Hotuba Upinzani bungeni katika wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, utekelezaji wa mpango wa maendeleo 2018/19 na 2019/2020

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA AFYA,MAENDELEO YA JAMII,JINSIA WAZEE NA WATOTO, MHESHIMIWA CECILIA DANIEL PARESSO (MB), KUHUSU UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO MWAKA WA FEDHA 2018/19 NA MPANGO WA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA, KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Januari, 2016
_____________________
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia uhai, afya njema na kunipa nguvu na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

2. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa napenda kuwashukuru wanachama pamoja na watanzania wote ambao waliacha majukumu yao na kusafiri kutoka majumbani kwao ndani ya jiji na nje ya Jiji la Dar es salaam kuja hadi gereza la Segerea kututakia hali mimi na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania na Mbunge wa Hai Mheshimiwa Freemani Mbowe.

3. Mheshimiwa Spika, aidha ni washukuru sana wananchi na wanachama wote wa Tarime Mjini kwa kunivumilia nakuwa na mimi kwa sala na maombi kwa kipindi chote cha siku 104 nilizokuwa gerezani, kwa umuhimu wa kipekee ni kwa familia yangu ambayo iliendelea kusimama na mimi katika kipindi hicho kigumu kwao ambacho sikuwa pamoja nao. Aidha napenda pia kuwatia moyo, Viongozi wengine wakuu wa CHADEMA ambao wanakabiliwa na kesi za uchochezi au kufanya mikutano ya kisheria katika mahakama mbalimbali hapa nchini.
4. Mheshimiwa Spika, Mwisho lakini sio kwa umuhimu ni kwa waheshimiwa wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa ushirikiano mkubwa mnaouonesha katika kipindi hiki kigumu cha Bunge la 11, kwani mazingira ya ufanyaji kazi ndani na nje ya Bunge haya akisi haki yetu ya kisheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

B. SEKTA YA AFYA NCHINI na UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019

5. Mheshimiwa Spika, Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa za kanda na hospitali ya taifa.
6. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua umuhimu wa sekta ya afya katika maendeleo ya Taifa. Hakuna na wala hakutakuwepo kamwe Tanzania ya viwanda pasipo kuwa na taifa la watu wenye afya bora. Nguvu kazi ya taifa lolote duniani ni uwepo wa watu wenye afya bora ya mwili na akili. Ni jambo la kushangaza sana kuona zaidi ya asilimia 71 ya bajeti ya afya iliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2017/18; ilitegemea wahisani huku fedha za ndani ikiwa ni asilimia 29 tu. Hii maana yake ni kuwa asilimia 71 ya maisha ya Watanzania imewekwa rehani kwa wahisani.

7. Mheshimiwa Spika, kimsingi majigambo ya Serikali kwamba imeboresha sekta ya afya nchini ni katika kujitafutia umaarufu wa kisiasa tu. Hii ni kwa sababu bajeti ya afya kwa mwaka mpya wa fedha 2018/19 imepungua kutoka shilingi trilini 1. 07 kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia shilingi bilioni 866.2331 kwa mwaka 2018/19 ikiwa ni punguzo la shilingi bilioni 211.468.

8. Mheshimiwa Spika, hili ni anguko la asilimia 19.622 la bajeti ya Wizara ya afya kwa kulinganisha na mwaka wa fedha 2017/18. Na kama ilivyo kawaida ya Serikali hii kutotekeleza bajeti inayoidhinishwa na Bunge.

9. Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji iliyotolewa na Wizara Mwezi March,2019 inaonesha kuwa fedha ambazo zimepokelewa hadi mwezi February, 2019 ni shilingi 304,707,109,084.00 kati ya shilingi 866,233,475,000.00 zilizokuwa zimeombwa na kuidhinishwa na Bunge, Kati ya fedha hizo fedha za maendeleo zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi 89,955,841,092.00 sawa na asilimia 16 ya shilingi 561,759,999,000.00 zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge kama fedha za miradi ya maendeleo. Aidha, shilingi 180,000,000,000.00 ambazo ni takribani mara mbili ya fedha za ndani zilipokelewa kutoka Mfuko wa Dunia (Global fund) wa kupambana na Malaria, UKIMWI na kifua kikuu nje ya mfumo wa Excheqer.

10. Mheshimiwa Spika, Lakini ukiangalia Randama ya Mpango na Matumizi kwa fungu 52 iliyotolewa mwezi March, 2019 Uk. Wa 3 inasema fedha zilizopokelewa kutoka Global Fund ni shilingi 75,427,463,684.27. Hii ni mkanganyiko wa takwimu kwa taarifa hizo mbili ile ya utekelezaji wa mwaka 2018/19 na hii ya 2019/20 fungu hilo hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaomba kupatiwa taarifa sahihi.
11. Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni kuwa afya ya watanzania imewekwa rehani na Serikali, siku tusipopokea fedha za mfuko wa dunia ni dhahiri Tanzania itapoteza sifa yake ya kuwa ni Taifa lenye watu wenye nguvu na afya bora na sio taifa lenye watu dhaifu.

12. Mheshimiwa Spika, aidha huu ni ushahidi wa wazi kwamba sasa afya si kiupaumbele tena cha Serikali hii ya awamu tano jambo ambalo ni hatari kwa afya za watanzania na ukuaji wa uchumi wa taifa ambao hutegemea nguvu kazi yenye afya.

13. Mheshimiwa Spika, upungufu huu wa bajeti ya afya hauendani kabisa na ongezeko la watu ambao pia hupelekea ongezeko la watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya. Aidha, bajeti hii haiakisi haja ya kufanya tafiti mbalimbali juu ya magonjwa mapya yanayoibuka mara kwa mara. Sekta ya Afya ina changamoto nyingi ambazo huongezeka siku hadi siku. Kitendo cha kupunguza bajeti ya afya hakuendani na kuongezeka kwa changamoto hizo.

14. Mheshimiwa Spika, Azimio la Abuja lililofanyika miaka 15 iliyopita linazitaka nchi kutenga asilimia 15 ya fedha zote za bajeti ya nchi katika sekta ya afya, ambapo nchini mwetu lengo halijafikiwa kwa kuwa bajeti ya sekta ya afya ni chini ya asilimia 10.
i. Upungufu wa Rasilimali Watu kwenye Sekta ya Afya

15. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya hapa nchini inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa rasilimali watu. Kwa mujibu wa Ripoti ya Madaktari wenza wa Afrika (Africa Cuamm); Wizara hii ilikuwa na upungufu wa watumishi kwa asilimia 49 katika mwaka wa fedha 2016/17.Hata hivyo, pamoja na kuwa serikali haijatoa tathimini ya uhitaji wa jumla wa watumishi katika sekta hii; katika taarifa ya utekelezajiwa bajeti ya Wizara(fungu 52) inaonyesha kuwa; Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilitoa nafasi za ajira 3,152. Katika nafasi hizo, ajira za madaktari bingwa zilikuwa 24, madaktari wasaidizi 45, wauguzi daraja wa pili 137 (nurses) na nafasi 2 za madaktari washauri 2(Medical Consultant) na wengine walipelekwa kwenye kada mbalimbali.

16. Mheshimiwa Spika, Alipokuwa akifungua mkutano wa 48 wa chama cha madaktari uliofanyika Novemba 2016, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema sekta ya afya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa takribani asilimia 52 wa wataalamu wa afya katika kila ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya huku akiutaja upungufu huo kuwa umezidi kuwa juu vijijini ukikadiriwa kufikia asilimia 74.
17. Mheshimiwa Spika, bado rasilimali watu katika sekta ya afya nchini ni tatizo hususani katika maeneo ya vijijini. Bado wataalamu wetu wa afya wanafanya kazi kubwa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa japokuwa wataalam wengi waliondolewa kwa kilichoitwa “vyeti feki” bila ya kuziba nafasi kwa idadi ya walioondolewa kazini. Pamoja na kuwa serikali imesema imetoa ajira tukumbuke kuwa ni serikali hiyo hiyo ndio inayotaka kufanya tafiti za upungufu wa watumishi na ndio hiyo hiyo inayoamua iseme nini kwa umma kuhusiana na ajira au mapungufu ya watumishi jambo ambalo linaathiri uhalisia wa matatizo katika sekta mbalimbali. Jambo ambalo linatia mashaka katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili serikali.
18. Mheshimiwa Spika, tukumbuke kuwa pale ambapo taasisi au watu mbalimbali wanakuwa huru kufanya tafiti ndipo serikali inaweza kujikosoa na kufanya maboresho. Upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ni tatizo linalohitaji umakini na weledi mkubwa la kulishugulikia kwani kuna hatari ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la vifo vinavyotokana na ukosefu wa tiba kwa wakati.

19. Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni serikali ilikiri uhaba mkubwa wa madaktari. Kwa mujibu wa kumbukumbu, Serikali hii ya awamu ya tano iliwahi kutaka kuwapeleka madaktari 500 nchini Kenya hili hali nchi ikikabiliwa na tatizo kubwa na sugu la uhaba wa madaktari. Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Mwaka 2012 idadi ya madaktari na wauguzi kwa Tanzania ilikadiriwa kufikia 2,250 ambapo ni sawa na uwiano wa madaktari 0.5 kwa watu 10,000. Kwa mujibu wa gazeti la Guardian on Sunday mwaka 2013 nchi ilikuwa na upungufu wa madaktari 2,7002. Uchambuzi uliofanywa na the Citizen Tanzania mwaka 2016 unaonyesha uwiano kuwa daktari 1:25,000 kinyume na muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO)

20. Mheshimiwa Spika, Serikali hiyo hiyo leo inatoa ajira 24 kwa madaktari na madaktari wa daraja la pili 45 tu kwa nchi nzima bila kujali ongezeko kubwa la watu kuanzia mwaka 2012 baada ya sensa ya taifa; ambapo idadi ya watu ilikuwa milioni 44 tofauti na sasa idadi ya watu kwa nchi yetu inakadiriwa kufikia takribani milioni 52.55 mpaka mwaka 2017 kwa mujibu wa Tume ya taifa ya takwimu. Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha uwepo wa idadi ya watu takribani milioni 56 mpaka mwaka 2017 huku nchi yetu ikitajwa kati ya nchi 5 Afrika zenye watu wengi zaidi kwa mujibu wa hotuba Waziri wa Fedha na Mpango ya mwaka 2017 kuhusu hali ya uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2017/20183.

