Hotuba ya waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo ya muswada wa sheria ya huduma za habari

Jay Milionea

JF-Expert Member
Apr 19, 2015
1,185
154

HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO MHESHIMIWA NAPE MOSES NNAUYE (MB.), 4 NOVEMBA, 2016

KUWASILISHA MBELE YA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA

TANZANIA, MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI, 2016 (THE MEDIA SERVICES BILL, 2016)

(Imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni ya 86(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)
___________________________

1.0 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa kanuni ya 86(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Januari, 2016), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lijadili na hatimaye kuupitisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari, 2016 yaani “The Media Services Bill, 2016.

Mheshimiwa Spika,

Kwa kuwa nasimama leo hapa kwa mara ya kwanza kuwasilisha muswada mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba uniruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema.

Namshukuru pia Rais wetu mpendwa, Dkt, John Pombe Joseph Magufuli kwanza kwa Serikali yake kuona umuhimu na kuruhusu muswada huu kuletwa Bungeni lakini pia kwa imani yake kwangu na watendaji wenzangu wengine waandamizi kwa kutupa jukumu la kusimamia tasnia hii na hususani ukamilishaji wa kazi hii.

Mheshimiwa Spika,

Napenda pia kukushukuru wewe binafsi, Katibu wa Bunge na wafanyakazi wote wa Bunge kwa uongozi na usimamizi thabiti wa shughuli za Bunge na kwa kutupatia ushirikiano wa kutosha wakati wote wa maandalizi ya muswada huu.

Kipekee pia nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Peter Serukamba (MB) na waheshimiwa wajumbe wote wa Kamati kwa kufanyakazi mchana na usiku kukamilisha maandalizi ya muswada huu. Kamati imefanya kazi kubwa sana na ya kihistoria itakayokumbukwa kwa miaka mingi ijayo katika kuhakikisha kuwa muswada huu si tu unakamilika lakini pia unaboreshwa ipasavyo.

2.0 CHIMBUKO, MUKTADHA NA MCHAKATO WA KUANDAA MUSWADA

Mheshimiwa Spika,

Itakumbukwa kuwa tangu kutambuliwa kwa haki za kibinadamu katika katiba
ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 baada ya mabadiliko ya tano ya
Katiba yaliyofanyika mwaka 1984, vuguvugu la kudai haki mbalimbali nchini lilishika kasi.

Tasnia ya habari nayo haikuwa nyuma katika vuguvugu hilo: baada tu ya kuingizwa kwa haki ya kikatiba ya kutafuta, kupokea na kutoa habari kwenye Ibara ya 18 (b) ya Katiba kutokana na mabadiliko ya 1984, kulianza kuibuka maoni mengi ya wadau juu ya hitaji la kuwa na sheria bora zaidi ya habari.

Tamko la Katiba pia lilitiliwa nguvu na ukweli kwamba Serikali pia ilikuja kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayoainisha haki na wajibu wa sekta ya habari. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 (Serikali iliuridhia Juni 11, 1976) na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (tuliouridhia 18 Februari, 1984).

Mikataba yote hii ya kimataifa; ule wa Umoja wa Mataifa wa 1966 katika kifungu cha 19 na wa Afrika katika kifungu cha 9 inaainisha kinagaubaga haki na wajibu wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,

Mabadiliko haya ya kimtazamo kuhusu haki na wajibu wa vyombo vya habari yaliwasukuma wadau wengi nchini kudhani kwamba sheria tulizokuwa nazo wakati huo hasa ile ya magazeti ya mwaka 1976 hazikuendana na wakati.

Ili kuitikia kilio cha wadau, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ilikuwa ni kuunda Tume ya Jaji Frincis Nyalali mnano terehe 27 Februari, 1991 kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa kisiasa na demokrasia nchini. Vilevile, Tume ya Jaji Nyalali ilipewa jukumu la kuchambua sheria na kutathimini namna zinavyoweza kuendana na uelekeo mpya.

Mheshimiwa Spika,

Mojawapo ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali yalikuwa ni kufanyika marekebisho mbalimbali katika sheria za habari zilizoonekana kukinzana na Katiba na mtazamo mpya wa dunia. Baadhi ya sheria zilizotajwa kuhitaji maboresho ni Sheria ya Shirika la Habari la Tanzania, Na. 14 ya mwaka 1976, Sheria ya Magazeti, Na. 3, 1976 na Sheria ya Magazeti (Zanzibar) Na. 5 ya mwaka 1988.

Mheshimiwa Spika,

Mapendekezo ya Tume ya Warioba yalianza kufanyiwa kazi kwa Serikali kuanza kutunga au kuboresha sera na sheria mbalimbali za habari. Juhudi hizo zilianza kwa kuwasilishwa katika Bunge hili Tukufu muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Taaluma ya Habari, 1993 (The Media Professions Regulations Bill, 1993).

