Dakika chache baada ya Jaji Salum Masati kuwaachia huru washitakiwa hao baada ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, kushindwa kuwatia hatiani, mayowe yalisikika mahakamani hapo yakitaja jina la zombe, zombe zombe kama ishara ya kufurahiswa na hukumu hiyo.
Hata hivyo, sambamba na washangilia ushindi huo, baadhi ya wananchi waliokuwepo mahakamani hapo walionesha hisia za kupinga wazi wazi uamuzi huo wa mahakama kwa kuzomea na kupiga mawe magari ya polisi yaliyokuwa mahakamani hapo. Awali, akisoma hukumu, Jaji Masati alisema kuwa, vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka ni vya kimazingira na hafifu na kwamba vimeshindwa kubainisha pasipo shaka kuwa, washtakiwa hao walitenda kosa hilo.
Sakata zima la kesi hii ya Zombe mwanzo mwisho (A-Z) linatiririka kama hivi: Januari 14, 2006 (mauaji) Oysterbay wawatia mbaroni wafanya biashara hao. Askari kutoka katika vituo vya polisi Chuo Kikuu, Urafiki na kuwatia mbaroni wafanyabiashara hao eneo la Sinza Palestina wakiwatuhumu kuhusika na uporaji wa pesa za Kampuni ya Bidco katika Barabara ya Sam Nujoma.
Januari 15, 2006: Zombe atamba kuua majambazi sugu. Januari 16/ 17 2006: Utata waibuka waliojitambulisha kuwa ni ndugu wa waliouawa wafika kwenye vyombo vya habari na kudai kuwa waliouawa ni ndugu zao na kwamba hawakuwa majambazi bali walikuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Wilaya ya Mahenge mkoani Morogoro. Vyombo mbalimbali vilifanya utafiti dhidi ya utata huo lakini Kamanda Zombe alisisitiza kuwa ni majambazi, alidai wao ni wataalamu ndiyo wanaojua majambazi na wafanyabiashara .
Vyombo vya habari vyajikita kufanya uchunguzi eneo la Sinza kwenye Ukuta wa Posta alikosema Zombe kuwa ndiko walikouliwa wafanyabiashara hao baada ya kurushiana risasi na polisi, wananchi wa eneo husika wakana kusikia milio ya risasi katika eneo hilo kwa siku iliyotajwa. Baadhi ya vyombo vya habari vilienda katika kampuni ya Bidco kuthibitisha madai ya kuporwa pesa. Bidco walikiri kuporwa pesa lakini walikana kuwa alizozionyesha Zombe siyo zao na kwamba za kwao zilikuwa hazikufungwa.
Vyombo vya habari vyamuuliza Kamanda Zombe kuhusu utata huo, lakini Zombe alishikilia msimamo wake na kufoka kuwa asifundishwe kazi. Januri 23, 2006: Rais Jakaya Kikwete aunda Tume ya Jaji Kipenka kuchunguza ukweli wa mauaji hayo. Januari 24. 2006: Tume yaapishwa na kupewa siku ishirini na moja za kufanya kazi siku hiyo hiyo ilianza kazi kwa kuweka sawa mikakati.
Januari 25, 2006: Tume yatoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuwataka watu wote wenye taarifa zozote kuhusu mauaji hayo wajitokeze kutoa ushahidi mbele ya tume hiyo. Januri 26, 2006: Tume yaanza kuwahoji mashahidi katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ilianza na askari waliohusika na wananchi wa kawaida, yahoji watu zaidi ya 90 Dar es Salaam, Arusha na Mahenge Morogoro. Mbali na kuandika yatumia vinasa sauti 36 kuhifadhi kumbukumbu za mahojiano.
Tume ilikabidhi ripoti kwa Rais Februari 17, 2006 Februari 20, 2006 mwanzo wa kesi askari kumi na moja bila Zombe walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za mauaji ya wafanyabiashara hao na kusomewa mashtaka ya kuua kwa kukusudia. Juni 9, 2006: Zombe apandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya mauaji peke yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Addy Lyamuya.
Juni 15, 2006: Zombe afutiwa shitaka la mauaji ya wafanyabiashara hao lililokuwa likimkabili peke yake na kuunganishwa na washtakiwa wenzake kumi na moja mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Sivangilwa Mwengesi na kuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.
Septemba 28, 2006 Washtakiwa wote walipandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mbele ya Jaji Laurean Kalegea . Mei 2008: Kesi yaanza kusikilizwa chini ya Jaji Kiongozi Salum Massati sehemu hiyo ya kwanza ilisikizwa kwa awamu tatu.
