Huu ni Ujasiri wa kijinga

Huu ni Ujasiri wa kijinga

KAUMZA

JF-Expert Member
Joined
Aug 31, 2010
Posts
699
Reaction score
240
Tarehe 23 mwezi aprili mwaka huu majira ya saa mbili usiku nilipokea ujumbe wa maandishi katika simu yangu kutoka kwa jamaa yangu mmoja akinishtua niangalie habari katika chaneli ya ITV. Wakati huo mimi nilikuwa naangalia katika chaneli nyingine. Bahati mbaya sikuweza kukiona kipande cha habari hiyo.

Hamadi!! Nilifanikiwa kuiona habari hiyo, ingawa nilichokiona sikuamini macho yangu. Nilidhani naota. Siku ya pili yake ilinibidi niingie katika youtube ili kuthibitisha kile nilichokiona kama ni kweli au zilikuwa ni ndoto.

Habari niliyoiona iliniumiza sana kana kwamba ni mimi ndiyo nilitendewa kitendo kile. Nilishuhudia kijana mmoja anayeonekana kuwa na akili timamu kabisa akimkunja askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza wajibu wake na kumnyang'anya ufunguo wa gari.

Kitendo kilichofanywa na kijana Yule ambaye sijui nimuite kwa sifa ipi ili imfae ni cha udhalilishaji wa hali ya juu kwa binadamu na kwa jeshi la polisi kwa ujumla wake. Nilitafakari na sikupata jibu. Ni nani asiyejua umuhimu na unyeti wa jeshi la polisi katika uhai wa jamii yoyote ile. Ni nani anayeweza kushabikia pindi anapoona jeshi la polisi linagaragazwa?

Katika siku za hivi karibuni vitendo vya kuwadhalilisha polisi na jeshi la polisi vimekuwa vikiongezeka sana. Miaka michache iliyopita, mfanyakazi katika ubalozi wa nchi moja ya Ulaya alifikia hatua ya kumtemea mate askari wa usalama wa barabarani kwa kuwa tu askari huyo alimsimamisha baada ya raia huyo wa kigeni kwenda kinyume na sheria zinazoongoza matumizi ya barabara. Si hayo tu, bali pia mwaka 2010 tulishuhudia mgombea mmoja wa ubunge akimkata mtama mkuu wa polisi wa wilaya moja katika moja za wilaya hapa nchini.

Ni vigumu sana kupita mwezi mmoja kama hujasikia askari wa polisi ameshambuliwa na watu wakati akitimiza wajibu wake. Wapo wanaouawa na mbaya zaidi wananchi wanathubutu hata kuvamia vituo vya polisi na kuvichoma moto.
Tumeshuhudia kuchomwa moto kwa kituo cha Hedaru ambapo mali na nyaraka za serikali ziliteketezwa, lakini pia tumeshuhudia mauaji ya askari wakiwa wanatekeleza kazi zao. Wananchi pia walimuua askari mkoani Tabora mwaka 2011 wakati akiwa katika operesheni ya kuteketeza mashamba ya Bangi.

Huwa najiuliza, je ujasiri huu wa raia katika kuwadhalilisha polisi, unatoka wapi? Inakuwaje kila anayesaka umaarufu mbele ya watu basi hakuna pa kuupatia zaidi ya polisi? Ukienda katika mikutano ya wanasiasa, ni vigumu kukuta mkutano umemalizika bila kuwatupia madongo polisi. Wasanii hasa wa vichekesho (comedians) huwa hawaamini kama kazi yao imekamilika kama hawataweka kejeli kwa jeshi la polisi.

Udhalilishaji huu kwa sasa unachupa mipaka hadi sasa vibaka nao, wanadhani wanaweza kuwachezea polisi.
Tunaweza kutafakari kwa pamoja. Kama inatokea mtu mwenye akili timamu anaweza kumdhalilisha askari mwenye sare kwa kumkunja mchana kweupe mbele ya kadamnasi, atashindwa vipi kumpiga na hata kumchania sare au kumnyang'anya silaha pale atakapokutana nae vichochoroni?