Muswada huo wa kwanza katika juhudi zilizokuja kuchukua miaka mingi ya mivutano, ulichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Juni 25, 1993 kwa lengo la wadau kutoa maoni yao. Akifafanua malengo ya muswada huo Waziri wa Habari na Utangazaji wakati huo, marehemu Dkt William Shija, alieleza kuwa, lengo kuu la kupendekeza muswada huo lilikuwa ni kuweka mfumo wa kisheria ambao ungewezesha kulinda haki ya msingi ya kupata habari nchini.

Hata hivyo, kutokana na maoni ya wadau mbalimbali kutaka muda zaidi wa kulijadili jambo hilo, Septemba, 1993 Serikali ilikubali kuuondoa muswada huo. Pamoja na kuondolewa, tangu mwaka 1993, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuifanyia mabadiliko sekta ya habari kwa kutunga sera na sheria mpya au kuboresha zilizopo. Sheria na sera hizo ni pamoja na:-

  1. Sheria ya Huduma za Utangazaji Na. 6 ya mwaka 1993 (The Broadcasting Services Act);
  1. Sheria ya Tume ya Utangazaji, 1993 (Tanzania Broadcasting Commission Act);
  1. Sheria ya Mawasiliano, No. 18 ya mwaka 1993 (The Tanzania Communications Act);
  1. Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003 (The Tanzania Communications Regulatory Authority);

  2. Sera ya Habari na Utangazaji, 2003;
  1. Sheria ya Huduma za Mawasiliano kwa wote Na. 11 ya mwaka 2006 (The Universal Communication Services Act);
  1. Sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta Na. 3 ya mwaka 2010 (The Electronic and Postal Communications Act);
  1. Sheria ya Makosa ya Mtandaoni Na. 14 ya mwaka 2015 (The Cybercrimes Act); na
  1. Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa Na. 6 ya mwaka 2016 (The Access to Information Act).

Mheshimiwa Spika,

Serikali ikiwa na nia njema ya kuendeleza azma ya kuwa na sheria bora zaidi na mahsusi ya huduma za habari nchini, katikati mwa miaka ya 2000, ilianzisha tena juhudi za kutunga sheria hiyo. Majadiliano na wadau yaliibua hoja ya kuwa na miswada miwili; Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari (Media Services Bill) na Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa (Access to Information Bill). Miswada hii haikufika Bungeni mapema kutokana na majadiliano na wadau kuchukua muda mrefu.

Ni katika kipindi hiki pia ambapo baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 shauku ya kuwa na sheria hizo iliongezeka kufuatia tathmini mbalimbali za utawala bora zilizohusu nchi yetu; ikiwemo ile ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review) na ile ya Umoja wa Afrika (African Peer Review

Mechanism), zote kuikumbushia Serikali juu ya umuhimu wa kukamilishwa kwa sheria za habari.

Hatimaye mwaka 2015 baada ya kuboreshwa miswada ya awali kutokana na maoni ya wadau sheria hizi ziliwasilishwa Bungeni. Hata hivyo pakaibuka tena majadiliano makali hasa kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari, 2015 (The Media Services Bill, 2015) ambao uliowasilishwa kwa hati ya dharura.

Nia ya Serikali kuwasilisha muswada huo kwa hati ya dharura ilikuwa ni kuhakikisha muswada huo uliokaa muda mrefu kwa hati ya dharura hatimaye kazi hiyo iliyochukua muda mrefu wa kujadiliana na wadau, kuvutana, kwenda mbele na kurudi nyuma, ifike mahali ikamilike kwa haraka.

Kwa mara nyingine tena, wakati Muswada wa Haki ya Kupata Taarifa (Access to Information Bill) ukiendelea na hatua zote hadi kupitishwa na Bunge mwezi Septemba mwaka huu (2016), Serikali yetu sikivu ilisikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Huduma za Habari na kuuondoa Bungeni kupisha maoni zaidi.

Mheshimiwa Spika

Wakati Muswada wa Huduma za Habari ukiondolewa Bungeni, hoja kubwa mbili zilikuwa ni: Mosi, muswada huo upate maoni zaidi ya wadau; na pili uletwe Bungeni kwa mtindo wa kawaida na sio wa hati ya dharura. Tangu kuondolewa

kwa muswada huo mwaka jana Serikali ilitimiza maelekezo hayo na ndio maana leo tunatoa hoja kwamba muswada huu sasa ujadiliwe.

Kuhusu ushirikishaji wa wadau, mara tu baada ya muswada kuondolewa Bungeni, wadau mbalimbali walitakiwa kuusoma kwa nafasi yao na kuwasilisha maboresho Serikalini na tunashukuru na kuwapongeza waliopata muda kwa raslimali zao wakakaa na kuuchambua muswada.

Wizara ilifaidika sana na maoni ya kina ya wadau. Katika andiko lao la Machi 31, 2016 kwa Wizara yangu, wakiwasilisha mapendekezo yao, wadau wote wakuu wa habari wakiwakilishwa na Baraza la Habari Tanzania (Media Council of Tanzania, MCT), waliwasilisha, tena kwa maandishi, uchambuzi wao wa kina kuhusu muswada (Maoni hayo yanawasilishwa mezani kwa ajili ya kumbukumbu za Bunge).