Mei 26, 2008: Mahakama yaanza rasmi kusikiliza ushahidi kutoka upande wa mashtaka. Mei 30, 2008: Zombe awawakia waendesha mashitaka awatuhumu kuwa wanachelekewesha kesi kwa makusudi kwa kuandaa mashahidi wachache ili waendelee kupata posho kubwa kutokana na kuendesha kesi hiyo.
Juni 9, 2008: Mashahidi wadai wao ndiyo majambazi ni shahidi wa ishirini na tano upande wa mashtaka (PW 25 Shabani Sain Manyanya) na PW 26 Ramadhan Said Tupa wadai wao ndio walipora pesa za Bidco ambazo washtakiwa walidai ziliporwa na marehemu (wafanyabiashara). Waliwaacha midomo wazi wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo mahakamani. Juni 12, 2008: mwisho wa awamu ya kwanza ya sehemu ya kwanza jumla ya mashahidi 29 watoa ushahidi.
Septemba 1, 2008, awamu ya pili (sehemu ya kwanza) shahidi afichua siri ya mauaji ni PW 30 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Emson Mmari alikuwa mjumbe kwenye timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema kuchunguza chanzo na ukweli wa mauaji hayo na alikuwa akifanya kazi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, alielezea mahakama kuwa wafanyabiashara hao waliuliwa katika Msitu wa Pande ulioko Mbezi Luis, alidai kuwa walikuwa wakirushwa kwenye gari mmoja mmoja na kulazwa chini na kupigwa risasi.
Septemba 2, 2008: Mahakama yazuru eneo la mauaji.
Mahakama ilianzia Sinza walikokamatwa wafanyabiashara kabla ya kuuawa kisha ikaenda Barabara ya Sam Nujoma lilikodaiwa gari la Kampuni ya Bidco lilikoporwa pesa, halafu Sinza Ukuta wa Posta yalikodaiwa kutokea mapambano baina ya polisi na wafanyabaishara waliouawa kisha mahakama ikaenda Msitu wa Pande. PW 30 alionyesha mahakama mahali wafanyabiashara walikolazwa na kupigwa risasi.
Yamaliza Bunju kulikodaiwa kuwa mshtakiwa wa pili alilazimisha baadhi ya washtakiwa wafyatue risasi hewani ionekane silaha zilitumika kwenye mapambano, wananchi waliwazomea akina Zombe.
Zombe, Koplo Lema wazozana Zombe na aliyekuwa mshtakiwa wa kumi na moja Rashid Lema wazozana chini kwa chini baada ya Zombe kuonyesha kushangaa msitu huo na kudai hajawahi kufika katika eneo hilo.
Septemba 7, 2008 Mwisho wa awamu ya pili sehemu ya kwanza jumla ya washahidi watatu tu ndiyo walioweza kupata nafasi walitoa ushahidi na kufanya mashahidi kufikia 32. Septemba 26, 2008 . Upande wa mashtaka wafunga ushahidi katika awamu ya tatu ya sehemu ya kwanza iliyoanza Septemba 22.
Februari 3, 2009. Sehemu ya pili utetezi Februari 4, 2009 Hoja ya utetezi. Mawakili upande wa utetezi wawasilisha hoja zao wakijaribu kupangua ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka wadai wateja wao (washtakiwa) hawana kesi ya kujibu kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka juu yao. Waiomba mahakama iwaachie huru . Febuari 5, 2009. Hoja upande wa mashtaka: Waendesha mashataka (PP) wajibu hoja za utetezi huku wakirejea ushahidi walioutoa wadai washtakiwa wote wanahatia.
Februari 9, 2009: Uamuzi wa Jaji Massati kuwaachia huru washtakiwa watatu PC Noel Leonard (4) Koplo Moris Nyengelela (6) na Koplo Felix Cedric (8) asema hawana kesi ya kujibu Zombe na wengine tisa wabanwa jaji asema wanakesi ya kujibu Zombe ataka aanza kujitetea siku hiyo . Februari 10. 2009: Zombe ajitetea apanda kizimbani na muongozo wa utetezi wa Jeshi la Polisi General Order (PGO). Ajitetea kwa saa tatu kesi yaahirishwa bila kumalizika.
Februari 12, 2009: Bageni naye kizimbani. Zombe amalizia utetezi wake na kueleza kilichomsikitisha ni kitendo cha kubambikiwa kesi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa zamani (DPP) Godfrey Shahid ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu.
Atumia saa nane kujitetea; mshtakiwa wa pili SP Christopher Bageni, Mkuu wa Upelelezi naye asononeka kizimbani ajitetea lakini naye aeleza kuwa anamlilia dada yake baada ya kusikia amekamatwa (Bageni) Februari 15, 2009 Makere alia na Zombe ni mshatakiwa wa tatu ASP Ahmad Makele Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki akili kuwakamata marehemu wakiwa hai lakini awatupia mpira askari wa Chuo kikuu kuwa wao ndiyo walioondoka nao na kusema Zombe alimbambikia.
