- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Kufuatia taarifa za visa vya Ebola nchini Kenya, kumekuwa na hofu na mijadala mtandaoni kuhusu namna virusi hivyo vinavyoenea, huku baadhi ya watu wakihofia kuwa mtu anaweza kupata Ebola kwa kupumua hewa moja na mtu aliyeambukizwa.
Lakini je, Ebola huenea kupitia hewa kama mafua, COVID-19 au surua?
Lakini je, Ebola huenea kupitia hewa kama mafua, COVID-19 au surua?
- Tunachokijua
- Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Kenya, Shirika la Afya Duniani (WHO) na CDC, Ebola haisambai kupitia hewa kama magonjwa ya kawaida ya mfumo wa upumuaji.
Ebola huenea hasa pale mtu anapogusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili wa mtu mwenye Ebola ambaye ana dalili, kupitia ngozi yenye jeraha au sehemu laini za mwili kama macho, pua na mdomo.
Majimaji hayo yanaweza kujumuisha damu, matapishi, kinyesi, mkojo, mate, maziwa ya mama na shahawa.
Maambukizi yanaweza pia kutokea mtu anapogusa vitu vilivyochafuliwa na majimaji ya mgonjwa, kama mashuka, nguo, sindano au vifaa vya matibabu, kisha virusi kuingia kupitia ngozi iliyojeruhiwa au sehemu laini za mwili.
CDC inaeleza kuwa Ebola haienei kwa kuwa tu karibu na mtu mwenye maambukizi, tofauti na virusi vya mfumo wa upumuaji kama mafua au COVID-19.
Hata hivyo, matone makubwa yenye majimaji kutoka kwa mgonjwa, kwa mfano wakati wa kutapika au kukohoa, yanaweza kuwa hatari yakifika moja kwa moja kwenye macho, pua, mdomo au ngozi yenye jeraha. Hii haitambuliki kama maambukizi kupitia hewa (airborne transmission).
Wizara ya Afya inashauri nini?
Wizara ya Afya imewataka wananchi kuwa waangalifu lakini wasiwe na hofu, na kuepuka kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mtu anayeshukiwa au kuthibitishwa kuwa na Ebola.
Mtu anayepata dalili au anayehisi kuwa huenda alikutana na mtu mwenye maambukizi anashauriwa kutafuta huduma za afya mara moja badala ya kujitibu nyumbani.
Kwa mwongozo na taarifa rasmi kuhusu Ebola, Wizara ya Afya imetaja nambari ya bila malipo 719.