21. Mheshimiwa Spika,Pamoja na ongezeko hilo kubwa la idadi ya watu serikali imeshindwa kuzalisha ajira za wataalamu na wanataaluma watakaoweza kukabiliana na changamoto zinazoibuka kila siku ikiwemo mlipuko wa magonjwa yale ya kuambukiza na hata yasiyo ya kuambuza. Hata hivyo kwa mujibu wa The Citizen Tanzania, kuna wanafunzi wengi wanaohitimu mafunzo ya tiba na afya lakini ni wachache sana wanaopata ajira ya serikali kwani wengi huishia kuajiriwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kuajiriwa kwenye sekta za ujuzi tofauti na hata kujiajiri wenyewe. Hii imejionyesha wazi kwenye randama ya Wizara Ukurasa wa 50 ambapo idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya afya nchini walikadiriwa kuwa 47,269 huku ajira zilionekana kutolewa chache sana.

22. Mheshimiwa Spika, inashangaza kuona serikali ilitoa nafasi 2 tu kwa Madaktari washauri (Medical Consultant) ambapo hata hivyo serikali imekiri kushindwa kujaza nafasi hizo mbili4. Nchi nyingi duniani hasa zile za uchumi wa kati na zile zilizoendelea zimeweza kupiga hatua kubwa katika kuwekeza kwenye afya za wananchi wao.Viwanda haviwezi kuzalisha pasipo watu kuwa na uhakika wa tiba bora na uwezo wa kuonana na tabibu pale wanapomuhitaji. Pamoja na hilo tafiti za magonjwa, chanjo na tiba zinaweza tu kufanyika vyema hapa nchini kama serikali ikijikita kwenye uwekezaji wa afya. Mfano; kwa kupitia Bodi ya Madaktari wa California (Medical Board of California) mwaka 2015, katika ajenda zake kuu ni kuhakikisha kunakuwepo na madaktari na wataalamu wabobezi wa afya ambao watahakikisha maendeleo ya nchi yanaakisi uimara wa afya za raia. Kwa mantiki hiyo,uwekezaji katika afya ndio unaotoa mwelekeo wa uwekezaji katika sekta nyingine. Naweza kusema kuwa sekta ya afya ndio uhai wetuna ndio kichocheo kikuu cha maendeleo. (Health sector is paramount of all other sectors).

23. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 uk 21& 22 unaonesha idadi ya wagonjwa waliopata huduma kwenye hosptali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa kwa kipindi hicho kuwa ni 920,245, ni jambo jema ila hatuambiwi wagonjwa hao wamehudumiwa na madaktari, manesi na wataalam wengine waliopo kwenye sekta ya afya wangapi? Ni vyema tuelezwe kwa uwazi rasilimali watu iliyopo na inayohitajika katika sekta ya afya ni kiasi gani kwa kila hospitali kwenye kanda zetu na mikoa pia?

24. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa afya ya Taifa ni jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na kwamba utoaji wa huduma za afya za kibingwa kwa wakati zinaokoa muda wa uzalishaji na hivyo kuongeza ufanisi. Aidha, dawa za kuzuia magonjwa ni muhimu sawa na zile za kuponya magonjwa kwa kuwa zinasaidia kwa kiwango kikubwa kujenga ustawi na Taifa kuwa na afya.

25. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inaamini kwamba utoaji wa huduma za afya sio tu huduma za kijamii bali pia ni biashara ambapo sekta binafsi inashirikishwa kama mdau mkubwa katika kutoa mafunzo ya kitabibu na kutoa huduma za afya. Hivyo basi, ni lazima ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kujenga, kuendelea na kutumia miundombinu ya afya, kuongeza udahili wa mafunzo ya watendaji katika sekta ya afya ili kukidhi mahitaji ya jamii kupitia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma lakini Serikali ikibaki kuwa mbia mkuu.

26. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini katika ubora wa huduma, hivyo itaanzisha mchakato wa kujitathmini kwa wahudumu wa afya kwa ajili ya maisha yao hapa Tanzania, viwango vyao vya maslahi, na ubora kwa ajili ya utoaji wa huduma5.

27. Mheshimiwa Spika, Randama inaonesha kuwa mwaka 2018/19 jumla ya wanafunzi 18,539 sawa na 123.59% ya malengo ya wanafunzi 15,000 ifikapo mwaka 2020 walichaguliwa kujiunga na masomo katika vyuo mbalimbali vya afya. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hivi ukidahili wanafunzi wa kuingia vyuo vya afya, ni kuwa tayari umekuwa na wataalam wa afya, je wakiondolewa kwa kushindwa masomo? Hii ni sawa na kuwa na mayai alafu unasema nina kuku tayari!!!!

ii. Uwajibishaji wa watumishi wa sekta ya afya
28. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa juu ya uwajibishaji wa watumishi wa sekta ya afya hasa madaktari; zipo hatua na taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuniza Utumishi wa Umma kwa madaktari wote waajiriwa . Na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni hizo hatua hizo ni pamoja na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) ama Baraza la Wauguzi kwa upande wa wauguzi wenye kupewa mamlaka ya kutoa onyo na kuwasimamisha ama kuwafutia sifa za udaktari, madaktari ama wauguzi watakaokutwa na hatia baada ya malalamiko ya kutowajibika ama makosa yao kufikishwa kwenye Baraza husika.
29. Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya awamu ya 5 iingie madarakani kumekuwapo na wimbi kubwa la wanasiasa na hasa wasiokuwa na mamlaka ya kinidhamu kuwawajibisha madaktari pasipo kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na hivyo kuzua sintofahamu katika jamii na kushusha hadhi za mamlaka za kinidhamu zinazostahili kuwawajibisha madaktari waajiriwa wa umma.
30. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na muendelezo wa matukio si tu yanayodhalilisha taaluma za watumishi wa sekta ya afya bali pia yanayoishusha thamani awamu ya tano na kuzipoka mamlaka husika wajibu wake na matukio haya ni kama ifuatavyo kwa uchache wake:
i. Mwezi Machi mwaka 2017, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai alitangazwa na Jumuia ya Madaktari Tanzania kuwa adui namba moja wa afya baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kumuweka mbaroni Mganga Mkuu wa wilaya ya Kilwa, Dkt Vitalis Katalyeba. Dkt Katalyeba alisimimashwa kazi kwa kutuhumiwa kuchelewesha gari la kubebea wagonjwa na kusababisha kifo cha mgonjwa huyo. Mara baada ya kusimamishwa, Dkt Katalyeba alihudhuria mkutano ambapo kitendo hicho kilimuudhi DC huyo na kuagiza Dkt. Katalyeba kutiwa mbaroni.
ii. Tukio jingine ni la Mkuu wa Mkoa wa Singida Bi. Rehema Nchimbi alipomuweka Rumande Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini DR, Erivk Bakuza,pamoja na kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiutendaji bado taratibu za uwajibishwaji wa kinidhadmu zilitakiwa kufuatwa.
iii. Katika tukio jingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Ndg. Mrisho Gambo alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Monduli kutoa maelezo ya malimbikizo mbalimbali ya stahiki za watumishi wa afya huku akijua wazi kuwa sio jukumu la Mganga wa WILAYA, Ikumbukwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameendelea kuwa na historia mbaya na Madaktari kuanzia alipokua DC katika awamu ya nne ya CCM.
iv. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi mwezi Septemba 2018 alimsimamisha kazi kwa madai ya wananchi ya kudhalilishwa na Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Ukami, Dk. Andrew Kitwanga. Hii ilipelekea kuwapo kwa mjadala mzito na hata Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Suleiman Jaffo aliomba radhi kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa na kuahidi kutoa mwongozo kwa viongozi hawa juu ya hatua za kinidhamu.
v. April 2019, Daktari wa Kituo cha Afya Ngarenaro, Dkt. Japhet Kivuyo, mkoani Arusha baada ya kukutwa hayuko kazini uamuzi wa kufukuzwa kwake ulitolewa na Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Levelosi.

31. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa matukio haya ya kudhalilisha hata kama yana uhalali na iwapo hayafuati taratibu na kanuni zilizowekwa, hupunguza morali kwa watumishi hawa MUHIMU. Kuongezeka kwa vitendo vya viongozi wa umma na sasa imehamia kwa viongozi wa Chama Tawala, kunafanywa ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na havina nia ya dhati ya kukabiliana na changamoto za kipaumbele za sekta ya afya nchini.
32. Aidha Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa kukosekana kwa vitendea kazi ikiwemo magari ya wagonjwa na vifaa tiba ni kutokana na ufinyu wa bajeti za afya na pia ukosefu wa watumishi wa kutosha wa kada hii muhimu. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza wajibu wake ikiwemo kuhakikisha watumishi na vitendea kazi katika sekta ya afya vinapatikana. Vilevile, Serikali itimize wajibu wake wa kuwalipa stahiki watumishi wa afya pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi wanaostahili na kuacha kuwasingizia waganga wakuu majukumu yasiyo yao pale Serikali inaposhindwa kutekeleza majukumu hayo.




iii. Afya kwa wote (Universal Health Coverage)

33. Mheshimiwa Spika, Malengo ya afya kwa wote: serikali kupitia Waziri wa Afya kwenye hotuba yake ya mwaka 2018/19 aya ya118 alisema serikali inalenga kufikia mwaka 2020 Watanzania asilimia 70 wawe na bima ya afya. Lakini taarifa inaendelea kuasema kuwa kwa sasa watu walio kwenye mfumo wa bima ya afya ni asilimia 32 na asilimia 68 ambao hawako katika mfumo huo. Maana yake ni kuwa kati ya watanzania 100 ni watanzania 32 tu ndio wana uhakika na matibabu ya afya zao na waliobakia 68 maisha yao yako mashakani.

34. Mheshimiwa Spika, kauli ya Waziri kwenye hotuba yake ni kauli ambayo haioneshi umakini wa serikali katika afya ya watanzania, hivyo Kambi ya Upinzani Bungeni haikuona kama ina mkakati wowote ambao serikali iliweka ili kuhakikisha watu 68 kati ya mia wanajiunga na bima ya afya. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa Bungeni ni wananchi wangapi mpaka sasa wamejiunga na bima ya afya hasa wale wa kipato cha chini.

35. Mheshimiwa Spika, nchi nyingi zimeweka utaratibu na mfumo wa kuhakikisha wananchi wake wanajiunga na bima ya afya. Mambo ya msingi ili kufikia lengo hilo ni pamoja na kuwa na mkakati wa kifedha wa kugharimia huduma za afya (Health Financing Strategy), mfumo wa kutoa ruzuku ya bima kwa watu wa hali ya chini (subsidized insurance), Sera na sheria jumuishi (Social participation). Mpaka sasa Serikali haijapitisha mkakati wa kugharimia huduma za afya toka mwaka 2015, na wala haijaweka mfumo wa kutoa ruzuku ya bima kwa watu wa kipato cha chini.

