Huenda hii ndio sababu ya Afande Sele, kugombana na wasanii wenzake

Intelligent businessman

JF-Expert Member
Sep 6, 2022
26,126
52,881
Kabla hujaanza kusoma vizuri, naomba kwanza urejee kichwa cha habari hapo juu, kielewe vizuri halafu ndiyo uendelee kusoma,

Binafsi ukija kwa mbele yangu na kunitupia swali la haraka, kutaka nikutajie wasanii watano ambao nawakubali sana,

Basi jina la Mfalme wa Rhymes (Afande Sele) litakuwa miongoni mwao,

Kwanini???

Afande ni miongoni mwa Wasanii ambao nawaelewa sana nyimbo zao, enzi za kutamba kwake kwenye gemu, Afande Sele alikuwa Balozi mzuri sana wa jamii ya watanzania,

Kwa sababu Mshikaji alikuwa anaimba nyimbo zenye kugusa jamii,

Mwenyewe katika kiitikio cha wimbo wa Ndugu Zangu anasema....

Napenda ndugu zangu
toka moyoni mwangu uuhh, siwezi idharau nchi yangu,

kutenga ndugu zangu

kwa iman yangu itakua dhambi mbele za mungu


Ndugu hao ambao Afande Sele amewaongelea katika wimbo huo, ni sisi Watanzania wenzake,


Ni wimbo mzuri sana ambao mtu ukiusikiliza unapata mambo mawili kwa wakati mmoja,

Kwanza kuelimika, wimbo huo unakuelimisha vizuri sana,

Pili burudani ambayo mtu unaipata wakati wa kuisikiliza ngoma hiyo, lakini pia Afande Sele kama binadamu ana kasoro zake, na moja ya kasoro yake kubwa, ni kupenda kuwapangia wasanii wenzake nini cha kuimba,

Kivipi???

Afande Sele anapenda kuzitoa kasoro nyimbo za wenzake, kitu ambacho alikuwa anakitaka Afande Sele kutoka kwa wasanii wenzake, watunge nyimbo zenye kugusa jamii kama vile yeye anavyofanya.


Hapa ndipo Mfalme huyo wa Rhymes anapokosea, na huenda ndiyo sababu ya kuingia kwenye bifu na baadhi ya wasanii wenzake,

Halafu kama hujui Afande Sele ni bingwa na mtaalamu kweli wa kuvunja darasa ambalo analitoa yeye mwenyewe, yaani Mshikaji anatoa wimbo uliyo na ujumbe wa kukemea jambo fulani, halafu yeye mwenyewe anakuja kutoa wimbo wa kufanya kile ambacho amekikemea katika wimbo wake wa kwanza,

Kivipi???

