umeshaandaa mrithi wako lkn kwa maana unaonekana umri umekutupa mkono, una labda 10-15 years max. left, sijawahi kusikia watoto wako wakiposti "historia ya muslims" nani ataendeleza kazi zako na maktaba yako au ndiyo utaenda na historia yako ya muslims? ...
Kijakazi,
Mtume Muhammad (SAW) amesema, ''Umma wangu umri wao ni miaka 60/70.
Mimi nina miaka 74.
Wewe unanipa miaka 10 - 15.
Hiyo mbona mingi sana?
Mimi nakula miaka ya bonus.
Niko departure lounge na tiketi yangu ni one way.
Nimeandika kila kitu nilichojifunza katika historia ya uhuru wa Tanganyika ila
vile ambavyo sikuwa na ithibati.
Nashukuru kuwa sitaondoka na kuingia mwanandani (kaburini) na elimu yangu.
Allah kanijaalia kuigawa elimu hii bila khiyana si hapa nyumbani tu bali hadi
nje ya Tanzania.
Hivi sikuviandika lakini katika mazungumzo nimepata kuwaeleza watu.
Mathalan kuna barua kati ya Mangi Mkuu Thomas Marealle na Ally Sykes wakati wa kupigania uhuru.
Chief Marealle na Abdul Sykes walikuwa marafiki wakubwa.
Nimeeleza urafiki wao huu katika kitabu cha Sykes.
Barua hizi zina mengi ambayo Chief Marealle alikuwa anahofia yatatokea
baada ya uhuru.
Hali kadhalika kuna barua za Mamboleo Makoko kwa Ally Sykes akimwandikia
kutoka London.
Hizi barua sikuzieleza katika kitabu cha Sykes kwa sababu ingebidi kupata
maelezo kutoka wote waliokuwa wanatajwa na wao niwasikilize.
Hili halikuwa jambo la busara nilivyoona kwa wakati ule.
Mifano kama hii ninayo mingi.
Haya ni maisha yangu sidhani kama ipo haja ya ati awepo mtu awe anafanya
haya niliyofanya mie.
Hii historia leo wapo walimu wanaisomesha kama historia nyingine zinavyosomeshwa.
''Kaka sijui kama una akiba ya picha hizi ziko Patwas Restaurant Tanga, kwenye hii nawatambua watu watano Mwalimu JK Nyerere na Bwana Sadiki Patwa kulia kwake unapoitazama picha. Kulia mwenye koti na kofia Mzee Rashid Makoko, babu yangu na wa pili yake baba yangu Rashid Mamboleo Makoko na kushoto mwenye koti na kofia Mzee Makata Mwinyimtwana wakiwa na baadhi ya Waasisia na wapigania uhuru wa Tanganyika.''
(Dessa Makoko)