Wajasiriamali wadai kutapeliwa
Wamtupia lawama Luhanjo
na Mwandishi Wetu
WAJASIRIAMALI waliokuwa wamehamasishwa na serikali kuja kufanya maonyesho ya shughuli zao wakati wa Mkutano wa Nane wa Leon Sullivan, wameitupia lawama serikali wakidai kuwa imewatapeli.
Wajasiriamali hao, kutoka mikoa kadhaa hapa nchini na nchi jirani, walidai kutozwa fedha nyingi kwa ajili ya kupatiwa mabanda ya maonyesho, lakini wakatelekezwa.
Wakiongea na waandishi wa habari jana katika viwanja vya maonyesho ya Nane Nane eneo la Njiro, wajasiriamali hao walisema kuwa serikali kupitia kwa viongozi wa Chama cha Maonyesho ya Kilimo na Mifugo Tanzania (TASO), wamewasababishia hasara kubwa na wanajiandaa kutafuta wanasheria, ili wafungue kesi.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, Thomas Mollel, alisema kuwa kuna kina mama wametoka Mkoa wa Iringa na wamekodi gari aina ya Fuso kwa gharama kubwa, lakini hadi jana walikuwa hawajauza kitu hata kimoja na wala hakuna mtu aliyetembelea mabanda hayo.
Aidha, alisema kuwa kuna wajasiriamali wengine wametoka nchi jirani ya Kenya na wengine Zanzibar na wote hivi sasa hawajui watarejeaje makwao baada ya kupoteza gharama kubwa wakiwa mkoani Arusha, bila hata kupata chochote.
Alisema katika mabanda hayo, kuna wajasiriamali waliolipa kiasi cha dola za Marekani 4,000 ambao wametoka Kenya na Watanzania kulazimika kulipa sh 75,000 kwa siku tangu Mei 28 hadi jana bila mafanikio yoyote.
Wajasiriamali hao wametaka serikali kulipa gharama zote walizoigia kusafiri kutoka makwao hadi Arusha na hasara waliyoipata kutokana na maonyesho hayo.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa TASO, Peter Ngasa, ambao ndio wasimamizi wa maonyesho hayo yaliyofunguliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alikiri kutokea kwa hasara hiyo na kutupa lawama zote kwa wizara ya Mambo ya Nje.
Ngasa alisema utaratibu mzima wa maandalizi ulihusisha kuwepo kwa maonyesho katika viwanja hivyo vya TASO, lakini wanashangazwa na wizara hiyo kutoweka ratiba ya wageni hao kutembelea maonyesho hayo.
Aidha, akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa maofisa itifaki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, alisema kuwa utaratibu mzima wa mandalizi ya mkutano huo umeharibiwa na wajumbe wa kamati waliokuwepo mkoani Arusha kwa kipindi cha miezi sita kabla ya mkutano.
Alisema walichofanya wajumbe wa kamati hiyo ni kuandaa malazi ya wageni na si kushughulikia masuala mengine.
I think its too much ndio mana watu wamechokaaaa