Nitakupa mfano ili twende sawa,


Nenda kasikilize wimbo wake wa Mtazamo, katika Verse yake Afande Sele anasema,


Asante Professor Jay

Majani na Ulamaa mmegusa n’napopataka

Nami kwenye mtazamo nina jambo nataka kuweka

Maana kila kukicha emcees wanaongezeka

Nasema very nice, yes rap kama dhehebu

Emcees kama wafuasi

Wingi wa wasanii unaonesha ni dini safi

Yaani imekubalika, waumini tuko wengi

Lakini bado nashaka

Sijapata uhakika, wote tumesadiki

Ama wengine ni fake mmetumwa kama mamluki

Maanake hamna maana

Mna-rap ili mradi rap, mistari imekosa vina

Yenye vina haina maana

Na kila mnapokaa mnapenda kusengenyana

Mnapenda kutetana na mnapenda kurumbana

Mimi naogopa sana

Kwa jinsi navyoelewa mwishoni mtatukanana

Ama inawezekana mwishoni mkaja chinjana

Na wote tunao-rap tuonekane hatuna maana

Wapi ilipo Taarab

Ilikuja kwa kishindo, hata wagumu walishausudu

Kwa ajili ya marumbano mwishoni ikafa kibudu

Shabiki piga simu, changia mawazo yako

Nani tutamlaumu, kama rap ita-cease kwa kuendekeza upuuzi

Nani tumchune ngozi, producer aliyerekodi

Ama labda DJ anaepiga kwenye kipindi

Wengi wanapenda rap, ajabu rap haiwapendi

Waungwana wanaiacha, wapumbavu hawaambiliki

Hivi kwani lazima tuwe wote wanamuziki

Mi nadhani ingetosha wengine mbaki ushabiki

Huu ni wangu mtazamo masela msijenge chuki

Hata na Majani, yoh


Unaona namna Afande Sele alivyosema, mimi nashika mistari yenye kusema,

(Mnapenda kutetana na mnapenda kurumbana

Mimi naogopa sana

Kwa jinsi navyoelewa mwishoni mtatukanana

Ama inawezekana mwishoni mkaja chinjana)

Katika mistari hiyo Afande Sele anaonekana ni kwa namna gani hafurahishwi na marumbano na kutetana, yeye ana hofu vitu hivyo huenda Baadaye watu wakaja kuchinjana,


Lakini upande wa pili kwenye wimbo wa Darubini kali, ni yeye Afande Sele anayaanzisha marumbano kwa kuwadisi Bwana misosi na O Ten, katika wimbo huo Afande Sele anamwambia Bwana misosi, "kuna vitu vya kuimba vyenye maana kila kona, na siyo nyimbo nzima anataja taja majina tu, tena kwa mistari isiyo na vina" Binafsi sijaona kosa la Bwana misosi katika ule wimbo wa Nitoke vipi,

Kwanini???

Mwanzoni wa ule wimbo ndiyo utaelewa vizuri nini maana ya msemo, pale Bwana misosi aliposema,

(Misosi Nitoke vipi nafanya tafiti ya ndani

Sitaki ulimbukeni nataka kuuza duka

Na hawa ni baadhi ya waliopanda chati Nchini

Na huu ni upeo wangu tu

Nitoke namna gani

Nasema upeo wangu tu

Nitoke namna gani)


Hata kwa akili za Chekechea utabaini Bwana misosi katika ule wimbo ni swali ambalo anatuuliza Mashabiki, na ndiyo maana anatutajia wasanii ambao tumeshazisikia kazi zao, na yeye anauliza atoke vipi? Bahati nzuri nusu ya wasanii ambao amewataja katika ule wimbo, wamempa kampani kwa kuonekana katika ile video, lakini pia hakuwataja kwa ubaya, hata yeye Afande Sele ametajwa katika ule wimbo, Bwana misosi alisema,

(Afande mkuki moyoni

Morogoro ukamuingia) kwa namna ninavyojua mimi Afande ni jina la heshima ambalo mwanajeshi au askari yeyote anamwita mkubwa wake. Inalingana na neno la Kiingereza "Sir" Lakini ajabu Afande Sele hakuwa akijua hilo, na pia hakutaka hata kuelewa nini maana ya upeo wangu!!! Uzuri ni kwamba Bwana misosi alilijua hilo la kukosolewa na Afande Sele, Bwana misosi alikuja na majibu pale alipomwambia Afande Sele katika moja ya nyimbo zake wenye Kiitikio chenye kusema,

(Nikitunga nyimbo haina vina

We kaishi palipo na vina

Uganda Bongo na Kenya

Ninatoa Radha bila kubana)


Hakukuwa na marumbano ya muda mrefu kwa wasanii hawa wawili, lakini iliripotiwa kwenye vyombo vya habari, kuwa wawili hawa haziivi kabisa, na chanzo ilisemekana ni katika hizo nyimbo zao,

Na kama ilikuwa kweli maana yake nini???

Hapo hakuna jibu zaidi ya kusema, Afande Sele alivunja darasa ambalo alilitoa yeye mwenyewe katika wimbo wa mtazamo,

Nitoke vipi ya Bwana misosi haikuwa mbaya, na hata Mashabiki tuliipokea vizuri, na kupitia wimbo huo ambao ndiyo ulibeba jina la Albamu, ilipelekea Albamu hiyo kufanya vizuri sokoni, na jina la Bwana misosi likawa kubwa ndani na nje ya nchi, wote tuliona namna Bwana misosi alivyokuwa akifanya kazi na wasanii mbalimbali wa kutoka nje ya nchi, kama Uganda na Kenya,


FB_IMG_17081684058197571.jpg
 
!

