Mwema ang`aka
2007-10-23 10:23:02
Na Mwandishi Wetu
Jeshi la polisi limeruhusiwa kisheria kutumia nguvu, hata kuua ikibidi, pale inapotokea raia kuvamia vituo vyao, kuvichoma moto, kuua au kutaka kutorosha watuhumiwa. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Bw. Said Mwema, alisema jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari juu ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, kuvamia vituo, kujeruhi polisi na kuua watuhumiwa.
Aliwataka raia kufahamu kuwa wanahatarisha maisha yao wanaposhiriki kwenye matukio kama hayo kwani Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Ibara ya 16 vifungu vya 18, 18b na 18c vinaruhusu matumzi ya nguvu katika kulinda maisha na mali.
Alitaja kifungu cha 29 cha Sheria ya Polisi kinaruhusu kutumia silaha ili kuzuia kutoroshwa kwa nguvu, watuhumiwa walio chini ya ulinzi na pia kuzuia polisi kukamata mtuhumiwa.
``Kuvamia vituo vya polisi, kuchoma moto, kutorosha watuhumiwa na hata kuwaua ni mazingira ambayo kisheria polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu na silaha na hata ikibidi kuua,`` alisema IGP Mwema.
Katika mkutano huo, Bw. Mwema alionya juu ya tabia ya kuwaua, kuwachoma moto na kuwatesa watuhumiwa mbalimbali mitaani na kusema vitendo hivi vinaendelea kujijenga kwenye jamii na vinahalalishwa kwa kisingizio cha `kupambana na wahalifu.`
``Vikiachiwa viendeelee vitazaa ukatili na kutengeneza mazingira yasiyoheshimu utawala wa sheria, watu kutoheshimiana na kuhatarisha amani na utulivu.`` Aliongeza kuwa huwezi kupambana na uhalifu kwa kufanya uhalifu mwingine na kwamba hiyo ni dhana inayohatarisha amani kwa jamii.
Bw. Mwema aliyekuwa na makanda wa jeshi hilo akiwemo Kamishna wa Polisi Zanzibar, Bw. Mohamed Simba, alikemea tabia ya kupambana na vyombo vya dola kama, polisi, mahakama na ofisi za serikali pale raia wanapodhani hawakutendewa haki na wanaowatuhumu.
Bw. Mwema aliwaona hata wale wanaovamia majengo ya ibada, ofisi za vyama, za serikali na za kazi.
``Kwa maoni yetu, hii siyo njia halali ya kushughulikia migogoro iliyoko katika jamii. Iwe ya kidini, wafugaji, wakulima, kisiasa na kadhalika,`` alisema.
Alisema uvunjifu huo wa amani hautaruhusiwa kuendelea na kwamba polisi itawaadhibu kisheria wanaoshawishi, kushiriki, kusaidia na kuchochea vitendo hivyo.
Aliwataka viongozi wote na kwa kila ngazi kupambana na uhalifu kwa kuwaelimisha wananchi kuacha uhalifu, mfano mauaji ya imani za kichawi, ubakaji, ulawiti na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Pia aliwataka wakemee uuaji wa vibaka kwa kisingizio cha `watu wenye hasira kali`, uvamizi wa taasisi za dola na pia kuelimisha jamii kuwa dawa ya uhalifu si kufanya uhalifu.
Mwezi huu matukio ya kujichukulia sheria mkononi yamejiri huko Singida ambapo wavamizi walivunja kituo cha polisi na kumua mtuhumiwa wa mauaji.
Wilayani Chato, Kagera wanavijiji walichoma makao makuu ya polisi ili kumuua mtuhumiwa anayedaiwa kukutwa akiwa na ngozi ya binadamu.
Huko Tanga raia walivunja ofisi ya kijiji kumuua mtuhumiwa wa mauaji aliyekuwa amefungiwa humo.
Wakati huo huo, Jumbe Ismailly anaripoti kutoka Singida kwamba Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilongero na watu wengine watano wanashikiliwa na polisi Mkoani Singida kwa tuhuma za kuvamia kituo kidogo cha polisi, kumshambulia askari na kumuua mtuhumiwa wa tukio la vifo vya watoto wawili wa familia moja.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bi. Celina Kaluba, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 20, usiku kwenye kituo kidogo cha polisi cha Ilongero, wilaya ya Singida Vijijini.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, wanaoshikiliwa kufuatia tuhuma hizo ni Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Issah Swedi, Hamisi Ally (Tall) (40), Yusufu Jumanne (19), Victor Soteli (30), Zena Yusufu (45), na Josephine George (Mwinda) (45), wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Ilongero.
Hata hivyo, Kamishna huyo alisema pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao, polisi bado wanaendelea kuwatafuta watu wengine ambao tayari wametambuliwa kuwa ndiyo walioongoza katika mashambulizi hayo na kusababisha mauaji ya mtuhumiwa huyo.
Bi. Celina alisema siku ya tukio, kulikuwepo na zaidi ya wananchi 200 wenye hasira kali, waliovamia kituo kidogo cha polisi Ilongero na hatimaye kumtoa nje kwa nguvu mtuhumiwa Khalfani Mohamedi maarufu kama Nkindwa Mile (28),ambaye alikuwa mkazi wa Kijiji cha Mrama, katika Halmashauri hiyo na kisha wakamuua kwa kumpiga mawe.
Aidha, Kamanda huyo alifafanua kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye sasa ni marehemu alikuwa amekamatwa Oktoba 20, 2007 usiku na kufikishwa kituoni hapo kwa kosa la mauaji ya watoto wawili, Twahiba Athumani (13), na Zulfa Athumani (7), Oktoba 14, mwaka huu.
Kamanda huyo alisema kwamba, wananchi hao waliokuwa na jazba walivunja mlango wa chumba cha mashtaka na hatimaye mlango wa chumba cha mahabusu, kwa kutumia mawe makubwa na kumtoa ndani hadi nje ya kituo mtuhumiwa, ndipo walipoanza kumpiga kwa kutumia mawe hadi kufa.
Baada ya kumuua, walimsogeza nje ya uzio wa kituo cha polisi na kumfunika kwa majani kwa lengo la kutaka kumchoma moto.
Lengo hilo halikutimizwa kutokana na kuwasili kwa askari kutoka Singida mjini na kuanza kuwatawanya kwa kupiga risasi hewani.
Kadhalika, Bi. Celina alisema kuwa kitendo hicho cha kufika askari kiliwazidishia hasira wananchi hao na kuanza kuwarushia mawe polisi.
Alisema kwamba gari la polisi lenye namba za usajili PT 0704, Landrover pick up, lilipigwa mawe na kuvunjwa kioo cha mbele.
Bi. Celina alisema amesikitishwa na kitendo cha wananchi hao cha kujichukulia sheria mkononi, hasa ikizingatiwa kwamba mtuhumiwa alikuwa tayari mikononi mwa polisi.
SOURCE: Nipashe