JAMANI KWANI LAZIMA?!-3
ILIPOISHIA
"Haya, kazi njema shemeji, sisi tupo bwana, kumekucha sasa kwa hiyo tunaangalia maisha yanakwendaje!" Paulina aliongea sana kiasi kwamba, siku hiyo baba Riziki akashangaa imekuaje, maana licha ya kumfahamu lakini si kawaida yake…
SEREREKA NAYO MWENYEWE…
Hapo walikuwa bado wamesimama wakiendelea kuzungumza…
"Sawa shemeji yangu, nisalimie familia, mzee na watoto pia," alisema baba Riziki licha ya kwamba alijua kuwa, Paulina hana mtoto hata mmoja achilia mbali watoto.
Paulina akaanza tena…
"Aah! Shemeji yangu wee, watoto wapatikane wapi? Ndiyo nahangaika sasa kutafuta, sijui Mungu atanisaidiaje? Lakini pia nategemea zaidi na misaada yenu nyie mashemeji zangu."
"Shemeji we mwombe Mungu tu, atakusaidia. Lakini shemeji kuna daktari mmoja ni mtaalam sana kwa wanawake wenye hali kama yako," alisema baba Riziki.
"Yupi huyo shemeji? Anaishi wapi? Anapatikanaje?" aliuliza maswali mengi Paulina.
"Mmmh! Anaishi Mikocheni, anaitwa Dokta Paul."
"Labda shemeji ungenipa namba yake na yako pia."
"Oke," baba Riziki alianza kwa kuzitaja namba zake kisha akamalizia na za Dokta Paul.
Wakaagana na kuondoka, baba Riziki alitembea kwa hatua kadhaa, akageuka nyuma kumwangalia Paulina lakini huku akiwa na tahadhari kubwa kwamba asije naye akageuka wakakutana macho…
"Lakini ana hoja!" alisema moyoni baba Riziki akiwa anatembea huku bado anamwangalia mwanamke huyo. Ghafla, Paulina naye akageuka kumwangalia baba Riziki, wakakutana macho, baba Riziki akakimbiza kichwa mbele, Paulina akachekea moyoni…
"Da! Kumbe na yeye alikuwa ananiangalia, baba Riziki bwana. lakini leo ni mara ya kwanza mimi na baba Riziki kuzungumza tukiwa tumesimama, mara nyingi inakuwa juujuu tu," alisema moyoni Paulina.
***
Baada ya kumaliza kazi zake za ndani siku hiyo, Paulina alikaa na kuanza kuwasiliana na Dokta Paul…
"Yeye Paul mimi Paulina," alisema moyoni akiwa anaseti namba, akampigia. Simu yake ilipokelewa upande wa pili na Dokta Paul mwenyewe ambapo alijitambulisha kisha akasimulia tatizo lake la msingi…
"Oke….oke oke…pole sana…sasa kwa tatizo hilo inabidi tuonane hospitalini kwangu siku ya Alhamisi saa kumi jioni ndiyo huwa nahudumia akina mama," alisema Dokta Paul…
"Sawa dokta, nitakuja."
Baada ya kukata simu, Paulina alisema moyoni…
"Ungejua nimeshakutana na madaktari kibao mpaka wale wakware lakini hamna kitu. Ninachotaka mimi ni mwanaume mweusi, ana midevu kama Osama na awe amavaa shati jekundu basi, labda uwe na wewe una sifa hiyo ya mganga wangu."
Aliiseti tena simu yake na kumtwangia baba Riziki sasa ambaye ndiyo chanzo cha msingi kwake…
"Haloo," baba Riziki alipokea kwa sauti nzito, ya kiume bila kumjua mpigaji maana namba ya Paulina hakuichukua muda ule…
"Shem, Paulina hapa…"
"Ooo! Shemeji, vipi ulimpigia Dokta Paul?"
"Ndiyo shemeji, ndiyo nimetoka kuwasiliana naye muda huuhuu…"
"Amesemaje?"
"Amesema niende Alhamisi jioni ya saa kumi ndiyo huwa anahudumiaga watu wenye hali kama yangu."
"Oke oke, si utakwenda shemeji?"
"Nitakwenda shemeji, mimi tena!"
"Basi sawa shemeji."
"Sawa shemeji, nilisema tu nikupe taarifa."
"Sawa shemeji."
"Lakini shemeji jambo moja please, huu mkakati wangu naufanya kuwa siri, mume wangu hajui. Kwa hiyo naomba usimwambie kitu shemeji!"
"Oke! Lakini si mista anatakiwa kujua?"
"Noo! Atajua mambo yakianza kuwa mazuri."
"Sawa, tufanye nimekuelewa shemeji."
"Nashukuru sana."
Baada ya kukata simu, baba Riziki akabaki na maswali kibao…
"Sasa mwanamke anatafuta ujauzito lakini hataki mume ajue! Mh! Huo ujauzito anamtafutia nani?" alijihoji baba Riziki…
"Wanawake wengine bwana," aliishia kusema hivyo.
***
Kwa upande wake, Paulina baada ya kukata simu alijisifu kwamba anakaribia kushinda masharti ya mganga wa kienyeji…
"Ina maana…Da! Mimi kiboko! Ina maana nakaribia kumnasa baba nanihii! Sasa siku ikifika akiwa amevaa shati jeusi itakuaje? Masharti mengine bwana, ni shiiida!"
Mchana wa siku hiyo, Paulina akamtumia meseji baba Riziki…
"Yaani shemeji nikifanikiwa sijui nikupe zawadi gani! Teh! Teh! Teh!"
Aliisubiria meseji yake kujibiwa kwa dakika tano, ikaingia ya baba Riziki…
"Mh! Shemeji we unataka kunipa zawadi gani kwani?" baba Riziki naye sasa alijitosa, akaanza kuhisi kama kuna ubwete kwa mwanamke huyo mwenye figa ya namba nane na sura ya kitoto achilia mbali miguu ya haja na midomo iliyoviringishwa vizuri kama pindo la kanga…
"Shemeji bwana! Yoyote ile utakayoipenda wewe."
"Aaa! Shemeji we si ndiyo utanipa zawadi umesema, mimi siwezi kusema, wewe ndiyo mwamuzi…"
"Hamna shemeji, zawadi za siku hizi anayepokea pia ana uhuru wa kusema anayoitaka. Naweza kusema nikupe zawadi ya Big G kumbe unapenda biskuti mwaya!"