SEHEMU YA PILI

Katika toleo lililopita niliishia pale kwenye disi ya Afande Sele kwa Bwana misosi,
Kuna baadhi ya watu wamepingana na hili, madai yao ni kwamba, katika wimbo wa Darubini kali, pale Afande Sele aliposema, (Kuna vitu vya kuimba vyenye maana kila kona sasa Inakuwa vipi unataja taja majina tu, nyimbo nzima Tena kwa mistari isiyo na vina) wanadai kwamba haya maneno hakuambiwa Bwana misosi kama mimi nilivyosema, isipokuwa dongo hili alipigwa King Crazy Gk....

Huenda wakawa wapo sahihi au la, lakini mimi nilivyokuwa nikijua disi hiyo ni ya Bwana Misosi,

Siwezi nikalichambua jambo hili la Bwana Misosi na Afande Sele, nilishasema limepita katika toleo lililopita, hivyo kuendelea kuliongelea hapa ni kuzidi kuwachosha wasomaji...

Tuangalie bifu la Afande Sele na Soggy Doggy, Kwanza naomba ujue bifu hili lilitokana na ushindi wa Afande Sele, kwenye kinyang'anyio cha taji la Mfalme wa Rhymes, Shindano la kumsaka mfalme wa Rhymes katika bongo flava ni moja ya shindano lililopata msisimko mkubwa kwa kipindi hicho, hii inawezekana ni kutokana na kukutanishwa manguli wa muziki kwa kipindi hicho, hali iliyopelekea uamuzi wa nani ashinde kuwa mgumu sana kwa walio wengi!

Shindano lilifanyika usiku wa tarehe 27 na hatimaye Afande Sele kutawazwa kama mshindi na kuwa mfalme wa rhymes, huku ushindi wa pili ukienda kwa Inspector Haroun na ushindi wa 3 wakichukua akina Mandojo na Domokaya!

Ushindi huu ulipingwa na watu wengi kuanzia watu wa kawaida mpaka wasanii wenyewe!!

NANI HASA ALISTAHILI KUSHINDA SHINDANO LA MFALME WA RHYMES 2004???

Ilikuwaje siku hiyo na shindano lote kwa ujumla mpaka Mshindi akapatikana?

Basi shuka na uzi huu toleo lijalo tutachambua ushindi wa Afande Sele,

Kwenye Miaka ya 2000 wasanii walikuwa wanafanya vizuri sana, ngoma zilikuwa kali sana, Haikuwa inafahamika nani mkali kuzid wengine, ndipo mmiliki wa Global publishers bwana Eric Shigongo, akaleta shindano hili ili kujua nani ni mkali....

Bwana Eric Shigongo alileta shindano hili kupitia magazeti yake ya Udaku kipindi hicho gazeti la Amani,Ijumaa na Uwazi,
Kumbuka kipindi hicho hapakuwa na Social media wala nini, habari zote ni kwenye magazeti hasa haya ya udaku, wasanii walikuwa wengi, kulitakiwa kumi tu,

Ili kuwapata washiriki hao ilitakiwa kupiga kura, katika upigaji wa kura ni Mashabiki ndiyo waliohusika, kura zilipigwa kupitia magazeti yake ya Uwazi,ijumaa na Amani, baada ya watu kupiga kura hawa ndio wasanii waliopigiwa kura nyingi na kuingia kwenye Shindano hilo,

1.Solo Thang-Simu yangu
2.Proffesor jay - Msinitenge
3.Afande SELE - Mtazamo
4.Inspector Haroon - Byebye
5.Jay Moe - Mvua na Jua
6.Mandojo na Domokaya - nikupe nini
7.Soggy Doggy - Kulwa na Dotto
8.Mwana FA - Alikufa kwa Ngoma
9.Madee - Kazi yake Mola
10.Dully Sykes

