Jaji Mkuu: Sasa nakwenda 'kushika chaki'


Rutashubanyuma

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Joined
Sep 24, 2010
Messages
169,611
Likes
639,488
Points
280
Rutashubanyuma

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Joined Sep 24, 2010
169,611 639,488 280
Jaji Mkuu: Sasa nakwenda 'kushika chaki' Thursday, 09 December 2010 22:02

Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani anastaafu siku chache zijazo baada ya kulitumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 40 katika ngazi na nyadhifa mbalimbali. Hivi karibuni alikuwa Lushoto, Tanga katika Chuo cha Mahakama (IJA) ambako alikutana na Mwandishi Wetu, BURHANI YAKUB na kufanya naye mahojiano.

Swali: Wakati ukitoa hutuba yako katika mahafali ya wahitimu wa stashahada na cheti cha sheria Chuo cha Mahakama (IJA) Lushoto ulidokeza kwamba siku chache zijazo utastaafu rasmi, je utajihusisha na shughuli gani bada ya hapo?

Jibu: Ni kweli siku 20 zijazo nitakuwa nje ya wadhifa huu kwani nimeshafikia umri wa kustaafu kulitumikia Taifa kama mtumishi wa Serikali. Nimetumika kwa zaidi ya miaka 40 na kama mtakumbuka nimekuwa Jaji Mkuu tangu mwaka 2007 nilipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Nashukuru Mungu kwamba nastaafu nikiwa na nguvu na akili hivyo nitatumia muda huo kwa kufundisha sheria katika vyuo vikuu ndani na hata nje ya nchi nitakapohitajika. Sitakaa nyumbani, napenda kufundisha kwa sababu ni jukumu linalompa mtu heshima katika jamii. Ni kazi ninayoipenda na nilishawahi kuifanya na hivi sasa ninajivunia kwani baadhi ya wanafunzi wangu wana nyadhifa madaraka mbalimbali. Wamo majaji na watumishi wakubwa katika masuala ya sheria ndani na nje ya nchi.

Nimeamua kufundisha kwa sababu moja kubwa, elimu ni msingi wa maisha ya kila binadamu na pia nataka niweze kutoa mchango wangu wa elimu niliyonayo na kipaji chagu kuwamegea vijana ili ujuzi wangu uwe endelevu.

Sifundishi kwa sababu nastaafu, hata nilipokuwa mtumishi wa Serikali nilikuwa nikifundisha. Nimefundisha sheria katika vyuo mbalimbali kikiwamo Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa ambako kwa sababu ya kupenda kwangu kutoa elimu kwa wengine nilikuwa nikienda kwa kuendesha gari mwenyewe. Nitakachofanya nitakuwa nikienda chuo chochote nchini na nje ya nchi pale nitakapopangiwa mada. Sitasita kwenda na ningependa kuwajulisha kuwa sitakuwa na gharama kubwa kama ilivyo kwa wengine.

Swali: Ni mambo gani unaweza kujivunia ambayo umeyafanya ukiwa Jaji Mkuu?

Jibu: Tangu nimeteuliwa na Rais kuwa Jaji Mkuu, kuna mambo mengi niliyoyafanya ambayo kama wenzangu wanaobaki watayaendeleza, mhimili huu wa Serikali utakuwa na hadhi na heshima kuliko ilivyokuwa awali. Katika kipindi cha miaka mitatu niliyokuwa Jaji Mkuu, mimi na wenzangu tumejitahidi kuiweka mahakama kuwa katika mhimili wake wa tatu wa nchi tofauti na hali niliyoikuta kabla ya hapo kwani mahakama ilikuwa imewekwa pembeni.

Kuna mihimili mitatu ambayo ni Rais, Bunge na Mahakama ambayo kimsingi ndiyo inayotegemewa. Mihimili hii miwili yaani Rais na Bunge muda wote iko imara kwa sababu inaingiliana, lipo Baraza la Mawaziri ambalo linawakilisha wabunge ambalo Mwenyekiti wake ni Rais hivyo hukutana mara kwa mara.