36. Mheshimiwa Spika, matokeo ya kutokuwa na bima ya afya kwa wote ni kuwa mtu akiugua na hana hela na huacha kwenda kutibiwa, na matokeo yake ni kuwa ugonjwa huwa mkubwa zaidi, husababisha usugu wa dawa na hatimaye kutozalisha na hata kusababisha kifo. Matokeo yake serikali na familia hutumia hela nyingi kumtibu mgonjwa aliyezidiwa kwa gharama kubwa. Familia zinaweza kusukumwa kwenye umasikini kwa sababu hizo.

37. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri serikali kufanya yafuatayo: (a) Kutangaza kuwa inataka kusiwepo na Mtanzania anayekosa huduma za afya kwa kutokuwa na hela, (b) Kuleta mpango mahususi wa mfumo utakaotumika kuhakikisha watu wa hali ya chini wanakuwa na bima ya afya, (c) Kupitisha na kutekeleza mkakati wa kugharimia huduma za afya (National Health Financing Strategy) na (d) Kuweka malengo ya kuongeza matumizi kwenye sekta ya afya kufikia asilimia 4-5 ya pato la taifa kama inavyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani. Kwa ufafanuzi zaidi rejea sera ya Chadema uk 44 -47

38. Mheshimiwa Spika, kufikia kiwango hicho cha asilimia 4-5 cha GDP kilichopendekezwa na shirika la afya la dunia kinawezekana kama Serikali itakuwa na nidhamu ya kujikita/ kubakia kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano kama ulivyopitishwa na Bunge. Tumeona hivi sasa miradi mikubwa inatumia fedha za ndani au mikopo ya kibiashara wakati mpango upo wazi miradi mikubwa ya kimkakati inatakiwa kutekelezwa kwa ubia na sekta binafsi.

iv. Huduma ya mama na mtoto
39. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yake ya mwaka 2017/18 Wizara ilieleza bunge lako tukufu kuwa kuanzia mwezi Oktoba ilianzisha utaratibu wa kutaka kila halmashauri na mikoa nchini kutoa taarifa ya vifo vinavyotokana na uzazi kila mwezi. Ikiwa imepita takribani miaka miwili toka utaratibu huo kuanzishwa Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hadi sasa ni halmashauri ngapi nchini ambazo zimetekeleza utaratibu huo na kwa halmashauri na mikoa iliyoshindwa kufanyia kazi utaratibu huu zimechukuliwa hatua gani? na kwa mujibu wa takwimu na taarifa hizo je Wizara imeafanikiwa kwa kiwango gani kwa kutumia taarifa hizo katika kukabiliana na vifo vya mama na mtoto?
40. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya malengo ya mkakati wa afya ya uzazi na mtoto wa mwaka 2016-2020 ni pamoja na kupunguza vifo vya watoto wa chini ya mwezi mmoja kutoka 21 hadi 16 ifikapo mwaka 2020 katika kila vizazi hai 1000 pamoja na vifo vya watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kutoka 45 hadi 25 katika kila vizazi hai 1000 na vilevile vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kutoka 54 hadi 40 kwa kila vizazi hai 1000.
41. Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa takwimu za vifo vinavyotokana na uzazi nchini zimeendelea kupotosha hali halisi kwani kina mama wengi na watoto hasa vijijini wanafariki na idadi inaongezeka kutokana na kutokuwa na huduma bora za afya, kuongezeka kwa gharama za maisha, ukosefu wa umeme lakini vilevile miundombinu duni pamoja na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya hasa madaktari wa akina mama na kukosekana kwa vitendea kazi na vifaa tiba vinavyotokana na ufinyu wa bajeti.
42. Mheshimiwa Spika, ifike mahali sisi kama Taifa, tuweke mbali siasa katika masuala muhimu nchini hasa masuala ya uzazi ili kuhakikisha adhma ya kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
Aidha, huduma ya afya bila malipo kwa wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ni mojawapo ya sehemu ya Sera ya Afya ya Tanzania lakini mpango huu bado una mapungufu makubwa nchini. Kwa mujibu wa Takwimu bado wanawake 11000 hupoteza maisha nchini sawa na kina mama 30 kila siku. Bado katika hospitali mbalimbali na vituo vya afya kina mama wajawazito wanatakiwa kujinunulia vifaa vya kujifungulia kama pamba, nyembe, gloves na hata wakati mwingine huambiwa wanunue mipira ya kulalia wakati wa kujifungusa pamoja na kuwa serikali imesititiza kuwa vifaa hivyi hupatikana bure hospitali.
43. Mheshimiwa Spika, bado kumekuwa na malalmiko kuwa baadhi ya vifaa tiba vinavyotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) havina ubora unaotakiwa na kuwa vinaharibika mapema na hivyo kuongeza changamoto katika huduma za kujifungulia.ni lazima wizara, iwajibike katika kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa kwa wakati.
v. Wakunga wa jadi
44. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa ukosefu wa huduma za afya nchini bado umeendelea kuwa changamoto hasa katika masuala ya uzazi hususani maeneo ya vijijini. Kwa mujibu wa Takwimu zilizotoloewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wanaojifungua vijijini nchini hukosa usaidizi wa wataalamu na hivyo kupelekea kina mama hao kutafuta huduma za wakunga wa jadi.
45. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya habari zilizowahi kuripotiwa na vituo vikubwa ulimwenguni vya habari ni pamoja na habari iliyoripotiwa na SHIRIKA LA HABARI LA UINGEREZA (BBC) tarehe 17 Aprili 2019 iliyokuwa na kichwa cha habari “Wakunga wa jadi wawazalisha wanawake kwa kutumia mifuko ya Rambo Tanzania. kwa mujibu wa chapisho hilo la habari ilionekana kuwa baadhi ya vijiji mkoani Tabora hasa wilaya ya Sikonge, wakunga wa jadi hulazimika kuwazalisha kina mama majumbani na mara nyingi hulazimika kutumia mifuko ya Rambo na hii uongeza hatari ya magonjwa sio tu kwa kina mama hata kwa wakunga wanaowasaidia hata kwa watoto wanaozaliwa.
46. Mheshimiwa Spika, pamoja na marufuku iliyotolewa na wizara ya afya ya kuwapiga marufuku wakunga wa jadi kuwazalisha kina mama wajumbani, Wizara ilieleze bunge lako ni njia gani kina mama wa vijijini watumie hasa ukizingatia kuwa kuna matatizo ya usafiri na uhaba wa vituo vya afya vijijini. Kuwazuia wakunga wa jadi sio tu kunaongeza idadi ya vifo vya mama na mtoto bali kunaathiri kina mama wengi hasa ukizingatia kuwa wakunga wa jadi ni wakombozi wa kina mama ambao wengi wanaishi katika umasikini uliokithiri. kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara ya afya kuweka mkakati wa kutoa elimu na mafunzo ya awali kwa wakunga wa jadi na kuwawezesha ili kuwa mbadala wa watoaji huduma za afya hasa pale kunapokua na changamoto isiyotarajiwa katika maeneo husika na kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi.
47. Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa ikiwa wakunga wa jadi watapewa mafunzo stahiki basi Taifa litaondokana na changamoto hii kama ambavyo kwa upande wa Zanzibar wamefanikiwa kuwashirikisha wakunga wa jadi na wataalam wa afya.
vi. Hali ya ugonjwa wa homa ya ini- (Hepatitis)
48. Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa Homa ya Ini au Hepatitis hutokana na kirusi kinachoambukizwa kupitia kwenye damu na majimaji mengine ya mwili, na ambacho huvamia ini na kusababisha vifo vya watu wapatao 650,000 kila mwaka, wengi wao wakiwa katika nchi za kipato cha chini na kipato cha wastani.
49. Mheshimiwa Spika, Shirika la Afya Duniani, WHO ambalo ni kinara katika magonjwa mathalani homa ya ini aina ya Hepatitis hivi karibuni limetoa mwongozo wake wenye mapendekezo sita kuhusu matibabu ya ugonjwa huo.
50. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania imesema kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Homa ya Ini au Hepatitis, yameongezeka mara mbili yakilinganishwa na Virusi vya Ukimwi HIV nchini. Aidha, ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis) unaongoza kwa kuua Watanzania kutokana na maambukizi yake kufikia asilimia 16, huku virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, ikiwa ni asilimia 5.3. Ugonjwa huo huua taratibu ukilinganishwa na magonjwa mengine kwa kuwa dalili zake huchukua muda mrefu kuweza kujulikana na kujitokeza wazi kwa mgonjwa.
51. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka wazi kwa watanzania ni jinsi gani ugonjwa wa homa ya Ini umeenea, na kinga au chanjo yake inapatikana vipi ili kukinga maambukizi, Matibabu yapi yatumike awali na yapi yafuatie ikiwa ya awali hayakufanya kazi, na pia jinsi ya kufuatilia mambo hayo manne tajwa sambamba na kuangalia kama kuna saratani ya ini, na kiasi gani ugonjwa wa ini unavyoendelea.
52. Mheshimiwa Spika, takwimu za shirika la afya la Dunia zinaonesha kuwa inakadiriwa watu milioni 240 kote duniani wana kirusi cha Hepatitis, idadi kubwa ya maambukizi ikipatikana bara Afrika na Asia6 hasa kwa watu ambao ni masikini.
vii. Hali ya maambukizi vvu na ukimwi nchini
53. Mheshimiwa Spika, mapema mwezi Machi mwaka huu wa 2019, tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) ilitoa ripoti yake kuhusu maambuzi mapya ya VVU nchini. Katika ripoti yake ilibaini kuwa takribani Watanzania 225 huambukizwa virusi vya UKIMWI kwa siku. Huku Watanzania takribani 6,750 huambukizwa kwa mwezi na kwa mwaka takribani watu 82,125 huambukizwa virusi vya Ukimwi. Katika ripoti hiyo maambukizi makubwa yalionekana kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-24 na wengi wao wakiwa ni vijana wa kike. Kwa mujibu wa tume ya taifa ya takwimu (NBS) mpaka 2017 takribani watu milioni 1.4 walikutwa na maambukizi ya Ukimwi7. Hii inaonyesha ongezeko la maambukizi tofauti na tafiti zilizofanyika mwaka 2010-2015 ambapo maambukizi yalipungua kwa asilimia 20 (UNAIDS 2017).8

