo wa kuhamasisha basi tuhamasishe ushiriki zaidi katika mijadalainayohusu mustakabali wa taifa letu.

Kwa pamoja tunasonga mbele,
Mungu Ibariki Tanzania.
 
Niko chattle nalinda kaburi namsubiri lissu aje kutubu amuamshe amwambie haya yote.
 
Back
Top Bottom