Ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), wadau wasisitiza kuimarishwa kwa Utawala Bora, Uwazi na Uwajibikaji

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Muungano wa Asasi za kiraia zunazopambana na umaskini Tanzania (GCAP Tanzania Coalition), leo Septemba 14, 2023 umeshauri kuwa utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika ngazi zote ukiimarishwa itawezesha ugawanaji wa rasilimali za umma na kukuza ufanisi wa huduma ambao unazingatia usawa.

"Kuimarisha utawala bora uwazi na uwajibikaji katika ngazi zote ili kuhakikisha ugawanaji wa rasilimali za umma na utoaji huduma unakuwa wa ufanisi na unafanyika kwa usawa" Taarifa ya wadau hao imeeleza.

Akizungumza mbele ya wanahabari, Mratibu Kitaifa wa SHRiNGON Tanzania Chapter/ GCAP Tanzania Coalition amesema kuwa katika jitihada za kupambana na umaskini nchini kumekuwepo na changamoto ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji.

Akisoma tamko la pamoja lililoandaliwa na wadau wa umoja huo amesema kuwa ni muhimu kwa kipindi hiki utekelezaji wa malengo endelevu ya maendeleo (SDGs) kuona kuwa ni kwa jinsi gani kunakuwa na uwezesho wa kuboreshwa katika maeneo hayo mwili yaani utawala bora na uwajibikaji kwa kuwahusisha wadau na wananchi ili kuweza kupambana na rushwa nakuweza kutekeleza dhana nzima utawala bora.

Aidha Afisa Uchechemuzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Nuru Maro amesema kuwa Taifa linapofikia kilele cha kuadhimisha nusu ya safari ya SDGs kwa mwaka huu 2023 ambayo kilele chake ni mwaka 2030. Amesema kuwa wadau hao wanaungana na washirika wao wa kikanda na kimataifa kuadhimisha wiki ya hamasa ulimwenguni (15/8/2023 mpaka 19/9/2023).

Nuru Maro akizungumzia maadhimisho katika upande wa haki za binadamu amesema kuwa ni muhimu kuwatambua na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu nchini akidai kuwa ndio vinara katika kuongoza mapambano ya kupigania haki na usawa kwa watu wote.

"Watetezi wa Haki za Binadamu lazima walindwe dhidi ya vitisho, unyanyasaji na madhara mengine yanyoweza kuyapata wawapo kwenye majukumu yao. Ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira wezeshi ambayo yatawasaidia Watetezi hawa wa Haki za Binadamu Tanzania (HRDs) wenye kufanya kazi zao bila kuhofia usalama wao au mali zao. Tunaomba Mamlaka kuchunguza na kuishtaki kwa wakati ukiukwaji wowote wa haki zao mara zinapovunjwa wawapo kazini " amesema Nuru Maro

Hata hivyo itakumbukuwa Serikali ya Tanzania Kupitia Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (awali akiongoza Wizara ya Fedha na Mipango) katikati mwa Mwezi Julai 2023 akiwasilisha taarifa ya Pili ya Mapitio ya Hiari ya Nchi katika Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka programu na mipango mbalimbali ya kupiga vita umaskini, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya teknolojia, ujenzi wa miji salama, usawa wa kijinsia na mambo mengine kadha wa kadha, licha ya kudai kuwepo kwa baadhi changamoto mbalimbali alizodai kuwa zinaihitaji kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo hayo.

“Ripoti hii imeweka mikakati mbalimbali ya kufikia ajenda ya maendeleo ya 2030 kwa kuainisha masuala ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia na namna ya kuwawezesha vijana kupitia mipango yetu ya maendeleo ya kitaifa” alisema Dkt. Nchemba

Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni pamoja na ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2021 wastani wa kiwango cha upatikanaji maji maeneo ya vijijini kilipanda hadi kufikia asilimia 74.3 ikilinganishwa na mwaka 2019 kiwango hicho kuwa asilimia 70.1.

“Kuna ongezeko pia la upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme ambapo idadi ya watu wanaopata huduma hiyo imeongezeka kutoka asilimia 67.5 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 78.4 mwaka 2021.

Ikumbukwe Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) ni wito wa kimataifa wa kuchukua hatua kukomesha umaskini, kulinda mazingira ya dunia na hali ya hewa, na kuhakikisha kwamba watu kila mahali wanaweza kufurahia amani na ustawi. Umoja wa Mataifa (UN) umekuwa ukiratibu kwa ukaribu malengo hayo kwa nchini Tanzania kuona yakitelezwa kama ilivyokusudiwa.

Umoja wa Mataifa na washirika wake nchini Tanzania wamekuwa wakichukua jitihada mbalimbali ili kuhakisha Malengo 17 yaliyounganishwa kwa lengo la kushughulikia changamoto kuu za maendeleo zinazowakabili watu nchini Tanzania na duniani kote yanafikiwa, licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitajwa kama kisiki kufikia malengo hayo, Serikali kwa mara kadhaa imekuwa ikisika ikiwataka wadau hao kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kutekeleza malengo hayo.
 
Back
Top Bottom