Jairo na wenzake sasa kuburuzwa kortini

Michael Amon

JF-Expert Member
Dec 22, 2008
8,775
3,610
VIGOGO wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kuhusika katika sakata la uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia kupitisha makadirio ya matumizi ya wizara hiyo ya 2011/2012 watafikishwa mahakamani.


Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anafanya ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) ambao unaweza kubaini kuwapo kwa makosa ya kijinai katika utaratibu huo.


Ukaguzi wa sasa wa CAG ni sehemu ya mchakato wa kukamilisha taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya Novemba 11, mwaka jana kuhusu uchangishaji wa fedha hizo ambao uliratibiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.


Baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo, Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe iliahidi kuyafanyia kazi na kuwasilisha majibu Bungeni.


“Kwa sababu ya ukubwa na uzito wa taarifa hii, ni vigumu kuitolea majibu yote hapahapa, ninachoweza kufanya ni kuipokea pia tutakapokuja katika Mkutano wa Sita, tunategemea kuleta majibu ya hoja zilizomo kwenye taarifa hii,” alisema Chakawe ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria.
Kauli ya CAG


CAG, Ludovick Uttouh akizungumza na Mwananchi alikiri ofisi yake kufanya ukaguzi huo ambao alisema unajulikana kama ‘ukaguzi wa utambuzi’ lakini akasema kazi hiyo ilikuwa bado haijakamilika. Hata hivyo, alisema hafahamu ni lini ukaguzi huo utakamilika.


“Niseme kwamba katika ukaguzi wa aina hii tunakwenda ndani zaidi na mara nyingi huwa unalenga kubaini iwapo kuna jinai katika hesabu zinazohusika na ukaguzi,” alisema Uttouh.


Mtaalamu mwingine wa ukaguzi wa hesabu anasema ukaguzi wa aina hiyo hufanywa ili kubaini kuwapo kwa makosa ya kimahesabu ambayo yatawezesha kubaini makosa ya jinai na hatimaye wahusika kufikishwa mahakamani.


“Huu ni utaratibu au niseme ukaguzi wa hesabu ambao lengo lake huwa ni kutafuta ushahidi wa kuwapo kwa makosa ya jinai kama rushwa au matumizi mabaya ya fedha,” alisema mmoja wa wataalamu wa fedha katika Wizara ya Fedha na Uchumi (jina tunalo).


Moja ya mapendekezo ya Kamati teule iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani ambayo baadaye yaliazimiwa na Bunge ni kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye taarifa hiyo.


Katika taarifa yake, Kamati Teule ilisema utaratibu wa uchangishaji wa fedha Sh418.081 milioni uliofanyika katika wizara hiyo haukuwa na uhalali kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.


Kadhalika, Bunge liliazimia kwamba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) wa matumizi ya Sh214 milioni ambazo kati ya hizo, Sh126 milioni, Kamati Teule ilikataa maelezo ya matumizi yake na Sh88 milioni ni zile zinazotajwa kwamba zilitumika katika kugharimia semina kwa wabunge.


Azimio jingine ni lile lililoitaka Serikali iviagize vyombo vya dola kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za kughushi na ubadhirifu zilizoelezwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kama ilivyoelekezwa.


Kwa maana hiyo ikiwa uchunguzi na CAG utafanyika na kubaini jinai, huenda wahusika waliotajwa katika ripoti hiyo wakafikishwa mahakamani kwa makosa yatakayobainishwa.


Serikali katika hatua za mwisho
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge.


“Tuko katika hatua nzuri sana na ikiwa Spika atatupa nafasi katika Bunge hili, Serikali iko tayari kuwasilisha majibu ya jinsi tulivyofanyia kazi maazimio yale ya Bunge,” alisema Lukuvi.


Waziri huyo alisema Serikali tayari ilikuwa imekamilisha kazi yake lakini ilikuwa ikisubiri pande mbili nyingine muhimu ambazo zilikuwa zikikamilisha kazi yake ili taarifa kamili iweze kuandaliwa na kuwasilishwa kwa Spika.


Hata hivyo, Lukuvi hakuwa tayari kutaja pande hizo mbili muhimu zaidi ya kusema tu kwamba: “Wewe fahamu kwamba tumeyafanyia kazi maazimio ya Bunge na majibu yapo tayari ikiwa tutapewa nafasi hata kama katika Bunge hili.”