Lakini pia, tunaweza kujiuliza! Kama anaweza kumkunja polisi namna ile, je ikitokea amekasirishwa na raia mwenzake atampa adhabu gani?

Cha ajabu ni kuwa, watu hawa wanaolidhalilisha jeshi la polisi, wanashindwa kufahamu kuwa ujasiri wote walionao unatokana na kazi nzuri inayofanywa na jeshi la polisi katika kuhakikisha kunakuwepo na amani na usalama katika nchi yetu.
Watu hawa wanadhani vitendo wanavyovifanya kwa askari wetu labda vitawajengea woga katika kutimiza majukumu yao. Wanasahau kuwa hizo ni changamoto katika kazi na kwamba vitendo hivyo ndo vinajenga na kuamsha ari ya askari katika kupambana na uhalifu wa aina yoyote katika jamii yetu.

Wanasahau kuwa kama usalama usingekuwepo, inawezekana hata huo muda wanaoutumia katika kuwadhalilisha askari na jeshi zima la polisi wasingeupata.

Baadhi yetu wananchi hatuelewi dhana ya polisi jamii na pia dhana nzima ya Utii wa sheria bila Shuruti. Tunadhani, Utii wa Sheria bila Shuruti kunatokana na polisi kushindwa kutumia maguvu. Uhuru tunaopewa na jeshi la polisi tunautafsiri kama uoga na kushindwa kutimiza majukumu kwa jeshi hilo.

Tunasahau kuwa lengo la utii wa sheria za nchi bila shuruti ni kupunguza uhalifu na matumizi ya shuruti katika usimamizi ya utiifu wa sheria za nchi. Lakini pia utaratibu huu pia unasaidia kupunguza gharama katika oparesheni za kupambana na uhalifu.
Watu hawa wanapendelea jeshi la polisi linalotumia maguvu kama polisi wa kikoloni, ambapo polisi na raia walikuwa na mahusiano ya kiuadui. Raia alipokuwa akimuona polisi hata kama hana kosa, alikuwa akitimua mbio.

Askari naye ni binadamu. Anatakiwa apewe haki zake zote na heshima yake kama binaadamu. Kumdhalilisha askari ni kuidhalilisha serikali.

Binafsi nimekuwa nikifuatilia sana ripoti za kituo cha Sheria na haki za binaadamu (LHRC). Katika taarifa zake za haki za binaadamu, sijawahi kukuta mahali walipoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu unaofanywa na wananchi wakora kwa askari wetu. Swali za kujiuliza ni hili! Je, hawaoni ukiukwaji wa haki dhidi ya polisi? Au wanaona lakini wanafumbia macho ili polisi wachukue hatua katika kujihami na wao wapate cha kusema?

Wanaharakati ambao ninaamini kwa sauti waliyonayo wanaweza kukemea utovu wa nidhamu unaofanywa na raia dhidi ya askari. Watumie nafasi waliyonayo katika jamii katika kuhakikisha kuwa wananchi, wanaheshimu sheria kwa kuwaacha askari na watumishi wengine wafanye kazi zao walizokabidhiwa na umma.

Nimalizie makala haya kwa kuwaomba askari wasifadhaike kwa matukio yanayofanywa na raia wachache wasiothamini kazi nzuri ya polisi. Endeleeni katika kuilinda nchi yetu. Sisi raia wema tunathamini na kuijali kazi yenu. Zidisheni mapambano dhidi ya wahalifu popote pale walipo bila woga wala huruma. Pia niwapongeze askari wetu kwa uvumilivu mkubwa walionao, hii ni ishara kuwa wamefunzwa na wameiva. Na kwamba wapo tayari kukabiliana na changamoto yoyote inayojitokeza kwao kwa sura yoyote ile.
 
