ManiTek TV
JF-Expert Member
- Jun 3, 2011
- 410
- 159
Ipad ndio tableti inayoongoza kwa mauzo katika soko Ulimwenguni kwa sasa, ingawa hisa ya mauzo ya tableti hii inaendelea kushuka mwaka hadi mwaka, utafiti unaonyesha kwamba hadi itakapofikia mwaka 2016 iPad bado itakuwa namba moja katika mauzo ya kompyuta za aina ya tableti pamoja na ushindani mkubwa unaotoka kwenye tableti za Android.
Hata hivyo ni wazi kuwa mauzo ya tablet kwa OS yatakuwa ni mbio za OS tatu, iOS, Android na Windows, hasa baada ya Microsoft kutoa toleo la Windows 8 ambalo ni lenye kulenga gajeti za skrini mguso. Utafiti huo umefanywa na kampuni inayoshughulika na takwimu za masoko ya bidhaa mbali mbali Ulimwenguni ijulikanayo kama International Data Corporation (IDC), ambapo hisa ya tablet za iPad ifikapo mwaka 2016 imetabiriwa kuwa ni 49.7% ya soko lote. iPad itafuatiwa na 39.7% ya Android. Windows nayo itapata ongezeko kubwa kutoka 2.9% mwaka 2012 hadi hadi 10.3% ifikapo mwaka huo.
Wakati Windows itapanda kwa kiasi kikubwa katika hisa hii, IDC imetabiri kwamba iPad na Android zote zitapoteza hisa kwa kiasi fulani. Hadi kumalizika kwa mwaka 2012 hisa ya iPad katika soko la tableti ilikuwa ni 53.8% kwa hiyo itashuka kwa 4.1%. Na Android itateremka kwa 3% kutoka 42.7%. Ipad pia imepoteza hisa ya 2.5% katika soko kutoka mwaka 2011 kwenda mwaka 2012. Hata hivyo iPad pasipo na matarajio ya wengi imefanya vizuri mno mwa mwaka 2012 kutokana na kampuni ya Apple kutoa tablet 3 kwa mwaka mmoja.
Apple mnamo wa mwezi wa nne walitoa iPad 3 na ilipofika mwezi wa 9 kwenda wa 10 Apple wakatoa iPad Mini na iPad with Retina Display, iPad Mini ndio iliyopata mafanikio makubwa katika mauzo, jambo ambalo limewashangaza hata Apple wenyewe. Itakumbukwa kuwa hayati Steve Jobs alipinga kabisa suala la kuifanya iPad kuwa ndogo kuliko 9.7" akidhani kuwa ukubwa chini ya huo hautavutia wateja kwa vile tableti itakuwa ndogo mno.
IDC pia imetabiri jumla ya tablet milioni 172 zitauzwa mwaka 2013 na ifikapo mwaka 2016 mauzo ya tableti yatapanda na kufikia milioni 282.7. Ni wazi kuwa tableti zinaelekea kuwa ndio kompyuta inayoongoza kwenye matumizi. Bado wapo wasioamini utabiri wa hayati Steve Jobs kwamba tumeshaingia kwenye "Post PC era" (kipindi cha PC kupitwa na wakati). Hoja kubwa za wanaopinga kompyuta kupitwa na wakati ni kuwa tablet haziwezi kufanya uandishi na kazi ngumu za kompyuta kwa vile hazina nguvu ya kutosha na pia nyingi hazina kibodi.
Tukiwa ni wenye kujiuliza swali hili, hivi karibuni tulibahatika kuhudhuria mhadhara wa Profesa Merlin Stone ambaye ni mwana masoko aliyebobea, tukamuuliza kama anadhani kuwa PC na laptop kweli zinatoweka na kupitwa na wakati, Profesa Stone alijibu na kusema "angalia ni kiasi gani cha muda wako ambacho unatumia kwenye simu na tablet halafu linganisha na muda unaotumia kwenye PC/laptop." Hivyo basi Profesa Stone naye anaungana na fikra za hayati Jobs kwamba huu ni wakati wa tableti na simu. Profesa Stone ametajwa kuwa ni mmoja kati ya watu 50 bora kifikra katika masuala ya masoko Duniani (marketing guru) hapo mwaka 2003. Pia ni mwandishi wa vitabu 30 tofauti katika fani za masoko, uchumi na usimamizi wa wateja (customer management). Ni mtu ambayo anapoongea huna budi kumsikiliza kwa makini sana.
Je unakubaliana na Steve Jobs na Profesa Merlin Stone? Weka maoni hapo chini.
Chanzo:
