Idadi ya watoto viziwi Mbagala yafikia 1,600 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Idadi ya watoto viziwi Mbagala yafikia 1,600

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, May 19, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  May 19, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,358
  Likes Received: 5,656
  Trophy Points: 280
  Idadi ya watoto viziwi Mbagala yafikia 1,600* Mkuu wa Mkoa sasa akiri , asema wamefikia 400

  Waandishi Wetu

  IDADI ya wanafunzi walioathirika na milipuko ya mabomu katika Shule za Msingi Mbagala Kuu na Maendeleo jijini Dar es Salaam, inazidi kuongezeka baada ya watoto 1662 kujitokeza kujiandikisha katika zoezi la kubaini walioathirika.

  Miongoni mwao ni wanafunzi 462 ambao walitajwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi jana kuwa wamejitokeza kuandikisha kuwa wameathirika na milipuko hiyo kwa namna mbalimbali, ikiwamo tatizo la kusikia vizuri.

  Ajali ya milipuko ya mabomu ilitokea Aprili 29 kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyo Mbagala na kuua wanajeshi sita na raia 20, huku yakijeruhi wengine kadhaa na kuharibu nyumba za wakazi wa jirani na kambi hiyo. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu na Maendeleo, ambazo zinapakana kwa karibu na kambi hiyo, waliliripotiwa kuathirika zaidi.

  Gazeti la Mwananchi liliripoti kuwa karibu watoto 200 walipata matatizo ya kutosikia vizuri na kuumwa kichwa, lakini siku moja baadaye Lukuvi alikanusha vikali habari hizo akisema hakuna mwanafunzi aliyepokelewa hospitali akiwa na tatizo hilo.

  Lakini jana wakati akitangaza kumalizika kwa zoezi la tathmini kwa walioathiriwa, Lukuvi alisema zaidi ya watoto 462 wamejitokeza kujiandikisha wakiwa na matatizo mbalimbali, yakiwemo ya kusikia.

  Wakati Lukuvi akitoa taarifa hiyo jana mchana, madaktari wa manispaa ya Temeke na walimu wa shule hizo kwa nyakati tofauti walilieleza gazeti hili kuwa hadi jana, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha na kugundulika kuwa na matatizo mbalimbali imefikia 1200.

  "Tumekuja na idadi ya wanafunzi 200 tuliopewa na manispaa kuja kuwafanyia uchunguzi, lakini tumefika hapa na kugundua kuna shule mbili ambazo wanafunzi wake wana matatizo mbalimbali," alisema Dk Laurent Chipata ambaye aliwauliza walimu wa Shule ya Mbagala Kuu kama wana orodha nyingine ya wanafunzi wanaohitaji huduma hiyo.

  Mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini kwa sababu ya serikali kuwapiga marufuku kuzungumzia masuala ya Mabomu, alimjini daktari huyo kwa kusema: "Wanafunzi tuliowagundua ni 842 ambao wana matatizo mbalimbali na kati yao, 287 wana matatizo ya kutosikia vizuri."

  Daktari huyo ambaye alifika katika shule hizo na jopo la madaktari na wauguzi akimwakilisha daktari wa Manispaa ya Temeke, Dk Sylivia Mamkwe, alisema kutokana na wingi wa idadi ya wanafunzi wanaohitaji uchunguzi, huduma hiyo sasa itachukua siku tatu badala ya siku moja.

  Hadi gazeti hili linaondoka eneo la tukio jana majira ya saa 9:00 alasiri, jopo hilo la wataalam lilikuwa limewafanyia uchunguzi wa masikio wanafunzi 20 na kubaini tatizo la hitilafu kwenye ngoma ya sikio.

  "Tangu nilipoanza kuwafanyia wanafunzi hawa, nimeibaini kuwa baadhi yao wana matatizo ya kusikia kwa sababu ngoma ya masikio imetingishika," alisema Dk. Chipata.

  "Ngoma ya sikio ina mfuniko mwembamba kuliko karatasi, nyuma mfuniko huo kuna mifupa mitatu ambayo kama mfuniko unapata mtikisiko, mifupa hiyo mitatu, inagongana na kusababisha sikio kuuma na kupoteza uwezo wa kusikia vizuri."

  Alisema pia kuwa muathirika anaweza kupoteza uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa maana ya kumtambua anayezungumza naye na mambo yaliyozungunzwa na kichwa kuuma wakati wote. Hata hivyo alisema tatizo hilo linatibika endapo mgonjwa anawahi matibabu.

  Kwa wa mujibu wa daktari huyo timu yake itawafanyia uchunguzi wa vipimo vingine, ikiwamo macho na kichwa.