Maoni hayo yalikuwa ni matokeo ya uchambuzi wa kina na wa pamoja wa taasisi zifuatazo zinazojihusisha na masuala ya habari na haki za binadamu:

  • Baraza la Habari Tanzania (MCT);
  • Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB);
  • Tanganyika Law Society (TLS);
  • Sikika;
  • Nola-National Organization for Legal Assistance;
  • Tanzania Editors Forum (TEF);
  • Legal and Human Rights Centre (LHRC);
  • Tanzania Media Women’s Association (TAMWA);
Tanzania Human Rights Defenders (THRDs);

  • Umoja wa wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT); na
  • Taasisi ya Wanahabari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA–TAN)

Mheshimiwa Spika,

Katika wasilisho lao hilo lililokuwa na mapendekezo zaidi ya 15; kuanzia jina la muswada, umuhimu wa kuainisha haki na wajibu wa wanahabari, kuanza kutumika kwa sheria, kulinda haki za wanahabari hadi taasisi za kusimamia habari, Serikali iliyapokea kuyachambua na kwa kiwango kikubwa kuyatumia kuboresha muswada uliopo sasa Bungeni.

Licha ya maoni ya wadau hao wakuu, Wizara yangu ilichukua tena juhudi za ziada za kuwashauri wahariri kuunda Kamati ya Wahariri kuuchambua tena muswada huo. Hawa wakiwa ndio watendaji wa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari walikuja na mapendekezo yaliyosaidia kuuboresha zaidi muswada huu. Kamati hiyo nayo ilifanya kazi kubwa na ya kupongezwa. Nawashukuru sana wahariri nao kwa maoni yao.


Mheshimiwa Spika,

Baada ya kupokea maoni hayo na majadiliano ndani ya Serikali hatimaye Baraza la Mawaziri (BLM) kupitia mkutano na. 1/2016-17 katika kikao chake cha tarehe 14 Julai, 2016, liliridhia na kuelekeza kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari. Hatimaye muswada ukachapishwa Agosti, 2016 na kisha Septemba 16 ukawasilishwa Bungeni kwa njia ya kawaida na kusomwa kwa mara ya kwanza.

Mara baada ya kusomwa mara ya kwanza na ili kuwakumbusha wadau zaidi umuhimu wa kuusoma, kuuchambua na kutoa maoni yao kwa Kamati za Bunge, Mimi waziri mwenye dhamana na habari siku hiyo hiyo ya Septemba 16, 2016 muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza, niliitisha mkutano na wanahabari na kuujulisha umma wa Tanzania kuwa tayari muswada huo ulikuwa kwenye tovuti ya Bunge na kwamba wadau wausome tena na kuainisha mapungufu yake ili Kamati za Bunge zitakapoanza wapeleke maoni ya kuboresha.

Mheshimiwa Spika,

Kwa hakika Serikali imefarijika kwa kutoa fursa ya wadau kutoa maoni kwa Kamati ya Bunge, sio fursa pekee ya kukusanya maoni bali ni muhimu pale wadau wanapodhani wana kitu cha kuboresha zaidi baada ya hatua za awali wafanye hivyo. Aidha baada ya muswada kusomwa Bungeni, ni jukumu la wadau kuusoma kwa kina muswada na kuona kama wana mchango zaidi au la.

Mheshimiwa Spika,

Kwa bahati mbaya, labda kwa sababu za mazoea yale yale ya miaka ya nyuma, baadhi ya wadau wa habari badala ya kutumia vyema fursa hii ya pili kwenda kutoa maoni kwenye Kamati, wakaanza kuibua sababu na visingizio vya kujaribu kutaka utungwaji wa sheria hii usogezwe tena mbele zaidi, uahirishwe au usiendelee.

Wadau hao walikuwa na sababu zinazobadilika kila siku kuhusu nini hasa ilikuwa hoja yao. Mfano ni tukio la Oktoba 19, 2016 ambapo wadau walikaribishwa kutoa maoni mbele ya Kamati ambapo baadhi yao waliieleza Kamati kwamba walikuwa tayari kutoa maoni yao na kutaka wawekewe vifaa kama meza na projekta ili wawasilishe maoni hayo. Baada ya muda wadau hao wachache wakageuka na kuibuka na hoja kuwa hawana maoni wapewe muda zaidi hadi mwakani.

Baadaye tena wakaja na hoja ya kutaka kupita mikoani kukusanya maoni ya waandishi wengine. Pamoja na Kamati kutoridhishwa na hoja hiyo na kuamua kuendelea na kazi yake ya kibunge ya kupitia muswada bado wadau hao walipewa siku 10 za ziada kwenda kujiandaa ili kuwasilisha tena maoni yao.