54. Mheshimiwa Spika, dhana nzima ya 90- 90- 90 iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/AIDS mwaka 2013 kwamba ili kufikia mwaka 2020 kusiwepo na maambukizi ya UKIMWI Duniani. Kwa maana ya kuwa 90% ya watu walioambukizwa virusi watakuwa wametambulika, 90% ya walioamtambulika watakuwa tayari wapo kwenye matibabu ya ARV na 90% ya walio kwenye matumizi ya ARV, virusi vitakuwa vimefubaa na hivyo hakutakuwa na maambukizi mapya. Hiyo ndiyo dhana nzima ya 90 90 90

55. Mheshimiwa Spika, Mkakati huo ulikuwa unajaribu kuzuia na kudhibiti maambukizi ya HIV kwa kutumia kanuni kuu ya kupima na kutibu (test and treat) wale wote wenye virusi ili kufikia lengo la 90 90 90. Kwa upande wa Africa nchi ya Botswana ndiyo inayokaribia kufikia lengo la 90-90-90 kwa kupima, kutibu na kufubaza virusi, na hili liliwezekana kwa nchi hiyo kwani ilikuwa nchi ya kwanza katika Africa kutoa matibabu ya ARV bure kwa watu wote wenye HIV tangu mwaka 2002
56. Mheshimiwa Spika, katika kongamano la siku latu lililofanyika Dodoma- kuanzia (June 20, 21, and 23, 2018) kuhusu jukumu na wajibu wa viongozi katika kufika lengo la HIV la 90-90-90 kwa mwaka 2020 Tanzania, ambalo liliandaliwa na Kamati ya Bunge ya UKIMWI kwa pamoja na Baraza la watu waishio na HIV/AIDS Tanzania (NACOPHA) ambao waliratibu wadau na asasi zisizo za kiraia chini ya Waziri Mkuu, Spika wa bunge na Mjumbe kutoka USAID wakiwa waongoza jopo. Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali kupitia TACAIDS inatekeleza mkakati wa kufikia lengo la 90 90 90.
57. Mheshimiwa Spika, kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu hadi sasa katika kufikia lengo la 90 90 90 Tanzania tumefikia wapi kwani tumebakiza mwaka mmoja na nusu kufikia muda uliowekwa na Umoja wa Mataifa?
58. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa Takwimu za UNAIDS za mwaka 2018 zinaonesha kuwa Tanzania ina watu milioni 1.5 wanaoishi na virusi vya Ukimwi (HIV) NA 4.5% ni watu wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wenye maambukizi na kuweza kueneza HIV, watu 65,000 wana maambukizi mapya(New HIV Infections) na vifo 32,000 vilisababishwa na UKIMWI, 68% ya watu wazima wapo kwenye matibabu ya ARV na 46% ni watoto walio kwenye matibabu ya ARV.

59. Mheshimiwa Spika, hali hii inatisha sana hasa tukizingatia kuwa maambukizi kwa vijana hawa wadogo ni asilimia 46. Wengi wa vijana hawa ni wale wenye umri wa kumaliza shule ya msingi mpaka chuo kikuu. Maana yake ni kuwa nguvu kazi ya taifa inapungua kwa kasi sana na pengine tatizo hili lisipochukuliwa kwa uzito mkubwa pengine miaka kadhaa mbele tutakakosa kabisa vijana wenye afya bora wa kulijenga taifa letu.

60. Mheshimiwa Spika,kuna haja sasa kuwekeza nguvu zaidi katika njia za kuzuia maambukizi mapya badala ya kutenga fedha nyingi katika kutibu magonjwa nyemelezi. Kwani kinga ni bora kuliko tiba. Ni muhimu kufanya tafiti zenye tija ili kuweza kubaini sababu zinazopelekea maambuzi makubwa kwa vijana wenye umri huu mdogo tofauti na miaka ya nyuma ambapo vijana wenye umri wa kati kuanzia miaka 35-49 ndio waliobainika kuathirika zaidi.

61. Mheshimiwa Spika, kubadilika kwa mfumo wa maisha, hali ngumu sana ya uchumi ambapo kwa sasa vijana hutumia lugha isiyo rasmi kuwa ‘vyuma vimekaza’, kupungua kwa jitihada za kupaza sauti na elimu juu ya masuala ya Ukimwi, ongezeko la ngono zembe na pengine changamoto za upatikaji wa dawa za kufubaza virusi zinaweza kuwa miongoni mwa sababu za maambukizi makubwa na ya kutisha kwa vijana hawa wadogo.
62. Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo pameibuka wimbi kubwa la ulawiti wa watoto hasa wa kiume. Jambo hili sio la kufumbia macho hata kidogo. Serikali na wadau mbalimbali lazima tuungane kukemea vitendo hivi viovu wanavyofanyiwa watoto. Japokuwa mambo haya huchukuliwa pia kwa usiri mkubwa kutokana na mila na desturi zetu lakini hatuna budi kama taifa kuanza kukemea hadharani mambo haya. Vitendo vya ushoga navyo vimeshamiri jambo ambalo linachochea kwa kasi maambuzi mapya ya virusi vya Ukimwi9

63. Mheshimiwa Spika,vile vile pamekuwa na malalamiko kwenye jamii juu ya uwepo wa takwimu zinazotolewa zisizo za kweli kuhusu maambukizi kwa sababu za kujipatia fedha kutoka kwa wafadhili. Takwimu za maambukizi zinatumiwa kama sehemu ya ‘miradi ya upigaji’. Novemba 28, Mwaka 2017Waziri Mkuu aliitoa kauli ya kukemea matumizi mabaya ya fedha za miradi ikiwemo miradi ya UKIMWI jambo ambalo linaonyesha dhahiri fedha nyingi za serikali zinazotengwa katika kupambana na janga la UKIMWI zinatumiwa kinyume na mpango wa matumizi na hivyo kuathiri juhudi za kupambana na janga hili.

64. Mheshimiwa Spika,kwa mwaka huu wa fedha takribani bilioni 84.9 zimetengwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi. Fedha hizi ni nyingi sana na hivyo ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe sasa ili kupunguza tatizo hili la sivyo, bajeti kubwa ya serikali itaendelea kutumika katika kupambana na ugonjwa huu bila mafanikio. Katika hotuba ya Waziri Mkuu aliyoitoa akifungua kongamano la kitaifa la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani Jijini Dar es Salaam alitoa kauli ya maazimio ya kumaliza tatizo la Ukimwi nchini ifikapo mwaka 2030.

65. Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali iliambie Bunge lako; ina mikakati gani ya kumaliza tatizo hili ifikapo mwaka 2030 iwapo kasi ya maambukizi kwa vijana wadogo inaongezeka, upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi ni wa kusuasua na maeneo mengi nchini hayapati dawa kwa wakati. Serikali ituambie ni nini mkakati wake katika kukabiliana na ongezeko kubwa la vitendo vya ulawiti na ushoga nchini ambapo tafiti mbalimbali zinaonyesha maambukizi ni makubwa zaidi hasa kwa wanaume wanaoshiriki ngono za jinsia moja (MSM).

viii. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza(Non communicable diseases- NCD)
66. Mheshimiwa Spika, magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, maradhi yanayohusiana na upumuaji na saratani yanazidi kuongezeka kwa kasi na yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani kote. Inakadiriwa Kisukari pekee kimeathiri maisha ya watu takriban 371 milioni duniani kote, huku 80% ya idadi hiyo ikiishi katika nchi zenye uchumi wa kati na nchi masikini. Kwa upande wa Tanzania, takriban watu wazima 9 kati ya 100 wana ugonjwa wa kisukari, na mtu mzima 1 kati ya 3 ana tatizo la shinikizo la juu la damu.

67. Mheshimiwa Spika, gharama ya kukabiliana na Magonjwa yasiyo ya kuambukiza duniani kote ni mabilioni ya dola na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa rasilimali finyu zilizopo. Kwa mwaka 2010 Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa jumla ya gharama za huduma za afya zinazohusiana na kisukari zilifikia dola 378 bilioni duniani kote, na kiasi hiki cha fedha kinaweza kufikia dola 490 bilioni ifikapo mwaka 2030.

68. Mheshimiwa Spika, nchi zinazoendelea kama vile Tanzania (na hata nchi zilizoendelea pia) hazina rasilimali za kutosha kutibu watu wote wanaobainika kuwa na kisukari. Hivyo, jitihada za kukabiliana na tatizo hili ni budi zikajikita zaidi katika mitazamo jumuishi inayolenga kukinga ili kupunguza kiwango cha Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye jamii yetu. Kinga ni bora kuliko tiba!!!!!

69. Mheshimiwa Spika, tatizo la Magonjwa yasiyo ya kuambukiza linakua kwa kasi katika nchi zinazoendelea, kama Tanzania. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 magonjwa haya yasiyo ya Kuambukiza yatasababisha asilimia 73% ya vifo vyote duniani na asilimia 60% ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.

70. Mheshimiwa Spika, visababishi vikubwa vya magonjwa yasiyoyakuambukiza ni: (a). Kutofanya mazoezi - kukaa darasani, ofisini, kuangalia runinga, kutumia lifti, kupanda magari na kutoshiriki michezo mbalimbali; (b). Ulaji usiofaa- kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, kula mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili, kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha; kula nafaka zilizokobolewa; (c) Matumizi ya pombe- tumbaku na madawa ya kulevya;(d) Msongo wa mawazo