Uchunguzi zaidi umebaini kwamba pande hizo mbili ni Ofisi ya CAG na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ilikuwa ikiyafanyia kazi masuala ya kisheria katika maazimio hayo ya Bunge.


Majibu ya Serikali kuhusu maazimio ya Bunge yalipaswa kuwasilishwa katika Mkutano wa Sita wa uliofanyika Februari, mwaka huu lakini haikuwezekana kutokana na Serikali kutokuwa tayari.


Katika mkutano uliofuata wa saba ambao ulifanyika Aprili, mwaka huu, Serikali iliwasilisha taarifa hiyo lakini Spika Anne Makinda aliirejesha kutokana na kubaini kuwa majibu yake hayakuwa yakikidhi matakwa ya maazimio ya Bunge.


Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Bunge lilikuwa halijapokea taarifa au kusudio lolote la Serikali kuwasilisha majibu ya maazimio hayo katika kikao cha Bunge la Bajeti... “Kwa sasa sidhani kama kuna taarifa hiyo, ila wakiwa tayari nadhani watatuarifu na taratibu zitafuata.”


Maazimio ya Bunge
Mbali na kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa ziada ili kubaini iwapo kulikuwa na jinai katika sakata hilo pia kutaka Jairo achukuliwe hatua kwa kuvunja sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za umma, pia kulikuwa na maazimio mengine kadhaa likiwamo la Serikali kutumia mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuainisha taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa na mihimili mitatu ya Dola nchini katika kutekeleza majukumu yao.


Kamati hiyo iliutaja muundo wa Bunge kuhusu utaratibu wa sasa wa Serikali kuwa ndani ya Bunge, mawanda (scope) ya mamlaka ya Bunge kuisimamia na kuishauri Serikali na mawasiliano baina ya mhimili mmoja na mwingine hasa katika mambo yanayogusa haki na madaraka ya mhimili zaidi ya mmoja.


Bunge lilitaja eneo jingine kuwa ni mipaka na ushirikishwaji wa mamlaka mbalimbali ndani ya mhimili mmoja wa Dola katika utekelezaji wa majukumu ya mihimili hiyo kusimamiana, kurekebishana na kukosoana bila ya kuathiri masharti ya sheria na katiba (checks and balances).


Maazimio mengine ni sheria, kanuni na taratibu zilizopo kufanyiwa marekebisho ili kutoa nafasi kwa makatibu wakuu kuwashirikisha mawaziri katika uamuzi wa kiutendaji hasa katika matumizi ya fedha.


“Hatua hii itawapa fursa mawaziri kutekeleza vizuri zaidi majukumu yao wakiwa wasimamizi wakuu wa uamuzi wa shughuli za Serikali Wizarani,” inasomeka sehemu ya maazimio hayo ya Bunge.


Pia Bunge liliazimia Serikali ifanye mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuweka utaratibu utakaowezesha mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wanaoteuliwa na Rais inaposhughulikia masuala ya nidhamu, ifanye hivyo kwa kuyaarifu mamlaka hayo ya uteuzi na Waziri Mkuu ambaye ni msimamizi mkuu wa kazi za Serikali.


Liliazimia kuwa Serikali iunde chombo maalumu cha kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaoteuliwa na Rais na kwamba itoe mwongozo kuhusu malipo posho ya takrima, ili kuainisha viwango vya posho hizo.


Azimio jingine ni lile lililoitaka Serikali itoe mwongozo kuhusu idadi ya maofisa wanaopaswa kwenda Dodoma kwa ajili ya mikutano ya Bunge na katika mwongozo matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, yasisitizwe ili kupunguza idadi ya maofisa hao.
 
...........anafanya ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) ambao unaweza kubaini kuwapo kwa makosa ya kijinai katika utaratibu huo...

Kumbe neno forensic lina matumizi mengi zaidi ya biological aspect inayotumika kwenye makosa ya jinai, aiseeeeeeee! Kuna tofauti yeyote kati ya 'special audit na forensic audit'? kweli bado nakua.

Hivi na yule aliyemsafisha Jairo kitaalamu naye utahusishwa kwenye hii kesi? Maana naona kuna kama kujichanganya flani hivi hapa!
 
Back
Top Bottom