Hapo kwenye red kuna walakini hebu soma hapa chini ushahidi wa Mh. Tundu Lissu (MB) kama ulivyonukuliwa kwenye utetezi wake kwenye kamati haki, maadili na madaraka ya Bunge.
JAJI WA RUFAA MBAROUK SALIM MBAROUK
Mbarouk Salim Mbarouk aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania mwaka 2008. Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa zimeainishwa katika ibara ya 118(3) ya Katiba:
Majaji ... wa Rufani watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ... zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano.
Kwa mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba ya Zanzibar, 1984,
Mtu hatoweza kuteuliwa kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu mpaka awe na shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha aina hiyo; au awe au amewahi kuwa Jaji wa Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi zote za jinai na madai katika Tanzania au sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au awe Mwanasheria wa Zanzibar au Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka saba; au awe na uzoefu wa Jaji au mwanasheria kwa pamoja usiopungua miaka saba.
Jaji Mbarouk hajatimiza hata moja ya masharti hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu hana shahada yoyote ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanzania kama inavyotakiwa na Ibara ya 109(7) ya Katiba.
Jaji huyu ana stashahada ya juu ya sheria (Post Graduate Diploma in Law) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha nchini Uingereza.
Uteuzi wa Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minongono mingi katika taaluma ya sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga anasemekana kufungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo, Wakili Kalunga alifariki kabla ya shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo liliondolewa mahakamani.
Aidha, monongono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi ninapoandika Addendum hii.