Msanii Dully Sykes yeye alijitoa hatua ya mwisho, waandaaji wakashindwa kuweka mbadala mwingine,
Shida kubwa ilipoanzia mpaka watu kuanza kuhisi mshindi alipangwa ni DJ JD, alikuwa moja ya majaji wa shindano lile, Alivujisha kuwa mshindi ni Afande sele na wasanii walisikia kabla ya siku yenyewe,

Pia kwa wakati huo kitu kilichofanya watu waanze kuhisi kweli mshindi alipangwa ni siku moja kabla ya Shindano lile, kupitia gazeti la Ijumaa kuchapisha ukurasa mzima wote wa katikati wimbo wa Afande sele Darubini kali na kuanza kuuchambua,
Kwa wakati huo ilikuwa bonge la promo,
Basi Bwana siku ya tukio ikafika, wasanii wakapanda jukwaani na kuanza kuchana,

Kwa wasanii waliopata shangwe sana siku ile ni inspector Haroon na Afande Sele,
Afande alikuja na mashabiki wake kutoka Morogoro na inspector Haroon alikuja na wana wa kitaa kutoka Temeke, kiliwaka sana siku ile,
Wakachana wote na Round ya kwanza ikapita,
Mchujo ukafanyika ili kupata top five,
Wasanii waliopita kwenda top five ni

1.Afande SELE
2.proffesor jay
3.Mandojo na Domokaya
4.Mwana FA
5.nspector Haroon

Baada ya kubaki Top Five wasanii wakakiwasha tena jukwaan huku shangwe kubwa likipigiwa kwa Afande Sele, na Inspector Haroon,
Hakika hawa walionekana kukonga sana hili Shindano,
Mchujo ukafanyika wakabaki wawili tu ambao ni

1.Afande SELE,
2.Inspector Haroon

Baada ya hapo mshindi akatangazwa ni Afande Sele, asikwambie mtu ukumbi ulilipuka kwa shangwe, ilikuwa moto sana pale Rose Garden, kwa raha alizonazo
Afande Sele akijikuta akiperform wimbo wake wa Darubini kali live siku hiyo kwa mara ya kwanza, kumbuka wakati huo wimbo wa Darubini kali ulikuwa ni hit song, ilirudiwa mara tano,
Baada ya hapo akapewa gari yake na kurudi mkoani Morogoro,

Na hapa ndipo bifu la Afande Sele na Soggy Doggy likazaliwa, na siyo Soggy Doggy tu, bali hata Madee na Profesa Jay pamoja na Solo thang, waliingia katika bifu na Afande Sele kutokana na ushindi huu, kwa sababu Baada Ya hapa kukaibuka sasa Mambo mengi na siri nyingi kuvuja kuwa Afande Sele alibebwa, Wasanii walipinga tena waziwazi akiwemo Solo thang, madee na soggy Doggy,

Kwa upande wa Profesa Jay yeye hasira zilimfanya kushindwa kabisa, kuungana na Afande Sele kwenye video ya wimbo wa Mtazamo, Profesa jay aligoma kabisa, na hayupo kwenye Video,
Haikupita muda Solo Thang aliandika wimbo akipinga kile kinachoitwa kupanga mshindi, namnukuu "wengine wananirubuni eti nashindania gari, kumbe washapanga wampe nani toka awali, sitarudia kosa hata zawadi waweke meli, wanipe ghorofa mbili wanikabidhi na sheli"

Solo Thang hakuishia hapo, katika wimbo wa Traveller anasikika tena akisema "Mi siyo mfalme njozi mi siyo mgambo sele"
Fid Q naye katika Mwanza Mwanza aliendelea kuthibitisha kutokukubalika kwa ufalme wa Afande, namnukuu "Mfalme wa Rhymes ambaye Soggy Doggy hamtaki, anamwita Kobe hawezi mzidi mbio farasi"
Madee naye alienda mbali na kudai hajawai ona mfalme ana nywele chafu!!