ix. MATIBABU NJE YA NCHI
71. Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG ya mwaka 2016/17 ilionesha kuwapo kwa mapungufu katika usimamizi wa madeni kwenye matibabu nje ya nchi kwamba kulikuwa na kiasi kikubwa cha madeni kilichofikia Shilingi trilioni 2.68 kiasi ambacho ni ongezeko la Shilingi trilioni 0.793 sawa na asilimia 36 kulingana na salio la Shilingi trilioni 1.979 kwa mwaka ulioishia 30 Juni 2016.
72. Mheshimiwa Spika,Pia kulikuwepo na ongezeko kubwa la deni la gharama za matibabu nje ya nchi kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika hospitali za India kutoka kiasi cha Shilingi 28,609,803,615.40 kilichoripotiwa tarehe 30 Juni 2017 hadi kiasi cha Shilingi 45,731,070,267.31 kufikia tarehe 31 Desemba, 2017 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 37.44 kwa kipindi cha miezi sita tu.
73. Mheshimiwa Spika, Matumizi ambayo hayajalipwa ya gharama za matibabu ya wagonjwa waliotibiwa katika Hospitali za rufaa nchini India, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2018 gharama za hospitali zilikuwa kiasi cha Sh.29,172,371,931.26 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita gharama zilikuwa kiasi cha Sh.28,609,803,615.40 kuna ongezeko la kiasi cha Sh.562,568,315.80, sawa na asilimia mbili
74. Mheshimiwa Spika, tunafahamu kuwa kupatiwa matibabu kwa mtanzania ni haki yake na pale sheria zinapotoa utaratibu wa haki hiyo, lakini kumekuwapo na utaratibu usioridhisha wa kiupendeleo kwa wagonjwa wanaostahili kupatiwa matibabu nje ya nchi kulingana na maradhi yanayowakabili. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kitendo hicho cha kibaguzi katika matibabu kwa watanzania kinaleta hisia kwamba kuna watanzania wa daraja la kwanza, daraja la pili na la tatu wakati watanzania wote hao wanalipa kodi moja kwa moja au sio moja kwa moja (direct or indirect tax payers).
75. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa mchanganuo mzuri wa fedha zilizotumika kwa matibabu ya vigogo nje ya nchi ili ionekana wazi kwa walipa kodi jinsi kodi zao zinavyotumika.
x. Taasisi ya Chakula na Lishe
76. Mheshimiwa Spika, Randama ya Wizara fungu 52 inaonyesha kwamba; Mradi Na. 5496, (Tanzania Food and Nutrition Center) katika Taasisi ya Chakula na Lishe; haukutengewa fedha yoyote kwa mwaka wa fedha 2017/18; na pia kwa mwaka mpya wa fedha 2018/19. Katika kitabu cha taarifa za utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa kipindi cha Julai mpaka Februari 2018 kimeonyesha kuwa serikali ina azma ya kupunguza vifo vya watoto vitokananvyo na udumavu, ukosefu wa madini joto na vitamin A.

77. Mheshimiwa Spika, Upungufu wa vitamin na madini joto ni tatizo kubwa sana inalowaathiri watoto na wanawake walio katika umri wa kuzaa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Demographic Health Survey 2010 Takwimu zinaonyesha kwamba takribani asilimia 59 ya watoto wadogo na asilimia 41 ya kina mama wajawazito wanaathiriwa na ukosefu wa madini joto. Pamoja na kwamba kitabu cha randama ukurasa wa 70 serikali imeonyesha kuwa inatoa Vitamini A na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wadogo takribani nchi nzima lakini uhalisia wa utekelezaji wa azma hii ya serikali unatia mashaka sana.

78. Mheshimiwa Spika, katika mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/19 taasisi haikutengewa fedha yoyote. Lakini katika taarifa ya utekelezaji kwa taasisi hii inaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2018 hadi February, 2019 taasisi imetoa mafunzo kwa wazalishaji wa chumvi 706 na maafisa wa afya, maafisa Lishe na wataalam wa maabara wapatao 65, katika halmashauri mbalimbali zinazozalisha chumvi kwa wingi. Hoja ya msingi fedha zimetoka wapi katika kutekeleza majukumu hayo? Na kwa bahati mbaya pia kwa mwaka huu wa fedha 2019/20 taasisi hiyo kwa fedha za maendeleo haikutengewa fedha yoyote.

79. Mheshimiwa Spika, mwaka fedha 2017/18, Kambi Rasmi ya Upinzani ilizungumzia kwa kina tatizo kubwa la udumavu nchini. Tatizo hili lina athari kubwa sana kwa taifa kwani kwa kadiri ongezeko la watoto wenye udumavu nchini linafumbiwa macho ndivyo hivyo taifa hili linavyozidi kuzalisha watoto wasio na uwezo wa kujifunza darasani na wasio na uwezo wa ung’amuzi wa mambo (reasoning ability) yaani ‘vilaza au mbumbumbu’. Kwa mujibu wa utafiti wa REPOA wa mwaka 2014 takribani watoto milioni 2.4 nchini walikuwa na tatizo la udumavu. Hali hii inatisha sana na inazidi kukua kutokana na ukweli kwamba siku hizi watoto wengi mashuleni hawapati lishe kutokana na serikali kupiga marufuku michango mashuleni na huku ikijua wazi haina uwezo wakugawa vyakula mashuleni. Jambo hili linazidi kuhatarisha zaidi afya za watoto hususani wale wanaotoka katika kaya maskini ambapo watoto walitegemea kula mlo mmoja tu shuleni kwa kuwa familia zao zinashindwa kupata angalau milo miwili kwa siku.

80. Mheshimiwa Spika, tatizo hili la udumavu lina athari za muda mfupi na zile za muda mrefu. Hata kama mtoto aliathirika na udumavu utotoni athari zake zinaweza kuonekana pale anapokuwa mtu mzima. Tatizo hili huonekana pia sio katika elimu pekee bali pia katika uwezo wa kawaida wa ubunifu na ufikiri wa hali ya juu. Jambo hili linajidhihirisha wazi kwani katika mkutano wa wafanyabiashara na Rais uliofanyika Ikulu Mwezi Machi 2018 mmoja wa wafanyabiashara alilalamikia uwepo wa waajiriwa wenye Shahada ya pili (Masters) lakini hawawezi kuandika barua za kitaalamu. Na ni kweli pia tumeona wasomi wa PHD wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na katiba na kuipeleka jamii katika mtafaruku usio na sababu.

81. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia nukuu iliyoitoa katika hotuba yake ya Afya kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 iliyosema “Hatuwezi kupata viongozi wa serikali wenye uwezo mkubwa wa kutafuta suluhu ya matatizo yanayolikabili Taifa kama utotoni waliwahi kuugua tatizo la udumavu au hawakupata lishe bora, kamwe hatuwezi kutengeneza think tank ya taifa kama taifa limejaa watoto wenye udumavu au walioathirika na udumavu utotoni. “Udumavu hudumaza akili, husababisha ubongo wa mtoto au mtu mzima kushindwa kufanya kazi kwa haraka na kwa ufasaha”.

82. Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, kitendo cha wizara kushindwa kutoa fedha katika kitengo hiki cha lishe maana yake ni kuwa tutakuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaougua minyoo au walioathirika na minyoo jambo ambalo ni hatari sana kwani wapo minyoo ambao huathiri ubongo na uwezo wa kufikiri wa mtoto.

83. Mheshimiwa Spika, tunakumbuka katika serikali zilizopita kitengo hiki hakikuwahi kukosa fedha hata kidogo. Tafiti za magonjwa yatokanayo na lishe zinaweza vipi kufanyika endapo kitengo hiki muhimu kinakosa fedha. Je, serikali hii ya awamu ya tano ina mkakati gani wa kupunguza tatizo la idadi kubwa ya watoto walio katika hatari ya kuwa ‘vilaza’ kutokana na ukosefu wa lishe bora ikiwa kitengo muhimu kinachohusika na utatuzi wa tatizo kiko taabani kwa ukosefu wa fedha?.

xi. Hali ya Afya ya Akili Nchini (Generalized Anxiety Disorder- Gad)

84. Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara hii; kwa miaka miwili mfululizo, imezungumzia kushamiri kwa ugonjwa wa akili nchini. Katika hotuba ya mwaka wa fedha 2017/2018 tulionyesha kwamba takribani watu 150-200 huhudhuria kliniki kwenye hospitali zinazotoa huduma kwa watu wenye matatizo ya akili kwa wiki kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee. Idadi hii ni kubwa mno!!!

85. Mheshimiwa Spika,pamoja na kwamba jambo hili linaonekana kupuuzwa na kutotiliwa mkazo na Wizara pamoja na wadau mbalimbali nchini vikiwemo vyombo vya habari, ni muhimu serikali hii ikatambua kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya kujiua, kuuana ndani ya familia, watu kutembea wakizungumza wenyewe barabarani n.k . Hali hii pengine inaweza kuchangiwa na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku pamoja na matukio yake hali inayopeleka watu wengi kuwa na wasiwasi na hofu za maisha.

86. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani tulikwenda mbali zaidi kueleza idadi ya madaktari ambao ni wataalamu wa magonjwa haya ya akili. Ambapo mpaka mwaka jana 2017; idadi ya madaktari hao walikuwa 26 tu kwa nchi nzima, huku hospitali Kuu ya Magonjwa ya akili Dodoma ikiwa na madaktari 5 tu.

87. Mheshimiwa Spika, hali ya hofu isiyo na kikomo huathiri zaidi uwezo wa mtu katika kufikiri na baadae huweza kuleta matatizo makubwa zaidi. Katika maadhimisho ya siku ya Afya ya Akili Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 10 ya mwezi Octoba kila mwaka, kwa mwaka 2017, kauli mbiu ilikuwa Afya ya Akili Mahali pa Kazi.

88. Mheshimiwa Spika, magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri au yanapeleka mabadiliko katika kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda mambo.Hata hivyo mabadiliko ya kitabia au mwenendo wa mtu huweza kuwa wa tofauti na usioendana na mwenendo wa jamii husika, mila au denturi. Magonjwa ya akili huathiri ufanisi wa utendaji kazi, na hivyo husababisha migogoro, na kuathiri uhusiano wa mtu husika na kuathiri jamii nzima inayomzunguka. Ni vyema pia jamii ikatambua matatizo ya afya ya akili hayaathiri watu maskini peke yao, bali pia hata viongozi. Tatizo hili lisipotafutiwa ufumbuzi linaweza kuleta athari kubwa hasa kwa watu walio katika ngazi za maamuzi (decision making)

89. Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua je, kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi katika vitengo vya afya nchini, serikali ina mkakati gani mahususi wa kuongeza rasilimali watu katika hospitali na vitengo vinavyoshughulikia matatizo ya Afya ya akili?Je, serikali inampango gani kupunguza matatizo ya afya ya akili mahali pa kazi na kuielimisha jamii kwa ujumla kuhusiana na matatizo ya afya ya akili ili kupunguza athari za matatizo yanayotokana na changamoto za kimaisha hususani hali ngumu ya maisha, madeni, unyanyapaa au kubaguliwa katika familia au jamii kwa ujumla.

xii. Afya na usafi wa mazingira
90. Mheshimiwa Spika, katika kikao ambacho Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Erik Solheim na Katibu Mkuu wa World Meteorological Organisation- Petteri Taalas waliwaalika wajumbe katika Mkutano wa Afya wa Dunia unaofanyika kila mwaka juu ya vipaumbele, fursa na changamoto katika miezi na miaka ijayo kuhusu Afya ya dunia.
91. Mheshimiwa Spika, Dr Tedros alisema kwamba "Ikiwa tunataka kufikia Afya kwa Wote, tutahitaji kuweka gharama katika afya kwenye mambo makuu, na hiyo ina maanisha mambo makuu hayo matatu ni: kuzuia, kuzuia, kuzuia". Aidha, alisema kwamba; "lazima tuhakikishe watu wanaweza kupumua hewa safi, kunywa maji salama, kuishi katika hali nzuri na kula chakula cha lishe bila ya uchafuzi."
92. Mheshimiwa Spika, Kulingana na takwimu za WHO, wastani wa watu milioni 7 hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa hewa, ikiwa ni pamoja na viharusi na ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa kupumua na kansa. Uchafuzi wa hewa katika miji mikubwa mikubwa unazidi viwango vya ubora wa hewa vya WHO.
93. Mheshimiwa Spika, hivyo basi kama ambavyo tumekuwa tukisema kwamba Mazingira ni mtambuka, na inategemea mazingira inatumika katika muktadha upi, katika sekta ya afya mazingira yanahusisha mambo kadhaa na machache tayari yameongelewa katika nukuu ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

94. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba mazingira katika sekta afya ni muunganiko mzima wa njia safi na salama ya matumizi ya vyoo, uteketezaji wa taka zinazotoka mahospitalini, usafi wa miili yetu kabla na baada ya kula chakula, usafi wa mazingira kwenye maeneo tunayoishi ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko na vievile kuangamiza mazalia ya wadudu waletao magonjwa.

95. Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji inaonesha tu kazi zilizofanyika hadi February, 2019, lakini haioneshi kazi hizo zilitakiwa zitumie kiasi gani cha fedha na fedha zilizotumika ni kiasi gani ili Bunge liwezi kupima, thamani ya fedha za walipa kodi kama zimetumika vyema.


C. MAENDELEO YA JAMII
96. Mheshimiwa Spika, sekta hii miongoni mwa majukumu yake ya msingi ni kushirikisha jamii katika kujiletea maendeleo, kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake, kukuza haki za mtoto na maendeleo ya familia katika jamii kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma za ustawi wa jamii katika makundi maalumu.
97. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 Sekta hii iliidhinishiwa jumla ya shilingi 32,140,649,000.00 lakini kati ya fedha hizo matumizi mengineyo zilitengwa shilingi 12,109,842,000.00 na fedha za maendeleo zilitengwa shilingi 4,913,845,000.00 hadi mwezi February fedha za maendeleo zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi 1,133,506,431.00 zote zikiwa ni fedha kutoka nje kwa wafadhili.
98. Mheshimiwa Spika, kama ambavyo mara zote Kambi Rasmi ya Upinzani inasema tusiweke rehani kwa wafadhili mambo yanayohusu maendeleo ya wananchi wetu, iwe kwenye afya (uhai), iwe kwenye elimu na ustawi mwingine uonahusu wananchi. Hili ni kosa ambalo linapelekea kuingiziwa mambo ambayo sio mila na tamaduni zetu katika mchakato mzima wa misaada hasa kwenye maendeleo na huduma kwenye jamii zetu.

i. Maendeleo na makuzi ya awali kwa mtoto--Early Childhood Development (ECD)
99. Mheshimiwa Spika,eneo muhimu katika maendeleo ya binadamu ni malezi na makuzi ya mtoto katika siku 1,000 za mwanzo (Early Childhood Development). Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 80 ya makuzi ya ubongo wa mtoto hufanyika kipindi hiki. Maendeleo na makuzi ya mtoto katika siku hizi 1,000 yana umuhimu katika maisha ya utu uzima kimwili, kihisia, kisaikologia. Hivyo kuwekeza katika umri huu ni kutengeneza ustawi mzuri wa watu wazima wa baadae.
100. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, kuwekeza dola moja katika kipindi hiki kunakadiriwa kurudisha dola kati ya 6 mpaka 1710. Madhara ya kutowekeza katika makuzi ya watoto yanaathiri katika kipindi chote cha maisha. Madhara hayo huwa katika maeneo ya uwezo wa kufikiri, afya, uwezo wa kuzalisha (Human Capital), kipato na usawia (equity). Kikubwa zaidi ni udumavu wa akili ambao unajitokeza katika kipindi ambacho mtu mzima anafanya maamuzi yake kulingana na mazingira yaliyomzunguka.
101. Mheshimiwa Spika; hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwaka wa fedha 2018/19 kuanzia aya ya 179 hadi 181 alilitaarifu Bunge kuhusu idadi ya vituo vya kulelea watoto (Day care centers) vimefikia 1,046 na kuwa chuo cha Kisangara ndicho pekee kinachodahili na kutoa wahitimu. Na kuwa Serikali ilifundisha walezi 600 kutoka manispaa nne za Dar Es Salaaam (Ubungo, Temeke, Ilala na Kigamboni). Serikali haikubainisha mikakati ya kuwafikia watoto wengine katika mikoa na wilaya nyingine za Tanzania na huko ndiko jamii kubwa ya wananchi ilipo.
102. Mheshimiwa Spika; Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaishauri serikali kulipa eneo hili kipaumbelee kwa kupanga mikakati ya kuwa na vyuo vya kufundisha wataalamu wa malezi na matoto wadogo, Kupanua wigo wa ECD zaidi ya Early Childhood Education (ECE), Kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya eneo hili, kuweka mkakati wa kufikia wilaya zote kwenye eneo la ECD ili kuwa na kizazi chenye ubora.
103. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inahitaji majibu kwa Maswali yafuatayo:
Je, serikali ina mpango gani wa kupanua wigo wa ECD kutoka ECE na kushirkisha maeneo ya afya, lishe na maji.
Wizara imepanga kiasi gani cha fedha kwa mwaka huu kwa ajili ya ECD? Na Kwa vile Bank ya Dunia iko tayari kuikopesha Tanzania Dola za Marekani Millioni 200 toka Nov 2017, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuomba hela hiyo?
Je, Serikali inaongeza lini vyuo vya kufundisha wataalamu wa ECD ili kukidhi mahitaji ya nchi kulingana ili kulingana na sense ya watoto chini ya miaka mitano?
Je, serikali ina mpango gani kufundisha walezi kwenye halmashauri zingine mbali na wale waliofundishwa kwenye manispaa za mkoa wa Dar Es Salaam?



ii. Matumizi Mabaya ya Madaraka na Athari zake kwa Watoto

104. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kwamba; mwaka 2009 serikali ilipitisha sheria ya kulinda haki za watoto (Law of the Child Act 2009). Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inalinda uhai, utu na heshima ya mtoto. Mnamo Mwezi Aprili, 2018; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliwaita kina mama wote ambao wametelekezwa na wazazi wenza katika malezi ya watoto ili ofisi yake iwapatie msaada wa kisheria.

105. Mheshimiwa Spika, Kitendo alichokifanya Mkuu huyo wa Mkoa kilikiuka kwa kiwango kikubwa haki za watoto. Pamoja na kwamba pengine Mkuu wa Mkoa hakuwa na utaalamu wa masuala ya haki za Watoto, lakini ilikuwa ni muhimu sana wito huo uwe na tahadhari ya kulinda haki za watoto; kwa kuhakikisha watoto hao wanalindwa dhidi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Matumizi mabaya ya picha za watoto hao kwenye mitandao yana athari mbaya za kisaikolojia kwao kwa siku za baadae. Kimsingi kitendo hicho ni kinyume kabisa na Mkataba wa kimataifa wa kuliinda haki za watoto (Child rights Conventions) na ni kinyume na Sheria za haki za watoto.

106. Mheshimiwa Spika,Sheria zinatambua kuwa mambo ya kifamilia hususani migogoro inayohusu watoto hutatuliwa katika njia za kisheria na njia ambazo ni faragha ili kumlinda mtoto. Vilevile katika taratibu za mila na desturi zetu tunatambua kwamba migogoro ya kifamilia inaposhindikana katika ngazi za familia basi tuna ofisi za maafisa ustawi wa jamii ambao kimsingi ndio waliokabidhiwa kushughulikia migogoro hiyo na pale inaposhindikana sheria zaidi huchukua mkondo wake.

107. Mheshimiwa Spika, masuala yoyote yanayohusu kulinda haki na utu wa mtoto yasichukuliwe kisiasa hata kidogo kwani madhara yake ni makubwa kwa watoto. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka viongozi wa kisiasa kufuata sheria za nchi zilizopo na sio kujiamulia mambo kwa utashi wao binafsi. Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea na itazidi kukemea tabia hizi zisizo za kistaarabu zinazoendelea kushamiri kila uchwao ambapo baadhi ya wanasiasa wanadhani wao wako juu ya sheria. Tuna wajibu wa kutengeneza taasisi Imara ndani ya nchi yetu na sio kumtengeza mtu kwani kwa kufanya hivyo tunaathiri mifumo mingi ya utoaji haki na utendaji kazi serikalini. Tuziachie taasisi zifanye kazi yake.

iii. Kukithiri kwa wimbi la mauaji ya watoto nchini
108. Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo na taarifa mbalimbali zinazoonesha kuwa tatizo la utekaji na uuaji wa watoto nchini limepunguwa ama kudhibitiiwa bado matukio ya upoteaji na mauaji ya watoto yamendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini. Ikumbukwe kuwa Taifa lilianza kupata hofu ya mauaji ya watoto kwa kasi iliyoanza katika Mkoa wa Njombe, kusini mwa Tanzania. Lakini pamoja na kuwa vyombo vya usalama vimetoa ripoti ya kuonesha kudhibiti matukio hayo kwa mkoa wa Njombe, matukio haya ya kusikitisha yameendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini na kuhusishwa na masuala ya imani za kishirikina.
109. Mheshimiwa Spika, Sheria ya kudhibiti uchawi namba 12 ya mwaka 1998 (The Witchcraft Act) inaainisha wazi adhabu kwa watu wanaondesha vitendo vya kishirikina vinavyoweza kuwadhuru wengine lakini mpaka sasa Mamlaka husika hasa vyombo vya dola vimeshindwa kutoa idadi ama takwimu ya watu ambao tayari wameadhibiwa kwa mujibu wa Sheria hii na hivyo kuendelea kutoa mwanya kwa mitandao yautekaji na mauaji ya watoto nchini kujenga mizizi.
110. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kwa Mwezi April matukio ya watoto kukutwa wamefariki yameendelea katika mikoa ya TABORA, KILIMANJARO,SIMIYU n.k. Kambi Rasmi ya Upinzani inazitaka mamlaka zenye dhamana ya kusimamia ulinzi wa watoto kuwajibika ipasavyo kwa kushindwa kuwalinda watoto chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Haki ya Kuishi ya Mwaka 1984. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji; ni kwa nini vyombo vya dola huweza kupata intelijensia ya vurugu za mikutano ya wapinzani nchini lakini ishindwe kupata intelijensia ya Raia wake wadogo wasio na hatia?

iv. Ukiukwaji Mkubwa wa Haki za Watoto unaofanywa na Jeshi la Polisi

111. Mheshimiwa Spika, Mwezi wa AprilI, 2018 palitokea kifo cha mtoto wa miezi sita kwa jina la Halfani Lema ambaye alikuwa mkazi wa Ibanda Kata ya Nyegezi jijini Mwanza. Mtoto huyo alifariki saa chache baada ya mama yake kuachiwa kutoka kituo cha Polisi cha Igogo Nyegezi. Mtoto Halfani aliingia mahabusu na mama yake akiwa mzima na baada ya siku mbili alitoka akiwa na hali mbaya sana iliyopelekea umauti wake. Pamoja na kuwa mama huyo alitoa taarifa ya kubadilika kwa hali ya afya ya mtoto wake lakini polisi hawakujali.

