Jaji Mkuu awaonya wanasiasa nchini

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
JAJI Mkuu wa Tanzania, Augustine Ramadhani amewaonya wanasiasa wanaozungumzia kesi mbalimbali zilizopo mahakamani, katika majukwaa ya siasa. Jaji Ramadhani alisema kuzungumzia kesi ambazo bado zinasikilizwa na mahakama mbalimbali, ni kinyume na sheria za nchi.

Katika uzinduzi wa kampeni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zilizozinduliwa Agosti 29, mwaka huu, kada wa chama hicho na mwanasheria mkongwe nchini, Mabere Marando aligusia kesi za wizi wa fedha za Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) zinazoendelea.

Mbali na kesi hiyo ya EPA, katika hotuba yake pia alisema kumfunga Amatus Liyumba pekee yake siyo dawa ya kumaliza ufisadi nchini, bali viongozi hao ndiyo wanaotakiwa kufungwa. Alisema wamemfunga Liyumba ili waonekane kwa wananchi kwamba wanapiga vita ufisadi. "Jamani hivi fedha zote zilizoliwa pale Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni Liyumba pekee yake aliyeziiba?, Tunajua ametolewa kama mbuzi wa kafara," alisema Marando.

Jaji Ramadhani alitoa onyo juu ya kauli hizo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kwa semina ya siku tatu ya majaji wa mahakama za nchi 12 za Afrika. Semina Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

“Kesi zote zilizopo mahakamani hazitakiwi kuzungumziwa nje ya mahakama, mimi mwenyewe wakati kesi ya mgombea binafsi ilipokuwa mahakamani nilikuwa sitaki kuizungumzia nje ya mahakama,” alisema Jaji Ramadhani.

Kuhusu hatua watakazochukuliwa watu wanaozungumzia kesi zinazoendelea mahamani, jaji huyo alisema hawawezi kutoka mahakamani na kwenda kuwashika watu na kuwafungulia kesi na kwamba mtu atakapeleka malalamiko juu ya vitendo hivyo, watayafanyia kazi.

Awali akifungua semina hiyo, rais Karume alisema bila kuwa na ushirikiano wa kutosha vitendo vya ugaidi na uhalifu wa kimataifa hautawezwa kukomeshwa.

Aliwataka majaji waliohudhuria semina hiyo, kubadilishana uzoefu ili kupata njia sahihi ya kukabiliana na matatizo hayo.

“Kutokana na kukua kwa na teknolojia uhalifu wa kimataifa na ugaidi unaendelea, kwetu ni matatizo makubwa, inatakiwa tukae pamoja na kujadili njia za kumaliza hili tatizo, tunatarajia mkutano huu utatoa majibu ya matatizo haya,” alisema Rais Karume.

Pia aliwataka majaji hao, kujadili na kuelewa ipasavyo juu ya mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC.

Naye Jaji Ramadhani akizungumzia mahakama hiyo alisema wanachukua tahadhari na kupata uzoefu wa kushughulikia kesi za ugaidi na uharamia kutokana na matukio yanayotokea katika nchi za jirani.

"Hivi karibunu watu wameuliwa na magaidi nchini Uganda, sasa kwanini na sisi tusijiadhari,” alihoji Jaji Ramadhani.

Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika semina hiyo ni pamoja na Ugaidi Mashariki na Kusini mwa Afrika, jukumu la mfumo wa kisheria wa thalifu katika kukabiliana na ugaidi na mapitio ya sheria ya kuzuia ugaidi ya Tanzania ya mwaka 2002.

Nyingine ni Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) na uwezo wake wa kisheria, hifadhi ya mashahidi, kinga na misamaha kwa wahalifu wa kimataifa na nguvu ya amani na haki katika mkitadha wa uhalifu wa kimataifa.