Kadhalika Rais huwa na muda wa kulihutubia Bunge wakati wa kulifungua na kulivunja na wakati mwingine inapotokea dharura au jambo. Lakini muhimili huu wa tatu ambao ni mahakama ulikuwa umeachwa pembeni na ilionekana kama ni idara isiyokuwa na hadhi kama inayostahili. Hivyo baada ya kushika madaraka ya Jaji Mkuu nilihakikisha Mahakama inarejeshwa katika hadhi yake na nashukuru hili limefanikiwa.

Mabunge yote matatu wakati Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria inasomwa, nilikuwa bungeni, nilihudhuria nikiwa mwakilishi wa mhimili wa tatu wa nchi tofauti na walionitangulia ambao hawakuwa wakipewa nafasi hiyo. Lakini nimekuwa nikifanya kila njia kuhakikisha mhimili huu unatambulika kwa kuweka msukumo wa kutandaa katika ngazi za wilaya na mikoa. Kila nilipofanya ziara katika wilaya yoyote ni lazima kwanza nipitie ofisini kwa mkuu wa mkoa na wilaya kusaini kitabu na kujitambulisha.

Katika hili kuna tukio ambalo sitalisahau, nilikwenda wilaya moja ambayo sitaitaja nilifika jioni nikalala asubuhi nikawahi ofisini kwa DC, lakini nikaambiwa amesafiri asubuhi hiyo kwa sababu ameanza rasmi likizo, nikajiuliza kwa nini asingesubiri nimuone kwanza halafu aendelee na safari yake?

Naomba ifahamike kuwa mihimili yote imebeba jukumu moja tu, kumtumikia Mtanzania kwa hekima na uadilifu mkubwa. Si vyema waliopo kwenye madaraka kudharau mihimili mingine. Jambo jingine ambalo nitastaafu nikiwa kifua mbele ni harakati nilizoanzisha za kuomba Mfuko wa Mahakama urejeshwe, kuna matatizo mengi yaliyopo katika mhimili huu ambayo yanatokana na kuwa na fungu dogo la uendeshaji.

Nafurahi kuwa Rais Kikwete amesikia kilio chetu na ameahidi kutoa ifikapo mwakani. Niliomba angalau hata tukipewa asilimia mbili utaisaidia mahakama, unafahamu kwamba mahakama ilikuwa ikipewa ruzuku ya asilimia 0.5 na ndiyo maana unakuta mambo mengi yanasuasua! Katika hili tunavyo vigezo vya kuomba tena vigezo vya kisheria kabisa, nina imani kwamba mambo yatakuwa mazuri mara nne ya ilivyo sasa.

Jingine nililolisimia kwa nguvu zote ni kufuatilia suala la Tume ya Utumishi ya Mahakama na kuona kuwa inapewa madaraka ya kushughulikia yenyewe jukumu la kuajiri, kupandisha vyeo kusimamia nidhamu kwa watumishi wasio mahakimu au majaji katika idara ya mahakama.

Hili lina umuhimu mkubwa katika suala zima la nidhamu kwa watumishi wasio mahakimu au majaji kama makarani, wahasibu, madereva na walinzi kwani wakati mwingine unapotaka kumuadhibu kwa kukosa nidhamu kazini inakuwa ngumu kutokana na kuwa na tume isiyokuwa na meno.

Majengo ya mahakama pia ni jambo ambalo nililisimamia kwa nguvu, kama mnavyoshuhudia majengo ya mahakama ni machakavu, mengi hali yake ni mbaya sana. Ningependa jamii hapa ione umuhimu wa majengo ya mahakama, wanasiasa wameweka kipuambele katika ujenzi wa madarasa, zahanati na miundombinu mingine huku wakidhani kuwa mahakama si jukumu lao, hayo ni makosa makubwa yanayoweza kuligharimu Taifa hili katika siku zijazo. Sambamba na ujenzi wa zahanati na madarasa, ni vyema majengo ya mahakama nayo yajengwe kwani hilo ni jukumu la jamii katika suala zima la kuimarisha hali ya usalama na utulivu kwenye maeneo wanayoishi.