112. Mheshimiwa Spika, kitendo cha kumuweka mama huyu mahabusu na mtoto mchanga, na hata alipoomba apewe ruhusu ya kumpeleka mwanaye hospitali alikataliwa mpaka hali ilipokuwa mbaya na kupelekea kifo cha mtoto huyo kutokea ni kitendo cha kinyama na kilaaniwe na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema. Uhai ni mali. Uhai wa mtoto ni maandalio ya nguvu kazi ya taifa.

113. Mheshimiwa Spika,Ili kukomesha matukio ya vifo kwa watoto vinavyosababishwa na uzembe au ukatili wa baadhi ya watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kulinda maisha ya watu na mali zao; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili; ni hatua gani ilizochukua dhidi ya waliohusika kusababisha vifo vya watoto; Halfan ambaye mama yake alinyimwa ruhusa na Polisi kumpeleka hospitali, pamoja na mtoto wa miaka 17 aliyejulikana kwa jina la Allen Mapunda aliyepigwa na polisi mpaka kufa na vingine vyote vilivyowahi tokea.

v. Sheria ya ndoa na ndoa za utotoni
114. Mheshimiwa Spika, ikiwa leo ni mwaka 2019, ni wazi kuwa Bunge linatakiwa liwalinde na kuwatengenezea mazingira bora zaidi watoto wa Tanzania ili kuendana na kasi ya dunia nzima ya kupinga ndoa za utotoni. Mojawapo ya Sheria tata ambayo imeendelea kuwa tanuri kwa watoto wa kike nchini ni Sheria ya ndoa ya 1971 (LMA, 1971) ambayo kimsingi inaruhusu wasichana wadogo wa miaka 15 kuolewa. Kwa wavulana umri huwekwa miaka 18.
115. Mheshimiwa Spika, katika majukumu ambayo Bunge tunayo na ndiyo yenye msingi wa uwepo wetu ni; 1. Kuwa wawakilishi wa wananchi lakini jukumu kubwa ambalo wananchi hawa wametuwekea dhamana; 2. Kutunga Sheria. Lakini ni dhahiri kuwa kuna baadhi ya sheria zimepitwa na wakati na sisi kama wawakilishi wa wananchi tuna jukumu la kutunga Sheria kuendana na mahitaji ya muda, mazingira lakini vilevile tamaduni zetu na kwa kuangalia Sheria nyengine ambazo zinalinda maslahi ya watu waliotupa dhamana.
116. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inahitaji mjadala mpana na ndio maana hata sasa zipo Sheria ambazo zinakinzana na sheria ya ndoa na ambazo zilipitishwa na Bunge ili kumlinda mtoto wa kike. Hizi ni pamoja na Kanuni za Adhabu, Sehemu 130 (2) (e) na 138, ambazo zinasema kuwa mtu anayefanya ngono kwa ridhaa au bila ridhaa na msichana chini ya miaka 18 anakuwa amebaka. Ikumnukwe kuwa Sheria ya ndoa inaruhusu msichana mwenye umri wa miaka 14 aolewe kwa ridhaa ya mahakama na kwamba ndoa imekamilika tendo la ndoa likifanyika. Chini ya Kanuni za Adhabu, ukamilifu huo ni kosa na hivyo kustahili adhabu.
117. Mheshimiwa Spika, Vilevile, tunayo Sheria ya Elimu, Marekebisho ya 2016, ambayo inasema ni kinyume cha sheria kuwa na mahusiano ya kingono au kumpa mimba msichana mwanafunzi. Lakini hapa hapa kuna mtanziko wa Kisheria kwa kuwa Sheria ya Ndoa hii imetoa mwanya wa wasichana wa miaka chini ya 18 kuolewa.
118. Mheshmimwia Spika, ni kwa masikitiko makubwa kuwa pamoja na kuwa sisi wabunge hasa wabunge wanawake tuna Mtandao wa wabunge wanawake hapa Bungeni bila kujali itikadi yetu TWPG, tumeweka msimamo wa pamoja wa kutaka Sheria hii ya Ndoa irekebishwe na kufuta kipengele kinachotambua ndoa ya mtoto wa kike kuanzia miaka 14. Lakini inapokuja katika kusimamia utekelezaji wa Azimio hili la TWPG, wabunge wanawake tunabebwa na misimamo ya vyama na sio maslahi ya pamoja ya kumlinda mtoto wa Kike.
119. Mheshimiwa Spika, katika Muktadha huu tunataka umma wa watanzania utambue kuwa iwapo Mtandao wa Wabunge Wanawake hautasimamia utekelezaji wa Azimio lake la Pamoja la kutaka Sheria ya ndoa ibatilishe kifungu hicho cha kuruhusu ndoa kwa mtoto wa kike chini ya miaka 18, basi Kambi Rasmi ya Upinzani itajitoa Rasmi kwenye umoja huu mapema iwezekanavyo ili kulinda maslahi ya watoto wa kike na kuanzisha Mtandao wa Hiyari ili kuhakikisha kipengele hicho kandamizi kinabadilishwa kabla ya Bajeti ya mwaka 2020/21.
120. Mheshimiwa Spika, Aidha, tunapenda kueleza masikitiko yetu juu ya upotoshwaji mkubwa uliofanywa na Profesa Kabudi kuwa bado kuna nchi zinazotekeleza ndoa za chini ya miaka 18 akitolea mfano nchi ya Uingereza chini ya Canon Law. Kwanza ikumbukwe; Tanzania ni Jamhuri lakini haifungani na Sheria za nchi yoyote pia; pili; Serikali haina dini; Lakini pia kigezo kuwa kuna nchi zinaruhusu ndoa za chini ya miaka 18; je kwa kuwa nchi hizo zimehalalisha pia mapenzi ya jinsia moja, basi na Tanzania tuhalalishe ili tupate uhalali wa Sheria ?
121. Mheshimiwa Spika, Vilevile, Nchi jirani ya Malawi, ambayo ni sehemu ya SADC, mwezi Februari 2017 ilibadilisha katiba yao ili kuzuia ndoa za utotoni kwa kuweka umri wa ndoa kuwa 18 kwa Wavulana na Wasichana.
122. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji ni kwa nini sheria nyingi zinazoathiri wanawake na watoto ndio ambazo zimekwama, miaka nenda miaka rudi lakini miswada mingine inapitishwa kwa dharura?
Utamaduni na Dini havipaswi kuwa sababu ya kumnyima mtoto wa kike haki zake za msingi. Kwa hiyo tunapaswa kuacha tofauti zetu za dini na za chama na tunahitaji kudai hii haki kwa kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
vi. Jukumu la serikali katika kuwasaidia watoto wa kike mashuleni
123. Mheshimiwa Spika,katika lengo namba nne la Mendeleo Endelevu (SDG’s) linasema “Achieving inclusive and equitable quality education for all”na katika lengo namba tano linasema “Achieving gender equality and empower all women and girls”.Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kuwa malengo haya mawili yanaitaka serikali kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote kwa kuzingatia jinsia katika kupata elimu bora huku watoto wa kike wakipewa kipaumbele kutokana na changamoto kubwa za kiafya zinazo wakabili ikiwa ni pamoja na changamoto za kibaiolojia na za kimazingira.

124. Mheshimiwa Spika, katika harakati za kumsaidia mtoto wa kike katika kupambana na ujinga, umaskini na maradhi ni pamoja na kutatua changamoto anazokumbana nazo kila siku katika jitihada zake za kujiletea maendeleo. Ni hivi karibuni ndani ya Bunge lako Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza alileta hoja ya kuitaka serikali kuanza kugawa taulo za kike mashuleni ili kunusuru afya za watoto wengi wa kike ambazo zipo hatarini kutokana na kukosa taulo safi za kujihifadhi wakati wa hedhi.

125. Mheshimiwa Spika, katika tafiti mbalimbali zinaonyesha ukosefu za taulo safi za kike kwa watoto wa kike mashuleni imekuwa ni miongoni mwa sababu za watoto wa kike kushindwa kuendelea na masomo,kukosa ufaulu mzuri na hata chanzo cha matatizo mengi ya uzazi na kansa. Ni dhahiri kabisa afya za watoto wa kike hususani maeneo ya vijijini yako hatarini kutokana na mifumo mibovu na mazingira duni yanayowafanya watoto wa kike wawapo katika siku zao kushindwa kuhudhuria masomo11

126. Mheshimiwa Spika, shule nyingi nchini hazina vyoo vya kutosha na hata vilivyopo havina mazingira mazuri kwa mabinti kubadili taulo zao wakati wa hedhi.Hivyo wengi huzitupa hovyo na wengine kulazimika kukaa nazo muda mrefu jambo linaloathiri afya zao.12
127. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta alisaini sheria ya marekebisho ya sheria ya elimu ya msingi,kuweka wajibu wa kutoa taulo za usafi (pads) za kutosha na zenye ubora kwa kila mtoto msichana aliyesajiliwa na kujiandikisha katika taasisi ya elimu ya msingi ya umma. Hii ni kuonyesha kuwa serikali ya Kenya imejizatiti kwa vitendo katika kumsaidia mtoto wa kike na sio maneno matupu.