Itaendelea
 
!!
SEHEMU YA MWISHO

Katika toleo lililopita tuliona jinsi Afande Sele alivyomdis O Ten, na chama la East Coast Team, kundi la East Coast Team lilikuwa likiundwa na vichwa sita vya kiume na kimoja cha kike, watu hao kwa majina wanatambulika namna hii,
King Crazy Gk
Mwana FA
AY
O Ten
Snare
Puff G na Pauline Zongo, kati ya hao wote, ni O Ten ndiye aliyejibu Mashambulizi kwa Afande Sele, pale alipoibuka na ngoma yake iitwayo "Mimi"

O Ten katika wimbo wake wa mimi kuna mistari anasema....

(Nilizaliwa Morogoro,
Hata siku nikifa
Maiti yangu iende Moro.
Naweka wazi adui yangu asinizike,
Hata muhuni yoyote asiyenipenda asisogee.
Kama vipi itupeni maiti yangu porini wale tai)

O Ten katika wimbo huo alienda mbali zaidi kwa kusema,
(Kama hunijui naitwa Filipo nyandindi,
Na adui yangu mkubwa ni Selemani Msindi(Afande Sele)

Nahisi hii ndiyo wimbo wa kwanza Nchini Tanzania,
Kwa msanii kumtaja jina adui yake, ni wimbo ambao ulijadiliwa sana na wadau wa Muziki, wenye busara wakaibuka hapa na kuwaweka Chini Afande Sele na O Ten, wakawapa maneno ya kiswahili yenye utamu wote, na hatimaye kufanikiwa kuwaweka sawa Wasanii hao..

Haraka sana wakaingia Studio na kutoka na ngoma ya "Tusahau" Verse 1: Oten anaimba kwamba..

Naepusha mbawa zangu
kwa kuonekana mjinga, naamini mti mwema ndio unaopigwa mawe.
Kila kukicha nyandindi ndio naonelewa,
nakabidhi roho yangu kwa baba aliye Mbinguni.
Rafiki yako mkubwa anaweza kua adui,
ila adui yako mkubwa hawezi kua rafiki
ila Oten nimesamehe, ninapotoka napajua, ninapoenda sipajui, ndio maana kila siku napunguza maadui,

Verse 2: Afande akaimba..

Na nywele ni kama akili,
yule ana nywele ndefu na yule kipilipili,
Au mwingine nyekundu,
na mwengine nyeusi tii
Ilimradi kuna toafauti,
kati yetu ndani ya jamii
Hivi nani angetambua, kwmaba kuna kipindi mwezi unapatwa na jua
Ndio mambo yalivyo duniani, vitu kama sunami sio vigeni
Zinagongana meli, magari na ndege juu angani
Hata vidole vyetu mkononi havifanani
Hujawahi ona mama na mwana mda fulani hawaelewani, Sembuse mimi na Oten, Amkeni.
Acheni bifu za kiuni,
kama kuanzisha bifu tuanzishe bifu na ukimwi
Yaliyopita sinndwele, sasa tugange ya mbele
Watu hatuna makucha vipi tunaomba Upele,
hatueleweki zipi ni pumba zipi ni mchele
Wote ni walewale, kutwa kunyosheana vidole.
Hilo halipo na kama halipo, basi nakula kiapo
Mnionapo na filipo, popote amani iwepo
Japo shetani hapendi, ila wote tuamini kwa Mungu ni zaidi ya ushindi!
Leo filipo nyandindi, yuko pamoja na mtu pori baba abdul na selemani msindi

Na Baada ya hapo hatujawahi kusikia tena wawili hao wamegombana, siku zikawa zinakwenda na miaka ikasogsa, ghafla bifu kati ya Afande Sele na Madee likaibuka,

Awali bifu hili lilianza chini kwa chini, hakuna shabiki yeyote ambaye alikuwa akilijua bifu hilo, tulikuja kujua kupitia nyimbo zao...