Vipi unaweza kumtetea na huyu au na kwakuwa kafinywa ASKARI mwenzio basi kelele keleleee!
attachment.php

View attachment 92319
 
Wape kichapo tu labda akili zao zitazinduka!Ni dalili mbaya,wananchi wameshawastukia unyanyasaji wanaoufanya kwa wananchi wao!polisi taratibu wameanza geuka maadui kwa wananchi badala ya kuwa watetezi wao.
 
askari wengi ni wanyanyasaji sana
wengi wana visasi
wengi wapenda rushwa na hawatumii busara kungamua jambo
wao wanajiona wako juu ya sheria zaidi wakati wanatakiwa kulinda sheria.
nadhani kichapo ni haki yao kwa wale wasiozingatia weledi wa kazi zao.
ukisoma katika machapisho unyanyasaji mkubwa hufanywa na polisi
sioni haja ya kuwatetea hapa.
 
Kiujumla umepotea mzee, binafsi niliangalia taarifa ya habari ITV siku ile, yule jamaa alimshika mikono tu yule traffic na ndipo alipoanza kutaka kujinasua toka mikononi mwa yule jamaa, hakuna udhalilishaji wa kutisha wala ukiukwaji wa haki za binadamu pale.

Hivi unazungumziaje uonevu wa polisi dhidi ya raia?, Tena wasio na hatia au wale wenye vikosa vya kuiba kuku, huku wakishirikiana na majambazi na wezi wakubwa?

Hivi unazungumziaje utumiaji nguvu kupita kiasi wa polisi, kama mauaji ya Mwangosi na namna walivyomkamata Mheshimiwa mbunge wa Arusha?

Ukiona raia wametaka au wamechoma kituo cha polisi jua kuwa wamechoka na unyanyasaji wa kutisha wanaofanyiwa na polisi, hawawezi kwenda kuchoma tu bila sababu ya msingi.

Binafsi sijaona lolote la kuwatetea polisi.
 
Mi naona........wote tuheshimiane......

WP Preta.....
 
  • Thanks
Reactions: Paw
Mleta uzi asingekuja na conclusion. Amani si matokeo ya kuwepo polisi au majeshi. Ni uzao wa nafsi zinazoridhika kutokana na kuwepo kwa haki. Labda mleta uzi si dereva au yuko kwenye tabaka lisiloguswa na hawa askari. Angeelewa madhila yanayowakuta watumia barabara angekuja na balanced story
 
mapolisi ndo wamejijengea uhasama na raia kwa vitendo vyao vya unyanyasaji,wanasahau kwamba na wao wanaishi kwenye society ya watu wanaoathirika na unyanyasaji wao,yaani polisi akishavaa magwanda tu anajiona anaweza akafanya unyanyasaji wowote kwa raia kwa kigezo tu amevaa uniform,na hapo raia akujitetea haki yake wanasema kavunja sheria,matendo ya polisi hasa hasa unyanyasaji wa watu wa hali ya chini ndo yanafanya wadharaulike na kutopendeka katika jamii.
 
Nafikiri kozi(mafunzo) ya udhalilishaji yaliyokuwa yakitolewa na askari kwa raia yamefika tamati na wahitimu(raia) wapo tayari kutekeleza mafunzo waliopata kwa vitendo.
 
Niliona akikunjwa vilivyo hahahahaaa! Wao pia waheshimu binadamu wengine, ingawaje police wananstahili kuheshimika ni vizuri pia na wao wakawa na heshima kwa watu wengine..
 
tanzania haina jeshi la polisi kuna genge la wahuni, wezi , wakabaji na wala rushwa.
kuna sheria gani inayo ruhusu askari wa uslama barabarani achukue funguo ya gari?
 
Mada yako ni Muhimu sana na kama kuna Polisi Mwenye Cheo cha Ofisa akisoma mada zinazotolewa hapa ampelekee IGP. Mchango wangu ni huu:-

Jeshi la Polisi katika nchi nyingi ni jeshi muhimu sana kama lilivyo JWTZ, tofauti zake ni kwamba JWTZ wanashughulikia kulinda mipaka ya nchi yetu. Jeshi la Polisi wanalinda Usalama wa Raia na Mali zao, kituo chao cha kazi ni Ndani ya Nchi.