Mheshimiwa Spika,

Napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa licha ya baadhi ya wadau kuchagua kutumia haki yao ya kutoa maoni kwa kuzungumza zaidi na kuuchambua muswada kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, badala ya kwenda kwenye Kamati, naomba nikuhakikishie kuwa Serikali na Kamati tumefaidika sana na maoni mengi yaliyotolewa kwa njia mbalimbali kiujumla, moja kwa moja kwa Wizara au kwenda kwenye Kamati na yametumika kuuboresha muswada huu.

Kwa hakika nimefarijika na tunavishukuru vyombo mbalimbali vya habari vilivyowapa fursa wananchi na wadau mbalimbali kuchambua na kutoa maoni yao kuhusu uboreshaji wa muswada huu ikiwemo kupitia magazeti, redio na televisheni.

Kipekee nazishukuru pia taasisi mbalimbali zilizowasilisha maoni yao kwa Kamati ya Bunge tena ya kina kwa maandishi kuboresha muswada huu hasa

Chama cha Mawakili Tanzania (TLS) na Taasisi ya Twaweza. Maoni yao ni sehemu ya maboresho muhimu ambayo Kamati na Serikali tumekubaliana kuyafanya katika muswada wa awali uliowasilishwa Septemba 16, 2016. Maboresho husika yameainishwa katika jedwali la maboresho (schedule of ammendment) la Serikali.

3.0 CHANGAMOTO ZA TASNIA YA HABARI NA MUKTADHA WA MUSWADA

Mheshimiwa Spika,

Kama nilivyosema, Bunge lako hili leo na kesho linakwenda kuhitimisha kazi ya kihistoria ya kutunga sheria hii. Ni kazi ambayo ni muhimu kwa Taifa na ni muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Tunakwenda kuhitimisha kazi hii wakati

ambapo nchi yetu ikiwa na sekta ya habari yenye changamoto kubwa sana ambazo muswada huu unajaribu kuzitatua.

Tunakwenda kutunga sheria, sababu za kuwa na sheria hii zikiwa ni zaidi ya zile za miaka ya 1990 ambapo tulilenga zaidi kutii matakwa na mtazamo mpya wa kikatiba. Leo tunakwenda kutunga sheria hii tukiwa na uzoefu wa kuwa na vyombo vingi vya habari nchini na tukiwa ni mashahidi wa changamoto za vyombo hivyo.

Kuwasilishwa kwa muswada huu leo, na kwa ridhaa ya wabunge ukipita, kutahitimisha safari ya zaidi ya takribani miongo miwili ya majaribio kadhaa ya kutunga sheria bora ya kuratibu tasnia ya habari nchini. Baada ya majaribio na majaribu ya mara kadhaa kutunga sheria hii, leo ninayo imani kuwa Bunge hili na mwaka huu tunakwenda kuweka historia kwa kulihitimisha jambo hili hasa tukizingatia dhima iliyonayo sekta hii muhimu.

Rais mmoja wa Marekani akionesha umuhimu wa sekta ya habari aliwahi kusema bora yawepo magazeti badala ya Serikali. Rais huyo, Thomas Jefferson, katika barua yake ya Januari 16, 1789 kwenda kwa rafiki yake kipenzi Kanali Edward Carrington, aliandika kuhusu ukweli huu akisema na (nanukuu):

"The basis of our government being the opinion of the people, the very first object should be to keep that right; and where it left to me to decide whether we should have government without newspapers, or newspapers without a

government, I should not hesitate a moment to prefer the latter." Mwisho wa

kunukuu.

Mheshimiwa Spika,

Kwa maneno machache, nukuu ya Rais Jefferson inafupisha nadharia nyingi, maelezo mengi na ufafanuzi mwingi unaoweza kutolewa kusisitizia ni kwa nini sekta ya habari ni muhimu sana kwa jamii. Na ni kwa sababu hii basi, sheria tunayoitunga leo, kimsingi, imechelewa sana na tuliihitaji ipatikane mapema zaidi.

Lakini pamoja na ukweli kuhusu umuhimu huo wa vyombo vya habari, lazima pia tukiri kuwa kuna changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa sheria zilizopo zinazosimamia Tasnia ya Habari na mabadiliko ya teknolojia ya habari, uchumi, siasa na jamii.

Vile vile, kutokuwepo kwa udhibiti na usimamizi wa viwango kwenye Taaluma ya Habari na Utangazaji kumechangia serikali na wadau wenyewe kuona umuhimu wa kuwa na Sheria itakayoainisha bayana sifa na viwango vya kitaaluma katika Tasnia ya Habari. Kukamilika kwa Sheria hii pia, kutapanua wigo wa upatikanaji wa habari kupitia mitandao ya intaneti na kukidhi kasi ya maendeleo ya haraka ya Teknolojia ya Habari na Utangazaji.

Mheshimiwa Spika,

Changamoto nyingine kubwa ya sekta hii ni kuibuka kwa ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uandishi wa habari nchini. Baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakikiuka maadili ya fani hii kwa kuandika habari ambazo zinapotosha umma, uchochezi na kupelekea usalama na amani ya nchi kuwa hatarini.