Pia washiriki wa semina hiyo watajadili mada kuhusu matatizo na ushirikiano wa mashirika yanayopambana na uhalifu katika kupambana na ugaidi.

chanzo: Jaji Mkuu awaonya wanasiasa nchini
 
SIKU chache baada ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando, kuwahusisha vigogo wa CCM na ukwapuaji wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), amemshukia Jaji Mkuu, Agustino Ramadhan, akimtaka aache kuikingia kifua CCM. Marando alisema kama Jaji Mkuu Ramadhan anataka kuingia kwenye siasa, ni vema akanunua sare za chama hicho na kupanda jukwaani kujibu hoja na tuhuma zinazoelekezwa kwa vigogo wa CCM wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi.
Akizungumza na Tanzania Daima, Marando alisema baadhi ya vyombo vya habari juzi vilimnukuu Jaji Mkuu akiwaonya wanasiasa akiwemo yeye (Marando) kuwa wanaotoa hotuba za kisiasa majukwaani juu ya kesi zilizo mahakamani wanafanya makosa.
Marando alisema anasikitishwa na kauli hiyo kwa kuwa jaji mkuu si mwanasiasa na hapaswi kusikiliza maneno ya kisiasa na kuyatolea ufafanuzi kama hayajafikishwa mezani kwake.
Alisema katika uzinduzi wa kampeni za CHADEMA, yeye (Marando) alisema watuhumiwa waliofikishwa mahakamani kwenye kesi za wizi wa EPA ni matawi tu na kuwataja baadhi ya vigogo wa CCM ambao walipaswa kuunganishwa katika kesi hizo kwa sababu wao ndio walioubariki wizi huo.
Alisema kauli hiyo si kuingilia mwenendo wa kesi bali kuonyesha kuwa kuna mafisadi wengi ambao walistahili kufikishwa mahakamani, lakini hawajafikishwa kwa sababu ya kinga ya chama au wanatumia madaraka yao.
"Jaji Mkuu anatumia kofia yake kuitetea CCM, anataka jamii ione ninachokifanya mimi na CHADEMA ni kosa, hii si sahihi, namuomba aache kubishana na mimi kuhusu masuala ya kisiasa," alisisitiza Marando.
Marando alibainisha kuwa kuna chombo kinachoshughulikia nidhamu ya mawakili hivyo kama yeye atakuwa amefanya makosa chombo hicho kitamuita kumuonya na ikiwezekana kumuadhibu lakini si anavyofanya Jaji Mkuu.
"Yeye kama ana hamu ya kupanda jukwaani si akanunue sare ofisi za CCM pale Lumumba ili tuweze kupambana naye kwenye uwanja unaostahili?" alisema Marando.
Aliongeza kuwa Jaji Mkuu ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, hivyo ana uwanja mpana wa kutolea uamuzi au ufafanuzi kesi inayopelekwa mezani kwake na si maneno yanayosemwa katika viwanja vya Jangwani au vinginevyo katika kampeni zinazoendelea hivi sasa.
Alisema ufisadi ni hoja nzito ambayo haipaswi kupindishwa pindishwa au kutetewa na viongozi kwa sababu imewafanya Watanzania waendelee kuwa maskini katika ardhi yao, huku watu wachache wakitumia rasilimali za nchi kwa maslahi binafsi.
Aliongeza kuwa kutokana na kutambua athari za ufisadi, CHADEMA imeamua kuuvalia njuga na kuwaumbua wale wote walioshiriki au wanaoendelea kutenda vitendo hivyo.
Juzi baadhi ya vyombo vya habari, vilimkariri Jaji Mkuu Ramadhan kuwa kujadili kesi zinazoendeshwa mahakamani kwenye mikutano ya hadhara ni kinyume cha sheria na mahakama itachukua hatua dhidi ya watu wanaofanya hivyo.
Vyombo hivyo vilimkariri Jaji Mkuu akisema kuwa sheria iko wazi kwa wanaoingilia mwenendo wa kesi na mahakama itawawajibisha wanasiasa wanaofanya hivyo bila hata kungoja vyombo vingine vya dola kuwachukulia hatua wahusika.



A very good response
 
Advocate Mabere Marando vs Jaji Mkuu, Mtu na Bosi wake! Kaazi kweli kweli!
 
Advocate Mabere Marando vs Jaji Mkuu, Mtu na Bosi wake! Kaazi kweli kweli!

Marando si muajiriwa wa mfumo wa mahakama, ni wakili wa kujitegemea, na kwa hiyo huwezi kusema hapa kuna "mtu na bosi wake".
 
Back
Top Bottom