Kitu kinachoitwa JESHI ni marufuku kukaa karibu na raia. Kosa kubwa lililopo hapa ni kuwaweka askari uraiani. Nitoe mfano wa kienyeji kulinganisha na hili, Mume ni kichwa cha nyumba au niite familia. Mume huyu kila kukicha anatoa maagizo kwa mke wake kujiepusha na UMBEA na mara nyingi kituo cha kupatia umbea ni kuketi pamoja akina mama na kuanza lecture za umbea. Mke anayemsikiliza vema mume wake akijiepusha na UKAAJI VIJIWENI KUPEPETA UMBEA kamwe hawezi kukumbwa na umbea. Uraiani ndiyo eneo la kazi la Polisi wetu kuja kufanyia kazi unapomuweka Polisi huyu aishi na watu ambao baadaye atakuja kuwakamata kwa ajili ya mahojiano fulani kuhusu tukio lililotokea USITEGEMEE UCHUNGUZI UTAKUWA BILA WALAKINI. Wahenga walishasema ZIMWI LIKUJUALO HALIKULI LIKAKWISHA. Polisi kuwa uraiani ni su-Sabotage kazi yao na kuhatarisha maisha yao. Ikiwa kuna mambo ya msingi kabisa ya Jeshi la Polisi kuweza kuyafanya basi ni kuwaweka hawa askari mbali na makazi ya raia.

Polisi Jamii ni janga lingine au niseme ni upanuzi wa wigo wa wahalifu waliobobea. Nasema Wahalifu waliobobea kwa sababu hadi sasa hawa vijana wanapata mafunzo ya kazi zao wakiwa kazini na sidhani kama hilo ni suluhisho la kupunguza uhalifu. Tumeshaona mara nyingi askari wakijihusisha na uhalifu halafu sasa tunaona vijana kupitia polisi jamii ambao ni vijana wasio na taaluma ya kijeshi wameingizwa katika jeshi la polisi kuashiria ni njia ya kupunguza uhalifu nchini. Sibezi hatua hii lakini tambueni kuwa hata polisi jamii nao wanajifanya maofisa wa jeshi la polisi "Baby Police" Suluhisho kwa hawa ni kwamba wapewe mafunzo wapewe miiko yao wajue mipaka yao ya kazi na nidhamu ya jeshi la polisi labda tutawaelewa, vinginevyo hawa baada ya kujua matumizi ya silaha tusishangae kuona mtandao mkubwa wa majambazi hapa nchini.
 
Nahakika mwandishi wa makala hii ni polisi, sielewi kwanini nae katumia nick name, imani kwa jeshi la polisi kwa wananchi wengi may be is only 20%, kama kuna hadi repoti za wao kuua raia, kubambikizia kesi, tena zingine kesi za mauaji n.k halafu eti mtu kufinywa kidogo tu unalalamika, hii ulipaswa kuipeleka pale polisi msimbazi na sio humu!
 
mi naona mleta mada ni askari na lengo lake ni kuwalalamikia kituo cha haki na sheria za binadamu kwa kutotoa tamko kushutumu kitendo alichofanyiwa askari mwenzao.
mi niliona ile habari japokuwa sijaweza pia kunote ni nani kati wa dreva wa daladala na yule mkwidaji alikuwa na haki, picha inaonyesha tukio la malumbano na askari kukwidwa, na pamoja na kuona hilo nisiseme uongo sijaweza hata kujudge kwamba mbaya ni nani. kwa sababu kwanza sijajua nan alikuwa na haki kati ya daladala na huyo mwenzie. pili askari nao mh! kama kuna askari wema ni wa kutafuta, wana mambo mengi sana kiasi cha kuwa kweli wanaweza kutokea kuonewa lakini wasipate simpathy yoyote hasa kutoka kwa raia, wajifikirie tu na wakubali kuwa wananchi hawawezi kuwafavour kirahisi kwa sababu ya character na behaviour zao towards wananchi wa kawaida, labda kwa wenzetu viongozi. kuna watu wanawatreat wenzao vibaya ila unawakuta wakitaka favour kwa watu hao hao, ukiwa mbaya kwa wenzio na wewe ukalipwa ubaya usilalamike.
 
Back
Top Bottom