Madee ana ngoma yake inaitwa 'jinsi game inavyochange' kashirikiana na Godzilla na kuna mstari godzila anasema 'nyimbo zenu (hip hop) hazina swagga halafu mnang'ang'ania airtime' kisha Madee akamalizia kwa kusema 'Nadhani unamaanisha yule mwenye rasta rasta' pia ndani ya wimbo huo huo kuna mstari Madee anasema 'bado hujaona mfalme mwenye rasta chafu? (bado)'.
Kwa upande wa Afande Sele ana wimbo unaitwa 'Kingdom' kuna mstari unasema 'hip hop itakulipa vipi wakati unaimba matusi, unatukana ma-ras, unadiss waasisi halafu bado unadiriki kujiita rais wakati huna hata ofisi labda ni rais wa huko kwenu uwanja wa fisi'
Madee tena ana ngoma yake inaitwa 'nisikilize' ambayo ndani yake kuna msitari unasema 'yule mkulima alidai eti nambeza, alitamba zamani miaka hii hajaweza, anaumia kwanini mwanzo alicheza, hawezi kuosha nywele ana uhaba wa fedha'

Na kama hiyo haitoshi miaka ya juzi juzi, wakati Magufuli ameingia madarakani kwa awamu ya kwanza kabisa, Afande Sele alishawahi kuhojiwa na kituo flani cha habari, katika mahojiano hayo Afande Sele aliponda sana vitendo vya wasanii kwenda Kushoot Video zao nje ya nchi,

Hapo chini nanukuu maneno ya Afande Sele....

“Kwenye kushoot video nje ni ulimbukeni,
Tanzania tuna kila kitu kuliko hata huko wanakoenda. Mimi hii naitafsiri ni usaliti wa nchi, sisi tunakosa nini hapa nyumbani? Tuna milima, mbuga, maporomoko mazuri, yaani tuna kila kitu. Unajua wasanii wengi walikuwa wanatumia mwanya wa kwenda kushoot video nje ili kufanya biashara zao za siri. Wengi wameutumia sana huu mwanya, sasa Magufuli alivyoingia atawanyoosha tu,” alisisitiza Afande.

Haikupita muda mrefu sana Kupitia Twitter, Madee aliandika,
"Kadri unavozidi kuzeeka na akili nazo zinarudi utotoni na kuambatanisha screeshot ya kichwa cha habari cha Afande.

Baadaye Madee akafafanua zaidi kupitia website ya Millard Ayo ambapo alimtaka Afande aombe radhi kwa kauli hiyo:

Hapo chini nanukuu maneno ya Madee,

"Unajua yale ni matusi kwenye muziki wetu wa Bongo Fleva, halafu watu kama Afande Sele ndio waanzilishi wa huu muziki sasa muziki unapoelekea sasa ni kwenye level ya kimataifa muziki unakua kwahiyo vitu alivyokuwa anafanya yeye mwanzo..kwasasa anaviona vipya anaona kama maajabu watu kumiliki hela nyingi…anastaajabu na kuhisi labda wasanii wanafanya ishu nyingi.
Labda tuchukulie mfano John Legend alipotoka kwao Marekani ambapo kuna vitu vingi na kuja Zanzibar kushoot video yake Je alikuja kufanya vitu vya siri eeeh! Hii ni katika harakati za kutanua wigo wa muziki, watu wanataka kufanya vile vitu ambavyo hatukuwahi kufanya ili twende sawa na soko la kimataifa.
Sasa wewe Baba au Babu yetu ambaye unastaajabu kuona watu wanatoka kwenda kushoot sehemu nyingine wewe unasema wanaenda kufanya vitu vya ajabu unakuwa unatukatisha tamaa sisi ambao tumeachiwa hii nafasi, kwahiyo nikiwa kama msanii namuomba Afande Sele awaombe radhi wasanii wote kwa ujumla, kutokana na kauli yake aliyoizungumza sio nzuri.