Kila mmoja wetu humu kwa namna moja au nyingine ni mwathirika wa uandishi usizozingatia weledi na unaoendekeza habari za uzushi, uongo, tetesi au visasi. Aina hii ya uandishi kwa upande mmoja imechangiwa na kutokuwepo kwa sifa zilizoanishwa za mwanahabari ni nani na matokeo yake kila mtu siku yoyote anapojisikia tu anaanza kufanyakazi ya uandishi wa habari.

Aidha baadhi ya waandishi wanapokuwa wamekiuka maadili haya, mara nyingi vyombo vyao ndio vimekuwa vikichukuliwa hatua kwa makosa ya mwandishi binafsi hivyo kuathiri wamiliki na wafanyakazi wengine wasiohusika. Mapendekezo yaliyomo katika Sheria ya Huduma za Habari kwa kiasi kikubwa yanalenga kutatua changamoto hizi zilizoainishwa hapo juu.

  1. MADHUMUNI NA MPANGILIO WA MUSWADA
Mheshimiwa Spika,

Madhumuni ya muswada huu ni kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari (The Media Services Acts, 2016) yenye lengo la kuweka masharti ya kukuza na kuimarisha taaluma na weledi katika Tasnia ya Habari, kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari, kuweka mfumo wa usimamizi wa huduma za habari na masuala mengine yanayohusiana na Taaluma ya Habari na Utangazaji.

Muswada umeandikwa katika mfumo unaotekeleza haki na wajibu wa vyombo vya habari. Kwamba vyombo vya habari viwe huru katika kutafuta, kuhariri na kuchapisha au kutangaza habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa haki yao ya kikatiba (ibara ya 18, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977) lakini pia ikiwa ni kutekeleza haki za kimataifa za uhuru wa habari (kwa mujibu wa Tamko la Haki za Binadamu, 1948, Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 na Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu na Watu, 1981).

Lakini muswada pia umeandikwa katika muktadha wa kutambua kuwa haki hizo pia zinaendana na wajibu ambao vyombo vya habari vinapaswa kuubeba. Kifungu cha 19 cha Mkataba wa Kimataifa wa 1966 nilioutaja hapo juu, kinaanisha ukomo wa uhuru wa habari ikiwemo wanahabari kutotakiwa kuandika habari za kashfa, kuhatarisha usalama wa nchi, amani ya nchi, afya ya jamii na maadili ya Taifa. Aidha mikataba ya kimataifa pia inataka vyombo vya habari kulinda haki ya usiri na utu.

Mheshimiwa Spika,

Pale ambapo muswada huu umeweka makosa mbalimbali na adhabu kwa wanahabari basi si kwa nia ovu ya kuzuia haki za binadamu za wanahabari bali kutekeleza matakwa haya ya sheria za kimataifa ambazo zinawapa wanahabari wajibu pia wa kulinda haki nyingine za raia na usalama wa nchi. Wanahabari wakisimama katika maadili yao na kutii sheria, hawana sababu ya kuhofu vifungu hivi, Serikali itakuwa mlinzi wao namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya sheria inayopendekezwa kutungwa ni

kama ifuatavyo:

  1. Kuwa na sheria inayotekeleza Sera ya Habari na Utangazaji, 2003;

  1. Kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kisheria wenye kukidhi mahitaji ya wakati katika usimamizi wa taaluma ya uandishi wa habari;
  1. Kuanishwa vyema kwa haki na wajibu wa wanahabari nchini;
  1. Kuwepo kwa wanahabari katika tasnia ya habari wenye sifa stahiki;
  1. Kuwepo kwa mfumo wa kutatua migogoro ya wananchi na vyombo vya habari;
Kuwepo kwa utaratibu na mfumo wa umiliki wa vyombo vya habari;
  1. Kuweka mfumo wa bima ya lazima kwa wanahabari;
Kuwepo kwa vigezo maalum vya usajili wa magazeti;
  1. Kuwepo kwa chombo cha kusimamia ithibati kwa taaluma ya habari; na,
  1. Kuwa na Baraza Huru la Wanahabari.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kusema hayo sasa niseme muswada huu umegawanyika katika sehemu kuu nane (VIII) kama ifuatavyo:-

Sehemu ya Kwanza: Inahusu na masharti ya awali ambayo ni jina la sheria, tarehe ya kuanza kutumika, matumizi na tafsiri ya misamiati na maneno yaliyotumika.

Sehemu ya II: Inahusika na Idara ya Habari kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, majukumu ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari, aina za umiliki wa vyombo vya habari, haki na wajibu kwa vyombo vya habari kutoa habari kwa umma na Serikali. Kuainisha wajibu wa vyombo vya habari binafsi kutoa habari na kulinda maadili ya kitaaluma ya vyombo vya habari na utoaji leseni kwa magazeti.

Sehemu ya III: Sehemu hii inaainisha masharti yanayohusu uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, muundo wa Bodi ya Ithibati, majukumu ya Bodi, mamlaka ya Bodi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Majukumu ya Mkurugenzi Mkuu, Watumishi wa Bodi, uthibitishaji wa wanahabari, kitambulisho cha wanahabari, Mfuko wa Mafunzo ya Wanahabari na vyanzo vya fedha za Mfuko.

