JE, UNATAKA KUOKOKA SASA?
Tunasoma haya katika LUKA 1:77, Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao. Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja. Je, kweli utasamehewa? Jibu ni Ndiyo! Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37,
.Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu. Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi? Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi.
Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa?
Najua uko tayari. Basi sema maneno haya,
Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani. Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa. Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni. Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen.
Sasa ninaomba kwa ajili yako, Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen. Tayari umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.
MUNGU AKUBARIKI!!!