Baada ya hapo haikueleweka kama Afande Sele alifanya kile ambacho Madee alimtaka akifanye, yaani kuomba radhi juu ya kauli yake, lakini naamini Afande hakuwahi kufanya hivyo, na mpaka sasa sidhani kama wanaelewana na Madee,

Binafsi juu ya ugomvi huu wa Madee O Ten na Soggy Doggy, ningepewa bakora nimchape mwenye makosa, basi Afande Sele fimbo zingemuishia yeye,
Kwanini???
Kwa sababu mtu ambaye alionekana ni mpenda amani kutokana na mashairi yake kubeba ujumbe unaokemea tabia za wanamuziki kulumbana, ndiye huyo huyo anayeonekana kushika kasi! Anataka tuamini katika msemo wa kiongozi wa dini feki eti “fuateni maneno yangu, si matendo yangu!”
Suleiman Msindi a.k.a Afande Sele anastahili adhabu, ndani ya nyimbo zake mbili, Mtazamo na Darubini Kali anakataza malumbano lakini ni yeye huyo huyo tukaja kumuona anatupiana madongo na marapa wenzake,

Ina maana Afande Sele hajui kuwa uungwana ni vitendo, muungwana hata asemwe vipi jibu lake ni kimya, Afande Sele ni mtu mzima, na mtu mzima akivuliwa nguo huchutama, na ndiyo maana nikasema kwa wakati ule ningepewa bakora ningezimaliza kwa Afande Sele,

mabifu hayo hayakufikia hatua
mbaya, pia niwapongeze Afande Sele na O Ten kwa kuwahi kuzimaliza tofauti zao, kuhusu Madee na Soggy Doggy naamini hata hawa ipo siku watapatana na Afande Sele, na kama tayari wameshapatana basi ni jambo zuri na la kheri, pia nimpongeze Afande Sele kwa kubeba Ufalme wa Rhymes nyakati zile, nimpongeze pia kwa nyimbo zake nzuri zilizokuwa na ujumbe ndani yake hakika zilitujenga na kutuburudisha sana nyakati zile....

Mwisho
FB_IMG_17081682401813150.jpg
 
Afande Sele anataka opinion anayotoa ndio iwe msahafu. Niliwahi kupishana nae mawazo kipindi flani anafanya kampeni za siasa mwisho wake akaamua kuhamisha magoli, badala ya kutetea hoja yake kwa hoja akanivaa personal ndio ukawa mwisho wa reasoning.
Sele ni egocentric person.
 
Afande Sele anataka opinion anayotoa ndio iwe msahafu. Niliwahi kupishana nae mawazo kipindi flani anafanya kampeni za siasa mwisho wake akaamua kuhamisha magoli, badala ya kutetea hoja yake kwa hoja akanivaa personal ndio ukawa mwisho wa reasoning.
Sele ni egocentric person.
Bahati mbaya sija mfahamu personal, na reference ya muziki tu
 
Afande Sele anataka opinion anayotoa ndio iwe msahafu. Niliwahi kupishana nae mawazo kipindi flani anafanya kampeni za siasa mwisho wake akaamua kuhamisha magoli, badala ya kutetea hoja yake kwa hoja akanivaa personal ndio ukawa mwisho wa reasoning.
Sele ni egocentric person.
Jamaa bangi nyingi na kujiona ana akili sana
 
Mtazamo ndio moja ya nyimbo nazozikubali toka kwake
Mle ndani wame toa madini mazuri, mtu aki tuliza kichwa Kuna mengi ya kuji funza.

Mfano, rap Kama dhehebu, mc Kama wafuasi- wingi wa waumini Ina onesha ni dini Safi.
Nina pata Shaka je wote tune sadiki au wengine ni mamluki.

Hoja zangu,
Tuchukulie rap Kama maisha, Kuna wengine Wana ishi katika misingi Safi na iliyo nyooka.
Wengine ni Kama wasindikizaji, Kutokana na kushindwa kuzingatia mambo ya muhimu.

Kutokana na Baadhibya vitu vina watoa mchezoni,
Tresor Mandala
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom