Hukumu za Watawala; mtawala yeyote asome hapa

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,338
51,860
HUKUMU ZA WAFALME/RAIS

Na, Robert Heriel

Kuna mambo manne yanayomuongoza mfalme/rais katika kutoa hukumu. Mambo hayo ni pamoja na;
1. Sheria za nchi (au imani kama taifa linaongozwa kidini)
2. Hekima/ Akili
3. Maslahi
4. Baraza la washauri

Tangu zamani mambo hayo ndio humuongoza kiongozi mkuu wa nchi kufanya hukumu pale zinapotokea kesi/shauri mbele yake. Kwa zamani Mfalme alikuwa ndiye kila kitu, yeye ndiye Mfalme, Hakimu, Amiri jeshi Mkuu, Kuhani mkuu na vyeo vingine. Ingawaje baadhi ya vyeo aliweza kuvigawa kwa watumishi wake aliowateua lakini bado yeye alibaki kuwa top manyota na mtawala wa kila kitu ndani ya nchi.

Moja ya mambo magumu kwenye utawala hasa kwa ngazi ya Urais/ Ufalme ni pamoja na KUTOA HUKUMU. Hapa ndipo kizaazaa kilipo.

Hakuna jambo gumu kama kutoa HUKUMU na wafalme/Marais wote duniani wamepitia changamoto hii, na wamekiri iwe kwa kusema au kutenda kuwa kutoa hukumu ni jambo gumu kuliko mambo yote ndani ya utawala.

Unajua ugumu wa Kutoa hukumu unakuja wapi?
Ipo hivi; unapoingia katika kumiliki nchi, kutawala au kuongoza watu basi ni lazima kuna watu wamekufanya uwe hapo, yaani wanamchango mkubwa kukuweka hapo Ikulu au jumba la kifalme. Iwavyo vile watu hao lazima uwaheshimu, na uonyeshe unyenyekevu mbele yao hata kama utazuga kuwa watu kuwa huogopi mtu.

Hukumu inahitaji mambo matatu tuu;
1. Sheria
2. Ukweli (Ushahidi au Uthibitisho)
3. Haki

Rais/ Mfalme huongoza watu, na ili aongoze ni lazima watu hao wafuate sheria za nchi. Lakini pia lazima Mfalme au Rais awe anafuata kanuni na sheria za nchi husika. Sasa mambo hayawezi kwenda sawia mara zote hii ni kawaida hapa duniani. Lazima itokee uvunjifu wa sheria iwe umefanywa na wananchi au viongozi, na hapa ndipo hukumu inapoingia kwenye suala zima la utawala.

Hukumu ni rahisi endapo unamhukumu mtu ambaye amefanya kosa la wazi alafu sio ndugu yako, rafiki yako wa karibu, au jamaa. Hapo Mtawala hatakuwa na wakati mgumu kutoa hukumu.

Lakini Hukumu huwa ni kazi ngumu pale anapofanya kosa tena la wazi mtu wako wa karibu, iwe ndugu, rafiki, au jamaa yako wa karibu. HAapo ndipo kazi ya Urais. au Ufalme au Utawala huwa ngumu kabisa.

Sio kazi rahisi kuhukumu mtu wako wa karibu, sio kazi rahisi kujihukumu wewe mwenyewe kama umetenda kosa. Ingawaje inawezekana kwa wachache.

Mtu anapohukumu huangalia Maslahi yake. Yapo Maslahi ya aina nyingi kama nilivyotaja hapo chini
1. Maslahi ya kimahusiano
2. Maslahi ya kiuchumi
3. Maslahi ya Kisiasa (Cheo) N.k

Ni ngumu kutoa hukumu ya adhabu kwa mtu uliye na maslahi naye, kama Mama, Baba yako, ndugu, Rafiki, na jamaa unayemfahamu.
Ni ngumu kutoa hukumu ya adhabu kwa mtu ambaye unajua fika kuwa ukimuadhibu maslahi yako ya kiuchumi yatatetereka.
Ni ngumu Kumuadhibu mtu kwa haki ambaye unajua ataleta athari kwenye cheo chako. Ndio maana kazi ya Utawala ni ngumu sana hasa kwenye kipengele cha Kutoa Hukumu.

Nitatoa Mifano rahisi;

Mfano No 1 HUKUMU YA PILATO DHIDI YA YESU
MASLAHI YA KICHEO(Kisiasa)
Katika kisa cha Hukumu ya Mfalme Pilato na Yesu tunaweza kuona na kujifunza mambo kadhaa.
Kisa chenyewe kwa Ufupi.

Yesu amekamatwa kwa hila. Anapelekwa kwa Mfalme Herode kuhukumiwa, Mfalme Herode anaona ugumu wa kumhukumu Yesu kwani haoni hatia. Anamtupia Mpira Mfalme Pilato kukwepa lawama. Mfalme Pilato naye anagundua Yesu hana hatia. Anarudisha Mpira kwa Mfalme Herode. Herode kuona zengwe linaweza kumuangukia, anaamuru Yesu achapwe viboko vya haja kisha aachiwe. Wanamchapa, lakini watu na wazee wa baraza wanasisitiza Yesu Asulubishwe. (Nauona ugumu anaoupata Mfalme Herode) Kwa ujanja tena Mfalme Herode anawaagiza wampeleke tena Yesu kwa Mfalme Pilato.

Hapa tayari watu wamechoka kuzungushwa mara kwa pilato mara Herode. Raundi hii wamedhamiria wakifika kwa Mfalme Pilato lazima Hukumu ya kusulubiwa kwa Yesu itoke. Wanaimba na kupiga kelele(wanafanya maandamano mpaka kwa Pilato).

Masikini Pilato! Mzani unalalia kwake licha ya kujitahidi kuukwepa. Mbaya zaidi Mke wake anamtumia ujumbe kuwa ameota ndoto kuwa mtu huyo(Yesu) ni mwenye haki hivyo asijetoa hukumu ya kumsulubisha. Pilato mwenyewe anajua kuwa Yesu hajatenda kosa lolote, hivyo anaona ugumu wa kumhukumu adhabu mtu mwenye haki.

Kwa ujanja Pilato anapata wazo, anamkumbuka BARABA ambaye ni mhalifu aliyefungwa jela. Sasa Pilato anapata ahueni kwa kuwa anajua akimleta Baraba mbele za watu kisha awaambie wamchague ni nani asulubishwe, basi watu wangesema Baraba. Wazo hili akalipa heko huku akishukuru.

Masikini! Mfalme Pilato anamtuma Liwali awaulize watu kati ya Baraba na Yesu nani Asulubishwe. Watu wote wakajibu; Asulubishwe huyo Yesu.

Unajua kwa nini watu walisema haYO? Jibu ni kuwa kuna wazee wa baraza waliunda vijana wakawashawishi waseme asulubiwe Yesu. Hivyo kwa sehemu kubwa watu waliokuwa siku ile katika Hukumu ya Yesu walishawishiwa na Wazee wa Baraza, hasa viongozi wa dini(Mafarisayo wakaao mbele ya Mfalme)

Kufikia hapo Pilato hakuwa na ujanja. Alikuwa na machaguo mawili. Mosi, asisaini hukumu ya Yesu alafu naye aache kuwa Mfalme(Kumbuka ulikuwa mwaka wa uchaguzi), au Akubalie wale watu kisha amhukumu Yesu.

Mfalme Pilato aliyaona maslahi ya kisiasa(cheo cha ufalme) kuwa ni bora, hivyo akakubali yaishe. Yesu akasulubiwa.

Katika kisa hicho tunaona mambo mawili yaliyomsukuma Mfalme Pilato kutoa hukumu isiyo ya haki

1. Maslahi ya kisiasa (Kicheo)
2. Baraza la wazee waliowashawishi watu kumshinikiza amhukumu Yesu.

MFANO WA 2. MFALME DAUDI NA AMNONI
Maslahi ya Kimahusiano.

Katika sheria za kiyahudi kwa zama za kale, moja ya makosa ambayo adhabu yake ni kifo ni pamoja na Kufanya uzinzi.
Taifa la kiyahudi liliongozwa kwa Torah(Torati) ambayo waisrael waliamini zilitolewa na Mungu wao.

Amnoni ni mtoto wa kwanza wa Daudi kwa mke wake aitwaye Ahinoamu. Huyu ndiye First-Born wa Daudi.

Sasa Amnoni alimtamani Dada yake ambaye amezaliwa na Mke mdogo wa Daudi aitwaye Maaka. Dada huyo aliitwa Tamari. Amnoni baada ya kufanya hila alifanikiwa kulala na Tamari(Baba mmoja Mama mbalimbali). Habari hizi zikamfikia mfalme licha ya kuwa zilienea mji mzima.

Hukumu inafahamika kwa mtu aliyefanya jambo hili; alipaswa kuuawa lakini Mfalme Daudi alishindwa kutoa hukumu hiyo.

Unajua kwa nini?
Kwa sababu Biblia inasema Mfalme Daudi alikuwa akimpenda sana Mwanaye Amnoni. Huenda ni kwa sababu ni mwanaye wa kwanza.

Tunaona maslahi ya kimahusiano yanavyoathiri hukumu kwa Mfalme Daudi licha ya sheria za nchi kuelekeza kuwa Amnoni anatakiwa kuuawa.

Hatimaye tunamuona Absalomu ambaye ni kaka yake Tamari wakuzaliwa(Baba, Mama mmoja) akiamua kumuua Amnoni(kaka yake Baba mmoja mama Mbalimbali). Hii ni kulipa kisasi cha Dada yake Tamari aliyebakwa na hakuna hukumu iliyotolewa.

Kisa hiki tunaona mambo mawili
1. Jinsi maslahi ya kimashusiano yalivyoathiri hukumu
2. Matokeo ya Maslahi ya kimahusiano yanavyoweza kusababisha uasi. Kwani baadaye Absalomu alikuja kuasi na kutaka kumpindua Baba yake ambaye ni Mfalme Daudi.

Baada ya maelezo hayo nafikiri tumepata mawili matatu.

Kuhukumu ni kazi ya Mungu kama zilivyokazi nyingine kama utabibu, ualimu, uinjinia, udereva miongoni mwa kazi zingine. Unapohukumu lazima ujue unafanya kazi ya Mungu, hivyo lazima utende kwa haki.

Biblia inasema; Usiwe na mawe mawili ya kupimia. Bali utende kwa haki.
Pia inasema, usimuonee huruma masikini kwa sababu ya umasikini wake, wala usimpendelee tajiri kwa utajiri wake. Bali kila mmoja umhukumu sawa sawa na anavyostahili.

Biblia inasema; Jicho lako lisiwe na huruma, uwe jasiri na hodari unapotoa hukumu kwani wakati mwingine anaweza akakosea hata Mama, au Baba au mtoto au ndugu au rafiki yako, hivyo usionee huruma, hukumu watu wote kwa usawa.

Nashauri walioko kwenye utawala;
Najua changamoto za kutoa hukumu hasa ukiziona zinaweza athiri ugali wako au cheo chako. Lakini ni heri utende haki bila kujali maslahi yako binafsi kama alivyofanya Gideoni.

Habari za Gideoni nitazileta panapoo majaliwa. Kifupi Gideoni alimuua Mwanaye(Binti yake wa pekee) kwa sababu mambo haya haya.

Poleni kwa andiko Refu. Natumai limetusaidia wote.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam
 
Back
Top Bottom