128. Mheshimiwa Spika, inashangaza sana kuona pamoja na jitihada mbalimbali za wadau na sekta binafsi, serikali hii ya awamu ya tano imekuwa mstari wa mbele katika kukwamisha jitihada za mtoto wa kike katika kujikwamua kwenye lindi la ujinga na maradhi yanayozidi kuwatesa wanawake kila kukicha. Serikali hii ya hapa kazi tu imekuwa mzigo mzito kwa watoto wa kike kwani haki zao nyingi zimekuwa zikivunjwa bila kuangalia athari za muda mrefu (long term impact). Kwa mfano, kitendo cha kukwepa au‘kupotezea’mjadala mzito wa kugawa taulo kwa watoto wa kike maana yake ni kutaka watoto wa kike wa taifa hili wazidi kudhalilika na kuathirika kiafya na kielimu. Na sio hivyo tu, wengine hujikuta katika matatizo ya kupata ujauzito kutokana na kurubuniwa wakati wakitafuta fedha za kununulia taulo (pads) nyakati za hedhi ili kukwepa fedheha. Na hivyo watoto hawa hujikuta kwenye matatizo makubwa zaidi ikiwemo kufukuzwa masomo. Jambo hilo linazidi kuwazamisha katika lindi la umaskini,ujinga na maradhi.

129. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali hii kuacha ‘hadaa’ na ‘kuwanyanyapaa’ watoto wa kike kwa kuwa elimu na afya bora kwa mtoto wa kike ni msingi wa kuzalisha taifa bora la baadae. Mama bora wa leo huleta mtoto mwenye matumaini ya kesho. Bila kuwekeza kwa mtoto wa kike hatuwezi kamwe kupata viongozi bora wa kesho na wataalam wazuri kama vile; madaktari, walimu, makandarasi, wanasheria n.k wenye weledi katika kujenga kesho ya taifa letu.

vii. Pensheni wa wazee
130. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Wazee ndani ya taifa hili wamekuwa na kilio kilichoshindwa kupata suluhu katika awamu zote za utawala wa Chama cha Mapinduzi.Ni masikitiko kuona watu waliolitumikia taifa kwa nguvu zao zote wakipata manyanyaso makubwa katika nyakati ambazo nguvu zao zinakwenda zikiisha.
131. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge (HANSARD) za tarehe 21/04/2016 uk. 32 &33 zinaonesha kuwa Serikali ilitoa tamko kwamba nyongeza ya pensheni za wazee kutoka shilingi 50,000 hadi 100,000 zitalipwa pamoja na malimnikizo yake kuanzia mwaka wa fedha 2017/18. Lakini Wastaafu waliokuwa wako PPF walilipwa kuanzia Januari 2017 bila ya malimbikizo yao ya kuanzia mwaka 2015. Kwa masikitiko makubwakwamba mifuko ya hifadhi mingine iligoma kuwalipa wazee nyongeza zao na malimbikizo.
132. Mheshimiwa Spika, mdhibiti wa mifuko ya hifadhi –SSRA ameshindwa kusimamia au kuchukua hatua dhidi ya mifuko ambayo imekataa kwa makusudi kutekeleza agizo la Serikali kuhusu kulipa nyongeza malimbikizo kwa wazee. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze wazee ni lini sasa nyongeza na malimbikizo ya pensheni mifuko ya hifadhi itaanza kuwalipa wazee wote kulingana na nani anatakiwa kulipwa nini katika nyongeza na malimbikizo au vyote viwili?

133. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kijana wa leo ni mzee wa kesho na hivyo hatuna budi kuwajali wazee wetu na kuhakikisha wanaishi maisha ya furaha baada ya kustaafu. Pamoja na malalamiko ya muda mrefu ya Wazee yaliyotokana na sheria kandamizi mfano; sheria ile ya kikoloni iliyojulikana kama “The Pensions Ordinance of 1954”iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 1999 na baada ya hapo ikatungwa sheria nyingine iliyojulikana kama ‘The Public Service Retirement Act ya mwaka 1999’iliyoanza kutumika kuanzi tarehe 01Julai, 1999. Pamoja na sheria hiyo ilienda sambamba na sheria ya ‘The Political Pensions Act No 3 ya mwaka 1999’ ambayo nayo iliwalenga watumishi wenye nafasi za kisiasa.

134. Mheshimiwa Spika, tunatambua moja ya ajenda kuu ya serikali ya awamu ya nne kwa wazee ilikuwa ni kuandaa mfumo wa pensheni kwa wazee wote yaani ‘universal pension’.Katika mijadala mbalimbali ya kitaifa iliyohusu haki za Wazee iliwagawa wazee katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni wazee waliokuwa wakifanya kazi katika mfumo rasmi na kundi la pili ni lile ambalo linajumuisha takribani asilimia 94 ya wazee wote walio katika mfumo usio rasmi. Kundi hili linahusisha asilimia kubwa ya wazee waishio vijijini wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, mafundi mchundo, wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mama lishe, n.k

135. Mheshimiwa Spika, pamoja na makundi hayo wazee waliokuwa katika mfumo rasmi nao wamegawanyika. Wapo wazee waliofanya kazi kwa mikataba (On contract basis) wapo wazee ambao waliajiriwa na serikali kwa muda mfupi tu (Temporary terms) na wapo wazee ambao walioajiriwa kwa masharti ya kudumu (Permanent and pensionable terms).

136. Mheshimiwa Spika, pamoja na ahadi hiyo ya uongozi wa awamu ya nne utawala huu wa serikali ya awamu ya tano uliwahi kuzungumzia kuleta Bungeni Sheria ya Wazee. Tutakumbuka mwaka 2016, tarehe 29 April aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya alizungumzia kuanzishwa kwa sheria ya Wazee ili kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wazee. Jambo hili limezungumzwa mara nyingi na Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuwa Kambi inaamini Wazee ni hazina ya taifa letu.

137. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika randama za Wizara ya Afya hakuna kipengele kinachozungumzia ahadi ya uwepo wa Pensheni ya wazee wote kama serikali ya chama cha mapinduzi kilivyowaahidi wazee, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua je, serikali hii ya awamu ya tano imeifuta rasmi hoja ya kuanzisha malipo ya pensheni kwa wazee wote? Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua mchakato wa kuuleta Muswada wa Sheria ya Wazee Bungeni umefikia wapi ili kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili wazee zinatatuliwa. Pamoja na hayo serikali ione umuhimu wa kuanzisha chombo kitakachowaleta wazee pamoja kama chombo cha kuwasemea na kutetea maslahi yao kama vilivyo vyombo vingine vilivyoanzishwa kutetea maslahi ya kada mbalimbali.

D. MAOMBI YA FEDHA ZA KUTEKELEZA MPANGO WA MAENDELEO 2019/20
138. Mheshimiwa Spika, sekta ya afya fungu 52 inaomba kuidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi 415,014,262,000.00 zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida na shilingi 544,137,902,597.00 zikiwa ni fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kati ya hizo shilingi 270,600,000,000.00 ni fedha za ndani na shilingi 273,537,902,597.00 ni fedha za kutoka kwa wadau wa maendelo wa nje.

139. Mheshimiwa Spika, katika miradi ambayo haimo katika mgawo wa fedha hiyo, huduma za dawa, fedha za maendeleo kwa Tanzania Food and Nutrition Centre-TFNC, mafunzo na maendeleo ya wataalam, kuimarisha vyuo vya mafunzo ya afya haikupewa hata shilingi. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza ni kwavipi tutaweza kujitegemea katika sekta ya afya kama mipango ya bajeti zetu hailengi kutatua tatizo la upatikanaji wa wataalam sambamba na kuwaongezea utaalam wale waliopo?
140. Aidha, Mheshimiwa Spika, kwa upande wa fungu 53, Wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 31,537,431,013.00 kati ya hizo za matumizi mengineyo ni shilingi 15,825,478,000.00 na shilingi 2,760,061,013.00 ni fedha za maendeleo. Katika hizo fedha za maendeleo shilingi 1,760,061,031.00 ni fedha za nje.

141. Mheshimiwa Spika, Sekta hii ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni idara muhimu sana katika kujenga jamii inayowajibika na hivyo kujenga taifa linalowajibika, hivyo fedha zinazotengwa kwa sekta hii ni kidogo kiasi cha kuleta mabadiliko katika jamii na nchi kwa ujumla. Kwani ukiangalia vyuo vyote nane vya maendeleo ya jamii vinavyosimamiwa na wizara vimepewa jumla ya shilingi bilioni 1 tu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati, hivyo hakuna fedha kwa ajili ya uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na wakufunzi.

142. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ni muda mwafaka sasa kwa Serikali kuliona hili la kuwezesha Idara hii ya maendeleo ya Jamii ili kujenga Tanzania mpya yenye maadili na mtazamo chanya wa kujiletea maendeleo na sio kutegemea wahisani kama ilivyo sasa.

E. HITIMISHO
143. Mhershimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba afya ya taifa ni jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kwamba utoaji wa huduma za afya za kibingwa kwa wakati zinaokoa muda wa uzalishaji na hivyo kuongeza ufanisi. Aidha, utoaji wa dawa za kuzuia magonjwa (chanjo) ni muhimu sawa na dawa za kuponya magonjwa kwa kuwa zinasaidia kwa kiwango kikubwa kujenga ustawi na Taifa kuwa na afya.
144. Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma ya taifa lenye afya, Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia Sera ya Afya ya CHADEMA itashirikisha sekta binafsi kupitia ubia na sekta ya umma (PPP), kujenga,kuendeleza na kutumia miundombinu ya afya, pia kuongeza udahili wa mafunzo ya watendaji katika ekta ya afya ili kukidhi mahitaji ya jamii kwa mfumo wa ubia lakini serikali ikibakia kuwa ni mbia mkuu.
145. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunaamini kuwa teknolojia ya afya ni matokeo ya tafiti bora za kitabibu, ambapo matumizi ya ujuzi na elimu katika sekta ya afya hususan dawa, vifaa tiba, chanjo na mbinu vinatumika kutatua matatizo ya kiafya na kuboresha maisha ya wananchi. Hivyo tutahakikisha tunakuza sayansi ya tiba na kuboresha vifaa tiba na mbinu mbalimbali za utoaji wa huduma bora za kitabibu. Sambamba na hilo tutahakikisha usajili wa taasisi za ndani za utafiti, tiba asili na tiba mbadala kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya. Rejea sera za CHADEMA uk 44 -48

146. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.


………………………………………….
Esther N. Matiko (Mb)
Kny: MSEMAJI MKUU WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
07 Mei, 2019
 

Attachments

  • HOTUBA YA KAMBI RASMI AFYA 2019- MATIKO.doc
    171.5 KB · Views: 60
Back
Top Bottom