Febuari 19, 2009, Koplo Lema bado hoi ashindwa kufika mahakamani kujitetea. Zamu yake mshtakiwa wa kumi na mbili Koplo Rajab Bakari, naye akwama kujitetea akidai kuwa kuna maneno ambayo ni lazima Koplo Lema aseme kwanza kwa mdomo wake ndipo na yeye aweze kujitetea.
Machi 2, 2009 Koplo Lema alazwa. Hali yake yabadilika na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa matibabu.
Machi 3, 2009: Ahamishiwa Hospitali ya Muhimbili Mchi 19, 2009: Ahamishiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road Aprili 3, 2009, Aaga dunia saa kumi alfajiri katika Hospitali Bingwa ya magonjwa ya saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Aprili 21, 2009: Wakili wa Zombe Moses Mailla alifariki dunia saa tano na adhuhuri kwa ugonjwa figo katika Hospitali ya Bentab Memorial Houston Texas nchini Marekani alikokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu.
April 28, 2009. Mahakama yafuta mashtaka rasmi dhidi ya Koplo Lema . Koplo Rajabu Bakari atoboa siri ya mauaji ajitetea kwa saa tano na dakika kadhaa akili kushuhudia mauaji na kuelezea ilivyokuwa hatua kwa hatua na kudai tukio hilo lilikuwa kubwa kwake hajawahi kuona aeleza viongozi wake kuficha ukweli wa tukio hilo huku wakitishiwa kuwa atakayetoa siri atabebshwa msalaba mwenyewe.
Aprili 29 na 30, 2009 Kesi yaahirishwa mara mbili baada ya wakili wa mshatakiwa wa kumi na mbili Denis Msafiri augua na kushindwa kuhudhuria mahakamani.
Mei 4, 2009: Zombe aomba kujiteta upya shahidi amwacha Zombe njia panda pia alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa na simu mahabusu vocha na pesa walizokuwa wanazitumia kuwasiliana na DPP na kwamba mkuu huyo wa Gereza la Ukonga ni shahidi wake.
Mei 5, 2009 Jaji Massati amgomea, adai sababu zake si za msingi. Asema hatua hiyo itaathiri mwenendo mzima wa kesi, Mawakili wa mshtakiwa wengine nao wamwekea ngumu. Mei 6, 2009: Mahakama yafunga rasmi ushahidi wa utetezi. Na kutaja tarehe nyingine ya mahakama.
Mei 7, 2009: Mawakili wa utetezi watupa karata yao ya mwisho kuwanasua wateja wao walia maelezo ya Koplo Lema wakiisihi mahakama isiyatumie katika mwenendo wa kesi hiyo. Juni 25 2009 upande wa mashtaka wajibu hoja ya utetezi wadai waweza kuthibitisha juu ya washtakiwa wote na kwamba wote wanahatia wamchambua mshtakiwa mmoja mmoja na kueleza jinsi walivyothibitisha mashtaka dhidi yake.
Juni 26, 2009: Majumuisho. Maoni ya wazee wa Baraza wamtakasa Zombe wadai hana hatia kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake kwa kuwa katika mashahidi wake 37 hakuna hata mmoja aliyeweza kuthibitisha Zombe kuhusika na mauji hayo moja kwa moja.
Agosti 17, 2009: Hukumu!!! Washtakiwa wengine waliobaki katika kesi hiyo baada ya wengine kuachiwa huru na mwingine kufariki Dunia ni pamoja na ACP Abdallah Zombe SP Christopher Bageni, ASP Ahmes Makele WP 4595 Jeni Andrew Koplo Emmanuel Mabula PC Michael Sonza CPL Ebeneth Salo C/CPL Rajab Bakari na D Koplo Festus Gwabisabi.
Wakati huo huo, jana majira ya saa 11 jioni, Uwazi liliongea na Mbunge wa Ulanga Mashariki, wanakotoka wafanyabiashara hao waliouawa, Mhe. Celine Ompeshi Kombani (CCM), ambaye alikiri kuwa marehemu walikuwa ni wapigakura wake na kusema kwamba hana cha kuchangia kwenye maamuzi yaliyotolewa na mahakama ila kama imeamua kuna watuhumiwa waliohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua stahili.
Nikweli marehemu walikuwa ni wapiga kura wangu ila kama mahakama imeamua sina cha kusema, kwani hayo ni masuala ya sheria, lakini kama pia imesema kuwa kuna watuhumiwa ambao walihusika basi watafutwe na sheria ichukue mkondo wake, alisema mbunge huyo kwa njia ya simu kutoka Morogoro alikokuwa kikazi.