Kipaumbele cha sita nilichofanyia kazi nikiwa Jaji Mkuu ni kuingiza teknolojia ya kisasa wakati wa utendaji kazi wa mahakimu na majaji hasa ikizingatiwa kuwa sasa inatumika njia ya tangu enzi za wakoloni ya kuandika kwa mkono wakati wa kuendesha mashtaka na hata kuandika hukumu. Tunashukuru mchakato utaanza hivi karibuni wa kuwafundisha majaji na mahakimu juu ya namna ya kutumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta kwani tayari tovuti ya Mahakama imeshazinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal.

Swali: Ni mambo gani ambayo hutayasahau yaliyokupa wakati mgumu ulipokuwa kwenye madaraka yako ya Jaji Mkuu?

Jibu: Jambo lililonipa wakati mgumu katika kipindi changu cha kuongoza mhimili huu wa Mahakama ni suala la baadhi ya watendaji kuchukulia uhakimu na ujaji kuwa ni kazi za kujipatia maslahi makubwa kama zilivyo nyingine. Nimekuwa nikiwakumbusha wenzangu kuwa uhakimu na ujaji ni wito na siyo kazi kipaumbele si maslahi, bali ni huduma kwa jamii hasa ya wanyonge.

Napata shida sana ninapopata tetesi kuwa baadhi ya mahakimu hasa wa mahakama za mwanzo hawafuati maadili ya kazi kama vile kuomba au kupokea rushwa na kutotenda haki. Huwakumbusha kila nipatapo nafasi ya kuzungumza nao maneno yaliyo katika kitabu maarufu kiitwacho “The Judge’s Book’’cha Alfread Di Bona anayesema kwa tafsiri ya Kiswahili “Usidhuru haki na sharti uwe mwadilifu. Usipokee rushwa kwani rushwa hupofusha macho ya mwenye hekima na kupotosha hata maneno ya ukweli.”

Lakini kubwa zaidi linaloniumiza kichwa hadi hivi sasa ni suala zima la uvumishaji juu ya ulaji rushwa mahakamani, uvumi ni mkubwa kuliko hali halisi. Ukitaka ushahidi katika hili hupati, na si kweli kwamba kuna ulaji rushwa kwa namna inavyoelezwa kuliko idara nyingine. Inavyoelezwa ni kubwa mno. Mahakama ya Rufaa nina uhakika hakuna rushwa kwani huendeshwa kwa jopo la majaji, kama mimi utanipa rushwa nimelitumikia Taifa hili kwa zaidi ya miaka 40 halafu nikubali rushwa wakati nitalipwa pensheni hadi nitakapokufa!

Swali: Unasemaje kuhusu uhaba wa mahakimu nchini.
Jibu: Uhaba wa mahakimu na majaji katika Idara ya Mahakama ni tatizo kubwa na ufumbuzi wake unahitaji uwanja mpana. Idadi ya mahakimu ni chini theluthi moja ya mahitaji na ndiyo maana mimi kama mzalendo nimeona muda wangu uliobaki nielekeze nguvu zangu katika kufundisha ili tuweze kuwa na ongezeko angalau tuvuke nusu yake.

Mahakimu nchini idadi yao haizidi 1,600 ukilinganisha na ukubwa wa nchi. Bila shaka unaweza kutetemeka lakini hiyo ndiyo hali halisi. Namshukuru Rais Kikwete katika kipindi chake alichokaa madarakani miaka mitano iliyopita ameweza kuteua majaji wakiwamo wanawake hilo ni jambo la kumpongeza kwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuthubutu kufanya hata mambo ambayo waliomtangulia waliona yanashindikana.

Picha nambari Aug 023,024 jpg ni Jaji Mkuu Augustino Ramadhani akiongoza maandamano ya majaji katika chuo cha uongozi wa Mahakama Ija Lushoto. Picha na Burhani Yakub
 

Forum statistics

Threads 1,239,097
Members 476,369
Posts 29,342,182