  Habari zilizopatikana shuleni hapo jana zinasema kuwa walimu hao wamefanikiwa kubaini matatizo ya wanafunzi hao baada ya kuwafanyia uchunguzi kwa kutumia mafunzo malum waliyopewa na wataalamu kutoka shirika la kuhudumia watoto la Uingereza, Save the Children.

  Kwa mujibu wa walimu hao, shule hizo sasa zitafungwa bila wanafunzi kufanya mitihani ya kumaliza muhula isipokuwa kwa wanafunzi wa darasa la saba.

  Taarifa ya watoto 462
  Awali mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari kuwa ofisi yake ina taarifa ya watoto 462 waliojitokeza kujiandikisha.

  Lukuvi alitaja matatizo waliyopata wanafunzi hao kuwa ni pamoja na kutosikia vizuri.

  “Tumepata watoto 462 waliojiandikisha kuwa wameathirika na bado tunatoa wito kwa wengine kama wapo wajitokeza kujiorodhesha kwa matatizo yoyote ili watibiwe kwa gharama za serikali,” alisema Lukuvi.

  Mbali na athari hizo, mabomu hayo yalisababisha vifo vya wanafunzi watano wa shule mbalimbali za msingi kata ya Mbagala Kuu, akiwamo Mariam Musa (7) wa darasa la kwanza katika Shule ya Mbagala Kuu na John Joseph, darasa la tano wa shule ya Maendeleo.

  Katika hatua nyingine, Lukuvi amesema serikali imefunga rasmi kazi ya kutathmini thamani ya nyumba zilizoathiriwa na milipuko hiyo na kwamba sasa wanasubiri hatua nyingine.

  “Mpaka sasa tumepata nyumba 7,874 na sitaruhusu tathimini nyingine kwa kuwa kuna mchezo mchafu unafanyika. Nimekuwa nikipokea ripoti mpya tofauti kila siku, hivyo nimefunga rasmi kupokea tathimni mpya kuanzia jana (juzi),” alisema Lukuvi alipoongea na waandishi wa habari jana.

  Lukuvi alisema kazi inayofuata ni kuwapiga picha wamiliki wa nyumba hizo na wapangaji wao tayari kuanza kazi ya kuwalipa.

  “Tutawapiga picha wamiliki na wapangaji wa nyumba ili kujua idadi ya mali zilizoharibika, zoezi ambalo litafanywa na polisi,” alisema Likuvi na kuonya:

  “Kama kutakuwapo na udanganyifu wowote katika tathimini hiyo, sheria itachukuwa mkondo wake na hivyo watu wawe makini kusitokee udanganyifu wowote. Pamekuwa na siasa katika eneo hilo, polisi hawatafumbia macho udanganyifu utakaojitokeza, uwe wa tathimini za mali ama nyumba.”

  Kuhusu majeruhi wa milipuko hiyo, Lukuvi alisema wamebaki wagojwa watatu katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke ambao bado wanaendelea na matibabu.
  Lukuvi hakuwa makini
  Katika hatua nyingine, Chadema imesema kauli iliyotolewa na Lukuvi kuhusu wakazi wa Mbagala kuzoea milipuko ya mabomu kumeonyesha ni jinsi gani serikali ya CCM imepoteza dira.

  Ofisa habari wa chama hicho, David Kafulila aliiambia Mwananchi jana kuwa huenda Lukuvi wakati anatoa kauli hiyo hakuwa makini.

  Kafulila alisema kwamba Lukuvi asione haya katika hili ni busara akawaomba radhi wananchi kwa kuwa kuwaambia binadamu wenzake wazoee kifo badala ya kuwafariji kutokana na baadhi yao kuwapoteza ndugu zao, si sahihi.

  Alisema hali hii ya serikali kuwaumiza wananchi sio ya kwanza kutokea hapa nchini na kutoa mfano wa sakata la bomoa bomoa ya jalala la Tabata iliyofanywa na Manispaa ya Ilala na kuharibu mali nyingi za wananchi bila kujali. Imeandaliwa na Hidaya Kivatwa, Jackson Odoyo na Fred Azza
   
 2. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #2
  May 19, 2009
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 308
  Trophy Points: 180
  He....!!!

  Usinikumbushe tena mimi mambo ya Mbagala...!

  Wameambiwa na `Mwenye Mkoa` kwamba wazowee

  mabomu kama wa Kipawa walivyozowea ndege! Jamani!!

  So wenye ndugu waliokufa... wazowee hiyo hali.

  Waliopata Uziwi ...Wazowee!!

  Hivi kuna kitu kinachoitwa `kuzowea matatizo`?

  Embu wanaJF mliosoma sheria mniambie judicial redress

  kwa mtu anayeumizwa kiasi hicho!
   
Loading...