Bodi ya ithibati itaainisha sifa za kitaaluma na nyinginezo za mwanahabari kwa kushirikiana na wadau wenyewe wakati wa hatua ya Waziri kutunga kanuni. Sehemu hii kimsingi inataka tuwe na wanahabari wenye elimu na uelewa wa kutosha kama alivyopata kutuasa hayati Mzee Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini kuwa (nanukuu):

A critical, independent and investigative press is the life blood of any
democracy.”
Mwisho wa kunukuu. Hatuwezi kuwa na “critical press” bila kuwa na wanahabari wenye sifa stahiki za kitaaluma na kimaadili.

Sehemu ya IV: Sehemu hii ina masharti yanayohusu uanzishwaji wa Baraza huru la Habari, wanachama wa Baraza, majukumu ya Baraza, mwenendo na mikutano ya Baraza, Mamlaka ya Baraza, majukumu ya Katibu wa Baraza na kuondolewa kwa Katibu wa Baraza. Vilevile, sehemu hii inaipa Baraza Mamlaka
ya kushughulikia malalamiko dhidi ya machapisho. Mtu asiyeridhika na uamuzi wa Baraza anaweza kukata rufaa Mahakama Kuu.

Sehemu ya V: Inahusika na masuala ya kashfa. Sehemu hii inatoa ufafanuzi endapo jambo lolote litachapishwa na kutangazwa na mtu na kusababisha kuharibu sifa ya mtu au kuchafua jina lake; mtu huyo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria. Aidha, sehemu hii imeainisha utangazaji wa mambo yenye kashfa ambayo yanaruhusiwa ikiwa mambo hayo yatatangazwa na Rais, Serikali au Bunge au jambo lolote litakalotangazwa mahakamani wakati wa kusikiliza shauri au kutangazwa jambo lolote kwa mujibu wa sheria.

Sehemu ya VI: Inaainisha masharti yanayohusu masuala ya fedha za Bodi na vyanzo vya mapato ya Bodi. Aidha, makadilio ya bajeti ya Bodi, utoaji wa taarifa za fedha, vitabu vya fedha vya Bodi pamoja na ukaguzi wake vimwekewa masharti.

Sehemu ya VII: Sehemu hii inahusu makosa mbalimbali ambayo yanahusu vyombo vya habari. Sehemu hii imeainisha makosa dhidi ya utangazaji wa habari ambao umepigwa marufuku, habari za kuchochea uasi, makosa ya uchochezi na utangazaji wa habari za uongo au za kutia hofu jamii.

Mheshimiwa Spika,

Makosa yote yaliyoainishwa yanaendana na matakwa ya sheria mbalimbali za kimataifa kuhusu ukomo wa uhuru wa habari kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia (1966) na Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu na Watu (The Banjul Charter, 1981).

Lakini pia nisisitize tena, fani ya habari ni sekta yenye haki na wajibu na ukiacha sheria hizi za kimataifa, wanafalsafa na hata wasomi wote mashuhuri wamepata kusisitiza kuwa uhuru wa fani hii una ukomo.

Kwa mfano, pamoja na mapenzi yake yasiyomithilika kwa sekta ya habari, Rais Jefferson wa Marekani niliyemnukuu awali, bado aliamini kuwa uhuru huo una mipaka. Katika barua yake kwenda kwa rafiki yake mwingine mkubwa, James Madison, wakati wa mjadala nchini Marekani kuhusu haki za kiraia, Jefferson alitaja mambo yanayoweza kuwa kizuizi halali (allowable restriction) cha uhuru wa habari kuwa ni pamoja na (naomba kunukuu):

Matendo yanayoweza kusababisha madhara kwa uhai wa mtu, uhuru wao kwa ujumla, mali zao au kushambulia heshima ya mtu au kuharibu amani na utulivu na ushirikiano wetu wa mataifa.”


Baba wa Taifa letu, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika tamko la ke la mwaka 1970 akiainisha sera ya uhariri kwa magazeti ya Serikali alipata kusema kuhusu wajibu wa magazeti na ukomo wa uhuru wao (namnukuu):

A newspaper only keeps the trust of its readers, and only deserves their trust, if it reports the truth of the best of its ability, and without distortion, whether that truth is pleasant or unpleasant.” Mwisho wa kunukuu.

Kwa upande wake mwasisi wa Taifa la India, hayati Mzee Mahatma Gandhi anayefahamika kuwa mpigania uhuru wa aina yake akitumia zaidi falsafa yake ya kutotumia nguvu, akipata pia kuwa mwanahabari, bado aliamini kuwa uhuru wa kweli wa kujieleza ni ule unaoweka mbele heshima ya watu wengine na
kuwalinda dhidi ya dharau, kebehi, kejeli na madhara mengine. Alisema kalamu
isiyoshikwa vyema hutoa mwandiko mbaya na namnukuu:

I venture to suggest that rights that do not directly form duty well performed are not worth having....Freedom of the press is a precious privilege that no country can forego….The sole aim of journalism should be service…even so an uncontrolled pen serves but to destroy.”

