Mkuu Nyenyere, inawezekana kabisa ulielewa vizuri kilichoelezwa kwenye Darasa hilo, tena sana. Tafadhali fahamu kuwa, kutokana na ukweli kuwa Mfumo wa HISA (VICOBA/VSLA) umeonyesha mafanikio ya juu sana kwenye Malengo yake ya Msingi hasa lile Lengo la kupeleka na kumfikishia Mwananchi huduma za kifedha mahali ambapo huduma hizo zinazotolewa na Mabenki na Taasisi mbalimbali za kifedha (Micro Finance Institutions) haziwezi kumfikia, "Makanjanja" wameuingilia, wameubaka, wameuchakachua Mfumo huu kwa manufaa binafsi wenyewe. Hili linakuwa rahisi kwa kuwa uendeshaji wa Mfumo wa HISA "sio rasmi" - Hakuna Sera yoyote rasmi ya Serikali inayovisimamia, na wahanga ni Wananchi wasionacho, wenye elimu duni, shida kibao na ambao ni rahisi kutapeliwa na kudhurumiwa.
Hivyo, kwa ufahamu wangu, hakuna Benki yeyote iliyoteuliwa "kusimamia Vikundi vya HISA" na UYAKODE hawana dhamana ya kusimamia Vikundi vya HISA hapa Nchini. Huenda wakawa wanasimamia Vikundi ambavyo ni Wanachama wao, hilo haliwahalalishi wao kusimamia Vikundi vilivyo katika Mfumo huo. Huenda Masomo mliyopewa ilikuwa ni sehemu ya Benki hiyo kwa kushirikiana na UYAKODE, kujitafutia Wateja, na kwa mantiki hiyo Somo lao lililenga kuwarubuni hivyo.
Ninaomba nigeukie suala la Mwanachama na Kikundi cha HISA kulazimishwa kuwa na Akaunti ya Binafsi na ya Kikundi Benki. Moja ya Malengo ya Msingi ya Mfumo wa HISA ni kupeleka huduma za kifedha kwa Watu ambao Huduma za Benki na zile zinatolewa na Taasisi nyingine za Fedha, zikiwemo MFIs, haziwezi kuwafikia. Hapa tunaongelea watu ambao uwezo wao wa kujiwekea Akiba ni mdogo na au haupo kabisa, wanaoishi Vijijini na Mijini, Watu ambao hawana dhamana inayowawezesha kupata Mikopo Benki na kwenye Taasisi nyingine za Kifedha na Watu ambao ni gharama kubwa sana kwa Taasisi hizo za kifedha kuwafikishia huduma za Kifedha.
Chukulia kwa mfano, Mtu anakiji-mghahawa chake kijijini umbali wa Kilomita 20 kutoka Mjini kwenye huduma za kifedha. Akiba anayoweza kujiwekea Benki kutokana na biashara yake ni Sh. 500/= kwa siku baada ya kutoa gharama za uendeshaji wa mghahawa wake na maisha yake binafsi. Nauli ya kwenda na kurudi mjini ili kuhifadhi hiyo akiba yake ni Sh. 2,000/=. Ili asafiri kwenda Benki Mjini, atalazimika kufunga Mgahawa wake kwa masaa kadhaa na inawezekana siku nzima. Akifika Benki atalazimika kujaza karatasi, kujipanga foleni na, pengine, kuvumilia "unyanyapaa" wa Wafanyakazi wa Benki hasa kwa Mtu anayetaka kuweka kiasi kidogo cha Fedha.
Hivyo kwa Mfano huu mdogo sana, Mfumo rasmi wa Benki na Taasisi nyingine za Fedha hazipo kukidhi mahitaji ya Masikini huyu.
Hapa ndipo Mfumo wa HISA unapata nafasi ya kuziba hilo pendo. Kwa maana ya kumwezesha Mtu huyu kwenye Mfano huo, kuweka akiba yake kwenye Kikundi chake cha HISA, na kutumia Akiba hiyo kama Dhamana ya Mkopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli yake na au kukidhi mahitaji yake ya msingi. Kumbuka, kama ilivyoelezwa na Wachangiaji hapo kabla, Kikundi cha HISA kinaundwa na Wanachama wanaofahamiana na wanaokubaliana kwa hiari yao binafsi kuunda Kikundi hicho. Hivyo Akiba ya Wanachama, na kwa kiasi kidogo mapato mengine madogomadogo kama faini za Kikundi zinazotozwa kwa Mwanachama anayevunja Kanuni na Taratibu za Kikundi, ndiyo inyotengeneza Mtaji ambao unatumiwa na Kikundi kukopesha Wanachama wake. Kiasi cha Mkopo unaotolewa na Kikundi, kwa Mwnachama wake, kina uhusiano wa moja kwa moja na kiasi cha Akiba alicho nacho Mwanachama kwenye Kikundi. Hivyo inashauriwa, Kiasi cha Mkopo kisizidi mara tatu ya jumla ya Akiba (HISA) aliyonayo Mwanachama kwenye Kikundi. Hapa kuna maelezo zaidi.
Riba inayopatikana kwenye Mikopo inarudishwa na kutumika kutunisha Mtaji wa Kikundi kwa ajili ya kutoa Mikopo zaidi kwa Wanachama wake. Mwisho wa Kipindi ambacho Kikundi kinakuwa kimekubaliana wakati wa kuanzisha Kikundi, Kipindi ambacho huitwa "Mzunguko" na ambacho inashauriwa iwe miezi 9 - 12, madeni yote hurejeshwa, hesabu hu[pingwa ili kujua Kikundi kimetengeza "faida" kiasi gani, na faida hiyo hugawanywa kwa Wanachama kwa kuzingati ukubwa au udogo wa Akiba aliyenayo Mwanachama katika Kikundi. Hivyo "aliyepanda Kingi kama Akiba, anavuna kikubwa kama Faida, na aliyepanda kidogo kama Akiba/HISA, anavuna kidogo kama faida".
Nimeandika hayo yote kwa sababu mimi ni mnufaika wa miaka kadhaa wa Mfumo wa HISA, ninaumia kuona "makanjanja" wakiwemo Mabenki, Taasisi na Makampuni ya Biashara yanachakachua Mfumo huu wa akili ya kutengeza faida kwa migongo ya fukara na masikini na kwa ajili ya kuchokoza Mada ili Wataalamu wenye Ujuzi uliobobea katika Mfumo huu wajitokeze kutuelemisha.
Wasipojitokeza, nitaendelea kuandika ninachokifahamu ambacho kinaweza kuwa sio sahihi sana kutokana na mabadiliko na maboresho makubwa yanayoendelea kila kukicha katika Mfumo wa HISA!