Kwa upande wake, msomi wa Kiingereza anayesifika sana kama “Baba wa Uhuru wa Habari” John Stuart Mill (1806-1873) katika fasihi yake “On Liberty” licha ya kubainisha vyema dhima ya vyombo vya habari na umuhimu wa kuwa huru bado alisisitiza yafuatayo kuhusu ukomo wa haki ya kupata habari kuwa unakoma pale haki za watu wengine zinapoanzia (namnukuu):

The only freedom which deserves the name is that of pursuing our own good in our own way, so long as we do not attempt to deprive others of theirs, or impede their efforts to obtain it.”

Mheshimiwa Spika,

Sehemu ya VIII na ya mwisho katika muswada; sehemu hii inahusika na masuala ya jumla ambapo inapiga marufuku uingizaji wa machapisho ambayo hayana manufaa kwa umma. Aidha, sehemu hii ina mpa Waziri mamlaka ya kutengeneza kanuni kwa ajili ya uendeshaji bora wa sheria na uanzishwaji wa masuala ya mpito. Sheria hii pia inafuta sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyokuwa ikilalamikiwa sana na wadau wa habari.

5.0 MABORESHO MUHIMU MUSWADA WA HUDUMA ZA HABARI, 2016

Mheshimiwa Spika,

Kama nilivyoainisha awali, kutokana na michango mingi ya wananchi wa kawaida, wanataaluma wenyewe wa habari, wanasheria na wadau wengine ikiwemo waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati husika na mchango wa wabunge wa Kamati nyingine za Bunge, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa baada ya mashauriano kuna maboresho kadhaa ya msingi yamefanyika katika muswada. Baadhi ya maboresho hayo ni kama ifuatavyo:

Kuanishia haki na wajibu wa wanahabari

Katika eneo hili muswada wa awali kwa kiasi kikubwa uliainisha zaidi wajibu wa wanahabari. Lakini kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu imesaini na kuridhia na matakwa ya Katiba, na maoni ya wadau eneo hili sasa limeboreshwa katika kifungu cha 7 kwa kuainisha pia haki za wanahabari kama vile uhuru wa kukusanya, kuhariri na kuchapisha/kutangaza habari.

Kuainisha haki ya chombo cha habari kukata rufaa

Katika kifungu cha 10 kuhusu utoaji wa leseni za vyombo vya habari, muswada wa awali haukuwa umeweka haki ya atakayekataliwa kupewa leseni na Mkurugenzi wa Idara ya Habari kuweza kukata rufaa. Kifungu hiki kimeboreshwa.

Sasa umewekwa mfumo wa wazi zaidi na wa kidemokrasia ambapo uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO hautakuwa wa mwisho. Chombo husika kinaweza kukataa rufaa kwa Waziri wa Habari na pia mwishowe

kisiporidhika na uamuzi wa Waziri sasa kinaweza kupinga suala hilo Mahakamani.

Uwakilishi wa wanahabari katika Bodi ya Ithibati

Eneo jingine lililoboreshwa ni uwakilishi wa vyombo vya habari katika Bodi ya
Ithibati. Kwa mujibu wa mapendekezo ya awali, Bodi hiyo itakayokuwa na
wajumbe 7 sasa itakuwa na wanahabari wanne (4) akiwemo Mwenyekiti. Hata hivyo ili kuboresha uwakilishi wa wadau wenyewe wa sekta ya habari,

vifungu vimeboreshwa ambapo sasa wawakilishi wa tasnia hiyo watakuwa ni
kwa uwiano kutoka sekta ya habari ya umma na ile ya binafsi.

Jaji Mkuu kuweka utaratibu kusikilizwa haraka kesi za kashfa

Moja ya malalamiko makubwa ya wadau katika utoaji wa haki zinapokuja kesi za habari hasa zinazohusu masuala ya kashfa ni kuchukua muda mrefu kwa kesi hizo. Ili kulinda maslahi ya kibishara ya vyombo vya habari vinavyokuwa na kesi nyingi zisizokwisha na kutishia biashara zao kwa upande mmoja lakini pia kuwapatia wananchi walioumizwa haki yao haraka, muswada umeboreshwa.

Katika maboresho hayo sasa Jaji Mkuu, kwa kuzingatia tathmini ya uwezo wa

Mahakama na raslimali zilizopo, na kama ilivyowezekana kwa kesi nyingine

kama za uchaguzi na zile za biashara, atatunga kanuni zitakazoweka muda wa
kumalizika kwa kesi hizo.

Kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi

Mheshimiwa Spika,

Moja ya mageuzi makubwa katika muswada huu ni kuviondolea vyombo vya habari au wamiliki wake adhabu katika baadhi ya makosa yanayoweza kusababishwa na uzembe wa mwandishi binafsi. Kwa sheria hii sasa mwandishi kama mwanataaluma kamili anaweza kuwajibishwa na Bodi ya Ithibati kwa makosa ya kimaadili badala ya mtindo wa sasa wa kila kosa la mwandishi linabebwa na chombo chake cha habari au mmiliki.

Vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari

Eneo hili lilipokea maoni mengi ya wadau na Serikali yetu sikivu imeridhika na hoja za wadau na kufanya maboresho. Maboresho yaliyofanywa kwanza
yamelenga kumuondoa Mkurugenzi wa Idara ya Habari kuwa na mamlaka ya kukamata mitambo hiyo.
Badala yake, kama kuna tuhuma kwamba chombo chochote kimetenda kosa na kuna hoja na haja ya kuzuia baadhi ya vifaa vyake kama sehemu ya vielelezo vya kesi (kama ilivyo katika makosa mengine yasiyokuwa ya habari) basi kazi hiyo ya upekuzi ifanywe na polisi kwa mujibu wa mfumo uliopo sasa wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Mitambo kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti

Mheshimiwa Spika,

Katika maeneo mengine ambayo wadau wengi walijenga hoja ni suala la mitambo ya uchapishaji (printers) kuwa sehemu ya wakosaji pale chombo cha habari kama gazeti kinapokuwa kimeandika habari ya uchochezi au yenye makosa mengine kama kashfa.

Serikali imekisikia kilio hiki, imetafakari na imeona kuna hoja katika hili. Kwa mujibu wa teknolojia ya sasa, kuwalazimisha wachapishaji waangalie kila

kinachokuja kuchapwa, au kuwahukumu moja kwa moja kwa kuzuia mitambo yao kwa kosa la mtu mwingine halikuwa jambo jema.

Eneo hili limeboreshwa kwa kuwaondoa wachapishaji kwa maana ya “printers” kwenye makosa yanayotokana na maudhui yaliyoandaliwa na watu wengine

isipokuwa pale tu itakapobainika kuwa katika suala mahsusi mwenye mtambo alijua kuhusu maudhui yenye kasoro au alijulishwa lakini akaendelea kuchapa kazi hiyo.

6.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,

Sheria hii inaleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa sekta ya habari hapa nchini. Ni sheria ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu itaigeuza rasmi sekta ya habari kuwa taaluma kamili na inayotambuliwa, kuenziwa na kuheshimiwa zaidi.

Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuwe tayari kuwa sehemu ya kuitimiza historia hii adhimu. Michango yetu, maboresho yetu na nguvu zetu tuzielekeze katika kuhakikisha tunaingia katika historia ya kuviachia vizazi vijavyo taaluma ya habari yenye watu wanaojiheshimu na waliotayari kushiriki katika kuijenga na si kuibomoa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Nihitimishe kwa kuwashukuru wafanyakazi wote wa Wizara yangu na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa pamoja wakati wote wa maandalizi ya muswada huu. Historia itawatambua kwa kazi njema ya mikono yenu.

Kipekee niwashukuru wafuatao kwa majina: Mhe. Anastazia James Wambura (MB), Naibu Waziri; Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu; Bi. Nuru Khalfan Millao, Naibu Katibu Mkuu. Nawashukuru pia Wakurugenzi wa Idara mbalimbali akiwemo, wakili Hassan Abbas, Mkurugenzi wa Idara ya Habari ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, wakuu wa vitengo na maafisa wengine Wizarani kwa kunishauri kila siku katika utendaji wa kazi zangu. Nawashukuru sana.

Mwisho kabisa lakini si mwisho kwa umuhimu, nitambue mchango wa mke wangu kipenzi, Roby Nape Nnauye na watoto wangu wapendwa. Hawa hawajapata kusita kunitia moyo na kuniunga mkono katika kuhakikisha natekeleza majukumu yangu ipasavyo. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya maelezo haya naomba sasa Bunge lako Tukufu liujadili muswada huu pamoja na jedwali la marekebisho na kuupitisha kwa manufaa ya Taifa.

Naomba kutoa hoja.
 
Utakuta watu wengi wala haielewi kuwa kuna mswaada kama huo ila ukiwauliza kuhusu ratiba ya ligi ya Uingereza hawakosei hata kidogo na wataanza kujua baada ya sheria kuanza kun'gata.
Wazee was kubet hao!
 
CvS7pKdXgAAVNY2.jpg:large


Dar es Salaam, Tanzania
Muswada wa Huduma za Habari una vipengele vingi kandamizi. Muswada huu ukipitishwa,uhuru wa habari utaminywa kwa kiasi kikubwa.
 
Yes....kama ni mbaya ni wetu sote na kama ni mzuri ni wetu sote.Leo mimi kesho wewe.
 
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa sheria na tayari kupelekwa kwa muheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwa sheria tujiandae wana JamiiForums.

Unganisha na yale maneno ambayo alisema mkuu kuwa malaika washuke kufunga mitandao ya kijamii.

Nyampua anatamani ahame nchi hahahahah
 
Back
Top Bottom